loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

'Kutokomeza vifo vya mama na mtoto inawezekana'

Mkoani Rukwa hali ya afya ya mama na mtoto inaelezwa kwamba imeendelea kuimarika. Mkoa huo umeendelea kushuhudia kupungua kila mwaka kwa vifo vinavyosababishwa na uzazi kutoka vifo 177 kati vizazi hai 100,000 mwaka 2010 hadi vifo 131 kwa kila vizazi 100,000 mwaka 2013 na vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 112 hadi 54 kwa kila vizazi hai 1,000.

Japokuwa idadi ya vifo imepungua kwa tarakimu wataalamu wa afya wanasema kuna haja ya kuongeza bidii katika eneo hilo na bidii hiyo ni kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kuokoa maisha ya mama ambao wanapoteza maisha katika harakati za kuleta uhai duniani. Mkoa wa Rukwa kitarakimu uko chini ya lengo la Kitaifa kwa kuwa na vifo 93 kwa kila vizazi hai 100,000.

Kushuka kwa vifo hivi ni juhudi zinazofanywa na mkoa kwa kushirikiana na halmashauri zake na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya aliitisha kikao cha kazi kujadili mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto mkoani Rukwa ambapo alionesha kughadhabishwa kwake na baadhi ya zahanati kutokuwa na vyumba vyenye staha vitakavyomvuta mzazi kujifungulia humo.

“Majengo ya baadhi ya zahanati zetu hayana vyumba vya kumwezesha mjamzito kujifungua kwa faragha... Nilitembelea zahanati kule vijijini, za Mawenzuzi na Mammbwe Kenya, wajawazito wanajifungulia chini. Sasa nauliza kwa nini mama ajifungulie kwenye udongo? Hii haikubaliki kabisa. Lazima kila mmoja wetu atimize wajibu wake na tukifanya hivyo tutakuwa tunaokoa maisha ya wajawazito na watoto,” anasema.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote, waganga wakuu wa wilaya na mkoa, wakuu wote wa idara na wakunga wa jadi.

Katika kikao hicho, Manyanya aliwataka wajumbe kuhakikisha kuwa mkoa, kwa kadiri inavyowezekana unapunguza vifo vya uzazi akisema 'Rukwa bila kuwa na vifo vya wajawazito inawezekana'.

“Tunao uwezo wa kusema sasa vifo vya wajawazito na watoto basi, ni pale kila mmoja wetu katika eneo lake atasema inawezekana na kutekeleza kwa juhudi jukumu lake," anasema.

Katika kikao hicho wajumbe walishuhudia maofisa watendaji wa kata na tarafa wakila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa watawajibika na kwamba wako tayari kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu iwapo watabainika kutotekeleza wajibu wao ipasavyo na kusababisha mjamzito kupoteza maisha yake.

Ilikubalika kwamba uwajibikaji wa watendaji kata, vijiji na tarafa utapimwa kwa kuhakikisha vifo katika maeneo yao vinatokomea na kwamba ndicho kigezo cha wao kupanda vyeo.

Watendaji walitakiwa waitishe mikutano ya hadhara ya kuufikisha ujumbe huo kwa wananchi na pia wanaume mkoani humo wakatakiwa wawajibike katika afya ya uzazi wa mama na mtoto.

Wajumbe walikubaliana kuwa kila kitongoji kiwe na mtu wa kuratibu kila mjamzito aliyepo katika eneo lake na kwamba kila mimba ijulikane na kutolewa taarifa kila mwezi kuanzia ngazi ya kitongoji, mtaa, kijiji, kata, ofisa tarafa hadi wilayani kwa wakurugenzi wa halmashauri ambao wataifikisha kwa mganga mkuu wa mkoa.

Akichangia katika mkutano huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Emmanuel Mtika, alibainisha kuwa katiya kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, vifo 55 vya wajawazito viliripotiwa kutokea katika vituo vinavyotoa huduma ya afya ambapo vingi vilitokea katika Hospitali ya Mkoa mjini Sumbawanga kutokana na wajawazito hao kucheleweshwa kuletwa.

Akasema vifo vitano kati ya hivyo vilitokea katika halmashauri ya Sumbawanga, 26 Manispaa, Kalambo 5 na 19 vilitokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Kadhalika, akasema katika kipindi hicho hicho vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 473 sawa na vifo 48 kwa kila vizazi hai 1,000 na kwamba vifo vya vya watoto wachanga vilikuwa 167 kwa maana ya vifo 3.3 kwa kila vizazi hai 1,000.

Aliainisha sababu kadhaa zinazosababisha vifo vya wajawazito mkoani humo kuwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa damu, wajawazito kutokwa kwa damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, maambukizi ya magonjwa, kupasuka kizazi, ugonjwa wa malaria na matumizi ya dawa za asili zisizopimwa kwa ajili ya kuanzisha uchungu wa uzazi.

Akichangia, Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Mathew Sedoyeka, alishauri wakunga wa jadi watambuliwe na kuona uwezekano wa wao kushirikiana na wakunga katika vituo vinavyotoa huduma ya afya vya jirani na wanakoishi ili washirikiane pamoja katika kuwazalisha wajawazito.

“Kuhusu wakunga wa jadi… Ninachoomba ni namna gani tunashirikiana maana kuna maeneo mengine hata zahanati hakuna, mnazidiwa nguvu, uwezekano wa kuwashirikisha hawa katika vituo vya afya wajisajili ili wawazalishe wajawazito kwa kushirikiana na wauguzi lingekuwa jambo zuri kama inawezekana," alisema.

Kadhalika alishauri wakurugenzi wa halmashauri kuona uwezekano wa wakunga wa jadi wanaotambuliwa katika vijiji kuokoa maisha ya wajawazito na watoto na kuona familia zinafurahi kupatiwa simu za viganjani hata, ikiwa ni kwa kuwakopesha ili akipata mzazi awe kiungo kati yake na wauguzi na wakunga wa zahanati jirani na anapoishi. Sedoyeka alisisitiza pia umuhimu wa lishe nzuri kabla na baada ya kujifungua.

Akataka elimu itolewe ili familia yote ijipange kuhakikisha mama anakula vizuri ili ajifungue akiwa ni mwenye afya bora. Baadhi ya akina mama waliozoea kujifungulia kwa wakunga wa jadi wanasema inawawiwa vigumu kwenda hospitalini kwa kile wanachoeleza kuwa wakunga wa jadi wanawahudumia kwa upendo mkubwa tofauti na hospitalini.

“Nimeshuhudia kauli za kejeli na matusi za wakunga wa hospitalini dhidi ya wajawazito. Baadhi ya akina mama pia tunaona aibu kujifungua mbele ya wauguzi wa afya na wakunga ambao wana umri mdogo sawa na watoto wetu," anasema Mariana Jacob, mama wa watoto watano.

Mashirika matatu yasiyo ya kiserikali ya Africare, Jhpiego na Plan International yanaugana na serikali ya mkoa wa Rukwa katika jitihada zake za kupunguza na vifo vya wajawazito na watoto kupitia mradi wao wa Wazazi na Mwana.

Ofisa Africare mkoani Rukwa, Gaspar Materu, anasema mashirika hayo matatu kwa pamoja, kupitia mradi wake wa Wazazi na Mwana wanaunga mkono jitihada za serikali kufikia Malengo ya Milenia, hususani lengo nambari nne na tano la kupunguza vifo vya watoto wachanga na vile vinavyotokana na uzazi mkoani humo.

Mradi huo anasema utekelezaji wake ulianza Januari 2012 na mashirika hayo matatu yasiyo ya kiserikali na kwamba unafadhiliwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Canada kupitia Shirika lake la Maendeleo la CIDA na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

“'Okoa maisha ya mjamzito, mtoto mchanga na watoto wenye umri chini ya miaka mitano', ndiyo kauli mbiu inayobeba ujumbe huu mzito wa mradi huu wa Wazazi na Mwana," anasema.

Anasema mradi umetoa msaada wa magari mawili ya kisasa ya kubeba wagonjwa yanayotoa huduma katika vituo vya afya vya Mtowisa katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga na Wampembe katika mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi. Mradi pia anasema umefanya ujenzi wa vyumba vya kisasa vya upasuaji katika vituo hivyo ambavyo vimekamilika.

Changamoto za afya ya uzazi mkoani Rukwa zinaelezwa kuwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya wenye ujuzi, miundominu isiyo endelevu ya kutolea huduma ya afya, mfumo usioridhisha wa kurufaa wagonjwa, mapokeo hasi ya huduma za njia za kisasa za uzazi wa mpango na mgawanyo usio linganifu wa rasilimali katika vituo vya kutolea huduma ya afya.

“WANAOFANYA shughuli za maendeleo katika vyanzo vinavyotiririsha maji ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi