loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Malinzi avutiwa na shule ya soka Alliance

Malinzi akiwa jijini Mwanza katika ziara yake ya kwanza kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa tangu achaguliwe kuwa Rais wa TFF, aliitembelea ASSA hivi karibuni na kuzungumza na uongozi wa ASSA juu ya juhudi wanazoonesha katika kufundisha na kuibua vipaji vya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 12, 15 na 17.

Katika ziara yake hiyo, aliongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana, Ayubu Nyenzi na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya TFF, Ramadhani Nasibu na viongozi wa soka wa Mkoa wa Mwanza na wawakilishi kutoka serikalini, wadau wa soka na waandishi wa habari.

Malinzi pia alishiriki katika kusaini mkataba kwa niaba ya TFF kati yake na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ajili ya kuuboresha uwanja wa kihistoria wa soka kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wa Nyamagana.

Makubaliano hayo kwa upande wa TFF yaliwakilishwa na Malinzi mwenyewe na Mjumbe wa TFF kwa Kanda ya Ziwa, Vedastus Rufano na kwa upande wa Jiji yaliwakilishwa na Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji, Hassan Hida.

Meya Mabula alisema makubaliano yamekuja wakati muafaka, ambapo yeye anatarajia kuanzisha “Meya Cup” ambapo alisema timu zitakazoshiriki mashindano hayo zitapata fursa ya kuutumia uwanja huo wa Nyamagana mara baada ya kuwa umekarabatiwa.

Naye Mkurugenzi wa Jiji, Hida alisema atahakikisha ukarabati wa uwanja huo unakamilika mara moja ili kuwezesha timu za Mkoa na Jiji la Mwanza na za kutoka nje zinautumia ukiwa umeimarika na kuwa wa kisasa zaidi.

Uboreshaji wa uwanja huo kwa mujibu wa Malinzi, utaenda sanjari na upandaji wa nyasi bandia, ambapo alisema Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), lilishindwa kutekeleza azma yake ya kusaidia ukarabati wa uwanja huo likisubiri kukamilishwa kwa taratibu za kisheria kati ya TFF na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

“Huu ulikuwa ni mradi wa Fifa na Fifa wao wanatujua TFF katika uboreshaji wa uwanja huu wa Nyamagana na ilichokuwa inataka ni uthibitisho kutoka kwetu kuwa sasa uwanja huu utatumika kwa shughuli za soka na sio kubadilishiwa matumizi yake kama ilivyokuwa imeelezwa awali.

“Kilichokuwa kinasubiriwa ni taratibu za kisheria na kusainiwa kwa makubaliano haya maana yake ni kuwa uwanja huu utakarabatiwa, ikiwa ni pamoja na kupandwa nyasi bandia ili utumike kwa shughuli za kisoka,” alifafanua Malinzi aliyeingia madarakani Oktoba 27, mwaka jana.

Utiaji wa saini makubaliano hayo ulithibitishwa pia na Mwenyekiti wa Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Jackson Songora, Katibu wa MZFA, Nasibu Maburuki, Mjumbe wa TFF Kanda ya Ziwa, Vedastus Rufano.

Baada ya utiaji saini ya ujenzi wa uwanja huo, TFF itatoa kiasi cha Dola za Marekani 500,000 na nyingine 100,000 zitatolewa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili kuendelea kuibua vipaji vya soka jijini humo na Taifa kwa ujumla.

Alipata fursa ya kuwa mgeni rasmi kwenye mechi ya ufunguzi ya Ligi Daraja la Nne Mkoa wa Mwanza, ambapo timu za Alliance School Sports Academy na Mwanza Terminal maarufu kama Chipukizi FC zilishiriki kwenye mechi ya fungua dimba ya ligi hiyo, ambapo ASSA iliifunga Mwanza Terminal kwa mabao 2-1.

Awali, akizungumza na wachezaji wa timu zote mbili, Malinzi aliwaasa wachezaji kuzingatia nidhamu katika soka akisisitiza kuwa hiyo ndiyo silaha pekee ya kuwainua katika soka.

“Niwaase muendelee kudumisha nidhamu katika soka, maana kwa sasa mpira ni ajira, niwatakie kila la heri,” alisema.

Akunwa na Alliance School Sports Academy Akiwa ASSA, Malinzi alishindwa kuzuia furaha yake, hasa baada ya kutembezwa na Mkurugenzi wa ASSA, James Bwire na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na kituo hicho katika kuendeleza soka la vijana.

Malinzi aliweza kutembelea makazi ya vijana wanaojifunza soka, viwanja, majengo ya utawala ambapo aliupongeza uongozi wa Alliance Sports Club kwa juhudi kubwa iliyofanya katika kuwekeza katika soka.

Malinzi alisema, “Hakika naweza kusema TFF sasa imechomoza, imepata mahali pa kutokea na sio pengine ni hapa Alliance Sports Academy kwa ajili ya kuendeleza soka la vijana, nichukue fursa hii kumpongeza Mkurugenzi wa ASSA, James Bwire kwa uamuzi wake wa kuwekeza katika soka, jambo ambalo limekuwa likiwashindwa watu na mashirika makubwa yenye fedha, maana soka ni gharama.”

“Changamoto kubwa iliyokuwa inakabili soka ni uwekezaji wa soka la vijana, sasa kilio hicho kinamalizwa maana sasa TFF imeangukiwa na nyota ya jaha, tumeuona mlango wa kutokea na sio mwingine ni Alliance School Sports Academy, jinsi ilivyowekeza kwenye mpira wa soka- hakuna shaka sasa Alliance kitakuwa ni kituo cha kuzalisha soka la vijana nchini.

Alisema kutokana na juhudi zilizooneshwa na Alliance katika kuwekeza katika soka, TFF imekiteua rasmi kituo hicho kuwa kitovu cha maandalizi ya soka la vijana (U17) kwa mwaka 2019.

“Programu maalumu ya vijana kitaifa ya maandalizi ya soka kwa vijana U-17 itafanyika katika kituo hiki cha Alliance, na huu ni mwanzo tu, niseme TFF hakika itaendeleza ushirikiano na kituo hiki katika kuendeleza soka la vijana nchini,” alisema Rais huyo wa TFF.

Malinzi aliukabidhi uongozi wa ASSA mpira wa saizi 3 uliopokelewa na Katibu wa ASA, Mariamu Lima na wa saizi 5 kwa timu ya Maveterani wa Mwanza uliopokewa na John Tegete ambapo alisema mipira yote miwili ilinunuliwa kutoka Marekani kwa madai kuwa haipatikani nchini.

“Naikabidhi Alliance School Sports Academy mpira huu ili uweze kuwasaidia katika soka na timu yetu ya Veterani ya Jiji najua michezo ni muhimu kwao pia,” alisema Malinzi.

Mkurugenzi Bwire alimshukuru Rais huyo wa TFF kwa kuwatembelea, jambo alilosema kimempa faraja kuona kiongozi huyo wa juu wa soka anathamini mchango wa uwekezaji uliofanywa na kituo chake.

Bwire alisema alianzisha kituo hicho kwa madhumuni ya kujenga, kuimarisha na kukuza vipaji vya vijana wa kike na wa kiume katika kukuza michezo mbalimbali kwa manufaa yao na Watanzania wote.

Aliongeza kuwa mwaka 2011 kituo chake kiliamua kufanya ziara za kimichezo kwa wilaya na mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kusaka vipaji vya soka kwa vijana, ambapo kiliwapata vijana 67 ambao wote wanasomeshwa na kituo chake katika kukuza vipaji vya soka kwa gharama ya Sh 4,192,500 kwa mwaka kwa kila mmoja, ambapo jumla kuu kwa mwaka kwa vijana wote ni Sh 278, 897,500.

“Ninakushukuru kwa ujio wako hapa kwetu, lengo letu kuu ni kuhakikisha kituo chetu kinakuwa bora na mfano wa kuigwa katika kuendeleza soka la vijana barani Afrika,” alisema.

Alisema changamoto kubwa inayokikabili kituo hicho ni kuwa na ufinyu wa bajeti kwa ajili ya ukarabati wa viwanja vya michezo vinavyomilikiwa na kituo chake ili viwe vya kisasa zaidi, ambapo aliomba TFF ione uwezekano wa kuwasaidia katika ukarabati wa viwanja hivyo. Anazungumziaje kuendeleza soka nchini?

Akizungumzia maendeleo ya soka nchini, Malinzi alikiri kuwa Ligi Kuu inayochezwa kwa mechi 26 pekee bado haikidhi kiu ya Watanzania, ambapo alisema iko mipango ya kuzungumza na wadhamini ili kuona uwezekano wa kuongeza idadi ya mechi kwenye Ligi Kuu.

“Ligi Kuu inayocheza mechi 26 bado haitoshi katika kuinua soka letu hapa nchini, hali hii itaendelea kuangamiza mashindano ya soka, iko mipango ya kuanzisha Federation Cup. Hivi sasa tunazungumza na wafadhili tuone ni namna gani tunaweza kuongeza mechi kwenye Ligi Kuu ili kuifanya iwe ya ushindani zaidi,” alisema Malinzi.

Alijigamba kuwa TFF imeanzisha rasmi programu ya kitaifa ya kuboresha soka la vijana, na aliwahakikisha wadau wa soka kuwa chini ya programu hiyo, atahakikisha mambo manne yanatekelezwa kuimarisha soka.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuanzisha mpango wa kufundisha walimu wa soka shuleni kwa shule za msingi 26,000 zilizopo nchini kwa jumla ya halmashauri 23, ambapo alisema kila shule ya msingi lazima iwe na walimu wawili wa kuimarisha soka, Mwalimu Mkuu wa soka akisaidiwa na mwalimu wa michezo.

Mambo mengine ni kuhakikisha kuwa vifaa vya michezo, viatu na mipira ya saizi 3 na 4 inayotambuliwa na FIFA inapatikana kwa wingi.

Alijigamba kuwa katika utawala wake, suala la vifaa litamalizwa na TFF.

“Mambo mengine ni pamoja na kuimarisha viwanja vyetu vyote vilivyopo nchini vilivyo chini yetu, tutahakikisha kuwa vitakuwa katika mazingira mazuri ya kuwezesha mipira kuchezwa na jambo la nne tutafanya kila tutakaloweza kuhakikisha kuwa vipaji vya soka vinaibuliwa nchini kote,” alijigamba Malinzi.

TFF kutojihusisha na migogoro ya klabu Malinzi alibainisha kuwa TFF haitakuwa tayari kuwa sehemu ya kusuluhisha migogoro katika klabu za soka nchini, na badala yake alisema itatumia muda wake mwingi kwa shughuli za maendeleo.

Aliwataka viongozi na wanachama wa klabu zote kutumia Katiba za vyama vyao katika utatuzi wa migogoro na kuwa TFF hivi sasa inaanza mchakato wa kuzifanyia ukaguzi Katiba zote za vyama ili ziende na wakati na zisiwe kisingizio cha kuanzisha migogoro kutokana na upungufu ilizo nazo.

“Katika utatuzi wa migogoro ya vilabu, TFF tutaanza na kazi ya ku-audit Katiba za wanachama wetu ili kuona ni wapi zina mapungufu ili ziweze kutumiwa na wanachama na kwa sasa TFF hatutakuwa sehemu ya kusuluhisha migogoro, tutatumia muda wetu mwingi kwa shughuli za maendeleo ya soka,” alieleza.

Kuhusu fedha zinazotolewa na wafadhili, alisema kuna tatizo kubwa la uongozi kwenye klabu, ambapo wamejitokeza viongozi wenye uchu wa kufuja fedha za wafadhili, ambapo aliwaonya viongozi wa aina hiyo kuacha mara moja tabia ya kufuja fedha na badala yake wazitumie fedha katika kuendeleza soka nchini.

“Wapo viongozi katika vilabu vyetu, ambao kazi yao kubwa ni kuja kusaidia matumbo yao yanenepe kwa kufuja fedha za vilabu na zile za wafadhili, sisi TFF hatutakubaliana na viongozi wa aina hii,” alionya.

Wachezaji mamluki Kuhusu wachezaji mamluki wanaolaghai kuhusu umri wao kwenye michuano ya mashindano mbalimbali nchini na ile ya kimataifa, Malinzi aliwataka waandaaji wa michuano kuhakikisha kuwa wachezaji wanaoruhusiwa kushiriki katika michuano hiyo ni wale waliokubaliwa kwa mujibu wa sheria za soka.

Kiongozi huyo alisema ipo tabia ya baadhi ya waandaji kuwashirikisha wachezaji mamluki huku wakitambua kufanya hivyo ni kosa.

Alisema kwa kushirikiana na wanachama wake mikoani, itahakikisha suala la kuwepo kwa wachezaji mamluki kwa baadhi ya timu linadhibitiwa kwa mujibu wa sheria za soka.

“Nitoe mwito kwa waandaji wa Copa Coca-Cola, Premier League na mechi zote nchini kuhakikisha kuwa wanawachezesha wachezaji wasio mamluki kwa mujibu wa sheria ili kuendeleza soka nchini,” alifafanua.

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi