loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kukithiri kwa ngono vyuo vikuu nani ataliponya taifa?

Kwa kutambua umuhimu wa elimu ya ngazi hii Serikali ya Tanzania na zinginezo duniani zimekuwa na utaratibu wa kugharimia elimu hii kwa njia mbalimbali ikiwemo kuwakopesha wanafunzi fedha za kujikimu, kununulia vifaa vya kitaluma, fedha za ada na hata fedha za mafunzo kwa vitendo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata taaluma husika bila vikwazo.

Serikali za nchi mbalimbali ni vyema kuwasomesha wanafunzi hata kama ni kwa njia ya kuwakopesha fedha ili warejeshe fedha hizo kipindi watakapoajiriwa au kujiajiri kutokana na unyeti na umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande mwingine wapo wazazi, ndugu na jamaa ambao kijana wao hukosa mkopo hujitahidi sana kuhakikisha wanamsaidia kijana wao kwa kadri inavyowezekana kwa matumaini kuwa yupo katika hatua za mwisho katika elimu yake na punde si punde matunda ya elimu ambayo ameipata yataanza kuonekana na kumnufaisha mwanafunzi, wazazi na jamii inayomzunguka.

Hapa jukumu kubwa hubaki kwa mwanafunzi husika kuhakikisha anatimiza matarajio ya serikali, wazazi na jamii inayomzunguka. Namna ya kutimiza matarajio hayo si nyingine bali ni kusoma kwa bidii na utii.

Suala la msingi huwa ni kuhitimu, yanayofuata kuhusu ajira ama kujiajiri ni mengine. Mbali na mwanafunzi kuhitimu chuo kitaaluma, jamii pia humtazamia mhitimu huyu kuwa mwadilifu pia akifanya matendo yanayokubalika na jamii.

Matarajio haya yote ya wanafunzi, serikali, wazazi na hata jamii yapo mashakani kwa sasa kwani utandawazi na mmomonyoko wa maadili vinatupeleka mahala pasipo salama hata.

Taasisi zetu za elimu ya juu zinaguswa pia utandawazi ambapo wanachuo ambao jamii kimsingi inawaona ni watu wazima wenye kuweza kufanya maamuzi salama hujiingiza katika matendo ya kushitua, kushangaza na hata kufadhaisha na kubwa ni kukithiri wa vitendo vya ngono.

Mbaya zaidi sio ngono tu bali mara nyingi kinachofanyika vyuoni ni ngono zisizo salama na picha za utupu. Ukweli juu ya kukithiri kwa vitendo vya ngono zisizo salama katika vyuo vyetu vikuu hapa nchini unafahamika kwa uongozi wa vyuo vyetu, wanafunzi, serikali za wanafunzi na hata Serikai Kuu lakini umekuwa ukifichwa fichwa, hausemwi na hata ukisemwa ni kwa chinichini.

Ukweli huu unafichwa bila kujali athari ambazo zinalinyemelea taifa letu katika siku za usoni kutokana na jambo hili kutosemwa kwa maana ya kukemewa kwa kinywa kipana na watu wote wapenda maendeleo na maadili.

Ukweli ni kwamba vitendo vya ngono zisizo salama katika vyuo vyetu vikuu hapa nchini vimeshamiri sana, vitendo hivi ni baina ya wanafunzi kwa wanafunzi, wanafunzi na wapenzi wao wasio wanafunzi na vitendo vya kusikitisha zaidi vya baadhi ya wanafunzi kujihusisha na biashara ya ngono ndani na nje ya vyuo vyao kama njia ya kujiingizia kipato.

Si vitendo hivi tu bali pia wanafunzi wetu wa vyuo vikuu hapa nchini wameingiwa na tabia mpya zisizo na maadili ikiwemo kupiga picha chafu za ngono au za kuchochea vitendo vya ngono na kisha kuziweka katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama facebook, twitter, instagram, watsapp, blogs na mingineyo huku lengo hasa la kufanya hivyo likiwa halifahamiki.

Ni kawaida sana siku hizi kukutana na picha za wanafunzi wa vyuo vikuu za ngono au zinazochochea vitendo vya ngono katika mitandao hiyo ya kijamii wakiwa wameziweka wenyewe au katika blogu mbalimbali zikiwa zimewekwa na waandishi wa blogu hizo kwa maelezo kuwa zimenaswa na wapigapicha wao au wamezipata katika kurasa za mitandao ya kijamii inayomilikiwa na wanafunzi husika.

Vitendo hivi vilipoanza kushamiri ilionekana kama ni uzushi tu dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu lakini wa sasa ni dhahiri na wazi kuwa wapo wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini, hususan jijini Dar es Salaam, wanaofanya biashara ya ngono hasa nyakati za usiku.

Lakini hata wale ambao hawafanyi biashara hii wamekuwa wakijihusisha na ngono zembe, zisizo salama na vitendo visivyo na maadili kama vile kupiga picha za utupu.

Wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wamekuwa wakifanya biashara ya ngono wamekuwa wakijitetea kuwa wanafanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha ikiwa ni pamoja na wale ambao hawakubahatika kupata fedha ya mkopo lakini ukweli ni kwamba ni suala la kuendekeza njaa.

Mbona kwa upande wa wavulana wanamudu kuishi kimkanda mkanda kwa nini wasichana washindwe? Lakini pia wale ambao wamekuwa wakipiga picha za utupu, hususan wasichana wamekuwa wakitetewa ama kujitetea kuwa huo ni uhuru na masuala yao binafsi na eti hawatakiwi kuingiliwa wala kuhojiwa na mtu yeyote.

Lakini wanasahau kwamba hata sheria zetu zinataka kuangalia picha za utupu, jambo ambalo mbali ya kutokuwa na maadili ya Watanzania, ni dhambi kwa mujibu wa dini zetu.

Uongozi wa vyuo vikuu vyetu pamoja na serikali za wanafunzi katika vyuo husika licha ya kuwa na taarifa juu ya kushamiri kwa vitendo hivi vya aibu na fedheha wamekuwa wakipata kigugumizi kukemea na hata kutunga sheria kali za kudhibiti vitendo hivi kwa kisingizio kuwa “wanafunzi wa vyuo vikuu ni watu wazima na wana uwezo wa kutambua suala baya na jema’’.

Ni ukweli usiopingika kuwa asilimia kubwa (karibu asilimia 98) ya wanafunzi wa vyuo vikuu vyetu hapa nchini wamefikisha na kuvuka umri wa miaka kumi na nane na hivyo tunaweza kuwaita watu wazima wanaojua baya na jema lakini kwa sasa ni lazima tuchukue hatua na kujiuliza kama ni kweli tabia za mtu mzima hazitakiwi kudhibitiwa pale zinapokuwa kinyume na maadili ya jamii inayomzunguka?

Kama uongozi wa vyuo vyetu usipoliona suala hili kuwa ni tatizo na kuliwekea mikakati ya kulitatua ni nani atafanya hvyo? Na kama atakosekana wa kuchukua hatua dhidi ya suala hili, jamii yetu itarajie wasomi wa aina gani miaka michache ijayo? Ni kweli kwa wasomi wa aina hii lengo hasa la elimu ambalo ni kuwaondoa maadui ujinga, maradhi na umasikini litafanikiwa?

Je, msomi anayepiga picha za utupu akidai ni halali kwake anaweza kuchangia nini katika jamii, mintarafu suala zima la maadili.

Mwaka 2012 zilisambazwa picha/video za ngono mitandaoni zikiwaonesha wanafunzi wawili wa chuo kikuu cha CBE, Dodoma wakifanya ngono. Katika video ile wanafunzi wale wanaonekana wakijirekodi wenyewe kwa kutumia laptop (kompyuta mpakato) yao.

Ni video iliyosikitisha na kushangaza wengi kwani hamna aliyeamini kama wanafunzi wenye akili timamu tena wa chuo kikuu wanaweza kufanya ngono na kujirekodi kisha mmojawapo kuzisambaza. Kiukweli wasomi hawa wa kisasa wanashangaza sana, hivi hawajui kuwa watakuwa watu wazima, watazaa watoto na watoto wao watazikuta picha zao za aibu kwani zinasambaa mitandaoni na pengine wasiwe na uwezo wa kuzifuta?

Hivi hawafahamu kuwa wazazi na ndugu zao au hata marafiki zao huumia sana pale wanapoziona picha hizi chafu za aibu? Ni ulimbukeni, kwenda na wakati au ndio usomi wenyewe?

Ni lazima sasa vijana hawa wa vyuo vikuu waache kuidhalilisha elimu ya chuo kikuu na kuonekana si lolote kwa kujirekebisha mara moja na kuachana na tabia hizi chafu, zisizopendeza na zisizokubalika katika dini zote wala katika jamii yeyote yenye maadili na inayoheshimu utu na mwili wa binadamu. Ni lazima pia vyuo vyetu vikuu viamue kulikabili tatizo hili kwa kutengeneza sheria kali zitakazowadhibiti wanafunzi wenye tabia za aina hizi na kuachana na utetezi dhaifu kuwa wanafunzi ni watu wazima wenye kuelewa jambo jema na baya hivyo hawahitaji usimamizi au uangalizi juu ya masuala binafsi. Wakati fulani miaka ya nyuma, kitu kinachoitwa mzee ama 'punch' kilikuwa kinasaidia kuwasema wanafunzi wanaopotoka kimaadili, lakini kwa bahati mbaya kilikuwa pia kinatumika hata kwa hila na fitna na kuna wakati kilisababisha hata kifo (Rejea kifo cha Levina Mukasa, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza akisomea shahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar eSalaam).

Mwisho jamii iungane kulikemea suala hili kwa nguvu zote ili kuhakikisha linakoma na kutoweka kabisa kwani tofauti na hapo jamii itakuwa ikishuhudia taifa likiangamia bila kuchukua hatua zozote na kwa hakika italaumiwa katika hili na itakosa cha kujitetea.

Tunawategemea sana wasomi wa vyuo vikuu kama nyenzo muhimu ya kupambana na adui ujinga, maradhi umasikini na ufisadi lakini lazima tuwe na wasomi waliolelewa vyema pia kimaadili na si kuiga hata mambo ya hovyo ya ughaibuni kwa kisingizio cha kwenda na wakati.

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC).

Anapatikana kupitia simu 0716719589 au wilflow101@gmail.com

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya ...

foto
Mwandishi: Charles William

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi