loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

KUELEKEA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO: Balozi Iddi: Wazanzibari wengi asili yao ni Bara

Dhamira ya Serikali zote mbili kama ilivyoelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, ni kuondoa mambo yanayoleta vikwazo kwa kuhakikisha yanatatuliwa ili muungano uendelee kuwa imara na uwe na faida kwa wananchi wa pande zote mbili.

Pamoja na kuchukuliwa kwa juhudi za makusudi za kuelimisha wananchi kuhusu faida za muungano na changamoto zake, taarifa mbalimbali zinaonesha kwamba umefaidisha Wazanzibari kwa kiwango kikubwa. Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Balozi Seif Ali Iddi, akizungumza hivi karibuni mjini Dodoma, anasema kuna haja ya kutafuta kila namna ya kuimarisha muungano ili uendelee kuwepo kutokana na manufaa yake.

Anasema suala kubwa linaloikabili nchi yetu ni kupatikana kwa katiba mpya itakayokuwa na manufaa zaidi kwa Watanzania ambapo mchakato huo umekuja baada ya kuonekana katiba ya mwaka 1977 haikidhi haja na imejaa viraka. Anasema muungano wa Tanzania utakuwepo na utaendelea kuwepo kwani hakuna mtu atakayeuzuia, kuuhujumu au kuuvunja kwa maslahi yake binafsi.

Balozi Iddi anasema matarajio ya Jamii ya Wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar ni kuendelea kuishi kwenye maisha ya furaha yaliyojaa matumaini ya kujengeka kwa hatma yao ya baadaye hasa katika kujikwamua kiuchumi.

Anasema hata kauli iliyotolewa hivi karibuni na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad kuwa Wazanzibari wanataka muungano wa mkataba si ya kweli na kwamba kiongozi huyo hakuwahi kuzungumza na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi na hivyo hiyo ni kauli yake binafsi na wananchi wasitishike.

Balozi Seif Iddi anasema Wazanzibari wengi wanathamini muungano kwa kuwa wenye manufaa kwao na hivyo wanachotaka ni kuuboresha zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili. Pia anasema katika mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba unaoendelea baadhi ya wanasiasa wanaonesha dhahiri wana nia za kutaka kuvunja muungano, jambo ambalo si zuri na wananchi wote wanaitakia mema nchi yetu wanapaswa kuwa macho.

Hilo, anasema, linajidhihirisha kutokana na kauli zao kwani kauli nyingine zinazotolewa zinachonganisha wananchi wa pande mbili za muungano. “Wazanzibari wako milioni 1.3. Walifanya nao wapi mazungumzo na wakawaambia kwamba wanataka serikali ya mkataba?” Anahoji.

Anasema kwa sasa kuna Wazanzibari takribani 800,000 wanaoishi Tanzania Bara na kufanya shughuli zao za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi na kwamba wanaotaka kuwagawa Watanzania hawa ni watu wenye choyo na hatari. “Muungano umekuwa na faida kubwa kwa Zanzibar kuliko Bara na pia umeimarisha umoja na kupanua wigo wa matumizi ya ardhi na hata uchumi,” anasema.

Balozi Iddi anasema kauli kuwa Wazanzibari wote hawataki muungano wa sasa na badala yake wanataka muungano wa mkataba hazina mantiki yoyote na ni za kupuuzwa.

“Naomba kuuliza, ni Wazanzibari gani hao wanaowasemea? Mbona sisi hapa pia ni Wazanzibari na hatuna msimamao huo wa mkataba?” Pia anasema kitendo cha baadhi ya viongozi hao wa kisiasa kuwataka Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara kuacha shughuli zao za kila siku na kurudi Zanzibar ni cha ajabu na hivyo hakina budi kupuuzwa,” anasema.

Anasema kiasili Wazanzibari wengi asili yao ni Tanzania Bara na hata ukienda Zanzibar kuna Wanyamwezi, Wasukuma na makabila mengine mengi ambayo yamekuwa Zanzibar kwa miaka mingi wakifanya shughuli zao, ikiwemo kilimo bila bughudha yoyote. Anasema suala la kuhoji uwepo wa muungano halina tija kwani wakati muungano ukiasisiwa mwaka 1964 hakukuwa na kura ya maoni na hivyo muungano huo utalindwa kwa sababu una maslahi kwa Watanzania wote.

Anasema katika muundo wa serikali mbili ziko changamoto, lakini nyingi zimeshafanyiwa marekebisho na utatuzi. Anabainisha katika katiba ya Zanzibar kinachosumbua watu ni Zanzibar kuitwa nchi na katika hilo anafafanua kwamba ilibadilishwa kutokana na makubaliano ya kuingizwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Aidha anasema jambo ambalo watu hawaelewi ni kwamba neno nchi halina maana ya utaifa kwani huwezi kwenda nchi za nje ukakuta kuna Ubalozi wa Zanzibar kwani Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano. “Muungano unatakiwa kuimarishwa zaidi kwani umekuwa na tija kubwa kuliko ilivyo kwa mitazamo ya watu wengine na tunachotaka sisi ni kuendelea kuwa na muungano wa serikali mbili,” anasema.

Akizungumzia Bunge la Katiba linaloendelea Dodoma, Balozi Iddi anasema mchakato wake umekuwa ukishuhudiwa na wananchi walio wengi lakini umekuwa ukitawaliwa na wanasiasa, baadhi yao wakionesha dhahiri wana nia za kutaka kuvunja muungano. Anasema hii ni kutokana na kauli wanazotoa na kushuhudiwa na wananchi kupitia vyombo vya habari kwamba zimekuwa na muelekeo wenye kuchonganisha wananchi wa pande mbili za muungano.

Anasema haipendezi kuona baadhi ya wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba wakiendeleza ushabiki wa kisiasa ndani ya vikao vya Bunge hilo kwa kutengeneza mbinu za kuongeza muda wa vikao wakisahau kwamba kodi za wananchi zinapotea bila kufanya kazi zilizokusudiwa.

Anasema pamoja na hatua inayofanywa na wajumbe wa Bunge hilo ya kujadili Rasimu ya Katiba na kuweza kubadilisha, kuboresha, kuongeza au kupunguza lakini bado zipo changamoto zinazolikabili Bunge hilo. Anazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kukosekana kwa uvumilivu miongoni mwa wajumbe na pia Bunge kutawaliwa na hisia za kisiasa zaidi badala ya kuweka maslahi ya Taifa mbele.

Kadhalika anasema kumekuwepo na vikundi vya watu wachache wasiotaka mchakato huo wa Katiba Mpya uendelee kwa ufanisi kutokana na utashi wao wa kisiasa na siyo suala zima la maridhiano bila kuangalia wachache wanataka nini. Akizungumzia suala la mikutano ya hadhara inayoanza kuchukua sura mpya ya kutaka kugawanywa wananchi Balozi Iddi anataka wananchi kuwa macho na tabia zinazoonekana kutaka kuwagawa Watanzania wa pande hizi mbili za muungano.

“Hata kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwataka wananchi wa upande mmoja wa muungano kuacha shughuli zao za kimaisha na kurudi katika makazi yao waliyozaliwa ni kuashiria jinsi viongozi hao walivyo na nia mbaya katika kuvunja muungano,” anasema.

Pamoja na hayo anasema ana matumaini kuwa Muungano uliopo sasa ambao unafikisha miaka 50 utaendelea kudumu, kuwepo na kuendelea kwa kipindi kirefu kijacho kwa vile bado unaridhiwa na kukubalika na jamii kubwa ya Watanzania. Pamoja na hayo anawatoa hofu wananchi kwani kamwe Zanzibar haijavunja katiba kwa vile haina Utaifa.

Anasema ulimwengu umekuwa ukishuhudia muungano wa mataifa kadhaa iliyoundwa katika mifumo tofauti hasa ule wa Shirikisho ambayo hatma yake ilikuwa ni fupi huku kukiwa hakuna mafanikio yoyote.

Anasema Muungano wa Tanzania ambao bado unaendelea kuwa wa pekee na wa mfano barani Afrika katika kipindi cha miaka 50 iliyopita ni taswira kuwa kuna umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi, jambo ambalo na zuri na linapaswa kuenziwa na mtu yeyote muungwana.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi