loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mahakama za kifamilia zitakomesha ukatili wa wanawake majumbani

Mahakama za kifamilia zitakomesha ukatili wa wanawake majumbani

Aidha, ukatili wa kijinsia ni kitendo chochote kiovu kinachofanywa kukidhi dhamira ya mtu dhidi ya mwingine kwa sababu ya jinsia yake na unaweza kufanyika kwa namna ya kimapenzi, kimwili, kisaikolojia na kiuchumi.

Ukatili dhidi ya wanawake hasa majumbani ni jambo la kihistoria kutokana na kutokuwepo kwa nguvu sawa kati ya mwanaume na mwanamke hali iliyosababisha wanaume kubagua na kuendeleza uonevu dhidi ya wanawake na kuzuia kabisa maendeleo ya mwanamke.

Hivi karibuni katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili nchini, Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) kilizindua mwongozo maalumu kwa wanawake walioathirika na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususan ukatili wa nyumbani.

Akizungumzia mwongozo huo Mwenyekiti wa Bodi ya WLAC, Nakazael Tenga anasema ukatili wa nyumbani ni wa kijinsia unaotokea kwa watu wenye uhusiano wa karibu.

Kwa mfano kati ya watu waliooana, mwanamke na mwanaume wanaoishi pamoja kinyumba, wenye uhusiano wa kingono na kwa wanafamilia wanaoishi pamoja wakiwamo watoto na wafanyakazi.

Wanawake na watoto ni kundi linaloathirika zaidi na ukatili wa nyumbani, wanawake wengi hawajaweza kutambua aina hiyo ya ukatili kutokana na mila na desturi nyingi ambazo bado zina nguvu kwenye makabila mengi nchini.

Suala la wanawake wengi kukubaliana na vitendo vya ukatili limeleta ukimya na ukosefu wa taarifa za matukio ya ukatili hivyo inabidi kuingilia kati ili kuondoa hali hiyo.

Suala la ukatili linaweza kuchukua muda mrefu kumalizika lakini ni muhimu kuelewa kuwa ukatili ni kitendo kinachofanyika kinyume na haki za binadamu, lazima upingwe na watu wachukue hatua dhidi ya vitendo hivyo.

Ni wajibu wa kila mmoja kuchukua hatua ya kuondoa vitendo vya ukatili, ukatili wa nyumbani ni tatizo kubwa na la kiujumla ikizingatiwa kuwa linahusisha haki za kibinadamu na kudidimiza maendeleo.

Ukatili wa nyumbani unahusisha pia kudhuru mwili kama kujeruhi, kupigwa kofi, kuchomwa moto, kipigo, kuteka, kulazimishwa kufanya ngono, kubaka, kudhalilishwa, kutishia kuua, shambulio la mwili, kulazimishwa ngono isiyo salama na kulazimishwa kufanya mapenzi bila rishaa.

Vitendo vya kulazimishwa vinahusisha kutishia, kuonya, kugombeza, kumtenga au kumnyanyasa mtu, pia ukatili wa nyumbani unahusisha jaribio la zuio, kuzuia na kufuatilia mienendo kama kumtenga mtu na familia au marafiki zake na kumzuia mtu kupata habari au msaada.

Aidha ni vyema kuzingatia kuwa ukatili dhidi ya wanawake ni kitendo chochote kiovu dhidi ya mwanamke na kinafanyika kwa sababu tu ya jinsi yake ya kike.

Kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo kwa yoyote aliyewahi kukumbana na kitendo cha aina yoyote katika maisha yake asinyamaze, achukue hatua kwa kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika au kutafuta msaada katika kituo cha msaada wa kisheria.

Nakazael Tenga anasema mkoa wa Dodoma unaongoza kwa kuwa na vitendo vya ukatili kwa asilimia 70.5, Mara asilimia 66.4, Ruvuma asiliamia 50.8 na Morogoro asilimia 50.1.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya afya ya mwaka 2010 asilimia 39 ya wanawake Tanzania wameathirika na vitendo vya ukatili wa kimwili kwa kuanzia wakiwa na umri wa miaka 15.

Kuhusu mwongozo huo anasema unalenga kuwawezesha wanawake waliofanyiwa ukatili kutoa taarifa na kutetea haki zao pindi zinapokiukwa pamoja na kufuatilia haki zao kwenye vyombo vya kisheria.

Mwongozo pia umeainisha aina za ukatili na hatua za msingi za kufuata, umeainisha watoa huduma mbalimbali za kijamii jijini Dar es Salaam pamoja na maeneo mengine mikoani ili kuwawezesha waathirika wa ukatili waweze kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Vituo vilivyoainishwa katika mwongozo huo vinatoa huduma kama malazi ya dharura, msaada wa sheria, unasihi, matibabu na kujikwamua kiuchumi pia kuanisha wadau muhimu katika kupambana na ukatili zikiwemo taasisi za serikali na za kiraia.

Aidha kwa kuongezeka kwa vitendo vya ukatili, Wizara ya Katiba na Sheria inaombwa kuanzisha mahakama ya familia au utaratibu maalumu wa kusaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia kuendesha mashauri yao haraka na kutoa adhabu mbadala kulingana na makosa yaliyofanyika.

Akizungumza katika uzinduzi wa mwongozo huo wa kupinga ukatili Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki anasema serikali inaandaa muongozo maalumu wa kusikiliza mashauri yanayohusiana na ukatili wa wanawake na watoto ambapo utaanza kufanya kazi katika mikoa ambayo imeathirika kwa kiwango kikubwa na vitendo hivyo.

Anawataka viongozi wa dini kushiriki katika kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa kuwahubiria waumini wao umuhimu wa kuishi kwa amani na kutafuta suluhu ya matatizo kwa amani. Anasema vitendo vya ukatili vimekuwa na madhara makubwa katika jamii ambapo serikali ina mikakati inayolenga kushughulikia masuala hayo na kuhakikisha yanatokomezwa kabisa. “Kwa sasa serikali inaandaa muongozo maalumu wa kusikiliza mashauri hayo yatokanayo na ukatili wa jinsia ….

Hata katika azimio la nchi la Maziwa Makuu linaazimia kuwa upelelezi utokanao na vitendo hivyo ufanyike kwa miezi mitatu huku uamuzi pia uchukue miezi mitatu,” anasema Angellah.

Ukatili ni jambo baya linaloathiri mhusika na jamii nzima na kwamba madhara yake hayaishi tu kwenye familia kwani watoto na wazazi walioathirika kisaikolojia na kimwili kutokana na ukatili hawatoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujiendeleza wao wenyewe na shughuli za maendeleo. Vitendo vya ukatili vinapaswa kupigiwa kelele na wanajamii wote na kwamba ifikie wakati kuwepo kwa mitandao ya wanaume wanaopinga ukatili wa wanawake na watoto.

Aidha wanawake wanatakiwa kupinga vitendo vya ukatili kwa vitendo na kwamba wanapokaa kimya wanakubali hali hiyo ambayo inadhalilisha na itakayoendelea kuchangia kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo.

Kuhusu viongozi wa dini anasema wana dhamana kubwa ya kuihubiria jamii kuhusu madhara yatokanayo na ukatili wa jinsia na kwamba ni jambo linalowezekana kuepukwa. Ukatili ni jambo baya na linaloathiri, madhehebu ya dini yanapokuwa na mikakati chanya ya kutokomeza ukatili wa kijinsia linakua jambo la furaha kwa jamii, hivyo wadau wote wajikite katika mchakato huo kwani ni jambo linaloweza kuepukika.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi