loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kliniki, madawati ya vijana yaanzishwe kutoa elimu ya afya ya uzazi

Kliniki, madawati ya vijana yaanzishwe kutoa elimu ya afya ya uzazi

Kukosekana kwake, kumechangia vijana wengi kukosa elimu hiyo muhimu katika kupanga uzazi na maisha yao. Vijana ambao ni rika muhimu katika taifa lolote, wanatakiwa kupewa mafunzo ya afya ya uzazi ili kupanda uzazi, kujua mifumo ya uzazi na kuamua uzazi wanaotaka, wanaopenda na wanaochagua.

Mafunzo hayo lazima yatolewe mahali kama hospitalini, na wataalamu waliosomea, jambo ambalo halipo kwa sasa. Kukosekana kwa mafunzo ya afya ya uzazi kwa vijana katika kliniki au dawati maalumu kwa ajili yao, ambao ni wale wa umri wa miaka 15 hadi 24, wanaofikia theluthi moja ya wananchi wote, kumechangia vijana wengi kutafuta habari hizo kwa marafiki, majirani na wazazi, ambazo nyingi kati yake zinakuwa hazina ukweli.

Ukweli huo umebainika kwenye semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari iliyofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro ambayo iliandaliwa na Shirika la Kimataifa la Utafiti na Dawa (AMREF).

Imebainisha kwamba japo huduma za afya ya uzazi ni muhimu kwa vijana, lakini wamekuwa wakiikosa. Mkufunzi kutoka AMREF, Meshach Mollel, anasema vijana wanahitaji elimu ya afya ya uzazi katika kupanga familia, kuamua uzazi, wakati wa kupata watoto, idadi na muda wa kupishana kutoka mtoto mmoja hadi mwingine.

Mollel anasema shirika lake kwa kugundua umuhimu wa elimu hiyo kwa vijana, limeamua kusaidia manispaa tatu za Ilala na Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Iringa, mkoani Iringa kuhakikisha zinakuwa na wataalamu wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana.

Wamechagua mikoa hiyo, kutokana na ukweli kwamba mkoa wa Iringa kwa wakati huo ndio ulikuwa wa kwanza kwa maambuzi ya Virusi vya Ukimwi kwa asilimia 14.7 kabla ya kugawanyika na kuunda mkoa wa Njombe ambao sasa ndio unaoongoza kwa asilimia 15.7.

Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa wa pili kwa kuwa na maambukizi mengi kwa asilimia 8.9, japo sasa kiwango kimeshuka hadi asilimia 6.9, hata kama ni zaidi ya wastani wa kitaifa wa asilimia 5.7.

Shirika limeamua kuwezesha wataalamu na kusaidia manispaa hizo kupitia mradi wa Haki za Afya ya Uzazi kwa Vijana (SRHR), kuhakikisha vijana wanapata haki hiyo ya msingi ya kupata mafunzo ya afya ya uzazi ambayo ni muhimu kuipita katika umri huo kwani ndio wa kuweka malengo na kupanga maisha ya kupata watoto.

Japo mradi huo unafanyika kwa majaribio, katika manispaa hizo tatu, lakini umeonesha mafanikio makubwa na umebaini wazi vijana wengi wamekuwa na taarifa za afya ya uzazi ambazo si sahihi kutokana na kuzipata katika vyanzo visivyo na uhakika na kukosa mahali sahihi pa kupata habari hizo ambako ni hospitalini.

Amref kwa kugundua hilo, limeamua kusaidia au kujengea uwezo hospitali za manispaa hizo, ili kuhakikisha zinatoa fursa kwa vijana kupata elimu ya uzazi.

Vijana wanakuwa na kliniki au madawati ya kupata habari zinazohusu afya ya uzazi. Lakini katika maeneo mengine, kumeanzisha vituo vya kutoa elimu hiyo, ambapo vijana wanaweza kufika na kupata machapisho na kupata elimu ya afya ya uzazi, bila kuhofia kukutwa na wazazi wao au kupewa lugha za kashfa na wahudumu wa afya katika hospitalini hapo.

Vijana wamekuwa hawapati elimu hiyo ya afya ya uzazi kutokana na sababu nyingi, zikiwamo za kupokelewa kwa lugha za kashfa na wahudumu wa afya. Wahudumu wengi wamekuwa wakiwatukana vijana wanaofika hospitalini kutafuta elimu au mafunzo ya afya ya uzazi, kitendo ambacho kimechangia kuwakimbiza wasifike tena.

Lakini mazingira yasiyo rafiki ya hospitalini, ambapo wanafika hapo na kushindwa kumpata mtu maalumu anayeweza kujua na kutoa mafunzo au elimu ya uzazi kwao, yamekuwa yakiwafanya vijana waishie kutafuta habari hizo kwa marafiki ambao wanakuwa hawana uhakika nayo.

Mollel anasema, hospitali nyingi zimekuwa hazina kliniki au madawati ya kujua au kutoa elimu kwa vijana, hivyo wamekuwa wakishindwa kufika hospitani na kujiunga na mama zao ambao wanakuwa wakipata huduma za uzazi kwenye kliniki zao. Vijana wamekuwa na wakati mgumu wanapofika hospitalini ili kupata elimu ya afya ta uzazi, kutokana na ukweli kwamba wahudumu wengi wa hospitali hawawapokei vizuri, hawawasikilizi na kuwapa mwanya kujieleza.

Baadhi ya wahudumu wamekuwa wakiwahoji vijana kwamba wanataka kujifunza afya ya uzazi hivi sasa wanaharaka gani, wangoje wakati ukifika wakimaliza masomo au kufikia umri wa kuzaa ndipo wajifunze, kitendo ambacho kinachangia kutafuta habari hizo kwa watu wanaowajua.

Wakati mwingine, kutokana na hali ya hospitali zetu, nyingi huduma hizo kutokana na uwingi wa watu, mjengo wa majengo yake, uchache wa wahudumu, vijana wanashindwa kupata muda, na mahali penye usiri ili kueleza nia yao ya kujifunza afya ya uzazi, hivyo wanalazimika kutofika kwa sababu wanaona aibu.

Vijana wangine wanaogopa kwenyda hospitalini sababu ya waga, wanaogopa kwamba watakutana wazazi wao. Hivyo kwa kuogopa kugongana na wazazi au walezi wao, hawaendi kabisa hospitalini badala yake wanatumia njia wanazojua wenyewe kupata elimu hiyo. Wengine wanatumia marafiki au kusoma vitabu mbalimbali hapa na pale, ambavyo vingine vinawapotosha na kuwaingiza matatizoni.

Kutokana na mfumo huo wa hospitali nyingi wa kutokuwa na kliniki za vijana au madawati ya kutoa ushauri kwao, vwengi wamekuwa wakiwatumia majirani, jamaa, ndugu wanaowaamini na marafiki kujifunza elimu ya afya ya uzazi, na wengi wanaotoa elimu hiyo wanakuwa hawana uhakika, baadhi yao vijana wanaishia kupata uja uzito na kutokana na kuwa wanakuwa bado shuleni au hawajajipanga vizuri, wanaishia kutoa mimba.

Amref imebaini hali hiyo katika hospitali za manispaa hizo, baada ya kuanza kutekeleza mradi huo. Imebaini kwamba vijana wamekosa mwanya wa kupata elimu ya afya ya uzazi kutokana na sababu za wahudumu wa afya kutoa lugha mbaya kwa vijana wanaofika kutaka huduma hiyo.

Kutokana na kubaini ukweli huo, AMREF inashauri kwamba halmashauri za manispaa husika na nyingine zinatakiwa kuongeza raslimali zake hadi kufikia walau asilimia 30 ili kuanzisha vituo vya vijana ambavyo vitakuwa maalumu kwa ajili ya kufanya mawasiliano na kutoa elimu ya huduma ya afya ambayo itakuwa rafiki kwa vijana.

Kwa kuongeza halmashauri zaidi ya asilimia tano zinazotengwa na halmashauri hizo kwa ajili ya vijana, kutasaidia vijana wengi kupata mafunzo ya kutosha ili kujua elimu ya afya ya uzazi ambayo ni muhimu katika maisha yao ili kupanga uzazi.

Lakini pia kutokana na kwamba yote yanafanyika kutokana na sera zilizopo, hivyo ni budi sera zinazohusu vijana zinatakiwa kufundisha na kuchambua kinagaubaga umhimu na mahitaji ya vijana ili kuwapa fursa adhimu ya kujua nafasi yao katika taifa kwa kupanga uzazi wao na hivyo maisha yao.

Halmashauri zinatakiwa kutenga raslimali fedha za kutosha ili kuhakikisha kunakuwapo na wataoa huduma ya afya ya uzazi kwa vijana, waliosomea au maalumu kwa kazi hiyo, ili kuhakikisha wanatoa huduma hiyo kikamilifu.

Watoa huduma hao wakijengewa uwezo kwa kusomeshwa au kupewa mafunzo maalumu ya kushughulikia vijana kama Tumaini Fute ambaye ni Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Iringa anavyosema, wanaweza kuwa msaada mkubwa katika kuokoa kizazi hicho ambacho hivi sasa hakina kliniki wala dawati la kupata elimu ya huduma za afya ya uzazi katika hospitali nyingi.

Kwa halmashauri kutenga fungu la kutosha, kutazifanya hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizomo kuwa na watalaam wa masuala ya afya ya uzazi kwa vijana ambao kwa sasa kutokana na uchache wa wahudumu wa afya unakuta wanatumia katika maeneo mengine na hivyo wanashindwa kutoa huduma hiyo kwa vijana.

Kwanini ni muhimu vijana kuwa na dawati lao au kliniki yao, hiyo inatokana na umuhimu wa kundi au kada hiyo katika taifa lolote, hao ndio nguvu kazi, hivyo wakajiua kupanga uzazi, lini na wakati gani wanatakiwa kupata watoto wataendesha vizuri maisha yao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Kadiri ya Taasisi ya Restless Development inayojishughulisha na vijana, zaidi ya nusu ya watu duniani ni vijana wa miaka 50. Na kwa Tanzania, asilimia 66 ya watu waliopo nchini, ni vijana wenye umri chini ya miaka 25 ambao wanatakiwa kujua elimu ya afya ya uzazi ili kusaidia kupanga maisha yao na kujenga uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Kutokana na umri wao, asilimia 52 ya vijana wa kike na asilimia 44 ya wavulana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 24, walifanya mapenzi kabla ya kuwa na umri wa miaka 18, wengi wao hawakuwa wanajua chochote kuhusu elimu ya afya ya uzazi. Wengi wao, takribani asilimia 44 ya akinamama au wasichana hao, walipata watoto wakiwa na umri wa miaka 19, umri ambao ni mdogo.

Ni wazi kwmaba wengi wao walizaa wakati wakiwa katika umri wa kuwa katika masomo ya sekondari au vyuoni. Kutokana na kutokuwa na elimu ya afya ya uzazi ya kutosha, katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, zaidi ya wanafunzi 55,000 waliondolewa shuleni kutokana na kupata mimba wakiwa shuleni, idadi ambayo kama wangekuwa na taaluma ya afya ya uzazi ya kutosha, ingepungua.

Takwimu hizo zinaonesha kwmaba vijana wengi wanakosa elimu ya afya ya uzazi, isipokuwa wachache tu ambao ni wavulana asilimia 22 na wasichana asilimia 28 tu, ndio wanapata elimu ya afya ya uzazi. Suluhisho la vijana wengi kupata elimu ya afya ya uzazi ni halmashauri au manispaa kuongeza bajeti kwa ajili ya vijana.

Bajeti ambayo itasaidia kuwaandalia vijana mazingira rafiki ya kupata huduma ya afya ya uzazi katika h o s p i t a l i kwa kuwaandalia kliniki zao au madawati maalumu ya kuwasikiliza.

Kwa kuongeza bajeti hiyo, kutasaidia kuongeza vituo vya kupashana habari kama Paul Mallimbo wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), anavyosisitiza kwamba habari za afya ya uzazi ni muhimu miongoni mwa vijana, fedha hizo zitaongeza uwanja wa taarifa au habari za vijana sahihi na kupatikana mahali sahihi kwa wakati sahihi na kutolewa na watu sahihi.

Kuwapo vituo hivyo, kusaidia kuwapa elimu ya afya ya uzazi, hivyo kupunguza kasi ya maambukizi mapya miongoni mwa vijana ambayo sasa yanafikia asilimia 60. Ni ukweli usiopingika kwamba vijana ni nguvu kazi ya taifa, ambao ni theluthi moja ya watu wote nchini, sawa na milioni 15. Halmashauri husika, ndizo zenye wajibu wa kutenga zaidi ya asilimia tano ya pato la halmashauri kwa vijana inayotengwa sasa.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi