loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mabilioni yatengwa kuondoa kero ya maji Mkuranga

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla baada ya kukagua kisima cha maji cha Mvuleni Kata ya Nyamato wilayani humo hivi karibuni. Kisima hicho cha Mvuleni kina uwezo wa kutoa lita 26,000 za maji kwa saa na kitahudumia wakazi wa vijiji vya Mvuleni, Nyamato na Kilimahewa.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo hilo, Makalla anaagiza kuwa ujenzi wa mradi wa Mvuleni ikiwemo ujenzi wa kisima, ukamilike mwezi wa Agosti. Anaahidi kuwa mwezi Septemba atakwenda tena kukagua.

“Mkandarasi lazima akamilishe haraka mradi huu. Nataka Septemba uwe umekamilika,” anasema alipotembelea wilaya hiyo kukagua miradi mbalimbali ya maji. Anawahakikisha wakazi wa Mvuleni, kuwa mradi huo utatoa lita 26,000 za maji kwa sasa. Tangi la mradi huo lina uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 na likijaa litasambaza maji katika vituo 13.

“Ningependa nitakapotembelea tena eneo hili Septemba, nisikie kero zingine kama vile vituo vya kuchotea maji havitoshi au idadi ya watu imeongezeka. Sitaki kusikia tena kuwa hamna maji,” anasema.

Anawataka wakazi wa kijiji cha Mvuleni, kutoa ushirikiano kwa kamati ya maji. “Lindeni chanzo cha maji, pandeni miti. Hakikisheni vyanzo vya maji, haviharibiwi wala kuhujumiwa,” anasisitiza.

Akiwa Mvuleni, Naibu Waziri huyo pia alielezea matatizo ya usambazaji maji nchini chini ya Mradi wa Vijiji 10 kwa kila wilaya, ambao hujulikana pia kama Mradi wa Benki ya Dunia.

Anasema mradi huo uliobuniwa mwaka 2007, una mlolongo mrefu wa masharti ya utekelezaji. Kwa mfano, katika mradi huo wananchi walitakiwa kuchangia fedha.

Ilikuwa lazima wananchi wachangie asilimia 5 za fedha zote zinazotakiwa kutekeleza mradi husika. Baada ya hapo, wananchi walitakiwa kubuni mradi. Sharti lingine ni mkandarasi kwenda kutafiti chanzo cha maji katika eneo husika.

Sharti lingine ni mkandarasi atakayejenga, siyo aliyefanya utafiti. Mjenzi ni mtu mwingine.

Sharti lingine ni mkandarasi aliyetafiti, itabidi ipeleke taarifa Wizara ya Maji, kisha taarifa hizo zipelekwe Benki ya Dunia. Kukiwa hakuna tatizo lolote, Benki ya Dunia huruhusu mradi husika kutekelezwa.

Urasimu huo umesababisha miradi mingi nchini, kuchelewa au kushindwa kutekelezwa. Makalla anasema kilichofanywa na serikali hivi sasa ni kupunguza masharti hayo. Anasema kwa sasa mamlaka yamebaki kwa wilaya husika.

Wilaya ndizo zinatafuta makandarasi kupitia kamati za manunuzi za wilaya. Kisha wilaya hizo hutaoa taarifa wizarani.

Pia, kwa sasa wanaotafiti, ndiyo watachimba visima hivyo. Wananchi wataendelea kuchangia asilimia 5 kutekeleza mradi husika.

Kwa ujumla, Makala anasema hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji wilayani Mkuranga ni mbaya, kwani kwa mjini ni asilimia 4.6 na vijijini ni asilimia 53.

Anabainisha kuwa maeneo mengi ya wilaya hiyo, iliyopo mkoa wa Pwani, yana tatizo la maji. Wananchi wengi wanategemea maji ya visima na vinachimbwa kila mahali penye eneo.

Kazi zinazofanywa ni kuweka mabomba, kujenga matangi ya kuhifadhi maji na kujenga vituo vya kusambaza maji. Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkuranga (MKUWASA), Filbert Pius anabainisha ukubwa wa tatizo hilo kwa mji wa Mkuranga.

“Mji wa Mkuranga una jumla ya watu 25,847, lakini wanaohudumiwa na MKUWASA ni 1,200 tu, sawa na asilimia 4.6 ya wakazi wote,” anaeleza hayo mbele ya Makalla.

Anasema MKUWASA ina visima vitatu, lakini kinachofanya kazi ni kimoja. Lakini nacho hakizalishi kwa sasa, kutokana na kuharibika.

“Tangu Jumatatu iliyopita hatuna maji. Hii inatokana na ukosefu wa pampu na mota kuharibika katika kisima chenye uwezo wa kuzalisha lita 26,000 kwa saa. Kwa sasa visima viwili havina pampu,” anasema Pius.

Anasema wameshamwarifu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, kuhusu kuharibika kwa pampu na mota ya kisima hicho.

“Tumeshamwarifu Mkurugenzi ili awasiliane mkandarasi aliyepo Dar es Salaam aliyechimba na kufunga mota katika kisima hiki,” anasema.

Makalla anasema tumaini kubwa la Mkuranga ni kisima kirefu, kinachochimbwa nje kidogo ya mji wa Mkuranga katika eneo la Kurungu. Makala alitembelea kisima hicho cha kurungu.

“Kisima hiki kina maji mengi ya kuweza kutosheleza mji wa Mkuranga. Kisima hicho cha Kurungu kinasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi Dar es Salaam (DAWASA) na kampuni ya Zitas,” anasema.

Kiongozi wa mafundi wa Kampuni ya CDM Smith, inayochimba kisima hicho kirefu, John Donoherth, anamweleza Makalla kuwa ujenzi wa kisima hicho kirefu ni moja ya visima 8, vinavyofanyiwa utafiti wilayani humo.

Mradi mwingine mkubwa unaotarajiwa kuondoa tatizo la maji katika wilaya ya Mkuranga ni visima virefu vya Mpera. Visima hivyo vimeanza kuchimbwa na DAWASA.

Mabomba yatalazwa kutoka kwenye chanzo hicho kikubwa hadi maeneo ya wilaya ya Mkuranga na eneo la viwanda jijini Dar es Salaam katika barabara ya Nyerere na maeneo Pugu, Ukonga hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Visima virefu vya Kimbiji mkoani Dar es Salaam na Mpera vitapokamilika, vitaongezeka kwenye mfumo uliopo wa usambazaji na kutoa lita 700 za maji yenye ubora wa hali ya juu kwa siku.

“Visima vya Mpera na Kimbiji ni vyanzo vya maji vinavyotia matumaini makubwa kiuchumi na kijamii. Vyanzo hivi viko chini ya ardhi na vilibuniwa muda mrefu,” anasema.

Wilaya ya Mkuranga ipo jirani na jiji la Dar es Salaam katika barabara kuu iendayo Lindi na Mtwara.

Ilianzishwa mwaka 1995 na ina tarafa nne, kata 18 na vijiji zaidi ya 100. Shughuli kubwa za wakazi wa wilaya hiyo ni kilimo cha muhogo, mpunga, maharage, nazi, mananasi na machungwa.

Wilaya hiyo ni kinara wa kilimo cha korosho nchini, ambapo hekta 35,000 zinatumika kulima zao hilo.

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba ...

foto
Mwandishi: Nelson Goima

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi