loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kriketi Tanzania itazamwe kwa jicho la pili

Kriketi Tanzania itazamwe kwa jicho la pili

Mchezo huu unaonekana kuwa ni kama wa watu fulani ambao labda ni wale ambao wanakuwa na fursa ya kuwa karibu na viwanja vya kuchezea mchezo huo. Inaonekana kuwa ni mchezo ambao unachezwa zaidi na Watanzania wenye asilia ya Kiasia, labda kwa kuwa wanakuwawapo karibu zaidi na mazingira ya kuchezea mchezo huo.

Hali hiyo inarudisha nyuma harakati za kuuendeleza mchezo huo na pia inakatisha tamaa vijana ambao wanaupenda mchezo huu. Hii inatokana na kwamba kunakuwa hakuna wadhamini wa kutosha wanaojitokeza kusaidia mchezo huo kutokana na udogo wa hamasa. Kassim Nassoro ni nahodha wa timu ya wachezaji wa kriketi wa chini ya miaka 18 ya Chama cha Kriketi Tanzania ambapo pia ni mchezaji wa timu ya wakubwa.

Akizungumza na gazeti hili, Nassoro anasema kuwa mchezo huo kwa sasa hamasa inaongezeka kwa kuwa vijana wengi wanataka kujifunza. Anasema katika timu ya vijana wapo wanafunzi ambao wanasoma shule mbalimbali wamejitokeza na kutaka kujifunza mchezo huo.

Anasema huku hamasa hiyo ikiwa ni kubwa, lakini inakosekana miundombinu ya kuwasaidia vijana hao kuyafikia mafanikio. Akizungumzia mikakati ambayo inatakiwa kuwepo ni suala zima la mafunzo ya mara kwa mara pamoja na kusafiri na kwenda kujifunza mchezo huo nje ya nchi.

“Najua huu ni mchezo ambao unahitaji zaidi kujifunza mbinu mbalimbali kutoka kwa wenzetu na kwa sasa inatakiwa kusafiri kwenda nchi ambazo michezo kama hii inachezwa ili kujifunza mengi,” anasema Nassoro. Akizungumzia harakati zilizokuwepo mwaka 2010, anasema kuwa wachezaji watatu walipata fursa ya kujifunza mchezo huo kwa miaka mitatu kwa kipindi cha miezi sita sita.

Anasema kuwa katika mpango huo, vijana hao walijifunza mambo mengi kuhusu mchezo huo. Anasema wachezaji wanne waliojifunza mchezo huo nchini Uingereza walipata pia nafasi ya kujifunza pia ukocha na wana vyeti vinavyowatambulisha kama makocha. Anawataja wachezaji hao kuwa ni kama vile Hamis Abdalla, Khalid Reemtullah, Athuman Kakonzi na Benson Mwita.

Kati ya hao, Abdalla na Remtullah wote wana cheti cha ngazi ya tatu. Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni wa timu hiyo ya chini ya miaka 18 ya kriketi, Paul Nilsen anasema kuwa Tanzania ina vipaji vingi katika mchezo huo. Nilsen anasema kuwa ni mchezo ambao unahitaji mikakati mingi ya muda mrefu ili kuweza kuijenga timu nzuri ya wakubwa.

Anasema kuwa iwapo timu ya wadogo ikiwa haina msaada ni vigumu kuwapata wachezaji wazuri wa timu kubwa. Anasema kuwa nchi kama za Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika zilizofanya vema ni kutokana na kusaidiwa na nchi zao katika kuukuza mchezo huo.

Anaongeza kuwa Kenya kwa Afrika na dunia nzima kwa ujumla ipo juu kwa kuwa ilianza kuimarisha timu za watoto na ndio maana kwa sasa ipo katika mazingira ya kufanya vema zaidi. Nilsen anasema kutokana na kutokuwepo kwa hamasa kubwa ya kusaidia mchezo huo ndio maana hakuna watu wengi wanaojitokeza kuudhamini mchezo huo.

“Najua tatizo lililopo ni kwamba watu wengi labda niseme hawaufahamu mchezo huu au kwa vile hautangazwi sana na hivyo inakuwa ni ngumu kuweza kufanikisha maendeleo yake ila kwa sasa kunatakiwa kuwepo kwa mikakati ya kusaidia kuukuza kama nchi nyingine zinavyofanya,” anasema Nilsen.

Lakini hata hivyo kwa Tanzania bado kuna nafasi nzuri ya kuwawezesha wachezaji wa kriketi kufanya vema zaidi. Katika michuano ya mwaka 2010 ya ICC World League iliyofanyika Italia, timu ya Tanzania ilishika nafasi ya nne huku ya kwanza ikiwa ni Marekani ikafuata Italia, Nepal na kisha Tanzania kuwa ya nne kati ya timu nane zilizoshindana.

Iwapo kwa sasa mikakati ikiwekwa kwa timu za chini hasa chini ya miaka 18 na 16 kuna uwezekano mkubwa kwa Tanzania kuja kufanya vema katika michuano hiyo. Ili kukabiliana na changamoto ya udhamini ya mchezo huo hapa nchini Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo imeanza kudhamini timu ya chini ya mikaa 19.

Amani Nkuru ni Ofisa Habari wa Tigo na anasema kuwa kwa sasa kampuni hiyo imeongeza wigo wa udhamini wake katika michezo na kuutazama pia mchezo huo. Anasema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kuwekeza kwenye mchezo huo kwa vijana wadogo, Tigo imeanza na timu hiyo ya watoto na kuahidi kuwa inaendelea na mikakati ya kusaidia mchezo huo.

“Kriketi ni mchezo kama michezo mingine ambayo inaweza kuitangaza Tanzania kimataifa zaidi na kwa sasa tunaona kuwa huu ndio muwa mwafaka wa kuanza kusaidia kwa kuanza na timu ya watoto,” anasema Nkuru. Timu ya chini ya miaka 18 ya kriketi ina wachezaji kama vile Salum Jumbe, Shafii Kolo, Athimani Siwa, Kassim Nassoro, Goodluck Andrew, Lazaro Festo, Rashid Awadh na Juma Masquatee.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi