loader
Kocha Ngabo aichambua timu ya Madola

Kocha Ngabo aichambua timu ya Madola

Tanzania katika michezo ya mwaka huu, ilipeleka wachezaji zaidi ya 40 ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kupelekwa katika michezo hiyo na mingine, lakini imeendelea kuvurunda. Timu ya Tanzania iliundwa na wachezaji wa riadha, ndondi, mpira wa meza, kuogelea, kunyanyua vitu vizito, judo na baiskeli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau wa michezo wamesema kuwa timu hizo hazikuwa na misingi imara ya ushindi, licha ya kupiga kambi nje ya nchi kwa takribani miezi miwili.

Timu ya ndondi:

Kocha wa muda mrefu wa ndondi za ridhaa ambaye ameshapeleka timu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, Olimpiki na ile ya Afrika, Remmy Ngapo anasema uongozi wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT), ndio ulaumiwe kwa kushindwa kwa timu yao.

Ngabo anasema kuwa uongozi huo unabidi kubeba lawama baada ya kushindwa kushauri mabondia kupiga kambi pamoja badala ya kundi moja kwenda China na jingine kupiga kambi Uturuki kila moja likiwa na kocha wake. Anasema kuwa baada ya kurejea nchini, timu hiyo ilikwenda Scotland ikiwa na kocha mmoja, hivyo tayari kila upande ulikuwa na mafunzo yao na tabia zao.

Anasema basi angalau makocha wote wawili wangeenda Scotland ili iwe rahisi kwa wale waliokwenda China ambao walikuwa chini ya Mzonge Hassan, kuendelea kupata mafunzo sawa na wale wa Uturuki ambao walikuwa chini ya Jonas Mwakipesile ambaye ndiye aliyekwenda nao Scotland.

Ngabo anasema kuwa kingine ambacho ni kibaya zaidi ni kwa kocha huyo (Mwakipesile) kutokuwa na sifa za kumpandisha bondia ulingoni na badala yake kuazima kocha kutoka Kenya mwenye sifa hiyo. Chama cha Kimataifa cha Ndondi (AIBA) hakiruhusu kocha asiye na nyota tatu kumpandisha bondia katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola pamoja na michezo mingine mikubwa.

Anasema kitendo cha kocha wetu kutokuwa na sifa za kumpandisha bondia, nacho kimechangia kwani bondia anatakiwa awe na mtu wa karibu ambaye kila raundi inapomalizika, anampa mbinu za kufanya kutokana na jinsi anavyomwona mpinzani wake, lakini kwa Tanzania hilo lilishindikana.

Anasema hata wakati mwingine huenda mabondia wetu hawakuelewana lugha na kocha huyo Mkenya na hata mbinu anazomuelezea kwani hajui bondia anayemsekandi ana udhaifu na nguvu gani.

BFT wanasemaje?

Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alizungumzia madai ya timu kufanya vibaya sababu ya kuweka kambi mahali tofauti na kutokuwa na kocha mwenye sifa za kuwapandisha mabondia ulingoni. Mashaga anasema kuwa hakubaliani na madai hayo kwani hao wanaosema hawana ujuzi wowote na masuala ya ndondi ila kwa sababu wana nafasi ya kuzungumza na ndio wanaongeaongea tu bila mpango.

Anasema kwa sasa sio kipindi cha kupeana lawama, bali kinachotakiwa ni kuwa watulivu na kusubiri timu irejee na ndio waeleze kulichowasibu na hapo ndipo zitaelezwa sababu za kushindwa kwa timu hiyo. Akielezea kuhusu suala la kutokuwa na kocha mwenye sifa, Mashaga anajitetea kuwa hilo sio tatizo la Tanzania tu kwani kuna nchi nyingi hazina makocha wenye sifa hizo za AIBA, lakini wanafanya vizuri.

Anasema mfumo huo wa timu kuwa na kocha mwenye nyota tatu, umeletwa na AIBA wakati BFT ilipofungiwa, hivyo kwa sasa Tanzania haina kocha mwenye sifa hizo ila huko mbele wanatarajia kuwa naye.

Mabondia wakongwe:

Ngabo anasema kuwa pamoja na baadhi ya mabondia wa Tanzania kucheza kwa muda mrefu na baadhi ya watu kusema kuwa `wamechoka’ hivyo watemwe katika timu hiyo, anapinga wazo hilo na kusisitiza kuwa bado wanahitajika kwa ajili ya kuwapa uzoefu chipukizi.

Ngabo anasema kuwa mabondia hao pamoja na kucheza kwa muda mrefu, lakini umri wao bado haujavuka ule unaotakiwa kucheza mchezo huo ambao ni miaka 40. “Katika wale mabondia hakuna aliyefika miaka 40 hivyo bado wako katika age limit (ukomo wa umri), hivyo tuwaache waendelee kuwepo ili wawape uzoefu mabondia wetu chipukizi,” anasema Ngabo.

Baadhi ya mabondia wanaodaiwa kucheza ngumi kwa muda mrefu na sasa kuonekana kuchoka ni pamoja na Nasser Mafuru, Emmilian Patrick na Joseph Martine.

Nini cha kufanya:

Kwa sasa BFT inatakiwa kuchagua wachezaji wengi chipukizi ambao watafanyishwa mazoezi ya muda mrefu na kuchezeshwa mapambano mengi ya kitaifa na kimataifa ili wafanye vizuri siku za usoni.

Anasema mazoezi na mashindano ya mara kwa mara itasaidia kuibua vipaji na kuwawezesha mabondia kupata uzoefu na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Alisema kuwa pia BFT ibadilishe mfumo wa kupata wachezaji kwani badala ya kuwatumia wale wa jijini Dar es Salaam, wakati umefika ivitumie vyama vyake vya mikoa kupata vipaji kutoka mikoani pia.

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi