loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maji ya uhakika kupatikana Dar es Salaam

Lakini, ni vema watu hao watambue kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za maji katika jiji hilo kubwa kuliko yote nchini.

“Tunateleza miradi mikubwa mingi ya kuondoa tatizo la maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na miji ya Kibaha na Bagamoyo, hivyo wananchi wengi watarajie kupata maji ya uhakika katika muda mfupi ujao,” anasema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), Archard Mutalemwa.

Anasema hayo kwenye Mtambo wa Ruvu Chini mkoani Pwani akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Dawasa, Dk Eve- Hawa Sinare na wajumbe wa bodi hiyo kwenye ziara ya kutembelea miradi ya DAWASA. Mutalemwa na Dk Sinare walijibu maswali kadhaa ya waandishi.

Akifafanua kuhusu miradi mikubwa inayotekelezwa, Mutalemwa alitaja mojawapo ni Mradi wa Upanuzi wa Ruvu Chini, unaohusu ukarabati wa mtambo sambamba na ulazaji bomba kubwa. Upanuzi wa Ruvu Chini ulikamilika na kukabidhiwa mwezi Februari mwaka huu. Mradi huo uligharimu Sh bilioni 60.35.

Fedha hizo zilitolewa na Serikali ya Watu wa Marekani kupitia shirika lake la Changamoto za Milenia. Kazi iliyofanyika ni kuongeza uwezo wa mtambo kutoka lita 180 kwa siku na kufikia lita milioni 270 kwa siku. Kuhusu ulazaji wa bomba kubwa, anasema bomba hilo jipya limelazwa kutoka Ruvu Chini wilayani Bagamoyo hadi matangi ya kuhifadhi maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam.

Kazi ya ujenzi wa bomba kutoka Ruvu Chini hadi matangi ya Chuo Kikuu cha Ardhi, inakaribia kukamilika. “Mradi huu unaendelea vizuri na utakamilika hivi karibuni. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 73,” anasema. Ujenzi wa bomba hilo lenye kipenyo cha mita 1.8 na urefu wa kilometa 56 utaongeza ufanisi wa huduma ya maji.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Sinohdro ya China na utagharimu Sh bilioni 120.2 kutoka Serikali ya Tanzania. Mutalemwa anataja mradi mwingine mkubwa kuwa ni Ruvu Chini. Dk Sinare na wajumbe wenzake wa Bodi, walitembelea pia mradi huo. Mradi huo unahusu upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu na ulazaji wa bomba kubwa la kusafirisha maji kutoka Ruvu Juu kwenda Kibamba hadi Kimara.

Upanuzi wa Ruvu Juu ulianza Februari 15 mwaka huu na utagharimu Sh bilioni 65.11. “Matarajio ni kumaliza kazi mwezi Agosti mwakani. Upanuzi wa mtambo ukikamilika utaongeza uzalishaji kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 za maji,” anasema Mutalemwa.

Bomba jipya kutoka Ruvu Juu hadi Kibamba, litakuwa na kipenyo cha milimita 1,200 na kutoka Kibamba hadi Kimara kipenyo cha milimita 1,000. Mradi huo utahusisha pia ujenzi wa tangi jipya huko Kibamba, lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10. Pia, utahusu ukarabati au ujenzi wa matangi mawili huko Kimara.

“Matangi matatu ya Kimara yamezeeka kwa sababu yalijengwa miaka mingi iliyopita. Yaliwahi kukarabatiwa mwaka 2007 kwa kuziba nyufa kwa zege. Kwa sasamawili yatavunjwa na kujenga mapya na fedha za kazi hiyo zipo. Katika matangi hayo matatu, mawili yamekuwa yakikosa maji, kutokana na maji machache kufika hapo kutoka mtamboni.

Kwa kawaida ni tangi moja ndilo linakuwa na maji kila mara. Michoro kwa ajili ya ujenzi wa matangi mawili mapya, ipo tayari na makadirio ya gharama halisi za ujenzi, yatapelekwa kwa mtaalamu mshauri wa ujenzi”, anasema Meneja wa Miradi wa Dawasa, Romanus Mwang’ingo.

Kampuni inayojenga Mradi wa Ruvu Juu ni VA TECH WABAG ya India, ambayo tayari imeanza kujenga eneo jipya la kuchujia maji au chujio (clarifier) huko Mlandizi. Ujenzi wa chujio hilo umefikia asilimia 19 hadi sasa na utakamilika Agosti mwakani. Kwa upande wake, mradi wa kulaza bomba kubwa kutoka Ruvu Juu hadi Kibamba na Kimara, unatekelezwa kwa pamoja na Dawasa na kampuni ya Megha Engineering and Infrastructural Ltd kutoka India.

Mradi huo utakaogharimu Sh bilioni 97.3, ulianza Machi mwaka huu na utakamilika mwezi Septemba mwakani. “Mkandarasi amekamilisha upimaji wa njia ya kupitisha bomba hilo kubwa , ameanza kutengeneza mabomba hayo huko India na pia ameanza kujenga ofisi ya mradi mjini Kibaha,” anafafanua Mwang’ingo, ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa Dawasa.

Mradi mwingine mkubwa unaotekelezwa na Dawasa, ambao ulitembelewa na wajumbe wa Bodi ni visima virefu vya Kimbiji na Mpera. Uchimbaji wa visima hivyo utakamilika Agosti mwakani. Maji kutoka katika visima hivyo, yatasambazwa katika maeneo ya Mbagala, Chang’ombe, Kurasini, Keko, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Gongo la Mboto, Ukonga na Segerea na mengineyo yasiyo na mabomba ya maji.

“Tunaipongeza serikali kwa kujitahidi kutafuta fedha na kisha kuipatia Dawasa mamilioni za fedha ili kutekeleza miradi mikubwa ya maji kama ya Ruvu Chini, Ruvu Juu na visima vya Kimbiji na Mpera,” anasema Dk Sinare. Aliahidi kuwa mamlaka hiyo itaendelea kujitahidi kusambaza maji katika maeneo mengi na kuunganisha wateja wengi.

Hata hivyo, aliomba Bunge kuongeza bajeti kwa ajili ya Wizara ya Maji ili wizara hiyo nayo itenge fedha nyingi kwa Dawasa, hatua itakayoiwezesha kutekeleza miradi yake mingi. Anasema bajeti ya maji inatakiwa kuwa kubwa kwa sababu mahitaji ya maji, hasa kwa jiji la Dar es Salaam, ni makubwa mno.

Aidha, mwenyekiti huyo wa bodi aliishukuru Serikali kwa kufanikiwa kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Kidunda mkoani Morogoro. Bwawa hilo litadhibiti mtiririko wa maji ya mto Ruvu kwa mwaka mzima. Mto huo ndiyo chanzo kikuu cha maji yanayozalishwa na Dawasa.

“Tupo katika mchakato wa kulipa fidia kwa wakazi wa Kidunda na pesa zimepatikana. Tayari watu watakaohamishwa Kidunda kupisha ujenzi wa bwawa wameshatengewa viwanja”, anasema Dk Sinare. Kwa hakika, upanuzi wa mitambo wa Ruvu Juu, Ruvu Chini na miradi mingine mikubwa inayotekelezwa na Dawasa, utaleta ahueni kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Nelson Goima

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi