loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Kujisalimisha kwa Kony kutakuwa mwisho wa LRA?

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako Kony na waasi wake amejificha, amesema kuwa Kony amezungumza na serikali yake na kuonesha nia ya kujisalimisha endapo atahakikishiwa usalama.

Taarifa hizo zilizopokelewa kwa hisia tofauti, huku wengine wakidai kuwa Kony hawezi kujisalimisha na wengine wakidai kuwa anaweza kufanya hivyo baada ya kubaini kuwa mwisho wake umefika.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa taarifa hiyo inaonekana kama kiini macho na baadhi wameshindwa kuamini kama imetolewa na Kony mwenyewe au washirika wake wa karibu kwa lengo la kupima upepo wa kisiasa.

Serikali ya Marekani ni miongoni mwa mataifa yanayotilia shaka taarifa kuwa Kony amefanya mazungumzo na Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kuhusu kutaka kujisalimisha.

Ofisa kutoka katika Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Marekani, amekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa baadhi ya waasi ndio walishauriana na Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na sio Kony mwenyewe.

Marekani imetaka taarifa hiyo ya Kony ichukuliwe kwa tahadhari kwa Kony hutumia mbinu mbalimbali pale ambapo yeye na kundi lake la waasi wanapotaka kupumzika, kujihami, kujikusanya upya na kisha kuanza kuteka nyara, kuua watu wasiokuwa na hatia pamoja na kujihusisha na vitendo vingine haramu.

Pia kuna baadhi ya wachambuzi wa siasa wanasema huenda kiongozi huyo ameona mwisho wake unafika, hivyo anataka kuihadaa dunia kuwa ameingiwa na utashi wa kufanya mazungumzo ya amani badala ya kudai haki kwa kutumia mtutu wa bunduki.

Inadaiwa kuwa Kony anataka kutumia mbinu kama iliyotumiwa na kundi lililoshindwa la M23 ya kujisalimisha baada ya kubaini kuwa maji yapo ‘shingoni’ ili kuihadaa dunia kuwa ameingiwa na utashi wa kisiasa wa kutaka kumaliza tofauti zake na Serikali ya Uganda kwa njia ya mazungumzao ya amani.

Tangu mwaka 2005 Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC imekuwa ikimsaka kiongozi huo kwa udi na uvumba ili aweze kusimamishwa kizimbani kujibu mashtaka yanayomkabili ya uhalifu wa kivita.

Marekani iliahidi kutoa zawadi ya dola milioni 3.3 kwa mtu yeyote mwenye taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa kiongozi huo ambaye amekuwa mafichoni kwa muda mrefu.

Kony mwenye umri wa miaka 51 alianzisha kundi la waasi la LRA, Kaskazini mwa Uganda, zaidi ya miaka 20 iliyopita, na waasi wake wanasifika kwa kuwateka nyara watoto kisha kuwapatia mafunzo ya kijeshi na kuwaingiza katika kundi la wapiganaji na wengine hutekwa na kubakwa, kunajisiwa na kufanywa watumwa wa ngono.

Waasi wa LRA walilazimika kutoroka Uganda mwaka 2005 na tangu hapo wamekuwa wakifanya vurugu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Inadaiwa kuwa mwaka 2008 Joseph Kony alifikia hatua ya kusaini mkataba wa Amani kwa sharti kuwa Mahakama ya ICC itupilie mbali kibali cha kumkamata. Hata hivyo Mahakama hiyo haikukubaliana na sharti hilo jambo lililosababisha Kony kukimbilia mafichoni na kuendeleza vita.

Mwaka 2001 Serikali ya Marekani ilituma wanajeshi wake nchini Uganda kusaidia katika shughuli za kuwasaka wapiganaji wa LRA, ili kukomesha ukatili unaofanywa na kikundi hicho dhidi ya raia wasiokuwa na hatia. Kikosi hicho cha Marekani kimekuwa kikisaidia majeshi ya Uganda na nchi jirani kumsaka Kony kwa kutumia vyombo vya teknolojia ya kisasa kwa lengo la kumkamata au kumuuwa ili kusambaratisha kundi lake.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya mambo katika eneo la katikati mwa Afrika, kundi la waasi la LRA limewaua takribani watu laki moja katika kipindi cha miaka 25 iliyopita. Kundi hilo la waasi pia linatuhumiwa kuwateka nyara watu 60,000 wakiwemo watoto 100 na kusababisha watu milioni mbili kuwa wakimbizi. Kundi la LRA ambalo linatajwa kuwa moja ya makundi yenye kutumia mabavu zaidi barani Afrika na linakuwa likitumia mapanga na mashoka kuua watu wasiokuwa na hatia.

Pia waasi wa LRA nchini Uganda wamekuwa wakijihusisha na uwindaji haramu wa tembo na kutumia fedha wanazopata kutokana na mauzo ya pembe za ndovu kufadhili machafuko katika nchi za Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Ingawa vikundi vingi vinavyojihusisha na ukosefu wa amani kama Al-Shabaab, Boko Haram na Al Qaida vinatokana na makundi ya Waislamu wenye msimamo mkali, kundi la NRA linatokana na kikundi cha dini ya Kikristo chenye msimamo mkali yenye makao yake makuu nchini Uganda. Kundi la NRA lilianzishwa mwaka 1998 huko Kaskazini mwa Uganda kwa shabaha ya kuasisi utawala uliosimama juu ya amri kumi za Biblia.

Mwaka 2005 kundi hilo lilijizatiti na kupanua wigo wa harakati zake Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na katika eneo la Maziwa Makuu ambapo hivi sasa limepenyeza harakati zake hadi Sudan Kusini.

Kama ilivyo kwa makundi mengine yaliyoanzishwa kwa mwavuli wa Imani ya kidini, kundi hilo la LRA lilibadilisha mwelekeo na kujihusisha na vitendo vya uhalifu, uvunjifu wa amani na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, mambo ambayo ni kinyume na maadili ya dini ya Kristo.

Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 1991 kundi hilo lilikuwa na wanachama 10,000 Kaskazini mwa Uganda ambapo miaka mitatu iliyopita, idadi hiyo ilipungua na kufikia kati ya wapiganaji kati ya 300 hadi 400.

Taarifa za hivi karibuni zinaonesha kuwa kundi hilo linapungua nguvu kadiri siku zinavyosonga mbele. Joseph Kony ambaye anaonekana mtu mwenye kupenda madaraka na utawala usiozingatia sheria anadaiwa kuwa na familia kubwa na watoto wengi.

Kwa mujibu wa kumbukumbu na rekodi za kiongozi huyo wa waasi, hadi kufikia mwaka 2006 alikuwa na watoto 24 na kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2007 alikuwa na wake 88. Joseph Kony ambaye awali alionekana kijana mwenye ushawishi mkubwa katika masuala ya dini hadi kufikia hatua ya kujiita msemaji wa Mungu.

Katika mahubiri yake alikuwa akidai kuwa alikuwa na uwezo wa kuzungumza na Mungu na kwamba kuna wakati alikuwa anatembelewa na malaika ambao walimpa ujumbe na kumjaza roho mtakatifu.

Hata hivyo haikuchukua muda mrefu alibadilika na kuonesha makucha tabia yake kwa kuhubiri na kupenda kujihusisha na uhalifu , tabia ambayo ilijitokeza tangu alipokuwa mtoto licha ya kulelewa katika familia bora ya inayomcha Mungu.

Kony alizaliwa mwaka 1961 katika eneo la Odek katika kijiji cha Gulu Kaskazini mwa Uganda. Wazazi wate wote wawili ni wakulima wa kabila la Acholi. Inadaiwa kuwa walimlea katika maadili mema.

Hata hivyo Kony hakufuata maadili na mafunzo ya wazazi wake kwa kuwa alionesha tabia ya ukorofi angali na umri mdogo na alipenda kupigana na ndugu zake mara kwa mara.

Makala haya yameandaliwa na KAANAELI KAALE kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari.

foto
Mwandishi: kanaeli kaale

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi