loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kupamba na mti wa Krismasi kulianzaje?

Kupamba na mti wa Krismasi kulianzaje?

Kabla ya Wakristo kuazimisha sikukuu hii kwa kupamba na mti wa Krismasi, miti na mimea katika kipindi hiki cha Desemba ambacho kwa kawaida ni majira ya baridi ilikuwa na maana kwa wakazi wa maeneo yenye baridi na barafu.

Kama vile watu wapambavyo hivi leo nyumba na makazi yao kwa mti wa Msonobari, vilevile watu walioishi kabla ya Kristo walining’iniza matawi ya kijani ya mti wa Msonobari kwenye madirisha na milango ya nyumba zao kwa imani kuwa kufanya hivyo kipindi hicho kunafukuza pepo wabaya, wachawi na magonjwa.

Katika pembe ya Kaskazini ya dunia, siku fupi na usiku mrefu unaangukia Desemba 21 au Desemba 22, na kipindi hicho huitwa Solistasi kipindi ambacho Jua linakuwa Kaskazini ambapo ni Kusini kabisa na Ikweta. Watu wengi enzi hizi waliamini kwamba Jua lilikuwa Mungu na kwamba kipindi hicho cha baridi kila mwaka kilikuja kwa sababu Mungu wao Jua alikuwa anaugua na kuwa dhaifu.

Hivyo, kusherehekea kwao Solistasi kulimaanisha Mungu wao ameanza kupata ahueni na mimea kuwa kijani yaani kustawi pamoja na matawi ya Msonobari ni ishara kuwa ihai umerudi tena kwa kuwa Mungu wao Jua amepona na majira ya joto yanarejea. Watu wa kale wa Misri waliabudu mungu aliyeitwa Ra, ambaye alikuwa na kichwa cha mwewe kilichovikwa taji linalometameta kama jua, na waliamini kuwa kipindi cha Solistasi mungu wao Ra alianza kupona.

Sababu hiyo, iliwapasa wao kusherehekea kwa kupamba nyumba zao na majani ya kijani ya mitende au michikichi wakiashiria alama ya ushindi wa maisha kutoka kifo. Pia enzi hizo kwa Warumi, kipindi cha Solistasi kilikuwa na maana ya sikukuu iitwayo Saturnalia yenye kumtukuza mungu wa kilimo.Warumi walijua kwamba kipindi hicho, mashamba yatabadilika na kuwa kijani na hivyo vyakula na matunda vitakuwa vingi.

Ili kuisherehekea sikukuu hiyo walipamba nyumba zao kwa majani ya kijani ya miti. Huko Kaskazini mwa Bara ya Ulaya kipindi cha Desemba wao walikuwa na utamaduni wa kupamba nyumba zao kwa matawi ya mti ya kijani wakimaanisha alama ya uzima wa milele, na walipamba hekalu lao ambalo walikuwa wakimtukuzia mungu wao wa kale aliyekuwa kipindi cha ancient Celts.

Ujerumani nao enzi hizo walianza kupamba mti wa Krismasi kwa kufuata utamaduni wao ambapo katika karne ya 16, Wakristo wenye kumcha Mungu walianza kupamba nyumba zao kwa mti ya misonobari na michikichi.

Wapo waliojenga mapiramidi ya mbao na kuyapamba na matawi ya miti ya kijani, na waliamini kwamba Martin Luther katika kipindi hicho alikuwa na kazi ya kufanya matengenezo ya Wakristo wenye imani ya Kiprotestanti ambapo alianza kwa kuongeza mshumaa unaowaka kwenye mti wa msonobari uliokuwa umepambwa.

Katika kipindi hicho cha majira ya baridi, nyakati za jioni, Luther alitembea kwenye nyumba yake akihubiri na alipofika sehemu iliyokuwa imepambwa na mti wenye taa zinazowaka aliuheshimu na kwa kuamua kuuchukua na kuuingiza sebuleni ambapo aliuviringishia taa zinazowaka pamoja na mishumaa ambapo ulizidi kupendeza.

Hata hivyo katika karne ya 19, Wakristo wa Marekani waliona miti ipambwayo Krismasi ni kitu kigeni kwao na tena ni kama kioja, ambapo kwa mara ya kwanza kuonekana kwa mti huo umepambwa nchini huko kulitokea mwaka 1830, baada ya mlowezi wa Kijerumani kupamba kwenye nyumba yake.

Walowezi wa Pennslavia ya Ujerumani walikuwa na tabia ya kupamba nyumba zao na miti hiyo tangu miaka ya 1717, na kuwa mwaka 1830 mti wa Krismasi ulionekana ni alama ya wapagani na Wamarekani wengi hawakuikubali kwa kuwa wao walikuwa na imani za dini.

Hata hivyo kama yalivyo mataifa mengine, utaratibu wa kupamba majira hayo ya baridi na mti wa Krismasi ulianza kuenea kwenye mataifa mbalimbali ambapo Marekani nao wakaanza kupamba kwa kutumia mti huo, ingawa awali waliona ni kitu cha ajabu tena ni upagani .

Kwa upande wao Waingereza Watakatifu, Krismasi kwao ilikuwa ni siku takatifu ambayo walipamba nyumba zao na miti hiyo na Gavana wa Pili aliyekuwa Hujaji, William Bradford, aliandika kwamba kipindi hicho alijaribu kukomesha dhihaka za wapagani waliofanya mambo yasiyo na maana kuhusu siku hiyo ya Krismasi.

Ilipofika mwaka 1959, Mahakama Kuu kwenye mji wa Massachusetts nchini Marekani ilipitisha sheria ya kuitambua rasmi siku ya Desemba 25, mbali na kanisa wanavyoitambua, na mtu aliyefanya fujo siku aliadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Ilipofika karne ya 19, wahamiaji wa Ujerumani na Ireland walianza kufurika kwa wingi Marekani na kudhoofisha urithi wa utakaso wa kuheshimu siku hiyo.

Mwaka 1846, Malkia Victoria na mumewe Mfalme wa Ujerumani Albert walichorwa katika picha inayoonesha wamesimama huku wamezungukwa na watoto wao kwenye mti wa Krismasi.

Kwenye miaka ya 1890, mapambo ya Krismasi yalianza kuingia Ujerumani na miti ya Krismasi ilishamiri kila pande nchini Marekani, ambapo watu wa bara la Ulaya walitumia miti midogo ya Krismasi kupamba nyumba zao ambazo zilikuwa na urefu wa futi nne tuu, wakati Marekani wao walianza kupamba siku hii kwa kutumia miti mirefu iliyoanzia chini sakafuni hadi kwenye dari.

Ilipofika karne ya 20, Wamarekani walianza kupamba siku hii kwa kutumia mti huo wenye kuongezewa mapambo yaliyotengenezwa wenyewe, wakati Walowezi Kijerumani waliolowea Marekani wao waliendelea kupamba mti huo kwa kutumia halua, njugu, tufaha, na bisi ziliwekwa kwenye mti huo baada ya kukaushwa na kupakwa rangi na hivyo kuufanya uwe na mchanganyiko wa marembo.

Hivi leo utambaji wa mti huo wa Krismasi umeongezwa marembo ya taa yenye kumetameta zitumiazo umeme na kuweka kadi za salamu ya heri ya siku hii. Zawadi nyingine zilizofungwa vizuri ziliwekwa chini ya mti huo, na utamaduni wa kupamba miti ulisambaa duniani kote hata kufika barani Afrika na Tanzania ambapo kila pembe majira haya watu hupamba na mti aina ya misonobari asilia au ile ya kutengeneza.

Kwa upande wa wakazi wa jijini Dar es Salaam, maduka mengi kwenye maeneo mbalimbali, yameuza miti jamii hiyo ambapo watu kwa kusherehekea siku hii wamepamba nyumba zao kwa kutumia mti huo, ama uwe wa kutengenezwa au ule wa asili, na hivyo kufanya kila kona ya mji kumeremeta.

Pamoja na kusherehekea siku hii, pia watu au vikundi mbalimbali hususani vijana kwenye maeneo mengi nchini hasa yale ya mijini ambayo miti ya misonobari haipatikani kwa wingi kama ilivyo maeneo ya vijijini, wamekijita katika biashara ya miti ya hiyo ambapo huikata matawi yake na kuyaleta mjini kuuza kwa ajili ya watu kupamba siku ya Noel au Krismasi.

Mti wa Krismasi unapendeza unapopambwa siku hii, na shamra shamra za Noel hufanya siku kupendeza zaidi na kuwa na mvuto wa aina yake, ambapo familia hukaa pamoja na kusherehekea siku hii na kupanga mipango ya mwaka unaofuata, kwa kuwa Desemba 25, ni takribani siku sita tu zimebaki kumaliza mwaka na kuanza mwaka mwingine.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi