loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maajabu duru la kwanza Ligi Kuu

Swali la kujiuliza kwa sasa, je, huu ni wakati wa Usimba na Uyanga kuanza kupungua? Ukitizama jinsi mzunguko wa kwanza ulivyochezwa, imeonekana kuwa na upinzani kutokana na matokeo yanavyoonekana kwa kila timu kukamia kutoa ubingwa na zingine kuepuka mkasi wa kushuka daraja.

Mzunguko wa pili utaanza Januari mwakani na mapumziko ya sasa mojawapo ni kupisha michuano ya Kombe la Chelenji inayoanza Nairobi kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12, mwaka huu. Timu ambayo mashabiki wa soka nchini wameshangazwa na kasi yao ni Mbeya City, ambayo kama Azam FC imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa haijapoteza mechi hata moja.

Mbeya City imemaliza katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 27 sawa na Azam FC, baada ya juzi Alhamisi kuilazimisha timu hiyo ya Chamazi sare ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Azam Complex, katika mechi yao ya kufunga mzunguko wa kwanza.

Mabingwa watetezi, Yanga walioanza kwa kusuasua mwanzoni mwa mzunguko huo wa kwanza, inaonekana kurudi katika mbio za kutetea ubingwa wake baada ya kushinda michezo minne mfululizo na kupanda mpaka nafasi ya kwanza ikimalizia kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu JKT.

Wakati mzunguko wa kwanza ukimalizika, Yanga ndiyo yenye safu kali ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao 31, ikifuatiwa na watani wao wa jadi, Simba wenye mabao 26. Azam FC inafuata kwa kuwa na mabao 23. Katika ngome, Coastal Union ndiyo imeruhusu mabao machache, saba.

Simba iliyoanza kwa kasi katika mzunguko huo, inaonekana kupunguza kasi hususani katika kipindi hiki cha lala salama ya mzunguko wa kwanza na hali imekuwa mbaya zaidi kwa klabu hiyo ndani ya Oktoba kwani kati ya michezo mitatu ambayo timu hiyo ilicheza, haikushinda mchezo hata mmoja.

Pengine hali hiyo inatokana na timu hiyo kukabiliwa na mechi ngumu kwani baada ya kuambulia sare kutoka kwa watani wao wa jadi katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 3-3, baadaye ilipata sare nyingine kutoka kwa Coastal Union na kisha kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa ‘Wanalambalamba’ Azam FC.

Hata hivyo, Simba ilizinduka katika mechi ya mwisho ya kumaliza mzunguko huu wa kwanza, iliibamiza Ashanti United kwa mabao 4-2, hivyo kupata ahueni ambayo mashabiki wake walishaanza kulalamika wakitaka benchi la ufundi linaloongozwa na Abdallah Seif ‘Kibadeni.’

Matokeo hayo angalau yameshusha pumzi kwa Simba ambayo ilianza vyema Ligi Kuu, lakini ikapepesuka katika michezo yake mbalimbali ikiwamo minne ya mwishoni ambayo badala ya kupata pointi 12, iliambulia pointi tatu, hivyo iliyozidisha sintofahamu katika Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo.

Simba baada ya kuongoza kwa muda mrefu katika ligi hiyo, sasa inakwenda mapumziko ya mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 24, na itabidi ifanye kazi ya ziada mwakani kama inataka kurejesha ubingwa ilioupoteza kwa Yanga msimu wa 2012/13.

Ligi hiyo ikiwa imepamba moto katika harakati za kuwania ubingwa wa msimu 2013/2014, vilevile inaonekana kuchangamsha mashabiki kutokana na upinzani wa hali ya juu unaooneshwa na Mbeya City, timu ngeni katika ligi huku baadhi ya timu zikionekana kukata tamaa na mbio za kuwania ubingwa.

Mbeya City inayonolewa na kocha Juma Mwambusi hadi msimu huu unapokaribia kukatika, imewashangaza mashabiki wengi kutokana na upinzani mkali iliyouonesha kwa kuzifunga timu mbalimbali huku ikizibana na kutoa upinzani mkali kwa vigogo wa ligi hiyo, Simba na Yanga ambazo ilitoka nazo sare, tena wakongwe hao wakilazimika kusawazisha ili kupata pointi moja.

Jambo la kujiuliza kama timu hiyo imefika mahali hapo ilipo hivi sasa kwa nini timu zingine zisifike hapo ikiwa zote zina wachezaji sawa uwanjani? Imani yangu ni kuwa suala la kujiamini ndilo kila kitu kilichoifikisha timu hiyo mahali hapo hivyo hakuna sababu ya timu zingine kuwa na hofu dhidi yake.

Timu kama Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Ruvu Shooting Stars, hali zao si mbaya sana, kwani ziko katikati ya msimamo wa ligi hiyo zikiwa katika nafasi ya tano, sita na saba. Mtibwa Sugar na ndugu zao wa Kagera Sugar wote wamemaliza mzunguko wa kwanza wakiwa na pointi 20.

Mtibwa Sugar chini ya Kocha Mkuu, Mexime Maxime, haijaonesha makali zaidi msimu huu, ikiwa imeshinda mechi tano, kutoka sare tano na kupoteza tatu sawa na Kagera Sugar inayofundishwa na Mganda Jackson Mayanja. Zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ruvu Shooting Stars ya Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ ni moja ya timu zilizoonesha soka ya kuvutia katika mzunguko wa kwanza, ikiwa katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 17, baada ya kushinda mechi nne, sare tano na kufungwa michezo minne. Kwa ujumla, kikosi hicho kinatakiwa kuongeza nguvu katika mzunguko wa pili ili kuwa na nafasi nzuri ya kushika moja ya nafasi za juu za Ligi Kuu msimu huu.

Timu ambayo mashabiki wengi walikuwa wakiipa nafasi ya kutamba msimu huu ni Coastal Union, lakini licha ya usajili wa ‘nguvu’ imepepesuka katika mzunguko wa kwanza na imemaliza katika nafasi ya nane. Wagosi hao wa Kaya wana pointi 16 baada ya kushinda mechi tatu tu, kwenda sare saba na kufungwa tatu, na imefunga mabao 10 tu katika michezo yake 13; hali ambayo kwa vigezo vyovyote vile inaacha maswali.

Coastal Union imesajili wachezaji mahiri kama Haruna Moshi ‘Boban’, Juma Nyoso, Mkenya Crispin Odulla, Mganda Lutamba Yayi ambao pamoja na wa zamani kama Jerry Santo, Danny Lyanga, lakini matunda ya usajili huo hayajawafurahisha siyo tu viongozi, bali mashabiki wake.

JKT Ruvu iliyoanza kwa kishindo Ligi Kuu msimu huu kiasi cha kuongoza kwa kushinda mechi tatu mfululizo, sasa imepotea na imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya tisa ikiwa na pointi zake 15. Baada ya kushinda mechi zake tatu, ilipata ushindi katika mechi nyingine mbili tu. Imepoteza mechi nane na imeweka rekodi kwa kumaliza mzunguko wa kwanza bila kupata sare yoyote.

Chini ya Kocha Mkuu Mbwana Makata, inabidi ijiulize maswali nini kimewakumba kiasi cha kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tisa na zaidi kupoteza mechi nane. Vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya mzunguko wa pili ambao kila timu itakuwa inawania kupata ushindi kunusuru kushuka daraja.

Timu nyingine ngeni katika Ligi Kuu msimu huu ni Rhino Rangers, ambayo mambo yake si mazuri sana kwani ilikuwa katika nafasi ya 10 juzi kabla ya Prisons katika mechi ya kumaliza mzunguko. Timu hiyo ya mkoani Tabora na pekee inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), inapaswa kufanya kazi ya ziada katika mzunguko wa pili ili isirudi Daraja la Kwanza.

Unaweza kujiuliza ni kwa sababu gani timu zinazomilikiwa na majeshi zimeendelea kudorora? Je, ni ukata wa fedha au la? Unakuta jibu ni hapana kutokana na udhamini mnono wa Ligi Kuu Tanzania Bara ukiwa inamilikiwa na wadhamini wawili ambao ni Vodacom na Azam TV kwa upande wa urushaji wa matangazo.

Ukiangalia msimamo, kuanzia timu ya tisa hadi ya 14 zote zinamilikiwa na majeshi isipokuwa Ashanti United katika nafasi ya 12. Timu hizo ni JKT Ruvu, Rhino, Oljoro JKT, Tanzania Prisons na Mgambo JKT. Oljoro JKT ambayo ni msimu wake wa pili sasa, iko nafasi ya 11 ikiwa na pointi 10 sawa na Rhino na Ashanti United, lakini zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Hali yake ni mbaya kama ilivyo kwa Ashanti United ambayo imerejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kuwapo katika msimu wa 2007. Timu hizo zinapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha hazitoi fursa ya kurejea Daraja la Kwanza ambako mchuano wake pia ni mkubwa.

Ashanti United ambayo ilianza ligi kwa kukung’utwa na Yanga mabao 5-1, ilijitahidi kuzinduka njiani mwa mzunguko huu wa kwanza, lakini hadi bado haijawa njema kwao na wana kila sababu ya kusaka dawa ya kubaki Ligi Kuu katika mzunguko wa pili, vinginevyo ifikapo Mei, hadithi itakuwa nyingine.

Mambo pia siyo mazuri kabisa kwa Tanzania Prisons ambayo inashika nafasi ya 13 kabla ya kuivaa Rhino Rangers juzi ikiwa na pointi nane. Hali yake ni mbaya kwani wakati wenzao wa Mbeya City wakitakata, wao wana dalili mbaya za kurejea Daraja la Kwanza ambako waliwahi kucheza.

Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania, wameshinda mechi moja tu hadi sasa, wakaenda sare tano na kufungwa sita, hali inayowaweka pabaya katika msimamo. Kama hawatabadilika, Ligi Kuu wataisikia katika vyombo vya habari msimu ujao. Hali mbaya zaidi ni kwa timu ya kutoka Kabuku wilayani Handeni katika Mkoa wa Tanga.

Mgambo JKT iko taabani. Baada ya mechi 13, imeshinda moja tu, imetoka sare tatu na kufungwa tisa. Yenyewe imefunga mabao matano tu na kufungwa mabao 23, mengi kuliko timu nyingine yoyote. Kikosi hicho cha Mohammed Kampira, kina uwezekano mdogo wa kubaki Ligi Kuu, kama matokeo hayo yanavyoonesha na kama uchezaji wake hautabadilika.

Makubwa yanapaswa kutendeka ili kuokoa hali. Licha ya ligi kuwa na udhamini mzuri, lakini safu ya washambuliaji wa Tanzania bado imeonekana kuwa ‘kichwa cha mwendawazimu’ kutokana na kuzidiwa mbinu za ufungaji na wachezaji wa kigeni wanaoendelea kuitawala ligi hiyo kwa kuzifumania nyavu mara kwa mara.

Mfano, mwaka jana wachezaji kama Hamis Kiiza ‘Diego’ kutoka Uganda, Didie Kavumbagu wa Burundi, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite wote kutoka Rwanda, waliwapa ubingwa Yanga SC huku wachezaji mahiri nchini wanaochezea klabu hiyo wakiishi kukalia benchi.

Msimu huo pia ilishuhudiwa mchezaji anayekipiga na Azam FC, Kipre Tchetche kutoka Ivory Cost akiibuka mfungaji bora. Na hata sasa, ushindani wa mabao umeshikwa na wageni. Amis Tambwe mchezaji mpya wa Simba kutoka Burundi anaongoza akiwa na mabao 10, akifuatiwa na Kiiza mabao manane, Tchetche, Juma Luizio (Mtibwa Sugar) na Elias Maguli (Ruvu Shooting) wenye mabao saba.

Ukifikiri kwa undani zaidi unakuta washambuliaji wa nchini kama Jerryson Tegete, Hussein Javu, Said Bahanunzi, Gaudence Mwaikimba, John Bocco, wanashindwa kuiga mifano ya wachezaji wa zamani kama wakina Nteze John, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ na Joseph Kaniki, katika kuzifumania nyavu.

SEKTA ya ubunifu (sanaa) na uchumi ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi