loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mabonde 9 ya maji yatanufaisha vizazi vingi vijavyo

Mabonde 9 ya maji yatanufaisha vizazi vingi vijavyo

Ili kukabiliana na uhaba wa maji, Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeainisha mabonde tisa ya maji, ambayo yanasimamiwa katika utaratibu maalumu ili kuliwezesha taifa kuwa na rasilimali endelevu ya maji. Mabonde hayo tisa yalitangazwa na Waziri wa Maji mwaka 1989 kwa kutumia Sheria ya Matumizi ya Maji, kanuni na taratibu Kifungu Namba 42 cha mwaka 1974 na marekebisho Namba 10 ya mwaka 1981.

Ili kuhakikisha kuwa mabonde haya yanasimamiwa vyema na kuweka mikakati endelevu ya upatikanaji wa maji, Serikali ilifungua ofisi katika serikali za mabonde hayo. Ofisi ya kwanza ilifunguliwa katika Bonde la Mto Pangani mwaka 1991. Bonde la Pangani lipo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania na lina kilometa za mraba 53,600.

Bonde hilo limepita katika wilaya 17 zilizopo katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga. Bonde la Pangani lina mabonde madogo matano, ambayo yapo katika mito mikubwa ya Pangani, Zigi, Umba, Mkulumuzi na Msangazi, ambayo inamwaga maji katika bahari ya Hindi.

Bonde la Pangani lina sifa ya kipekee, kwani linajumuisha mabonde yanayotitirisha maji kutoka milima ya Kilimanjaro, Meru, Usambara na Upare. Pia, bonde hilo linajumuisha maji ya ziwa Chala, Jipe, Duluti na Karamba pia mabwawa ya Nyumba ya Mungu, Mabayani na Kilimawe.

Matumizi makubwa ya maji katika bonde hilo ni matumizi ya nyumbani, kilimo, uzalishaji viwandani, uzalishaji wa umeme na uvuvi. Bonde la Mto Rufiji lilipata ofisi ya maji mwaka 1993 na linajumuisha eneo lote, ambalo mwelekeo wa maji yake huingia Mto Rufiji, kisha kumwagwa katika Bahari ya Hindi.

Bonde hilo lina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 177,420 na lina mito mikuu minne ambayo ni Ruaha Mkuu wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 82,970, Kilombero wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 39,990. Mto mwingine ni Luwegu wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 26,300 na Mto Rufiji wenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 22,160.

Bonde la Ziwa Victoria lilipata ofisi ya maji mwaka 2000, Bonde hilo liko ndani ya Ziwa Victoria ambalo ni ziwa kubwa kuliko yote Barani Afrika, ambalo chanzo chake ni Mto White Nile. Bonde hili ni miongoni mwa mabonde ya kimataifa kwa kuwa linajumuisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Mito mingine inayomwaga maji yake Ziwa Victoria ni mito ambayo inamwaga maji Ziwa Victoria ni pamoja na Mto Kagera, Simiyu, Mbarageti, Gurumeti, Mara na Mori. Bonde la Mto Wami na Ruvu ililipata ofisi ya maji mwaka 2001. Ofisi hiyo inasimamia shughuli za upatikanaji wa maji katika mikoa ya Dar es Saalam, Pwani, Morogoro na mikoa mingine ya karibu.

Bonde la Wami Ruvu linajumuisha mito mikuu miwili ambayo ni Wami wenye kilometa za mraba 400,000 na Ruvu wenye kilometa za mraba 17,700. Bonde hili kwa ujumla lina ukubwa kilometa za mraba 72, 930 pia lina maeneo ya tambarare na safu ndefu za milima ya Uluguru, Nguru Rubeho na Ukaguru.

Milima hiyo inaaminika kwa kuvuta mvua ambayo maji yake kutiririka haki katika mito ya Wami na Ruvu. Bonde la Ziwa Nyasa lilipata ofisi ya maji mwaka 2001 (2001). Bonde hili liko katika nchi za Tanzania, Malawi na Msumbiji, na lina ukubwa wa kilometa za mraba 132,000. Ziwa Nyasa lina ukubwa wa kilometa za mraba 33,000.

Eneo la bonde linalotiririsha maji ndani ya Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania ni kilometa za mraba 37,000. Mito mikuu ndani ya bonde hili ni Songwe, ukishirikiana na mto Malawi, Kiwira, Lufirio, Ruhuhu na Rumakali. Bonde la Ziwa Rukwa ni bonde ambalo linaingiza maji kutoka kwenye vijito vidogo vidogo kuingia kwenye Ziwa Rukwa bila kumwaga nje.

Ziwa lina eneo la kilometa za mraba zipatazo 2,300 na bonde Zima lina ukubwa wa kilometa za mraba 88,000. Bonde hili limegawanyika katika wilaya mbalimbali. Tabia za bonde ni za mfumo wa bonde la ufa la Afrika Mashariki. Upande wa Magharibi wa Ziwa lipo katika miinuko ya Ufipa.

Eneo lina vijito vingi vinavyomwaga maji yake katika bonde la Mto Rukwa kutoka upande wa Kaskazini Mashariki kwenda upande wa Kusini Mashariki. Upande wa Kaskazini wa bonde umeinuka kuelekea upande wa bonde la Ziwa Tanganyika, na upande wa Mashariki umetawaliwa na safu ya milima ya Mbeya.

Bonde hilo lilipata ofisi ya maji mwaka 2001 ambayo inasimamia utaratibu wa kugawa maji kwa matumizi ya nyumbani, viwandani pia kwa ajili ya kilimo. Bonde la Kati linajumuishwa na mito na vijito vinavyoingiza maji yake katika ziwa lililopo katika Kanda ya Kati ya Kaskazini.

Vijito vidogovidogo vinavyotoka Ziwa Natron mpakani mwa Kenya kuelekea Tanzania kwenye bonde la Bahi. Eneo la bonde kwa upande wa Tanzania ni kilometa za mraba 153,800. Maziwa makuu yanayomwaga maji katika bonde hili ni Ziwa Eyasi linalopokea maji kutoka katika Mto Wembere na Manonga iliyopo Kaskazini mwa Tabora na Mashariki mwa Shinyanga.

Ziwa Manyara hupokea maji yake kutoka kwenye ardhi chepechepe ya Bubu. Maziwa mengine madogo yaliyopo katika bonde hilo ambayo hayamwagi maji yake nje ni ziwa Basuto na Natron. Bonde hilo liko katika maeneo kame ya Tanzania, ambapo wastani wa mvua kwa mwaka ni kati ya 500 milimita katika maeneo ya Bahi na 900 milimita katika vilima vya Mbulu.

Bonde la Ziwa Tanganyika liko Magharibi mwa nchi ya Tanzania na linajumujisha mabonde yote madogo yanayomwaga maji yake katika Ziwa Tanganyika. Bonde lina ukubwa wa kilometa za mraba 239, sehemu kubwa ya bonde ni Mto Malagarasi lenye ukubwa wa kilometa za mraba 130,000.

Mto Malagarasi umeanzia katika maeneo ya milima ya mpakani mwa Burundi na Tanzania. Mto unateremka Kaskazini Mashariki kupitia kwenye vilima na miteremko kuelekea kwenye ardhi chepechepe ya Malagarasi. Vijito vikuu vya Mto Malagarasi ambavyo ni Myowosi na Igombe vinakutana katika Ziwa Nyamagoma.

Mito ya Ugala na Ruchungi inakutana na Mto Malagarasi upande wa chini wa Ziwa Nyamagoma, Kwa upande wa Magharibi unapita kwenye majabali ya Misitu ambapo yanatengeneza maporomoko kabla ya kuingia Ziwa Tanganyika. Mto Ugala unapokea maji kutoka katika eneo la kilometa za mraba zipatazo 52,000 na kabla haujakutana na mto Malagarasi unapita katika maeneo oevu na kutengeneza ziwa la muda la Ugala na Sagara.

Vijito vingine vikubwa ni Ruchungi unaopokea maji kutoka vilima vya Kaskazini vya Kasulu kuelekea upande wa Kusini na kupitia katika maeneo oevu kabla ya kuingia Mto Malagarasi maeneo ya Uvinza. Pamoja na Mto Malagarasi Ziwa Tanganyika pia linapokea maji kutoka katika mabonde madogo madogo, upande wa Kaskazini Magharibi wa Kigoma kwenye Mto Luiche, ambao hufurika wakati wa mvua.

Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini limepata ofisi ya maji mwaka 2004 ambayo hufanya kazi usimamia rasilimali za maji, uchunguzi na uchimbaji wa maji chini ya ardhi, vilevile kuweka mipango na kufanya utafiti, usimamizi wa sheria na utunzaji wa mazingira ya vyanzo maji. Mabonde yanasimamiwa na maofisa mabonde wa maji.

Bonde hilo la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini lina mito mikuu mitano inayomwaga maji yake katika bahari ya Hindi. Mito hiyo ni Matandu wenye kilometa za mraba 18,565, Mto Mavuji wenye kilometa za mraba 5,600, Mto Mbwemkuru wenye kilometa za mraba 16,255, Mto Lukuledi wenye kilometa za mraba 12950 na vijito vya mto Ruvuma.

Pia bonde hilo linajumuisha Mto Ruvuma unaoshirikiana kati ya Tanzania na Msumbiji na kuingiza maji yake katika bahari ya Hindi. Mto huu una urefu wa kilometa 800 kati ya hizo kilometa 650 zipo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. Bonde la Mto Ruvuma lina ukubwa wa kilometa za mraba 152,200 kati ya hizo kilometa 52,200 sawa na asilimia 34 zipo Tanzania zilizobaki ziko Msumbiji na Malawi.

Vijito vikubwa vya mto huu kwa upande wa Tanzania vimeanzia katika wilaya za Mbinga, Tunduru na Masasi. Wastani wa maji yanayoingia Mto Ruvuma kwa mwaka ni mita za ujazo 15,000 milioni. Bonde la Mto Ruvuma na pwani ya Kusini lina ukubwa wa kilometa za mraba 104,270 na hutumiwa na watu zaidi ya milioni mbili.

Kwa ujumla mabonde hayo yanahifadhi maji, kuweka mandhari nzuri yanayovutia watalii wa ndani na nje ya nchi. Pia mabonde hayo yanajumuisha mito inayotumiwa kwa shughuli za usafiri, uvuvi, kilimo cha umwagiliaji na vyanzo vya nishati ya umeme unayotumia nguvu ya maji. Pamoja na uhumimu wa mabonde hayo.

Yanakabiliwa na hatari ya kupoteza maji mengi kutokana na uharibifu wa mazingira ambao unasababisha mabadiliko ya tabia nchi. Ili kuhakikisha kuwa mabonde hayo yanaendelea kukinufaisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, kila mtu anapaswa kutunza mazingira na kuheshimu vyanzo vya maji kutokana na ukweli kwamba bila maji hakuna uhai.

“TUNALIMA, tunavuna sana kuliko kawaida, unaweza ukajikuta unauza ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi