loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lala salama Ligi Kuu na makocha wapya

Mabingwa hawa watetezi wa taji hili, hawakuanza vizuri sana raundi ya kwanza, walianza kwa kusuasua, lakini wakamaliza wakiwa kileleni chini ya kocha wao Mholanzi Ernie Brandts. Brandts aliyekuwa akisaidiwa na mzawa Fred Minziro, aliiongoza Yanga na kumaliza raundi ya kwanza ikiongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Azam. Yanga ina pointi 28.

Lakini pamoja na kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kinara, Brandts alijikuta akila Krismasi bila kibarua chake, baada ya kupewa notisi ya mwezi mmoja na uongozi wake.

Ingawa sababu za Yanga kusitisha mkataba wake tena ukiwa 'mbichi' na Mholanzi huyo, inadaiwa ni kocha huyo kushuka kiwango, lakini taarifa za ndani zinadai kuwa chanzo kikubwa ni kushindwa kupanga timu yenye ushindani katika mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya hasimu wake, Simba ambapo Yanga ilifungwa mabao 3-1.

Yanga imekwenda mbali zaidi katika hilo, kwani ilivunja benchi lake lote la ufundi na hivyo inaanza raundi ya lala salama ikiwa na benchi jipya la ufundi ambapo sasa Mholanzi mwingine, Johannes van der Pluijm amechukua mikoba ya Brandts.

Charles Boniface Mkwasa, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, atasaidiana na Mholanzi huyo huku Juma Pondamali akichukua nafasi ya Mkenya Razack Siwa kuwa kocha wa makipa.

Akizungumza kwenye tovuti rasmi ya Yanga, Pluijm ambaye alitarajiwa kurejea nchini jana na timu yake kutoka Uturuki, anasema anaona mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake licha ya kuwa nacho kwa takriban wiki moja.

Awali, kocha huyo hakuongozana na Yanga kwenye kambi hiyo ya wiki mbili Uturuki, lakini akaungana nao wiki moja iliyobaki.

“Timu imecheza vizuri nawapongeza vijana kwa kujituma, hakuna lisilowezekana katika mpira, wachezaji wangu sasa hivi wanajiamini na wanajua wanatakiwa wafanye nini kwa wakati muafaka, ilikuwa mechi nzuri sana hata kocha wa Simurq PIK amefurahia uwezo wetu,” alisema.

Anasema kocha huyo baada ya mechi ya kirafiki dhidi ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Azerbajain ambapo katika mechi hiyo ya mwanzoni mwa wiki, zilitoka sare ya mabao 2-2.

Aidha, kocha huyo anazidi kukimwagia sifa kikosi chake kwamba sasa kimeiva na kiko tayari kupambana kwenye Ligi Kuu na michuano mbalimbali ya kimataifa.

Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame). Yanga pia katika kujiimarisha imefanya usajili wa kipa Juma Kaseja, Hassan Dilunga na Emmanuel Okwi ambaye hata hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezuia usajili wake mpaka litakapopata ufafanuzi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Simba: Simba inajipanga kurudi kileleni baada ya kuporomoshwa hadi nafasi ya nne licha ya kuongoza msimamo kwa karibu raundi nzima ya kwanza. Imefanya mabadiliko kwenye benchi lake la ufundi kwa kumwondoa mzawa, mchezaji wake wa zamani Abdallah Kibadeni.

Nafasi ya Kibadeni sasa imechukuliwa na kocha raia wa Croatia, Zdravko Logarusic aliyeajiriwa Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya. Kwa mechi chache alizoiongoza Simba, Mcroatia huyo ameonekana kukubalika kwa uongozi na mashabiki, na hasa baada ya kuifunga Yanga kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe (kama ilivyo kasumba ya timu hizi kutaka kufungana zenyewe pasi kuangalia mustakabali mzima wa timu husika).

Logarusic 'Loga' aliiongoza Simba kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mapema mwezi huu, na kushika nafasi ya pili nyuma ya KCC ya Uganda iliyoifunga bao 1-0 katika fainali.

Loga akisaidiwa na wachezaji wa zamani wa timu hiyo, Seleman Matola na Iddi Pazi anayefundisha makipa, anasema hana wasiwasi na kikosi chake licha ya kuwa mgeni kwenye Ligi ya Tanzania, lakini ana imani atafanya vizuri.

“Najua wazi kwamba kila timu imejiandaa, na najua Simba ni moja ya timu kubwa ambayo itapata wakati mgumu na upinzani mkubwa lakini naamini tunaweza kupambana,” anasema Logarusic.

Simba nayo imefanya marekebisho katika kikosi chake kwenye usajili wa dirisha dogo, ambapo imewaongeza makipa wa zamani wa Yanga, Ivo Mapunda na Mghana Yaw Berko. Pia imewaongeza Uhuru Selemani, Ali Badru, Awadh Juma na Donald Mosoti.

Azam: Azam ambayo hakuna siri kwamba ndio tishio kwa wakongwe Simba na Yanga katika soka kwa sasa, walisitisha mkataba na kocha wao Stewart Hall siku ya mwisho ya mzunguko wa kwanza.

Timu hiyo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 27, inaingia kwenye mzunguko wa pili ikisaka taji lake la kwanza la Ligi Kuu tangu kuanzishwa kwake ikiwa na kocha mpya Mcameroon Joseph Omog akisaidiwa na mzawa Kalimangonga 'Kally' Ongala.

Azam pamoja na kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya pili, lakini mwenendo wake kwenye ligi hiyo haukuwa wa kuridhisha na inadaiwa hiyo ndio sababu ya uongozi kusitisha mkataba na kocha Hall.

Kocha Omog aliiongoza Azam kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, lakini ikajikuta ikiutema ubingwa ilioutwaa mara mbili mfululizo baada ya kuishia hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya mwaka huu. Azam imefanya usajili wa mchezaji mmoja Mouhamed Kone kuimarisha kikosi chake. Ashanti, Coastal Union:

Ashanti na Coastal Union nazo zina makocha wapya, ingawa tofauti ni kidogo kwamba Ashanti inaanza mzunguko wa pili na Kibadeni aliyetupiwa virago na Simba huku Coastal ikiwa na Mkenya Yusuph Chipo aliyeanza kukinoa kikosi hicho mechi chache kabla ya kumaliza mzunguko wa kwanza akichukua nafasi ya Mzanzibari Hemed Morocco ambaye amechukuliwa na JKT Oljoro.

Kocha Kibadeni anasema kikosi chake kiko vizuri kupambana huku akitambia mazoezi iliyoyapata kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Ashanti ilichukua nafasi ya Yanga iliyojitoa dakika za mwisho. Hata hivyo, Ashanti haikufanya vizuri kwenye michuano hiyo baada ya kuishia kwenye makundi.

“Timu yangu imetolewa, lakini kama mnavyojua ndio kwanza nimeanza kuifundisha timu hii, hivyo nimepata nafasi ya kukiona kikosi changu na kuona wapi kuna mapungufu niongoze, nashukuru kwa hilo,” anasema Kibadeni.

Ashanti ndio timu inayoongoza kufanya usajili wa wachezaji wengi kwenye dirisha dogo ambapo imewasajili wachezaji 15, Kassim Kilungo, Mohamed Banka, Bright Obinna, Victor Costa, Juma Mpongo, Juma Jabu, Ally Kondo, Shafii Rajab, Mohamed Faki, Abubakar Mtiro, Patrick Mhagama, Ally Kabunda, Hassan Kabuda, Idd Ally na Rahim Abdallah.

Inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo ikiwa na pointi 10. Coastal Union ambayo iliweka kambi ya mazoezi ya takriban wiki mbili Oman, haikufanya usajili wa dirisha dogo.

Timu nyingine ambayo haijafanya hivyo ni Kagera Sugar na Mtibwa Sugar. Coastal Union ni ya nane ikiwa na pointi 16 ilizomaliza nazo mzunguko wa kwanza.

Ruvu Shooting: Kocha Tom Olaba ni mgeni Ruvu Shooting, lakini si mgeni kwenye soka ya Tanzania. Amekuwepo kwenye Ligi Kuu kwa takriban miaka 10 kwa vipindi tofauti akiwa na Mtibwa Sugar.

Olaba sasa ndio Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting akichukua mikoba ya Mkwasa aliyekwenda Yanga. Akizungumzia mikakati yake, Olaba anasema anaifahamu ligi ya Tanzania na karibu timu zote zinazoshiriki anazifahamu.

“Kama unavyojua sikutoka muda mrefu Mtibwa Sugar hivyo bado kuna wachezaji nawafahamu, pamoja na kwamba sikusajili timu na nimeikuta katikati ya mashindano, nataka imalize vizuri,” anasema Olaba. Ruvu Shooting iko nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na pointi 17. Wachezaji iliowaongeza kwenye dirisha dogo ni Ally Khan na Jumanne Khamis.

Mbeya City, Mtibwa, Kagera Sugar: Ikiwa ipo katika msimu wa kwanza wa Ligi Kuu tangu kuanzishwa kwake, Mbeya City imekuwa ikifanya vizuri ambapo haijapoteza mechi katika raundi ya kwanza.

Mbeya City inafundishwa na kocha wa siku nyingi kwenye Ligi Kuu, Juma Mwambusi akiwahi kuzifundisha baadhi ya timu za ligi Kuu kama Tanzania Prisons na Moro United.

Chini ya Mwambusi, Mbeya City imefanya vizuri na kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo ikifikisha pointi 27 sawa na Azam iliyo nafasi ya pili.

Kocha Mwambusi anasema anazifahamu hila za klabu kongwe kwenye soka ya Tanzania, lakini atapambana nazo kufanya vizuri.

“Najua kila kitu kuhusu timu kubwa, sisi ndio kwanza tumeingia kwenye ligi tunataka kutoa upinzani na naamini tunaweza,” anasema Mwambusi. Anazungumzia mikakati yake kwamba anataka kumaliza ligi katika nafasi tatu za juu, kama ikitokea akakosa ubingwa. Imemuongeza mchezaji mmoja kwenye dirisha dogo, Saad Kipanga.

Mtibwa Sugar ni ya tano kwenye msimamo mpaka leo ikiwa na pointi 20 sawa na ndugu zake wa Kagera Sugar.

Mtibwa Sugar ambayo miaka iliyopita ilikuwa ikitoa ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu, miaka ya karibuni imekuwa ni kama haina madhara licha ya kutoa wachezaji kadhaa nyota kwenye Ligi Kuu ambao wananunuliwa na klabu za Simba na Yanga.

Kocha wake, Mecy Maxime anasema sio kwamba timu hiyo imelala, lakini yanayotokea ni mambo ya soka.

“Ni soka tu, lakini sio kwamba hatutaki kuwa kwenye ushindani… ila timu yangu imefanya maandalizi ya kutosha kukabiliana na timu yoyote ile,” anasema Maxime, mchezaji wa zamani wa timu hiyo. JKT Ruvu, Oljoro, Rhino:

Hizi hazikuwa na madhara makubwa sana kwenye mzunguko wa kwanza, Oljoro inaanza mzunguko wa pili ikiwa na kocha Morocco aliyetoka Coastal Union.

JKT Ruvu ni ya tisa ikiwa na pointi 15 kwenye msimamo wa Ligi ikifuatiwa na Rhino yenye pointi 11 na Oljoro inafuata ikiwa na pointi 10. Prisons, Mgambo Shooting: Hizi ni timu mbili zinazoshika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Prisons ikiwa ya 13 na Mgambo ni ya 14.

Tofauti na Prisons ya miaka ya nyuma iliyokuwa ikitoa upinzani kwa timu mbalimbali za Ligi Kuu, timu hiyo ya Mbeya inayomilikiwa na Magereza, sasa imeonekana haina madhara na haiogopeshi tena.

Imekusanya pointi tisa katika mechi 13 za mzunguko wa kwanza huku Mgambo Shooting ambayo msimu uliopita ilizichachafya timu kadhaa ikifikisha pointi sita katika mechi zake 13.

Hii ndio raundi ya lala salama, atakayelia, atakayecheka itajulikana mwishoni mwa raundi hii Aprili 27, mwaka huu huku macho na masikio ya mashabiki yakielekezwa kwa Yanga, Simba, Azam na Mbeya City.

foto
Mwandishi: Zena Chande

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi