loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kupungua kwa ajali, si kukomesha maafa

Ukilinganisha na mwaka 2010, ambapo kulikuwa na ajali 24,665,vifo 3,582, na majeruhi 20,656, mwaka 2011 matukio hayo yamepungua zimetokea ajali 18,733, vifo 3,062 na majeruhi 16,179.

Takwimu hizo za Polisi, zinaonesha wazi kuna juhudi zimefanyika mwaka jana, ukilinganisha na miaka iliyopita ambayo kila mwaka unaingia ajali zilikuwa zikiongezeka, lakini mwaka 2011 zimepungua.

Pamoja na kupungua huko, bado ajali, watu mamia na majeruhi wametokea, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na nchi zilizoendelea au zinazodhibiti ajali. Vifo vinavyosababishwa na magari ni vingi, vinafukuzana na vifo vinavyotokana na malaria ambao ni ugonjwa unaoangamiza zaidi watoto wa chini ya miaka mitano.

Hivyo, hata kama kiwango cha ajali kimepungua mwaka 2011, hatuwezi kujivunia bado ajali za barabarani, zinaangamiza watu wengi sambamba na maradhi. Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mohamed Mpinga anaonesha wazi juhudi zimefanyika kupunguza idadi ya ajali, vifo na majeruhi mwaka jana.

Jitihada hizo za Jeshi la Polisi kuendelea kupunguza kasi ya ajali, vifo na majeruhi, zinatakiwa kuongezeka zaidi, ili kupunguza kasi ya kuua nguvu kazi na kupoteza raslimali zao. Kutokea kwa ajali hizo, vifo na majeruhi, madereva wanaendesha magari, wanaobeba abiria na mali zao.

Madereva wengi wanaendesha bila uangalifu wa kutosha kiasi cha kusababisha ajali ambazo zingeweza kuepukika. Stanslaus Kwitema wa Kimaramwisho anasema ajali nyingi zinatokea kutokana na kuendesha magari kwa mwendo kasi, bila matengenezo.

Magari hayo yanaendeshwa kwa kwenda kasi zaidi ya ule wa kilometa 80 kwa saa uliowekwa na vidhibiti mwendo. Ajali zinazotokea sababu ya kutaka kuyapita magari mengine kwenye kona au kwenye vivuko vya miguu, au kwenye misururu mirefu ya magari, zinatokana na uzembe wa madereva.

Abiria wengine wamekuwa chanzo cha ajali kutokana na mtindo wao wa kuwashawishi madereva kuendesha au kuchochea mwendo bila kuwa na uhakika wa magari yaliyo mbele yao au kutokea kwa tatizo lolote mbele yao.

Lakini pia kuna madereva ambao hawana leseni za udereva, ni ‘jua kali’ ambao wamejifunza michangani na hawajapitia katika vyuo vya ufundi kama Veta wanaendesha magari bila utaalamu na hivyo kusababisha ajali.

Kuna madereva ambao pia wanasababisha ajali kutokana na kuendesha magari wakiwa wamelewa, hivyo mara kinapotokea kipingamizi chochote mbele yao, wanashindwa kuhimili mikikimikiki hiyo ya barabarani na kusababisha ajali.

Ajali hizo za b a r a b a r a n i zimekuwa nyingi licha ya kuwapo kwa teknolojia ya kutumia vidhibiti mwendo, tofauti na siku za nyuma ambapo kulikuwa hakuna teknolojia hiyo.

Kitu cha kushangaza, Mwamidi Kideu wa Manzese anasema, ajali nyingi zinatokea licha ya kuwapo kwa Wiki ya Nenda kwa Usalama, ambayo ingetegemewa kuwa chachu ya kupunguza au kukomesha kabisa ajali hizo.

Utafiti ulifanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umebainisha kwamba asilimia 76 ya ajali za barabarani zinazohusisha mabasi ya abiria zinatokana na mambo ya kibinadamu wakati asilimia 17 ya ajali hizo zinatokana na magari yenyewe, kumbe asilimia 7 ni sababu nyingine zisizoweza kuzuilika.

Wataalamu hao wa masuala ya usafiri wamebaini kuwa asilimia 17 ya ajali, zinazotokana na magari yenyewe. Mengi ya magari hayo ni mabovu na usalama wake sio thabiti kwa lengo la kusafirisha abiria na mali zao.

Vyanzo hivyo vya utafiti vinaainisha kwamba asilimia 78 ya waathirika wa ajali za barabarani ni abiria na watu wanaotembea kwa miguu. Mfano katika takwimu za kuanzia miaka ya 2000, zinaonesha kuwa asilimia 40 ya wanaokufa kwenye ajali za barabarani ni abiria ndani ya magari hayo na zaidi ya asilimia 38 ni ya watembea kwa miguu.

Kwa ujumla wake, takwimu za ajali za barabarani zinaonesha kuwa viini vya ajali zinazosababishwa na uendeshaji wa hatari au uzembe ni zaidi ya asilimia 54. Ubovu wa magari unachangia ajali kwa zaidi ya asilimia 16, wakati uzembe wa watembea kwa miguu unachangia kwa asilimia 6.8 katika ajali zinazotokea.

Mwendo kasi unachangia kwa asilimia 3, uzembe wa wapanda pikipiki zaidi unachangia asilimia 3 na uzembe wa wapanda baiskeli kwa asilimia 6. Madereva walevi wanachangia kwa asilimia 1.2 na sababu nyingine ni pamoja na utelezi na ukungu ambavyo kwa pamoja vinasababisha asilimia 6 z a ajali barabarani.

Mwaka 2011, kwa mfano, ajali za barabarani zimetokea karibu katika kila mkoa nchini Tanzania, mkoani Morogoro, Iringa, Arusha, Morogoro, Mbeya na Pwani pamoja na maeneo mengine nchini.

Ni kawaida, ajali zinazotokea, ukiachilia mbali watu wanaopoteza maisha, wapo watu wanapoteza viungo vyao na mali zao, wapo wanaokuwa yatima, wajane na wategemezi kutokana na ndugu zao.

Kutokana na kuwepo ajali nyingi kwa mwaka, tunapongeza msimamo wa serikali kufuatilia ubadilishaji leseni daraja C ili kuhakikisha madereva wanaokuwa na leseni ni wale waliofuzu mafunzo.

Hivyo, kubadilisha leseni ni kutumia wakati huo kubaini madereva ambao hawana taaluma wala maarifa ya udereva kujichomeka kwenye fani hiyo na hivyo kuchangia ajali. Ubadilishaji wa leseni japo unaonekana unaleta usumbufu kwa abiria, lakini ni msingi mzuri katika kupunguza ajali ambazo zinaondoa maisha ya watu na wengine kuwaacha walemavu.

Kwa kubadilisha leseni kutapunguza asilimia 76 ya ajali zinazotokana na sababu za kibinadamu, ambazo zinapoteza nguvu kazi ya taifa na raslimali ya umma kwa wingi zaidi.


Utafiti unaonesha kuwa ajali hizo zinapoteza zaidi ya Sh bilioni 20 kwa mwaka, hasara ambayo ni kubwa kwa nchi inayoendelea kama Tanzania.

Kiufupi, asilimia 94 ya ajali za barabarani zinaweza kuzuilika na jamii yenyewe, maadamu mwaka 2012 itaamua kuzingatia sheria za barabarani.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi