loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

KUELEKEA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO: ‘Muungano umewaunganisha wanawake Bara na Visiwani’

Wanawake wa Zanzibar walipita katika harakati mbalimbali za kutafuta haki, ambapo awali walikuwa hawaruhusiwi kupiga kura katika chaguzi mbalimbali visiwani Zanzibar.

“Wanawake Zanzibar tumetoka mbali katika kudai haki zetu ikiwemo ya kupiga kura…wanasahau kwamba awali tulikuwa hatupigi kura hapa,” ni kauli ya Mama Fatma Karume. Fatma Karume ni mke wa kwanza wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume ambaye alifanya kazi kubwa za kuwaunganisha wanawake katika kipindi cha harakati za kupigania uhuru.

Mchango wake kwa wanawake ulikuwa mkubwa kwa sababu alifanya kazi pamoja na mumewe Abeid Amani Karume ambaye baadaye alikuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar. Mama Karume anasema uhusiano wa viongozi wakuu waliopigania uhuru akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere pamoja na Karume kwa kiasi kikubwa ulichangia kuwepo kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa mfano, anasema wakati wa harakati za kuzaliwa kwa ASP, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alikuwa Zanzibar na alishuhudia akisema, huo ndiyo mwanzo mzuri wa harakati za kuelekea uhuru. “Tulikuwa na Mama Maria Nyerere katika sherehe zile ambazo tuliwashuhudia waume zetu wakiweka mikakati ya nchi zao kupata uhuru,” anasema Mama Fatma.

Anasema Tanganyika ilikuwa nchi ya kwanza kupata uhuru kutoka Uingereza, uhuru ambao ulichochea pia ukombozi wa mataifa mengine ya Afrika ya Mashariki. Kwa mfano, anasema wakati Tanganyika ikipata uhuru mwaka 1961, baadhi ya wanawake wa TANU walifanya kazi kubwa kuwasaidia wanawake wenzao wa ASP ili kuhakikisha wanatoa mchango mkubwa wa nchi kujikomboa.

Anawataja wanawake waliokuwa manaibu mawaziri katika Serikali ya Mwalimu Nyerere ni pamoja na Lucy Lameck na Bibi Titi Mohamed ambao waliamsha shamrashamra za kupigania uhuru na kuona wanawake wenzao wa Zanzibar wanajikomboa.

“Namkumbuka sana Bibi Titi Mohamed. Alikuwa mwanamke shujaa aliyesaidia wanawake wenzake kuona wanajikomboa kiakili na kiuchumi na kupiga hatua kubwa ya maendeleo,” anasema Mama Karume. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulizaliwa Aprili 26 mwaka 1964 na kuzaliwa kwa taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwalimu Nyerere akawa rais wa kwanza na Makamu wake akawa Karume. Mama Karume anasema kuzaliwa kwa Muungano kuliwaunganisha wanawake wa Zanzibar na Tanzania Bara kuwa kitu kimoja na hasa ushauri ulipoanza kutolewa wa kuwepo kwa taasisi moja itakayowakusanya na kuwaunganisha wanawake wote wa Tanzania.

“Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, baada ya kuwaunganisha wanawake kutoka Bara na visiwani kuwa kitu kimoja hatimaye ukazaa chombo kipya cha Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT),” anasema. Mama Fatma Karume anasema mara baada ya kuzaliwa UWT, wanawake wa pande mbili za muungano walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha haki zao zinapatikana na kuimarika.

Mmoja wa viongozi waandamizi wa umoja wa wanawake Tanzania kwa upande wa Zanzibar, Asha Simba Makwega, anasema umoja wa wanawake ulianza kujiimarisha kiuchumi na kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuwasomesha wanawake ndani na nje ya nchi.

“Umoja wa wanawake ulifanya kazi kubwa ya kuwasomesha wanawake nje ya nchi kwa lengo la kuwa na wanawake wasomi watakaokuwa viongozi wa baadaye wa nchi,”anasema. Dk Sirra Ubwa, Naibu Waziri wa Afya ni miongoni mwa wanawake waliopata nafasi za kusoma elimu ya juu nchini Urusi kwa ufadhili wa jumuiya ya wanawake UWT.

Anabainisha, umoja wa wanawake UWT bado ni chombo imara chenye uwezo wa kuwaunganisha wanawake nchini na kupiga hatua kubwa ya kiuchumi na maendeleo. “UWT bado ni chombo imara chenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kuwaunganisha wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupiga hatua kubwa za maendeleo,” anafafanua.

Dk Msimu Abrahman alikuwa Katibu Mkuu wa UWT, anasema umoja huo kwa kiasi kikubwa umeleta mafanikio na kuwaunganisha wanawake. Anasema wanawake wengi wa Tanzania mara baada ya uhuru na Muungano walihamasishwa na kutambua haki zao ikiwemo za kupiga kura katika chaguzi mbalimbali.

“Ona leo hii wanawake wamehamasika wanatambua kupiga kura pia ni haki yao, wanajitokeza kupiga na kuwania nafasi mbalimbali, awali hali haikuwa hivyo”, anabainisha Dk. Msimu. Makamu Mwenyekiti wa UWT, Asha Makame anasema wanawake wa Tanzania wamepiga hatua kubwa ikiwemo kuzitambua haki zao na kupambana na udhalilishaji wa kijinsia.

Makame anasema kazi kubwa inayofanywa na umoja wa wanawake nchini ni kuhakikisha wanawake wanajikomboa na umasikini kwa kuwezeshwa na kupata mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuendesha biashara zao. Kwa mfano anataja juhudi za UWT ni pamoja na kuanzishwa kwa benki ya wanawake nchini ambayo itaweka kipaumbele kwa wanawake kupata mikopo ya biashara.

“Hizo ndiyo juhudi za umoja wa wanawake nchini kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanaondokana na umasikini na utegemezi kutoka kwa wanaume na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia,” anabainisha Makame. Waziri wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake,Watoto na Vijana, Zanzibar, Zainab Omar Mohamed anabainisha kuwa wanawake nchini wana nafasi kubwa kuendelea iwapo watakuwa kitu kimoja na kupambana na mifumo kandamizi.

Anasema serikali ya Tanzania imeridhia mikataba yote ya kimataifa na kikanda ambayo itahakikisha inakomesha vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

“Kikwazo cha mwanamke wa Tanzania kwa sasa ni kuwepo kwa mifumo ambayo inarudisha nyuma juhudi za maendeleo na kiuchumi ambayo lazima imepigwe vita,” anasema Waziri Zainabu. Aidha anabainisha kuwa serikali zote mbili, Zanzibar na bara wameshaanzisha taasisi ikiwemo benki ya wanawake kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu itakayowakomboa kutoka kwenye umasikini.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi