loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kizinga FC: Klabu ndogo FC mipango mikubwa

Kizinga FC: Klabu ndogo FC mipango mikubwa

Iko chini ya klabu ya soka ya Kizinga yenye makazi yake Mbagala Msikitini. Ni klabu ambayo ina jina dogo lakini mipango mikubwa. Ilianzishwa mwaka 1985 na wazee wa Msikiti huo wa Mbagala wakati huo ikiwa na malengo ya kucheza soka kiburudani zaidi, tofauti na sasa ambapo wamefanya mabadiliko makubwa na kuwa na malengo yenye kuinua soka la vijana.

Kama zilivyo kwa klabu nyingine ina malengo yake mengi na kubwa zaidi ni kuhakikisha wanaboresha na kuwa klabu kubwa kama ilivyo kwa Simba, Yanga na Azam. Ili kufikia huko tayari wamefanya usajili wa klabu ndani ya Manispaa hiyo ili kuhakikisha inatambulika na kupata nafasi ya kucheza kwenye mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na Wilaya.

Kizinga Fc ina wachezaji wa mtaa wa Kizinga pekee wenye vipaji lukuki wadogo kwa wakubwa. Sio kwamba wana pesa sana bali wanajitolea kwa uwezo wao na mapenzi yao katika kuinua wachezaji wenye uwezo kisoka kupata nafasi ya kutambulika. Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ally Haji anasema ndani ya klabu kuna vijana wenye umri chini ya miaka 12 hadi 20 na kuendelea.

Wote wamekuwa wakiingia huko ili kufundishwa na kuweza kutimiza malengo yao waliyojiwekea. Anasema katika kutambulika timu hiyo mwaka 2011 ilishiriki kwenye mashindano ya Kombe la Kova kwa mara ya kwanza ili kuwapima wachezaji walioko katika kikosi hicho ambapo hawakushinda lakini walionekana kupiga hatua kwa kuingia hatua ya nusu fainali.

“Yalikuwa ni mashindano yetu ya kwanza lakini timu ilijitahidi kwa kuonyesha kiwango chake,” anasema Haji ambaye pia aliwahi kucheza soka miaka ya 1975 katika timu ya Mogadishu Somalia. Pia, wamewahi kushiriki kwenye mashindano mengine makubwa ya mtaani kama Kombe la Diwani Kijichi ambayo yamewaimarisha.

Anasema mwaka huu kwa mara ya kwanza wameingia kucheza ligi daraja la nne hivyo mipango yao kuanza kusogea hatua kwa hatua, lengo ni kufuzu hatua ya 16 bora Wilaya ya Temeke. Pamoja na kufikia hatua moja mbele, anasema bado wana changamoto kubwa mbele hasa ikizingatia kwamba ni timu inayojitegemea kwa kila kitu, hawana ufadhili wowote kwa ajili ya kuwaunga mkono.

Viongozi wa timu wakishirikiana na wachezaji wamekuwa wakijichangia fedha za kununua jezi, mipira na vifaa vingine vya michezo. Pia, wanapohitajika kwenda kushiriki kwenye mashindano ndani ya Wilaya wanakuwa hawana fedha za chakula wala maji. Licha ya kupitia magumu yote, nia yao imekuwa ni moja, kuendelea kujitegemea wakati wanaendelea kutafuta udhamini, na ikitokea wako tayari kushirikiana katika kuwasaidia vijana wengi kutimiza ndoto zao.

Anasema mpira wa miguu umekuwa ukiwaepusha vijana hao kushiriki vitendo viovu vya matumizi ya dawa za kulevya au bangi, kwa sababu huwafundisha nidhamu, michezo itakayowaweka bize na kuchoka. Jambo ambalo ni la kufurahisha ni kuona kuwa hata makocha wenyewe wamekuwa wakijitolea bila kulipwa chochote.

Hayo yote ni kwa sababu wao wenyewe walipitia katika michezo. Kocha wao mkuu William Noel aliwahi kuichezea timu ya Yanga B, miaka ya nyuma hivyo anaelewa umuhimu wa soka na ndoto za vijana wengi walioko mtaani wakiwa na hamu ya kupata nafasi kwenye timu kubwa.

Anasema: “Mimi mwenyewe niliwahi kucheza soka hivyo naelewa mazingira ya mtaani ya vijana wengi, wengi wana ndoto na wanatamani kufikia, kwa kushiriki kwetu kwenye mashindano makubwa kutatutambulisha kwenye anga ya michezo”. Licha ya juhudi zao, wamekuwa wakikatishwa tamaa na wazazi wa wachezaji wanaowazunguka.

Kwanza wanapofanya vibaya wamekuwa wakilaumiwa na kupewa maneno ambayo ni ya kuwavunja moyo. “Watu wengi waliotuzunguka hawajui kuwa soka lina msingi wake hivyo wanapofanya vibaya huwavunja moyo badala ya kuwahimiza, kwa kweli tumekuwa tukivumilia kwa sababu tunaamini kuna vipaji vya kweli hapa ila vinatakiwa kuvumiliwa vije kufanya mambo makubwa,” anasema.

Kocha huyo anasema, amekuwa akifanya kazi yake katika mazingira magumu kwa sababu ya kukosa viwanja vya kufanyia mazoezi yao. Wametengeneza uwanja wao kwa kutumia jembe la mkono na ndio ambao hukutana kila siku kwa ajili ya kufanya mazoezi yao na kufikia malengo yao.

Kwa vile ni timu yenye malengo makubwa wangependa kuona wanaungwa mkono na wadau mbalimbali wanaopenda soka hasa wakiamini kwamba timu ya Taifa inatengenezwa na vijana wa mtaani. Katibu Mkuu Haji anasema ligi za mtaani zinahitaji kusaidiwa na Shirikisho la Soka Tanzania, macho yao yote yaelekee kwenye soka la mchangani na ndipo wataweza kuwapata wengi.

Anasema Kizinga inatamani siku moja kucheza Ligi Kuu Tanzania bara ili iweze kufika huko kunahitajika sapoti ya wadau na TFF angalau kwa kutambua mchango wao wawape jezi, mipira na vifaa vingine. Yote yanawezekana kama ombi la Kizinga litafanyiwa kazi na wadau wa michezo. Ni timu ndogo yenye malengo makubwa nayohitaji kutimiza ndoto zao.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi