loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kuoga, kufua kwa baadhi ya wananchi Dodoma ni anasa

Kuoga, kufua kwa baadhi ya wananchi Dodoma ni anasa

Miongoni mwa miradi aliyoitembelea ni ule wa Kijiji cha Ng’ong’onha, Ntytuka na Mkonze katika Manispaa ya Dodoma.

Licha ya mradi wa maji wa Ng’ong’onha kuchelewa wananchi nao walionesha kukerwa kwao hali iliyolazimu kumzunguka, Naibu Waziri kusikia iwapo atakuwa na maneno yoyote ya matumaini huku wengine wakidai kwa kuoga au kufua kwao ni kama anasa.

Kijiji hicho chenye wakazi 13,000 kina visima viwili tu vya maji ambavyo havitoshelezi mahitaji hali inayosababisha wanawake kushinda kwenye makorongo kutafuta maji lakini hali huwa mbaya zaidi wakati wa kiangazi ambapo maji hupatikana kwa tabu sana kutokana na makorongo mengi kukauka.

Wako hatarini kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali kutokana na ukosefu wa maji salama, hali inayopelekea kuishi muda mrefu bila kuoga na kufua nguo.

Magdalena Mazengo anasema pamoja na kuwepo karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambacho kipo eneo la kijiji hicho, hajawahi kunywa maji ya bomba bali miaka yote wamekuwa wakitumia maji wanayochota kwenye makorongo.

“Ni vema wakazi tunaoishi jirani na UDOM tukafikiriwa kupata maji,” anasema Peter Kushoka ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho.

Mwenyekiti huyo anasema kwa kipindi kirefu hawana maji salama badala yake wamekuwa wakichota maji kwenye makorongo ambayo hata hivyo upatikanaji wake umekuwa wa tabu kwa vile yanatumika kwa kunyweshea mifugo mbalimbali.

Pamoja na kijiji hicho kuwa ndani ya Manispaa ya Dodoma wakazi hao wamekuwa wakitumia muda mrefu kuyasubiri maji hayo hali ambayo imekuwa ikisimamisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Pia kutokana na hayo, wakazi walio wengi wamekuwa wakiishi zaidi ya wiki moja bila kuoga na kufua, suala ambalo limekuwa likitishia kuibuka kwa maambukizi ya magonjwa mbalimbali kila wakati.

“Wengi wanaona ni afadhali kupata maji hayo kwa matumizi ya kunywa tu na siyo kwa kuoga na kufulia nguo zao na wakiona kuna umuhimu zaidi wanaishia kunawa uso tu”.

Kwa upande wake, Sospeter Maregani anasema wamekuwa wakipata tabu kutokana na kununua ndoo moja ya maji kati ya Sh 300 hadi Sh 700. Maji wanayonunua hawajui yanatoka wapi na hata usalama wa watumiaji umekuwa mashakani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Robert Kitimbo, mradi wa maji wa Ng’ong’onha mkataba wake ulikuwa na miezi minne na ulisainiwa Septemba 24 mwaka jana na ulitarajiwa kukamilika Machi 3, mwaka huu.

Kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa tangi la ujazo wa lita 90,000, ujenzi wa nyumba mbili za pampu za jenereta, uchimbaji wa mitaro, kulaza bomba na kufukia mita 18,220, ujenzi wa vituo 20 vya kuchotea maji na mifumo ya uvunaji wa maji ya mvua katika taasisi za Serikali.

Mkurugenzi huyo anasema ujenzi wa tangi umefikia hatua ya kuweka plasta ya nje na ndani, uunganishaji wa mabomba za kuingiza na kutolea maji.

Anazitaja changamoto zilizojitokeza katika utekelezji wa ujenzi wa mradi wa maji ya Ng’ong’onha ni kubainika kuwepo kwa mapungufu ya usanifu wa awali na hivyo kulazimu kufanyika usanifu wa mara ya pili.

Kitimbo anasema mkandarasi huyo ameshindwa kukamilisha kazi kwa wakati na mpaka ifikapo Desemba 28 mwaka huu, anatakiwa kukabidhi mradi huo na akishindwa atafukuzwa na kisha kupelekwa mahakamani.

Anapohojiwa kwa nini ameshindwa kumaliza mradi huo kwa wakati, Meneja Mradi wa Kampuni ya Dabengo Enterprises inayotekeleza mradi huo, Emmanuel Wambura, anasema alikuwa akisubiri fedha kutoka Manispaa ndipo aendelee na kazi ya kuchimba mitaro iliyobaki na kuweka mabomba.

Lakini baada ya Manispaa ya Dodoma kuahidi kumlipa Sh milioni 51 atahakikisha anakamilisha mradi huo Desemba 28 mwaka huu kama alivyoamriwa. Hata hivyo, Naibu Waziri anasema iwapo mradi huo hautakamilika Desemba 28, mwaka huu, mkandarasi huyo ataondolewa kwenye orodha ya ujenzi wa miradi ya maji nchini.

Anasema serikali imekuwa ikitoa fedha kwenye miradi ya maji lakini miradi mingi imekuwa haikamiliki kwa wakati na kufanya wananchi kuhangaika jambo ambalo halitavumiliwa tena.

Anamtaka Mkurugenzi wa manispaa kuacha kukaa ofisini na badala yake atembee na kuona miradi imefikia hatua gani kwani kupata tu taarifa za makaratasi haitoshi.

Mradi mwingine wa maji aliotembelea katika manispaa ya Dodoma ni ule wa Kijiji cha Ntyuka. Mradi huo mkataba wake ni wa miezi minne na ulisainiwa Mei 13, mwaka huu na ulitarajia kukamilika Oktoba 11, mwaka huu.

Kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa tangi la ujazo wa lita 90,000, ujenzi wa nyumba moja ya jenereta, uchimbaji wa mitaro, kulaza mabomba na kufukia mita 10,450, ujenzi wa vituo 20 vya kuchotea maji na ujenzi wa mifumo ya uvunaji maji ya mvua katika taasisi za Serikali.

Aidha mkandarasi wa mradi wa Ntyuka ni kampuni hiyo ya Dabenco.

Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa kampuni hiyo, Wambura mradi huo ulianza kutekelezwa Mei mwaka huu mpaka sasa kilichofanyika ni kuchimbwa kwa msingi wa tangi la kuhifadhia maji na mradi huo unasuasua kutokana na fedha kutopatikana kwa wakati.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa Dodoma anasema mkandarasi huyo alipewa fedha za kianzio Sh milioni 50 lakini hata alipopeleka cheti kazi ya Sh milioni 50 iliyofanyika haikuonekana. Waziri Mahenge anasema maagizo ya Serikali kulipa fedha pale ambapo kazi inaonekana.

“Ninachokiona hapa ni ufuatiliaji dhaifu kwa upande wa manispaa kwani Sh milioni 50 zimetumika na hakuna kilichofanyika na mtu anadai fedha nyingine,” anasema. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Manispaa, Kitimbo, mradi wa Ng’ongonha utagharimu kiasi cha Sh milioni 488.3 utakapokamilika na mradi wa Ntyuka utagharimu jumla ya Sh milioni 387.4 huku ule wa Mkonze umegharimu jumla ya Sh milioni 497, 263.

Kitimbo anasema licha ya kusuasua kwa miradi hiyo lakini miradi mingine miwili ya Mkonze na Chididimo imekamilika na wananchi wanapata maji.

Aidha katika mradi wa Mkonze hali inaonekana kuwa tofauti kwani tayari wananchi 11,000 wameanza kupata maji chini ya mradi unaotekelezwa na fedha kutoka Benki ya Dunia. Mwenyekiti wa kamati ya maji katika kijiji hicho, Benedicto Mgimwa anasema mradi wa Mkonze una vituo 18 vya kusambazia maji ambapo kisima kilichopo kina uwezo wa kutoa lita 16,000 kwa saa.

Anasema mradi huo ni katika ya miradi 10 inyotekelezwa na Benki ya dunia. Kulingana na Mwenyekiti huyo ndoo moja ya maji imekuwa ikiuzwa kwa Sh 100 na fedha zinazopatikana zimekuwa zikitumika kununua mafuta kwa ajili ya kuendeshea jenereta la kusukuma maji.

Anasema kiasi cha Sh milioni nne kimekuwa kikikusanywa kwa mwezi na mpaka sasa wana kiasi cha Sh milioni 17 benki. Naibu Waziri anasema kuanzia sasa atakayepewa kazi ya ya ujenzi wa mradi wa maji ni yule atakayetafuta chanzo.

“Zamani ilikuwa anayetafuta chanzo mwingine na anayepewa kazi ya ujenzi wa mradi mwingine sasa hatutaki tena hilo fedha nyingi zimekuwa zikitumika bila kuwa na sababu,” anasema pia kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 10 imeongezeka baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kutangaza kuondolewa kwa vibali mbalimbali (‘no objection’’) katika hatua za manunuzi.

Anasema kuondolewa kwa vibali hivyo kwa kiasi kikubwa kumepunguza urasimu unaosababishwa na taratibu za manunuzi, lakini urasimu unaosababishwa na tabia za watendaji bado unaendelea katika mamlaka za Serikali za mitaa.

“Katika mkoa wa Dodoma, hakuna Halmashauri ambayo imetimiza lengo tuliyojiwekea la kufikisha vijiji vitano ifikapo Septemba 2013. Lakini pia, zipo Halmashauri ambazo hazina nia ya dhati ya kukamilisha vijiji vyote ifikapo mwezi Juni 2014.“

Anataka watendaji kukumbuka ahadi waliyojiwekea kwenye mikataba ya 'Big result now' kwa kila moja kutimiza ahadi yake ili kwenda sambamba na kasi ya 'Tekeleza sasa kwa matokeo makubwa' yaani 'Big result now'.

Anasema pamoja na kushindwa kufikia lengo hilo, Halmashauri nyingi hazijakamilisha mradi hata mmoja.

Aidha, ipo miradi ambayo imeanza kufanyiwa majaribio na wananchi wameanza kupata huduma ya maji. Naibu Waziri anasema Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ilifanya uamuzi wa kuhakiki eneo la kuchimba kisima kwa kutumia ofisi za Bonde kabla ya kuanza kuchimba. Kati ya visima 10 walivyochimba, visima tisa vimepata maji ya kutosha.

Kisima kimoja kilichokosa maji kilikuwa cha kwanza katika uchimbaji ambapo hakikufanyiwa uhakiki. Anabainisha kuwa, usimamizi wa huduma ya maji katika Manispaa ya Dodoma unaridhisha.

Anaitaka manispaa ya Dodoma kukagua Miradi ya maji katika vijiji vya Mkonze, Ng’ong’onha na Ntyuka kutokana na kubaini mapungufu mbalimbali na halmashauri ihakikishe inasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maji.

Aidha anaitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kujitanua kwenye kijiji cha jirani cha Ng’ong’onha ambapo kina wakazi wengi wanaoweza kuhudumiwa na miradi ya maji inayotekelezwa UDOM.

Anasema ni muhimu kuangalia suala hilo ili wananchi wa Ng’ong’onha waweze kupata maji hali ambayo pia itaongeza mapato kwa mamlaka kutokana na kijiji hicho kuwa karibu na huo Kikuu cha Dodoma ambacho kina huduma nzuri ya maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Injinia Peter Mokiwa anasema mamlaka hiyo itaangalia namna ya kushughulikia suala la kukipatia maji kijiji cha Ng’ong’onha.

Pamoja na hayo, mhandisi wa maji Mkoa wa Dodoma, Bazil Mwiserya anasema utekelezaji wa miradi ya maji katika mkoa wa Dodoma unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uwezo mdogo wa makandarasi kifedha na rasilimali watu wakati wakitekeleza miradi hiyo. Anasema pindi wanapotangaza zabuni wanapata wakandarasi wenye vigezo lakini baadaye mambo yanakuwa tofauti. “Sisi tunapotaka vigezo wanaonekana kukidhi lakini ukimpa kazi hamalizi kwa wakati kama mlivyokubaliana,” anasema. Hata hivyo anabainisha kuwa mpaka sasa hakuna mkandarasi aliyechukuliwa hatua ya kisheria lakini wamekuwa wakiandikiwa barua za onyo watunze mkataba yao. Anasema katika miradi ya BRN wanachukua hatua za kusukumana mpaka wamalize kazi kwani wakati mwingine kuvunja mkataba kumekuwa kukisababishia Serikali hasara kubwa.

“Pia wataalamu washauri wa makampuni binafsi hawatoi ushirikiano wa kutosha katika miradi inayotekelezwa hali ambayo pia inachangia kuchelewa kwa miradi mingi,” anasema.

Akitoa mfano anasema kuna mradi wa maji Kijiji cha Mvumi Makulu Wilaya ya Chamwino, mkandarasi alisimama kazi kwa kusubiri maelekezo kutoka kwa mtaalamu mshauri ili aendelee na kazi wakati ambapo mtaalamu mshauri alikuwa Jijini Dar es Salaam.

Anasema mambo kama hayo yamekuwa yakikwamisha kukamilika kwa wakati utekelezaji wa miradi ya maji kutokana na ukweli kuwa mtaalamu mshauri anatakiwa kuwa kwenye eneo la mradi kutoa maelekezo mpaka utakapokamilika lakini anapokuwa hayupo inakuwa ni vigumu kwa mkandarasi kuendelea na kazi.

“Mkandarasi kwa kiasi kikubwa anategemea mtaalamu mshauri katika kutimiza majukumu yake,” anasema.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi