loader
Dstv Habarileo  Mobile
Makocha bora ni wale wanaojifunza wakati wote

Makocha bora ni wale wanaojifunza wakati wote

Hata hivyo kuna tofauti kati ya makocha wanataaluma Watanzania wanaofundisha mpira wa miguu nchini na wale wanaofanya kazi hiyo nchi nyingine. Kwa makocha wanaofanya kazi nchi nyingine, namaanisha ambao si Watanzania pamoja na wale wageni waliobahatika na wale wanaoendelea kupata ajira za ukocha wa mpira wa miguu nchini. Tofauti zao ni mbili tu.

Kwanza, wale wa nje ukocha wa mpira wa miguu ndiyo kazi yao (ajira) na wengi wao hawana taaluma nyingine zaidi ya hiyo ingawa wana elimu ya kati inayowasaidia katika ufahamu wa kawaida wa mambo mengine pamoja na mawasiliano. Pili ni kuwa wengi wa makocha Watanzania, tena wa kiwango cha juu kazi ya ukocha si mkate wa kila siku kwao.

Makocha wa aina hii wana taaluma zao nyingine ambazo ndizo zinazowafanya waangalie familia zao na kuishi maisha mazuri. Lakini ukweli bado unabaki kuwa kama wangetilia mkazo taaluma ya ukocha wa mpira wa miguu ingewalipa vizuri zaidi kuliko hizo nyingine ambazo wanazo baada ya kukaa darasani kwa muda mrefu.

Uamuzi wa kuufanya ukocha kuwa shughuli ya ziada umechangia kwa kiasi kikubwa taaluma hiyo kutokuwa na nguvu mbele ya klabu nyingi nchini ikiwa kocha anayetajwa ni mzawa. Pia hali hiyo imefanya makocha wengi wa Tanzania wasiwe na nguvu kabisa ya kupigania mikataba bora pale wanapotaka kupewa kazi ya ukocha katika klabu za nyumbani.

Lakini pia ni wazito katika kuomba kazi hiyo pale nafasi za ukocha katika sehemu mbalimbali zinapokuwa wazi. Tunayo orodha ndefu ya makocha wa kigeni waliofundisha mpira wa miguu nchini Tanzania, iwe katika ngazi ya klabu au timu za Taifa. Lakini wengi wao hawakupata mafanikio yoyote ya kuridhisha walipopewa wajibu wa kuongoza mabenchi ya ufundi katika timu hizo.

Wataje akina Nabi Camara, Slomir Wolk, Dk Victor Stanslescu, Tambwe Leya, Rudi Gutendorf, Wonder Moreira, Ernest Mokake, Clovis Oliveira, Jeff Hudson, Dusan Kondic, Razak Siwa, Dimitir Samsarov, Jack Chamangwana, Jackson Mayanja, Tom Olaba, Raoul Shungu, Patrick Phiri na Tauzany Nzoyisaba.

Wengine ni James Siang’a, Manfred George, Hussein Kheri, Anteneh Eshete, Rashid Shedu, Marcio Maximo, Itamar Amorin, Kostadin Papic, Dragan Popadic, Jean Polycarpe Bonghanya, Sredojevic Milutin ‘Micho’, Moses Basena, Stewart John Hall, Ernie Brandts, Neider dos Santos, Edson Silva na Trott Moloto.

Hao ni baadhi ya rundo la makocha waliopo au waliopata fursa ya kufundisha mpira wa miguu katika klabu mbalimbali nchini pamoja na timu za Taifa, lakini ni wachache wanaoweza kutembea kifua mbele kuwa kuna vitu vya msingi wamevifanya vilivyochangia mafanikio yaliyopatikana uwanjani.

Vilevile wapo makocha Watanzania waliopata fursa ya kufundisha mpira wa miguu katika nchi jirani au Bara Arabu (Arabuni). Baadhi ya makocha Watanzania waliofundisha mpira wa miguu Uarabuni ni akina Mansour Magram, Abdallah Kibadeni na Zakaria Kinanda. Lakini wapo makocha Watanzania waliopata fursa ya kufundisha mpira wa miguu katika nchi jirani ikiwemo Kenya.

Makocha hao ni kama akina Zakaria Kinanda, Sunday Kayuni na wengine. Changamoto kwa makocha ni kubwa. Pengine umefika wakati kwa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) kuitisha au kuandaa kongamano la makocha ambalo litatafuta ni kwanini bado mafanikio kutoka kwa makocha wazawa ni tatizo katika maeneo mawili.

Maeneo hayo ni jinsi ya kuwafanya makocha Watanzania kusimamia taaluma kuhakikisha kile wanacholipwa kilingane na utaalamu wao. Ni lazima iwepo nguvu ya kitaaluma kwa makocha wanapokaa kwenye meza ya majadiliano kwa ajili ya kupata mikataba bora. Nyingine ni jinsi ya kuhakikisha wanapata mafanikio uwanjani wanapoingiza timu katika mashindano mbalimbali.

Hakuna ubishi kuwa kongamano la aina hiyo si tu linaweza kuja na suluhu ya matatizo hayo, bali pia nini kifanyike katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana. Kwa upande wangu naamini kuwa bado tuna tatizo katika kujifunza. Nasema hivyo kwa sababu mpira wa miguu ni mchezo ambao mbinu zake zinabadilika kila siku kutokana na maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi.

Je, ni kweli kuwa makocha wetu wanajifunza kila siku? Lakini katika dunia ya leo wale wanaoaminika kuwa ni makocha bora na wakubwa, suala la kujifunza kila siku si mjadala tena bali ni wajibu. Mpira wa miguu sasa hivi kutokana na mabadiliko hayo umekuwa kama taaluma ya sheria.

Ili uwe mwanasheria mzuri ni lazima usome kabla ya kuingia mahakamani, kwani katika hoja yako unaweza kusimamia sheria ambayo tayari imeshafanyiwa mabadiliko. Hivyo kwa wanasheria suala la kujifunza kwao ni jambo la kila siku. Kusoma au kujifunza kila siku kumpa mtu fursa ya kujua mambo au vitu vipya vinavyotokea.

Suala la kujifunza binafsi kwa kocha kwa kweli halikwepeki. Nasema hivyo sababu kama ni kozi za ukocha chini ya wakufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zimeshafanyika nyingi Tanzania, pengine nyingi kupita nchi yoyote katika ukanda huu na Afrika kwa ujumla.

Lakini kupata kozi ni kitu kimoja, na kujifunza kwa maana ya kutafuta maendeleo au elimu mpya kwa kitu unachokiamini au ambacho ni sehemu ya maisha yako ni jambo lingine. Kwa sasa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, suala la kocha kujifunza utaalamu mpya si tatizo tena.

Vifaa vya kujifunza vilivyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa vipo, tena njia ya kupata mbinu mpya za ukocha hivi sasa ni nyepesi kuliko wakati wowote ule uliopita.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi