loader
Dstv Habarileo  Mobile
Maji yanavyokwamisha maendeleo ya Sekondari ya Mt Vicent Urambo

Maji yanavyokwamisha maendeleo ya Sekondari ya Mt Vicent Urambo

Nami nikiwa mmoja wa wanafamilia wa wanafunzi wa shule hiyo siku hiyo nikiwa nimeambatana na kaka yangu Cassian Clovis aliyekuwa ametoka Kahama ambako anafanyia kazi tulikwenda pale kwa nia ya kumjulia hali mdogo wetu Leah G. Chitete mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni hapo.

Baada ya kufika getini na kuzungumza na mlinzi juu ya taratibu za kuonana na wanafunzi shuleni hapo, kwani ilikuwa mara ya kwanza kwetu kuhudhuria siku hiyo na mlinzi kutueleza kwamba tulikuwa tumekuja kabla ya muda hivyo tuendelee kusubiri hadi hapo muda utakapokuwa umefika wa kuonana na ndugu yetu, tulikubaliana na utaratibu tuliokuwa tumepatiwa na ndipo tukapaki usafiri pembeni kusubiri muda uwadie hapo ndipo nikapata fursa ya kuandika makala haya.

Wakati tukiwa ndani ya gari tuliwaona makundi kwa makundi ya wanafunzi wakitoka nje ya geti la shule huku wakiwa wamebeba ndoo hali iliyoashiria kwamba walikuwa wakifuata maji nilitafakari jambo hilo lakini sikushangaa kwani ni kawaida kwa shule nyingi za bweni kufanya hivyo hususani kipindi hiki ambacho kumekuwa na uhaba mkubwa.

Baada ya muda wa kuonana na wanafunzi kufika tulibahatika kuonana na mdogo wetu Leah lakini hali tuliyomkuta nayo ilikuwa inasikitisha kwa mtu kumuona nayo ndugu yake, pamoja na kujaa vumbi katika mwili na nguo zake lakini pia alikuwa anaonesha dalili kwamba alikuwa amechoka na kazi ngumu aliyotoka kufanya.

Nilipomhoji juu ya hali tuliyomkuta nayo alitueleza wazi kwamba muda huo ndiyo anafika kutoka kisimani kuchota maji na ndiyo sababu tumemkuta yuko katika hali hiyo hatukutaka kumwamini moja kwa moja kwa hisia kwamba hiyo ni mbinu tu ya kujitetea kutokana na hali tuliyomuona nayo hasa ukizingatia ujio wetu ulikuwa wa kushtukiza na wala hakuutarajia.

Tuliamua kuita wanafunzi wengine ili tupate kuuliza juu ya habari hiyo na hapo ndipo tulipopata ukweli huu ambao hakuna mzazi au mlezi yeyote atakayependa utokee kwa mtoto wake hususani anapokuwa shuleni Kila siku iendayo kwa Mungu wanafunzi wa shule hii wanawajibika kuchota tripu si chini ya tatu za maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile kuoga kufua hali kadhalika kuoshea vyombo na hiyo ni bila kusahau maji kwa ajili ya kupikia huchotwa na wanafunzi. Suala la kuchota maji si tatizo ila ni wapi maji hayo wanapoyatoa ndio tatizo.

Kwa maelezo ya wanafunzi niliobahatika kuwahoji ni kwamba maji hayo wanayatoa katika kijiji cha jirani cha Ndorobho ambacho kiko umbali wa zaidi ya kilometa 2 kutoka shuleni hapo kwa hesabu hiyo basi kila siku wanawajibika kutembea zaidi ya kilometa 6 huku wakiwa na mzigo wa ndoo za maji ambapo ni sawa na zaidi ya km 42 kwa wiki na km 168 kwa mwezi.

Lakini pia huko wanakoyafuata maji hayo ni nje ya eneo la shule na pale wanapokwenda wanakwenda wanafunzi wenyewe ingawa wanakuwa katika makundi lakini wanakuwa hawana msimamizi yeyote aidha mwalimu au mlezi wa kuangalia usalama wao huko waendako.

Wanapita kwenye mapori hadi kufika kisimani. Hivyo je, hadi kufika huko hawawezi kukutana na vitu vya kuhatarisha afaya au hata ustawi wa tabia zao, kwa mfano wanafunzi hao kujiingiza katika mahusiano ya kingono wao kwa wao au wao na wanakijiji, utumiaji wa pombe , sigara pamoja na dawa za kulevya ?

Lakini pia suala la maji lianapokuwa tete ustaarabu huwa unatoweka kwa wanayoyatafuta na mara nyingi huwa unatokea ugomvi usiomithilika sasa kwa kuwa maji ya kisima hicho yanatumika kwa matumizi ya pamoja kati ya wanafunzi na wanakijiji na kipindi hiki kuna mahitaji makubwa sana ya maji ni wazi kuwa wanakijiji hawawezi kuvumilia wanapoona wanafunzi wakichota maji kwa makundi na pia wanafunzi nao hawawezi kukubali kuvumilia kuchelewa ratiba zao za shule eti tu wafuate foleni watakayokuwa wameikuta na hapo nahisi ndipo inaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.

Pia ni vizuri kuangalia afya zao watoto wetu na athari ambazo zinaweza kusababishwa na hali hiyo ya kuchota maji nje ya eneo la shule, kama kweli tunazithamini afya zao ni lazima tujiaminishe kwamba hapo siyo mahali salama kwao, fikiria hili katika jamii kila binadamu ana ustarabu wake mwenyewe na hata katika matumizi ya maji kati ya wanafunzi na wanakiji vipi siku mtu atakapoamua kuwakomoa wanafunzi (ingawaje hatuombei iwe hivyo ) hatuoni kwamba idadi kubwa ya wanafunzi itakuwa hatarini ?

Tukubali tukatae lakini hili ni tatizo na linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwani tatizo hili si laleo wala la jana na wala haijulikani litaisha lini kwa sababu hata katika mahafari ya shule hiyo mwaka 2011 Samuel Sitta mbunge wa Urambo Mashariki na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa mgeni rasmi aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo hilo ingawa hadi leo miaka miwili imepita na tatizo bado liko pale pale .

Nimalize kwa kusema tatizo hili lina weza kuisha tu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake serikali kwa upande wake unawajibika katika hili uongozi au wamiliki wa shule wanawajibika hali kadhalika wanafunzi wazazi na jamii ya wana urambo kwa ujumla vinginevyo hili ni bomu limetegwa na lina subiri kulipika na siku likilipuka halitatuachasalama ni kama waswahili wasemavyo usipoziba ufa utajenga ukuta tusingoje kujenga ukuta muda ndio huu.

Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa HabariLeo, anapatikana kwa simu namba 0757605586.

 

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Matthew Chamballa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi