loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kunahitajika mikakati wasomi waweze kujiajiri

Hawa ni vijana wa kike na kiume wenye umri kati ya miaka 22 na 30 ambao pia walichujwa tayari kutoka idadi kubwa ya waombaji kazi ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji 20,000 walituma maombi na kuwa na sifa za kuwania nafasi hiyo.

Kama alivyothibitisha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani , Isack Nantanga, nasi tunaungana naye kwamba hii ni idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea kwa waombaji wengi kiasi hicho kuwania nafasi za ajira kiasi kidogo kilichotangazwa.

Kwa upande mmoja, tuna haki ya kujivunia kwamba mipango yetu ya elimu ya juu inaelekea pazuri kwani kinyume chake tusingekuwa na mkusanyiko wa wahitimu wa shahada ya kwanza kiasi kama hicho kama mikakati ya kupanua elimu ya juu isingezingatiwa ipasavyo na Serikali na wadau wengine wa elimu. Lakini pia kila penye mafanikio hapakosi changamoto.

Juhudi zetu za kujipanua katika elimu ya juu ndiyo pia inayotuletea sasa changamoto ya ukosefu mkubwa wa ajira. Kwa maneno mengine kadiri tunavyozidisha kuzalisha wasomi wengi ndivyo ongezeko la ukosefu wa ajira nalo linavyozidi kupanuka.

Swali kubwa la kujiuliza hapa ni kwamba je; ipo mikakati ya kuweza kukabiliana na tatizo hilo la ukosefu wa ajira ambalo lipo siyo Tanzania tu bali ulimwenguni kote?

Tunapenda kuunga mkono kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya kwa wahitimu wa vyuo vikuu kwamba kutegemea kuajiriwa badala ya kutafuta mbinu ya kuweza kujiajiri wenyewe hakutoshi.

Waziri huyo alitoa changamoto hiyo kwenye mahafali ya wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali vya Mkoa wa Dodoma ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni wazi kwamba hakuna nchi duniani inayoweza kutoa ajira rasmi kwa wasomi wake wote kwa sababu ajira zenyewe nazo ni chache. Lakini hii haina maana kwamba vijana wetu wasiendelee kusoma bali kusoma na kujipatia elimu ni muhimu kama ambavyo tumekuwa tukisema wakati wote kwamba elimu ni ufunguo wa maisha.

Kwa vijana wetu wasomi wakiwemo hao wanaosaka kwa udi na ubani nafasi hizo 70, tunawashauri watambue kwamba uhaba wa ajira unaweza kupungua tu iwapo kila mmoja wao atajitahidi kubuni na kusaka fursa mbalimbali za kujiajiri ama kwa kutumia taaluma aliyosomea au mbinu nyingine ya kujipatia kipato.

Moja ya mbinu ni kwa kuanzisha miradi midogomidogo ya kujikimu au pia kujiunga katika makundi ya ushirika ili kutafuta mikopo ya kuwawezesha kuanzisha miradi ya pamoja.

Hilo linawezekana iwapo wadau wote ikiwemo Serikali, wahitimu, wazazi na wananchi kwa ujumla tukishikamana kwa kila mmoja wetu kwa nafasi yake, ili kulikabili tatizo hili la kitaifa.

WIKI hii kumekuwa na taarifa za Yanga kutakiwa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi