loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lusonga ilivyojikomboa na adha ya zahanati

Yote yamefanyika kwa ushirikiano wa wananchi, mbunge na hususan Taasisi ya Medical Peace Foundation ya Korea Kusini iliyofadhili ujenzi wa kituo cha Afya katika eneo hilo kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni 100.

Wakazi wa Lusonga wana bidii katika shughuli za kujitolea kimaendeleo kutokana na falsafa waliyojengewa tangu zamani na muasisi wa jina hilo, 'Lusonga', Gerevas Kumbukira (sasa marehemu).

Kayombo anasema, Lusonga imepata bahati kukubaliwa kujengewa kituo hicho cha afya kwa sababu, Medical Peace Foundation hujenga kituo kimoja tu kwa kila nchi duniani kwa mwaka.

“Ina maana kwa hapa nchini ni kitongoji hicho pekee kilichoangukiwa na ngekewa hiyo baada ya kituo kilichojengwa mwaka jana huko Tanzania Visiwani,” anasema.

Akizungumzia changamoto zilizo mbele ya mradi huo, Mbunge huyo anasema, waganga ni eneo ambalo linahitaji msukumo wa pamoja ili huduma hiyo ilete tija kwa wananchi wa Lusonga na Mbinga kwa ujumla.

Anasema, kwa kuwa taasisi hiyo inalijua tatizo hilo imekubali kutoa mganga mmoja atakayekuja kufanya kazi kwa muda mfupi wakati mchakato endelevu wa kuwatafuta waganga wazalendo ukiendelea.

Wakazi wa Lusonga, walionesha ushirikiano kwa kutoa muda wao na nguvu katika kuchoma matofali, kusomba mawe kwa mtindo wa msaragambo katika kuhakikisha kituo hicho cha afya kinakamilika kwa wakati.

Mwandishi wa makala haya alishuhudia tangu watoto hadi wazee wakijituma kikamilifu katika harakati hizo za kuhakikisha huduma ya afya iliyokuwa inapatikana mbali sasa inakuwa karibu. Kresensia Turuka ni miongoni mwa wazee ambao waliokuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi kwa kujitolea katika ujenzi wa Kituo hicho ambacho kwa sasa kimekamilika.

Akizungumzia mwamko uliooneshwa na baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho hususani rika la wazee na watoto, anasema baada ya diwani na viongozi mbali mbali kutoa hamasa kuhusu jukumu hilo, waliamua kujitokeza kwani kazi hiyo ni kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.

Anawatahadharisha vijana ambao hawakuwa wengi katika jukumu hilo akisema huko mbele ya safari ikiwa vijana hawatajirekebisha na kujituma katika kazi za kujitolea utafika wakati watakosa misaada kutoka kwa wahisani.

Kijiji cha Lusonga kina idadi ndogo ya wafugaji wa ng’ombe licha ya kuwa mazingira mazuri yanayofaa kwa shughuli.

Ufugaji ulioshamiri Lusonga ni wa nguruwe na mbuzi, jambo linalosababisha maziwa kuwa bidhaa adimu kwenye ardhi yenye majani mengi.

Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Mbinga mjini, Calvin Mapunda Kata ya Kilimani kwa kiasi fulani ina mwamko wa ufugaji wa ng’ombe ikilinganishwa na Lusonga na kwamba Kata hiyo ndiyo inayosambaza maziwa katika migahawa mingi Mbinga mjini na kwa watu binafsi.

Bila shaka Wachaga wanaogombana wakigombea vihamba vidogo kule mgombani inawafaa wakatembee Mbinga na kuona fursa za kuwekeza.

Asilimia kubwa ya wakazi wa Lusonga, ni kabila la Wamatengo ambao shughuli zao kuu ni kilimo cha mahindi na maharage kwa mazao ya chakula wakati kwa zao la biashara wanalima kahawa kwa baadhi ya maeneo machache hasa milimani.

Ugali kwa maharage na dagaa wa ziwa Nyasa, wali na samaki maarufu eneo hilo aitwaye mbasa ni chakula cha asili cha wakazi wa eneo hilo.

Lusonga ukitaka kukorofishana na watu basi wewe wanyime pombe yao ya asili iitwayo ngelenge inayotengenezwa kwa mahindi na ulezi, wakati ngoma yao maarufu inajulikana kwa jina la Linguga.

Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Mbinga mjini, Calvin Mapunda kata hiyo ina vijiji vitano ambavyo ni Ruhuwiko, Matarawe, Masasi, Masumuni na Mbinga yenyewe.

Kata nzima ina jumla ya watu 10,788 mgawanyo ukiwa 5,259 wanaume na wanawake wakiwa ni 5,479. Kati ya watu wote wa Kata ya Mbinga mjini, watu wa kitongoji cha Lusonga wanakadiriwa kuwa 3,251, wanaume 1,420 na wanawake 1,831. Kitongoji kina shule za msingi saba na sekondari tatu.

Kwa upande wa maji safi na salama, diwani huyo anasema maji wanayo ya kutosha isipokuwa changamoto wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa miundombinu bora na ya uhakika ya kuyasafirisha maji hayo yaweze kuwafikia wananchi karibu na makazi yao. Lusonga linaaminika kuwa jina lililobuniwa na Gerevas Kumbukira mwaka 1940.

Asili ya jina hilo, ni mchanganyiko wa maneno ya lugha ya Kimatengo na Kiswahili lenye maana ‘piga hatua mbele’.

Jina Lusonga, wakati huo halikuonekana tofauti sana na majina ya vitongoji vingine. Sababu mojawapo ikiwa ni umasikini wa kipato uliokuwa ukiwakabili wakazi wengi wa eneo hilo.

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi ...

foto
Mwandishi: Innocent Mallya

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi