loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

M23 yatangaza kumaliza uasi

Kikundi hicho sasa “kitatumia njia za kisiasa, kutafuta suluhu kwenye sababu zilizofanya kikaundwa,” kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa jana na Rais wake, Bertrand Bisimwa na kuisambaza kwa njia ya barua pepe.

Waasi hao walijiondoa kwenye Jeshi la Serikali ya DRC Machi mwaka jana, baada ya kuituhumu Serikali kushindwa kuheshimu makubaliano ya amani ya mwaka 2009, ambayo yaliwezesha wao kujiunga na vikosi vya Serikali.

Wapiganaji hao waliukamata mji wa kibiashara wa Goma, Mashariki mwa DRC kwa siku 11 Novemba mwaka jana kabla hawajaondoka, kutokana na shinikizo la kimataifa la kuwataka kuanza mazungumzo ya amani.

Jeshi la DRC lilianza kukomboa maeneo ya Goma Kaskazini Agosti kwa msaada wa Brigedi mpya ya Umoja wa Mataifa, ikijumuisha vikosi vya Tanzania. Umoja huo una walinzi wa amani 19,000 nchini humo.

Mapigano makali yalianza Oktoba 25 baada ya kuvunjika tena kwa mazungumzo ya amani, ambapo majeshi ya Serikali yalitwaa ngome ya mwisho ya M23 ya Bunagana Oktoba 30.

“Tumekamilisha kazi yetu,” Msemaji wa Jeshi la DRC, Luteni Kanali Olivier Hamuli, alisema kwa njia ya simu kutoka Chanzu, Mashariki mwa DRC.

“Sasa tutafuatilia vikundi vingine vya kijeshi,” alisema DRC imehangaika kumaliza mgogoro uliopo katika eneo hilo la Mashariki lenye utajiri wa madini, ambao ulianza katikati ya miaka ya tisini baada ya mauaji ya kimbari ya nchi jirani ya Rwanda.

Wapiganaji wa DRC na wa kigeni wako bado katika eneo hilo lenye utajiri wa madini ya bati, dhahabu na koltani, ambayo hutumiwa kutengenezea simu na kompyuta za mikononi. Uhusiano na Rwanda M23 ni kikundi cha hivi karibuni miongoni mwa vinavyoungwa mkono na Rwanda, kwa mujibu wa Serikali ya DRC.

Hata hivyo, Rwanda imekuwa ikikanusha kusaidia waasi, ambao, kama ilivyo kwa Serikali ya Rwanda, wengi wanaundwa na kuongozwa na Watutsi. Hamuli alisema lengo lifuatalo ni Jeshi la FDLR, kundi ambalo linaongozwa na waasi wa Kihutu wanaopinga Serikali ya Rwanda.

Rwanda inasema baadhi ya wapiganaji wa FDLR walihusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambapo inakadiriwa watu 800,000 walipoteza maisha. Kutokomezwa kwa FDLR ilikuwa moja ya masharti ya M23.

Kundi hilo pia linataka kurejeshwa kwa maelfu ya wakimbizi wa Kitutsi wa DRC, ambao wamekuwa wakiishi katika kambi za Rwanda kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Madai mengine ni pamoja na kuwa na ulinzi kwa vikundi vya wachache, kusambaza madaraka kwenye majimbo na kuwa na mpango wa makusudi wa kupeleka maendeleo Mashariki mwa nchi.

Lakini bado waasi hao watatakiwa kusaini makubaliano na Serikali na kukabidhi vikosi vyake kwa Serikali ili kumaliza rasmi uasi huo, Waziri wa Habari wa DRC, Lambert Mende alisema kwa njia ya simu kutoka Kinshasa.

Serikali itatangaza jinsi waasi wa M23 wasiokabiliwa na uhalifu wa kivita, watakavyojiunga na jamii, alisema. Nchi baadaye itaendelea na mchakato wa kufikiria hatma ya M23 na vikundi vingine Mashariki mwa DRC, Mende alisema.

“Tunahitaji kufikiria upya sababu hasa ya migogoro hii ambayo imegusa eneo la Mashariki mwa nchi kwa miaka sasa,” alisema Mende.

Viongozi washinikiza Wakati huo huo, Mwandishi Wetu anaripoti kutoka Pretoria, kwamba viongozi wa Nchi za Afrika wametaka waasi wa kundi la M23 kujitangaza kuwa ni waasi na watangaze kumaliza vita ili kusaini mkataba wa amani na Serikali ya DRC.

Viongozi hao wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mkutano wa Kimataifa wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGRL), walikubaliana kuwa waasi wa kundi la M23 kujitangaza kuwa ni waasi kwanza, kabla ombi lao la kusitishwa kwa mapigano kukubaliwa na Serikali ya DRC.

Viongozi hao walikutana Afrika Kusini kujadili maendeleo ya Mashariki mwa DRC baada ya M23 kupigwa na majeshi ya Serikali yanayosaidiwa na ya UN. Wiki iliyopita, majeshi ya UN yalipambana kwa mara ya kwanza uso kwa uso na M23 na kushikilia maeneo yote yaliyokuwa ngome kuu ya M23.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa waasi wamekubali kusitisha mapigano bila masharti na kutaka ushirikiano wa majeshi hayo na Serikali ya DRC.

Alisema sasa wanaona mwanga wa kutimia kwa ndoto za kupatikana amani Mashariki mwa Kongo. Majeshi UN yakihusisha ya Afrika Kusini na Tanzania yalikwenda DRC kuhamasisha amani baada ya M23 kuvamia na kutawala eneo la Kaskazini mwa Kivu.

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imepongeza uthubutu ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi