loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

KUELEKEA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA MUUNGANO- Wasomi: Maamuzi kuhusu Muungano yasiwe ya kukurupuka

Sio Tanzania nyingine, bali yenye Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na inayosifika kwa kuwa na amani na utulivu. Mungu ibariki Tanzania. Nimeanza makala haya kwa kumwomba Mungu aibariki Tanzania kwa sababu, sio kila anaye itazama anapenda iendelee kuwepo.

Vile vile, ni kwa sababu imekuwa kawaida kwamba siku zote jambo au kitu chenye mafanikio ndicho kinachonyooshewa vidole na wasiopenda kushamiri kwake. Wengi wape. Muungano unahitajiwa na wengi kutoka Zanzibar na Bara pia. Unaweza ukasema mwandishi ana ushahidi gani wa kuhalalisha kupendwa kwa Muungano na wengi.

Jibu linakuwa rahisi kwamba watanzania kutoka maeneo hayo mawili, yaani Zanzibar na Bara wamehakikisha hivyo kutokana na maoni yao kwa gazeti hili. Vile vile wamekuwa wakitoa maoni ya aina hiyo wanapokuwa katika mikutano mbalimbali. Mfano mmoja wa mikutano hiyo ni kongamano la vijana lililofanyika Dar es Salaam hivi karibuni (Jumapili ya Tar 30/3) kuhusu wajibu wa vijana katika kuimarisha muungano.

Kati ya wengi niliowasikia wakizungumzia Muungano na aina ya serikali wanayoitaka katika kongamano hilo ni wasomi kutoka katika vyuo mbalimbali nchini, kikiwemo cha Zanzibar, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Chuo cha Diplomasia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa nyakati tofauti katika kongamano hilo, wamekataa Muungano usivunjwe na kusisitiza kuwa ulindwe kwa nguvu zote kwa sababu una manufaa kwao na kwa watanzania wengine wanaopenda amani, Bara na Visiwani. Miongoni mwao ni Dorcas wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) anayetaka matatizo ya Muungano kama yapo, yatatuliwe kwa njia zinazowezekana na si kuuvunja.

Mwasunda anasema kuwa wanandoa, ndugu na hata jamaa hukwaruzana na hata kugombana, lakini mwisho wa siku huamua kutatua matatizo yanayojitokeza na kuendelea kuwa pamoja.

“Muungano ni kama ndoa inayostahili kuendelea kuwepo kwa kutatua matatizo yanayojitokeza na si kuuvunja. Tukiuthamini utanzania wetu, tutaulinda, kuutunza na kuutetea Muungano,” Mwasunda anasema na kuungwa mkono na mshiriki mwingine wa kongamano kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Lugano Mwakyusa anayetaka wasiouthamini Muungano waeleweshwe faida zake ili waulinde pia.

Katika kuonesha kuwa Wazanzibari nao wanataka Muungano udumu, Mshiriki kutoka kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Zanzibar, Juma Juma anasema, kuna baadhi ya watu wachache hawautakii mema Muungano kutokana na matamshi ya uchochezi wanayoyatoa siku hadi siku.

“Tena wengine ni viongozi wetu wanaoheshimika, wanatuchochea vijana na kutuweka njia panda kuhusu Muungano. Watu hawa wanawapata zaidi wasioelewa umuhimu na faida za Muungano hivyo wasiendekezwe, kwa sababu hawataki amani itawale Tanzania...”.

“Wanzanzibari tunauhitaji Muungano kwa sababu umetufaa na unaendelea kutufaa. Tatizo linalojitokeza ni kwamba makongamano kama haya yenye kutoa elimu hayatufikii visiwani tulipo hivyo kuwaacha wengi wakijazwa elimu tofauti na wasio uhitaji Muungano kwa sababu ya maslahi yao. Fikisheni makongamano haya Zanzibar wananchi waujue ukweli wa Muungano usivunjike,” Juma anasema.

Mbali ya wasomi, imezidi kudhihirika kuwa Muungano huo unaliliwa na kuhitajiwa na wengi na Mwenyekiti wa Mtandao wa Watanzania wenye asili ya Pemba waishio Bara (NEPPELTA), Sheha Haji Faki anathibitisha kwa kusema kuwa Muungano unastahili kuimarishwa kwa sababu una faida na maslahi kwa wananchi wa nchi washirika.

Faki anataja baadhi ya faida hizo kuwa ni kukua kwa biashara zao na kukuza mtaji wao kufikia Sh trilioni 1.2. Anasema, “Muungano hauna budi kuimarishwa kwa sababu umetunyanyua si tu kibiashara na ajira serikalini, bali umetuwezesha kuoana na kuishi kwa amani katika maeneo yote mawili bila kubaguliwa”.

“Sisi Wapemba tuishio Bara tunauhitaji sana Muungano kwa sababu tunaona kuwa chokochoko za baadhi ya watu kutaka usiwepo, zinalenga kuhatarisha usalama na kamwe haziwezi kuwa na msingi wowote,” amesema Mwenyekiti huyo.

Anaongeza kuwa wanatambua kuwepo kwa dalili zozote za kuvunjika Muungano hakuwezi kuwaacha salama, hivyo, hawako tayari kuangalia zikitokea bali watasimama kidete kuhakikisha kuvunjika huko hakutokei.

“Tunamhakikishia Rais Jakaya Kikwete na watanzania kuwa hatuko tayari kuona Muungano ukivunjika kwa sababu umetuletea udugu. Pia hatuko tayari kuona waasisi wake wakipuuzwa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume wakipuuzwa kwa kuwa walitumia busara na muda wao mwingi kuuanzisha. Tutawaenzi kwa kuuimarisha,” Faki anasema.

Kushiriki katika kilimo na ufugaji kwenye ardhi ya Tanzania Bara ni jambo jingine linalotajwa na Mwenyekiti huyo kwamba lisingewezekana endapo kusingekuwa na Muungano.

Ingawa matumizi ya ardhi ya Tanzania Bara yanayofanywa na Wazanzibari yamekuwa yakitafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni ‘kuporwa’ na watu hao, kutokana na kile wanachokilalamikia kuwa watu wa Bara hawaruhusiwi kumiliki au kutumia ardhi ya Zanzibar, wanaelezwa kuchangia kukua kwa seka ya kilimo na ufugaji katika Jamhuri ya Muungano.

Hoja ya Wazanzibari kumiliki na kutumia ardhi ya Bara, na wa Bara kukataliwa kumiliki ardhi Zanzibar, imejitokeza hivi karibuni, kwenye kongamano la vijana kuhusu wajibu wa vijana katika kuimarisha Muungano ambapo, Profesa Issa Shivji ambaye ni Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mwanasheria ‘akaipangua’ kwa kueleza kuwa ni hoja yenye nia ya kutengeneza uadui na sio kuimarisha Muungano.

Profesa Shivji anasema, ili Muungano uimarishwe na pande zote mbili, hoja kama hizo zisizo na ukweli lazima ziepukwe. “Kuna mambo mengi ya kujadili katika Muungano, si maneno yasiyo na ukweli kwamba Wazanzibari wanamiliki ardhi bara na wabara wananyimwa kisheria kumiliki ardhi Zanzibar. Ni vizuri Watanzania hasa vijana wakafikiri sana na kutafuta ukweli kabla ya kuzungumza juu ya jambo lolote...”. “Yapo masuala kama uwekezaji, wanapaswa waangalie huko kwamba wawekezaji wanapata ardhi kubwa na pia wanapaswa wajiridhishe kuwa wapo watu wa Bara wanawekeza katika ardhi ya Zanzibar, lakini si kusema kuwa hawa hawaruhusiwi na wale wanaruhusiwa,” Shivji anasema.

Anaongeza kuwa hoja kama hizo ndio zinazoweza kusababisha chokochoko zinazoweza kuvunja Muungano. Anashauri kuwa ni vema hoja ikatazamwa kwanza vizuri na kuchambuliwa kabla ya kutumiwa kama kigezo cha kufanya uchaguzi wa ama kuwa na Muungano au la, viginevyo, mchaguaji anaweza kujikuta amefanya uchaguzi mbaya uliosababishwa na kukurupuka.

“Faida za Muungano ziainishwe. Hata suala la Serikali moja, mbili au tatu lisiwe ndio hoja kuu ya kusababisha kuvunjika kwa Muungano. Watanzania watambue kuwa mshikamano wao ndio mafanikio yao na kwamba lengo likiwa moja mafanikio yanayokusudiwa yatapatikana,” Profesa Shivji anasema.

Kutokana na Watanzania Bara kuwathamini wenzao wa Zanzibar, kwa maelezo ya Mwenyekiti wa NEPPELTA, idadi ya Wapemba waishio Tanzania Bara imekua kufikia watu zaidi ya 800,000 mwaka 2012. Naye Profesa Gaudens Mpangala wa Taasisi ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema ni wajibu wa vijana kufanya uchambuzi kuhusu Muungano kabla ya kuamua uendelee au la.

Profesa Mpangala anayeuzungumzia Muungano kwa mtazamo wa historia zaidi, anatofautiana na Profesa Shivji katika mtindo wa kuuelezea Muungano huo tu kwa sababu Shivji, anauelezea kwa mtazamo wa kisheria zaidi, lakini, hoja yao ni moja kwamba inayosisitiza kulindwa, kutetewa na kuimarishwa kwa Muungano.

“Nawasihi vijana muheshimu rai ya serikali mbili huku mkifanya uchambuzi wa kina. Sioni sababu ya kukashifu au kubeza maoni ya watu wengine wanaohitaji Serikali tatu au moja kwa sababu, kila mtu anauhuru wa maoni. Cha msingi, ni kutumia busara, kuheshimu rai ya viongozi wetu na kufanya uchambuzi yakinifu badala ya kukurupuka na kusema hiki hakifai kama wengine wanavyosema kuhusu Muungano,” Profesa Mpangala anasema.

Anaongeza kuwa, mafanikio hayaletwi kwa kunyoosheana vidole kati ya Wazanzibari na watu wa Bara, wala kwa kuisema vibaya Tume ya Warioba, bali kwa kuwa na lengo moja, huku kila uamuzi ukifanyiwa tafakuri ya kina kwanza.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Namsembaeli Mduma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi