loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kuelekea Krismasi…..Siri ya Nyota ya Bethlehem, iliyoongoza mamajusi

Kuelekea Krismasi…..Siri ya Nyota ya Bethlehem, iliyoongoza mamajusi

Tukio hilo kwa upande wa kisayansi nalo halikuachwa, unajimu ulichukua mkondo wake, ambapo simulizi zinaeleza nyota nzuri yenye ajabu ilitokea Mashariki, masultani watatu wakaiona na kuifuata hadi iliposimama pale alipozaliwa Yesu. Watu hao wanaodhaniwa pia kuwa na utaalamu wa nyota ni Balthazar, Gaspar na Melkior, waliofika na kutoa zawadi zao za dhahabu, uvumba na manemane.

Leo hii, wanaastronomia wanajitokeza baada ya kufanya utafiti wa kina, wakisema ni tukio la kisayansi lililosababishwa na kusogea kwa sayari ya Jupiter. Dk Mark Thompson wa Taasisi ya Unajimu ya Uingereza anasema alifanya utafiti wa kina juu ya nyota hiyo inayozungumziwa katika Injili ya Mathayo, iliyoongoza wasafiri kutoka mbali.

Dk Thompson ametumia kompyuta kurejesha hali ya anga ilivyokuwa enzi Yesu alipozaliwa, kisha kufuatisha uwapo na hali ya nyota mbalimbali. Mtaalamu huyo anasema tukio lenyewe halikuwa la kawaida katika dunia ya unajimu. Kwamba kati ya Septemba 3BC na Mei 2BC palikuwapo matukio matatu, ambapo sayari ya Jupiter na nyota iliyoitwa Regulus zilipitana karibu kwenye anga la usiku.

Jupite iliipita Regulus, kwanza katika kusonga kwake kwa kawaida kimashariki. Kisha ilionekana kubadili mwelekeo kwa kurudi nyuma na kuipita tena safari hii ikisonga kwa Magharibi. Baada ya hapo, inasemwa kwamba ilibadili tena mwelekeo kwa mara ya tatu, ikirejea katika msongo wake wa Mashariki na ikaipita nyota ile kwa mara ya tatu.

Dk Thomspon baada ya kukamilisha kazi yake hiyo, alikuwa katika hatua za mwisho kuanza uwasilishaji mada kwenye Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC). Hapo ni katika kipindi kipya kiitwacho ‘Stargazing Live’ pamoja na mtaalamu mwingine wa astronomia, Profesa Brian Cox, aliyepata umaarufu mkubwa kwa kuchambua mambo ya anga za juu.

“Wale watu watatu wenye hekima waliaminika kuwa makasisi pia, lakini walikuwa wanajimu waliosifika enzi zile. “Wafalme wa sayari walipita karibu sana na mfalme wa nyota mara tatu lazima lingekuwa tukio kubwa na lenye umuhimu mkubwa na lingeweza kutafsiriwa kama kuzaliwa kwa mfalme mpya. “Kinachovutia zaidi hapa ni kwamba, katika ulimwengu wa unajibu, Jupiter inachukuliwa kuwa mfalme wa sayari na Regulus ndiyo nyota inayong’aa zaidi kwenye eneo la Leo, ndiyo mfalme wa nyota,” anasema.

Kwa muda mrefu pamekuwapo nadharia nyingi tofauti zilizobuniwa na wanajimu nyakati zilizopita, kama maelezo ya kisayansi juu ya Nyota ya Bethlehemu au Nyota ya Mashariki. Dk Thompson anasema alitazama hoja zote kabla ya kufikia hitimisho lake. Alizingatia nadharia ya ‘retrograde motion’, ambayo ni sayari au nyota kuacha mwelekeo wake wa kawaida na kuanza wa upande mwingine kwa muda fulani.

Anasema hiyo inawezekana kwa sababu sayari nyingine nje ya mfumo wetu wa Jua hulizunguka Jua taratibu zaidi ya Dunia, hivyo wakati mwingine sayari yetu huzipita.

“Kwa mwelekeo huo, maana yake ni kwamba sayari ile ilikuwa ikisafiri kuelekea Magharibi angani na mamajusi wale (waliotumia ngamia) wanaweza kuwa waliifuata kutoka Persia. “Kwa kutumia ngamia, mamajusi wale yaweza kuwa iliwachukua kama miezi mitatu, na cha kushangaza ni kwamba ni muda kama huo huo ambao Jupiter ilikuwa ikisafiri kwa mwelekeo wa Magharibi. “Si juu yangu kwa kweli kusema iwapo Biblia ipo sawa au la. Ninachofanya mimi ni kutafiti kwa kuchora na kuweka matukio kwa kuhusisha na ukweli ulio mbele yangu,” anasema msomi huyo.

Wakale waliamini kwamba hali ya kinajimu ilihusiana na matukio ya kidunia. Ilikuwa kawaida kwa miujiza kuhusishwa na kuzaliwa kwa watu maarufu, wakiwamo mababu wa Kiebrania na mashujaa wa Kigiriki na Kirumi. Nyota ya Bethlehemu au Nyota ya Mashariki inahusishwa na Nyota ya Uaguzi katika Kitabu cha Hesabu kinachosema: “Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea kwa Yakobo; Fimbo itainuka katika Israeli, Na kugonga ukingo wa Moabu, Na kuharibu wana wote wa ghasia.”Katika mapokeo ya Kikristo, Nyota ya Bethlehemu hujulikana pia kwa jina la Nyota ya Krismasi, na maelezo yake huonekana katika simulizi za uzao wa Yesu, ikiongoza mamajusi wa Mashariki.

Hao, baada ya kufika na kukutana na Mfalme Herode wa Yudea, walimuuliza ni wapi alizaliwa mfalme. Herode alifuata maelezo ya Kitabu cha Mika, akatafsiri uaguzi wa nabii na kuwaelekeza Bethlehemu. Hata hivyo, aliwataka wakishafika huko warejee kwake, ili naye aende kumwona mtoto.

Bali moyoni mwake alikuwa na wazo la kwenda kumuua, maana hakutaka mfalme mwingine kuchukua nafasi yake. Ni baada ya kutoka hapo, masultani wale walitumia nyota hadi kufika, kisha kurudi kwao kwa njia nyingine, baada ya kuonywa na Mungu katika ndoto. Wataalamu wa tauhidi wanasema kwamba nyota hiyo ilikuwa ishara ya muujiza, kutia alama uzao wa Yesu au Masiya.

Kwa kawaida maadhimisho ya kuwasili kwa masultani hao watatu wakiongozwa na nyota hufanyika kila mwaka Januari 6. Makala haya yameandaliwa na Mwandishi Wetu kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi