loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lala salama Ligi Kuu

Mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati nje kidogo ya jiji hilo lenye raha na karaha kibao, katika kitongoji cha Mbagala kwenye Uwanja wa Azam Complex, kutakuwa na mechi kati ya wenyeji Azam FC na Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.

Coastal Union na Oljoro JKT zitaumana kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Kagera Sugar ikiikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la Soka la Tanzania, raundi ya 14 ya ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili. Kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, itakuwa kati ya Simba na Rhino Rangers kutoka Tabora wakati maafande wa JKT Ruvu na Mgambo Shooting watapambana Uwanja wa Azam Complex.

Kwa mujibu wa TFF, viingilio kwenye mechi ya Ashanti United na Yanga vitakuwa Sh 5,000, Sh 15,000 na Sh 20,000.

Viingilio mechi ya Mkwakwani vitakuwa Sh 10,000 kwa Sh 3,000, Uwanja wa Azam Complex Sh 10,000 kwa Sh 3,000, Uwanja wa Kaitaba ni Sh 5,000 kwa Sh 3,000.

Yanga ambayo ilitua nchini jana alfajiri ikitokea Antalya nchini Uturuki, inaingia uwanjani kuanza mzunguko wa pili ikiongoza kwa kuwa na pointi 28, moja zaidi ya Azam FC na Mbeya City katika nafasi ya pili na tatu, na pointi nne zaidi ya watani wao wa jadi, Simba katika nafasi ya nne.

Mbali ya hilo, mabingwa hao watetezi pamoja na Azam FC, Simba na Ashanti United zinaanza mzunguko wa pili zikiwa na sura mpya za makocha baada ya kuwafukuza makocha iliyokuwa nao awali.

Yanga ilivunja benchi lote la ufundi chini ya Mholanzi Ernie Brandts na wenzake Fred Minziro, Razak Siwa na daktari Nassoro Matuzya na kuwaleta Mholanzi mwingine Johannes van de Pluijm, Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali, katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuondokana na kushuka kwa nidhamu katika timu.

Pluijm ambaye alikuwa akifundisha soka Ghana katika klabu ya Berekem Chelsea, atasaidiwa na Mkwasa aliyekuwa Ruvu Shooting kuhakikisha wanapata ubingwa tena Jangwani msimu huu.

Kwa upande wa Simba, waliwafukuza Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na kuwaleta Zdravko Logarusic, raia wa Croatia na Selemani Matola ambao walianza kazi kwa kuipa Simba taji la Nani Mtani Jembe katika pambano lililofanyika Desemba 21, mwaka huu.

Logarusic na Matola watakuwa na kazi ya kuhakikisha wanaipa Simba ubingwa kwa mechi 13 zilizobaki, kama ilivyo kwa kocha mpya wa Azam FC, Joseph Omog, raia wa Cameroon ambaye alirithi mikoba ya Mwingereza Stewart Hall aliyefukuzwa siku ya mwisho ya mzunguko wa kwanza.

Omog alianza kwa kupoteza taji la Kombe la Mapinduzi kwa KCC ya Uganda, na sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwapa taji la kwanza la ligi vijana hao wa Bakhressa ambao tangu waanze kushiriki Ligi Kuu ya Bara hawajawahi kulinyakua zaidi ya kuishia nafasi ya pili.

Kibadeni baada ya kutupiwa virago na Simba amebadilisha mitaa na sasa yuko mitaa ya Ilala kwa vijana wa Ashanti United ambako atakuwa na kazi moja ya kuhakikisha hawarudi Daraja la Kwanza kwani leo wanaikabili Yanga wakiwa katika nafasi ya 12 kati ya timu 14.

Yanga itaikabili Ashanti United ikiwa imefanya usajili wa wachezaji watatu wapya katika dirisha dogo, kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja, kiungo nyota wa Ruvu Shooting Stars, Hassan Dilunga na mshambuliaji nyota wa zamani wa Simba, raia wa Uganda, Emmanuel Okwi.

Hata hivyo, Okwi ambaye aliichezea Yanga katika mechi ya Nani Mtani Jembe itabidi asubiri kabla ya kucheza Ligi Kuu kwani pingamizi lililowekwa na Simba, limekubaliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambayo sasa wameomba ufafanuzi kwa Fifa kuhusu mchezaji huyo ambaye aliuzwa na Simba kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, kabla ya kurejea SC Villa ya Uganda.

Kumekuwapo na mzozo kati ya Simba na timu hiyo ya Tunisia kwa sababu klabu ya Msimbazi inadai haijalipwa ada yake ya uhamisho Dola za Marekani 300,000 na Okwi pia amekuwa na matatizo nayo, kiasi cha kuidhinishwa na Fifa kucheza Villa kwa muda, suala ambalo sasa limezua mgogoro nchini.

KLABU ya Chelsea imemtangaza ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi