loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MAKUMBUSHO: Kijiji katikati ya Jiji la Dar es Salaam

Ni katika kijiji hiki ambako mtu unaweza ‘kukutana’ na makabila 18 kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania yakiwa ‘yamejikusanya’ pamoja. Kwa lugha nyingine, bila kufika hapo, ungelazimika kutembea siku kadhaa kuzunguka katika nchi nzima ya Tanzania ili kuyapitia makabila haya na kuyajua undani wake.

Hii ni sawa na kusema kwamba kufika katika Kijiji cha Makumbusho, humfanya mfikaji kutumia muda mfupi kukutana na kujifunza namna Tanzania ilivyoundwa na makabila yenye mila na tamaduni mbalimbali zenye historia nzito inayopaswa kuenziwa na kizazi cha sasa ambacho kinazidi kujichimbia katika tamaduni za kigeni.

Katika Jiji la Dar es Salaam, bila shaka kuna vijana wenye asili ya Kisukuma, asili ya Kichaga na kadhalika lakini hawatembelei sana katika maeneo yao ya asili ili kujua chimbuko la makabila yao, lakini mbaya zaidi wamerahisishiwa mahala pa kujua mengi kuhusu makabila hayo lakini hawaendi!

Wapo wale ambao hawaendi kwa sababu ya kutothamini utalii wa ndani sambamba na kujiburudisha kwa kuangalia mandhari mbalimbali na wapo wale ambao wanadhani maeneo ya utalii ni kwa ajili ya wageni, hususan watu weupe!

Ukiwa nje ya eneo la Kijiji cha Makumbusho, hakuna ubishi utakuwa unajisikia kwamba uko katika eneo la Jiji la Dar es Salaam, lakini ukipiga hatua chache na kuingia ndani ya uzio wa kijiji hiki utajisikia umebadilisha madhari ghafla na sasa uko katikati ya kijiji fulani.

Yaani kwa lugha nyepesi, Makumbusho ni kijiji ndani ya Jiji. Mwandishi mmoja wa makala katika jarida la Utalii la Traveller’s Roundabout, Melkizedck Karol anasema: “Ingawa nilikuwa ninapapita mahala hapo mara kwa mara kwa ajili ya shughuli zangu, nilijishangaa na kujiona mjinga ni kwa nini nilikuwa sijachukua hatua ya kuingia kwenye hiki kijiji kuona kile ambacho kinawafanya watu, hususan kutoka mataifa ya nje kwenda mahala hapo.

Kile ambacho kilikuwa kinaniijia kwenye mawazo yangu kabla ya kuingia kijijini hapo ni kwamba ‘hakuna jipya humo’.” Karol anazidi kusimulia: “Kuna siku nilishawishiwa na rafiki zangu kuingia kwenye hiki kijiji. Ni siku hiyo nilipogundua kwamba fikra zangu kuhusu kijiji hicho hazikuwa sahihi.” Karol anasema katika makala yake hayo kwamba alipoingia kwenye kijiji hicho aliona vitu vya aina mbalimbali ambavyo hakutegemea.

“Ilikuwa ni kama nimesafirishwa kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi kwenye kijiji chenye mandhari nzuri kwa safari ya kufumba na kufumbua.” Karol anaandika kwamba alipoingia Makumbusho alijifunza mengi na kupata uzoefu mpya ambao hakuwahi kuota kwamba angeupata kwa mara moja kama ilivyotokea.

Mwandishi huyo anasema alipoingia Makumbusho, aligundua kwamba si suala la kuona kitu kigeni ama kipya pekee, bali ni kupata uzoefu tofauti kadri unavyouhitaji.

Anasema kwa vile huwa inatokea mtu kutamani kuwa katika mazingira tofauti, kumbe moja ya eneo ambalo, kama wewe ni mkazi wa Dar es Salaam linakufikisha kwenye mazingira tofauti kwa muda mfupi ni Kijiji cha Makumbusho ambacho kiko umbali wa takriban kilometa nane tu kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam, katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Kimsingi, katika kijiji hiki Karol anasema ni mahala ambako mtu anaweza kujikumbusha mandhari ya kijijini kwao (kwa wale waliokulia vijijini) na pia kujisahaulisha hata kama ni kwa muda mfupi na vurugu za Jiji.

Kijiji cha Makumbusho ambacho kimekuwa kikiwavutia watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia kinaonesha kipande kingine cha Jiji la Dar es Salaam ambacho ni kijiji! Ama kwa hakika, mgeni ambaye nia yake ni kujua na kujifunza mengi kuhusu makabila mbalimbali ya Tanzania na hata kwa Mtanzania pia, Kijiji cha Makumbusho humrahishia kujua mengi kwa muda mfupi.

Baadhi ya makabila ambayo mtu anaweza kujua habari zake, aina za nyumba zao mila na desturi kupitia Kijiji cha Makumbusho ni pamoja na Wamasai, Wachaga, Wasukuma, Wanyamwezi, Wanyakyusa, Wamakonde, Wahaya, Wangoni Wayao na mengine mengi. Hiki ni kijiji kilichifadhi mifano ya nyumba 22 na vifaa vya tamaduni mbalimbali zinazopatikana katika nchi ya Tanzania.

Kijiji hicho kilianzishwa mwaka 1966 kwa ajili ya kuonesha na kutunza tamaduni ikiwemo tamaduni za asili, ngoma na tamaduni za makabila mbalimbali. Kadhalika kijiji kina migahawa ya kisasa ambako mwendaji anaweza kupata vinywaji na vyakula vya kienyeji na pia kina maeneo malumu kwa ajili ya familia na watoto.

Lakini kubwa, hususan kwa wanafunzi, ni ukweli kwamba Kijiji cha Makumhusho ni eneo muhimu la kujifunza mengi kuhusu mila na utamaduni wa Mtanzania. Makala haya yameandikwa na Hamisi Kibari kwa msaada wa jarida la Traveller’s Roundabout na mtandao wa kompyuta.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi