loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kulikoni utii huu wa abiria kwa makondakta?

Licha ya kwamba abiria anao uwezo wa kumwambia dereva moja kwa moja aliyekaa karibu naye, lakini utaratibu wa kuwasiliana na kondakta ndiyo umezoeleka. Ndiyo utii uliojengeka. Lazima itifaki izingatiwe.

Abiria huhofu kukiuka itifaki. Vinginevyo, akikutana na kondakta, dereva mbabe au katili, anaweza kupitilizwa kituo. Atapitilizwa hadi kondakta atakako tena bila kurudisha nauli.

Kama ni wewe umepitilizwa kituo, uombe uwe na fedha ya ziada! Kama huna, utajikuta ukihesabu hatua kurudi kituoni kwako huku ukilaani.

Lakini dua la kuku halimpati mwewe. Ukitaka kushuhudia utii mwingine wa abiria kwa makondakta wa daladala, subiri askari wa kikosi cha usalama barabarani akamate gari husika.

Bila kujali kama dereva/kondakta wamevunja sheria, utasikia abiria wakisaidia kwa kulalamika na kutoa shutuma kali kwa matrafiki.

Utasikia kauli za kushutumu kuwa askari wanataka fedha. Huungana na madereva kwa kuwashawishi watoe chochote kwa askari hao, safari iendelee.

Tena wakati mwingine, wapo abiria ambao huamua kununua kesi kwa kujibizana na askari wa usalama barabarani wakiwatuhumu kuwaonea makondakta na madereva.

Abiria hukubali kuaminishwa na wafanyakazi hao wa daladala kwamba kila askari anayewakamata, lengo lake ni kupokea rushwa.

Ingawa wapo baadhi ya askari wanaojihusisha na vitendo hivyo, lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba wako askari makini, wanaowajibika na kuzingatia sheria ya usafirishaji barabarani. Lakini kwa kuwa abiria wanataka kuwahishwa wanakokwenda, hata gari lao kama limekatisha njia au kuiba njia nyingine, abiria huendelea kutii mamlaka ya makondakta kwa kuona askari hawatendi haki.

Nidhamu ya abiria wa daladala hupitiliza pale ambapo wafanyakazi hao wa daladala huamua kuwaadhibu kwa njia tofauti. Mojawapo ni kuamua kuwashusha popote bila kuhojiwa.

Vitendo hivyo vimekithiri katika kipindi hiki ambacho ujenzi wa barabara ya Morogoro unaendelea chini ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart). Utashangaa kuona namna abiria wanavyokubali kuamriwa kushuka licha ya kwamba hawajafika ukomo wa safari yao. Mfano mzuri, wanaopanda mabasi yanayotumia Barabara ya Mandela kwenda Ubungo, wanafahamu hilo. Siyo ajabu kushuhudia kondakta akiamuru abiria washuke eneo la Daraja la Riverside.

Ni abiria wachache wenye ujasiri wa kudai haki ya kufikishwa wanakokwenda. Lakini hata hivyo hushindwa kufanikisha mapambano kutokana na kukosa nguvu ya pamoja na abiria wenzao. Matokeo yake, huishia kubezwa.

Mambo mengine ambayo ukiwa mtaani kwenye usafiri wa daladala ni nadra kuyakosa, ni ugomvi juu ya haki ya kupatiwa tiketi.

Makondakta huona kutoa tiketi ni suala la uamuzi. Ikitokea abiria jasiri akaamua kuhoji sababu za kutopatiwa tiketi, hapo ndipo utashuhudia majibizano ya aina yake. Bahati mbaya, baadhi ya makondakta wamejaliwa ‘midomo michafu’.

Kejeli na kebehi, apewavyo abiria mpambanaji, vinatosheleza kumnyamazisha siku zote asithubutu kufunua kinywa chake kudai haki yake kwa hofu ya kudhalilishwa mbele ya abiria wengine. Sasa kubwa lililoibuka hivi karibuni, ni la kupandisha bei ya daladala wakati wa jioni.

Licha ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kuweka viwango halali, inapofika jioni, makondakta na madereva huwaendesha abiria wanavyotaka. Kama hufahamu juu ya hili na unataka kuthibitisha, nenda kwenye vituo kama vile Posta, Ubungo na Mwenge.

Badala ya nauli ya kati ya Sh 400 na 500, abiria hulazimika kulipa kati ya Sh 1,000 na 2,000. Hata kama ukiingia kwenye daladala husika ukaamua ‘kulianzisha’ kwa kulazimisha kulipa nauli halali, lazima utashindwa maana abiria wenzako watasaidiana na kondakta kukuzodoa mpaka utatamani dunia ikumeze.

Katika kushinikiza ama ulipe nauli wanayotaka au ushuke, dereva atagoma kuondoa gari. Hapo utasikia abiria wanaojifanya wana fedha ya kutosha, wakitamba kukulipia kiasi cha fedha unachodaiwa.

Lakini wengine utasikia wakibeza, ‘kwani hukusikia konda akitangaza bei?’ Swali la kujiuliza ni, je, kwa nini abiria hawa wakubali kugeuzwa watumwa wa daladala?

Ni kwa nini abiria wote wageuzwe mbumbumbu wa sheria na kanuni za usafirishaji? Ni kwa nini abiria wawe na utii kiasi hicho? Hapa kinachokosekana ni umoja wa abiria kukabili unyanyasaji wa makondakta na madereva wa daladala.

Umefika wakati, abiria, Sumatra, Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, wawe kitu kimoja katika kumaliza kero katika usafiri huo wa umma.

Ushirikiano ndiyo utawatia adabu makondakta na madereva wanaotumia kero ya usafiri jijini Dar es Salaam kujigeuza miungu watu. Utii huu wa abiria kwa makondakta si wa hiari, bali unalazimishwa na hali halisi ya usafiri wa umma katika Jiji hili la Dar es Salaam.

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Riadha ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi