loader
Dstv Habarileo  Mobile
Malisho duni ya mifugo hukosesha mifugo ubora

Malisho duni ya mifugo hukosesha mifugo ubora

Ufugaji huo huitwa ufugaji huria ambapo wafugaji kuhamahama kutafuta malisho na maji, ikiwa una faida ya kujihami na ukosefu wa maji na malisho hasa wakati wa ukame kipindi cha kiangazi pia gharama za kuendesha kwa mfumo huo huwa kidogo.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa kuhamahama kwa mifugo hupoteza nguvu nyingi kwa kutembea masafa marefu, pia huchukua muda mrefu kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa, kuathiri mazingira ikiwemo mmomonyoko wa ardhi hasa mifugo ikiwa mingi kuliko uwezo wa eneo la malisho, uzalishaji kuwa duni.

Hali ya ukosefu wa majani au nyasi kwa mifugo inasababisha kukosa lishe bora ikiwemo protini ambapo hufanya hata soko la uuzwaji wa mifugo hiyo kusuasua ingawa baadhi ya wafugaji hulenga hasa kuwa na idadi kubwa kama ufahari na sio kibiashara kwa kutotilia maanani suala la malisho bora.

Majani au nyasi na mikunde ndicho chakula kikuu cha ng’ombe wa nyama ambapo malisho haya hupatikana kwenye mbuga za malisho ya kutosha mojawapo ya nguzo muhimu katika kufanikisha uzalishaji wa mifugo bora na yenye faida.

Wataalamu wanaeleza kuwa ng’ombe akipata malisho bora atakua haraka na kufikia uzito wa kuchinjwa katika kipindi kifupi, pia akikua kwa muda mfupi faida inakuwa kubwa kwa sababu gharama za uzalishaji hupungua.

Hapa Tanzania asilimia kubwa ya ng’ombe hufugwa huria wakitegemea malisho na maji katika mazingira ya asili, ambapo maeneo ya malisho ya asili huwa na malisho pamoja na maji yanayotosheleza mahitaji ya mifugo kwa kipindi kifupi cha mwaka.

Chakula kikuu cha ng’ombe ni nyasi na majani jamii ya mikunde, malisho haya hupatikana kwenye nyanda za malisho, uwezo wa nyanda za malisho kuhimili mifugo ni hekta tatu hadi nane kwa ng’ombe mmoja mwenye kilo 250.

Sehemu kubwa ya mbuga za malisho Tanzania iko kwenye ardhi kame. Kwa sababu ya mifugo mingi pia kuna uharibifu wa ardhi na malisho hivyo eneo kubwa liko wazi bila majani na miti, vilevile hali hii imesababisha majani ya asili kupotea na nafasi yake kuchukuliwa na magugu pamoja na majani yasiyofaa kwa malisho ya mifugo.

Malisho ya asili kwa kawaida hukua haraka na kupoteza viinilishe muhimu wakati wa muda mfupi baada ya mvua, malisho ya asili huwa na viinilishe vinavyotosheleza mahitaji ya mifugo ikiwa wakati wa kiangazi malisho huwa duni na yasiyotosheleza mahitaji ya mifugo.

Wakati wa masika malisho hutosheleza ng’ombe huwa na uzito wa kuridhisha tofauti na wakati wa kiangazi ambapo hupungua uzito ikiwa malisho ya asili yana tabia ya kuwa na upungufu wa viinilishe hasa protini kutokana na upungufu wa majani jamii ya mikunde.

Mikunde ina tabia ya kutopungua viinilishe haraka ikilinganishwa na nyasi, hukua na kukomaa haraka na kupoteza viinilishe katika muda mfupi, kwa mfano protini hupungua kutoka asilimia 15 hadi kufikia asilimia mbili. Upungufu wa protini kwenye malisho ni mojawapo ya sababu zinazopunguza uzalishaji wa mifugo nchini ambapo wakati wa kiangazi mifugo huweza kupungua uzito asilimia 15.

Malisho ya mabaki ya mazao mashambani Karibu ya masalia ya aina yote kutoka mashambani na kuweza kutumika kama malisho ya mifugo ingawa hutofautiana kwa kiwango kikubwa katika ubora wake.

Hivyo mfugaji hashauriwi kutumia sehemu kubwa ya mlo wa wanyama utokane na masalia ya mavuno mashambani ikiwa baadhi ya masalia yaliyofanyiwa utafiti na kituo cha utafiti wa mifugo Uyole ni pamoja na masalia ya mahindi na masalia ya maharage kwa viini lishe vilivyomo.

Mashudu yatokanayo na pamba ni lishe bora Utafiti uliofanyika mwaka 1986 ulibaini kuwa mashudu yanayopatikana baada ya mbegu kutolewa tayari kwa kusindika mafuta ya pamba huwekwa pembeni na kuwa kama uchafu, yalifanyiwa utafiti kuwa chakula cha mifugo yakiwa makavu kwa asilimia 95.8.

Watafiti hao wanabainisha kuwa ndani ya hayo mashudu kuna mchanganyiko wa vitu kama madini kwa asilimia 6.2, mafuta asilimia 10.3, nyuzi asilimia 14.4, protini asilimia 42.2 na naitrojeni asilimia 26.9.

Mbegu ya pamba ikitoka shambani inakuwa na nyuzi asilimia 33, mbegu halisi asilimia 66 na uchafu uliomo ni asilimia moja. Pia mbegu hiyo ikibanguliwa ina mafuta asilimia 13.2 na mashudu ni asilimia 44 asilimia inayobaki ni makapi na nyuzinyuzi ambayo mifugo wakila ni kama chakula cha ziada cha kumuongezea lishe.

Ofisa mifugo wa mkoa wa Shinyanga, Beda Chamatata anasema mashudu ni chakula cha ziada ikiwa ng’ombe mmoja hulazimika kula asilimia tatu ya uzito wake, ambapo chakula kinachotakiwa ni kikavu bila maji.

“Wafugaji wanashindwa kumudu lishe ya mashudu kutokana na gharama kuwa kubwa, huku wakimiliki idadi kubwa ya mifugo”, anasema Chamatata.

Ng’ombe aliyekuwa kwenye uzito wa kilo 250 atakula chakula kilo 7.5 huku mfugaji ana idadi ya mifugo zaidi ya 300 kilo moja ya mashudu shilingi 300, hapo anaona afadhali kuhamahama kutafuta malisho ya nyasi au majani ambayo nayo yanakuwa yamekwisha poteza protini kwa wingi.

Ambapo wafanyabiashara wa ng’ombe hutumia mashudu kunenepeshea mifugo hiyo kwa siku za minada ili kuwaboresha kwa lishe na kuonekana wenye afya lengo kupata soko zuri.

Upungufu wa madini, protini, wanga na vitamini kwa mifugo Wataalamu wanasema kuwa protini ni kiinilishe muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mnyama kwani hupata upungufu wa protini kwa kula nyasi au majani yenye protini pungufu ya asilimia 4 ambapo hukua taratibu, huchukua muda mrefu kufikiwa uzito wa kuchinjwa, majike kutokwa na mimba na kuchelewa kupevuka, ikiwemo kuzaa kuchukua miaka minne hadi mitano badala ya miwili.

Wanga ni muhimu kwa mnyama kupata nguvu, hupata upungufu kwa kutopata malisho ya kutosha hasa kipindi cha kiangazi ambapo mifugo hupungua uzito badala ya kuongezeka, majike hutokwa na mimba hushindwa kutoa maziwa.

Upungufu wa vitamini hususani A huathiri mifugo hasa wakati wa kiangazi ambapo hukosa hamu ya kula, majike au mitamba kutopata mimba, kondo la nyuma kubakia baada ya ndama kuzaliwa.

Pia upungufu wa madini unaathiri mpangilio wa uzazi na hivyo ng’ombe hushindwa kuzaa kila mwaka kwa ujumla athari za upungufu wa madini katika nyanda za malisho Tanzania ni mdogo dalili hukosa hamu ya kula ambapo mara nyingi hutokea kwa ndama sababu wana akiba ndogo ya madini mwilini.

Utunzwaji wa ng’ombe kwa wafugaji Imeonekana kuwa asilimia kubwa ya ng’ombe wanaozalishwa nchini ni daraja la nne, ambao wamekonda na mifupa inaonekana mwili mzima, wembamba nyuma kuliko mbele, wadhaifu na hawawezi kuswagwa kwa muda mrefu wengi wanafia njiani, wengi hukosa maji na malisho kwa sababu ya ukame.

Wataalamu wa mifugo wanasema kuwa ng’ombe kuwa daraja la nne linatokana na matunzo mabaya kwani kiafya hawatakiwi kuonekana mbavu, ng’ombe wa hapa nchini hawapati malisho bora ndio maana wanashuka mpaka daraja hilo.

Sifa ya kuwa ng’ombe daraja la kwanza ni misuli imekaa sawa, minene kiasi, mapaja na miguu ya nyuma ni minene pia umbo pana kiasi, wale ambao hawajapevuka wanaonesha mifupa mikubwa kiasi kwamba wakipevuka watakuwa wazuri zaidi ya hapo.

Ufugaji wa ng’ombe wa asili ni mojawapo ya shughuli muhimu ambayo tangu awali imekuwa ikiendeshwa na makabila mengi hapa nchini kama vile kabila la Wamasai, Wasukuma, Wagogo, Wahehe na Wambulu.

Madhumuni ni mengi ya ufugaji ikiwa ni pamoja na kujipatia nyama, maziwa, hifadhi ya mali, nguvu kazi na kuuza ili kujipatia kipato kutokana na sensa ya mwaka 2012 mkoa wa Shinyanga unakadiriwa kuwa na jumla ya ng’ombe milioni 1.2, mbuzi ni 586,125, kondoo ni 301,023 na punda 19,104.

Maji ni muhimu kwa mifugo Wataalamu wanasema kuwa licha ya majani au nyasi pia maji ni rasilimali muhimu katika kuendesha shughuli za uzalishaji wa mifugo, ikiwa ukosefu wa maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo husababisha uzalishaji kuwa duni.

Changamoto kubwa imekuwepo kuhusu malambo ya kunyweshea mifugo baadhi hukauka kipindi cha kiangazi, ambapo pia idadi ya yaliyopo hayatoshelezi kwa idadi ya mifugo inayofugwa ndio maana wafugaji wamekuwa wakihamahama katika maeneo.

Mkoani Shinyanga, Chamatata anasema kuna malambo 44 ila tisa kati yake hayafanyi kazi, na kwamba idadi hiyo hayatoshelezi kwa idadi ya mifugo iliyopo ikiwa kipindi cha kiangazi hukauka pia na hakuna bwawa hata moja. Wakati wa mvua maji sio tatizo, kipindi cha kiangazi maji ni tatizo mara nyingi ng’ombe huwa analazimika kutembea hadi kilomita 15 kufuata maji.

Pia ardhi ni rasilimali ya msingi katika kuanzisha ufugaji wa mifugo kuwa na malisho na maji ambavyo ni vya msingi ikiwa kuna sheria ya ardhi ya mwaka 1999 ambazo ni sheria ya ardhi ya vijiji Na 5 kanuni ya ardhi za vijiji ya mwaka 2002 chini ya sheria ya ardhi Na 4.

Ardhi ya kijiji iliyo ndani ya mipaka ya kijiji ambayo imesajiliwa kwa kufuata sheria zilizowekwa, ikiwa utaratibu uliopo ni kutengwa maeneo ya malisho ya mifugo kwenye kijiji husika na kuweza kuboresha kwa kupanda nyasi ili kuondokana na wafugaji kuhamahama kwa kutafuta malisho, migogoro ya wafugaji na wakulima kupigania maeneo au mipaka.

Pia kutokana na sheria ya malisho kifungu cha 13 ya mwaka 2010 imeonekana kutofanya kazi sababu bado haijatenga matumizi bora ya malisho ni eneo gani lifanye kazi na lipi lisifanye kazi ndio maana kumekuwepo na migogoro inayoendelea ya wafugaji na wakulima kuhusu maeneo ya malisho kwa ufugaji holela.

Changamoto zilizopo dhidi ya wafugaji Changamoto zilizopo kwa wafugaji ni elimu duni kuhusu ufugaji bora, idadi kubwa ya mifugo kuliko eneo la malisho, miundombinu ya mifugo isiyotosheleza, kutotekelezwa kwa sheria ya matumizi bora ya ardhi, ufugaji wa kuhamahama usiozingatia matumizi bora ya ardhi pamoja na kuwepo kwa magonjwa ya mifugo.

Pia wadau wengi hawafahamu umuhimu wa kupanda na kuwa na malisho bora, kutothamini malisho kuwa ni sawa na mazao mengine kama mahindi, mpunga, kahawa, uhaba mkubwa wa ardhi hasa kwa wafugaji wadogo hivyo kutotoa kipaumbele cha kupanda malisho kwenye maeneo yao bali hutoa umuhimu mkubwa kwa mazao ya chakula na biashara.

Ufugaji wa kiholela pia unachangia kutokuwepo upandaji wa malisho au mbegu za malisho sababu za wafugaji kutokuwepo na ukomo wa maeneo ya kuchungia mifugo yao.

Wadau wengi kutothamini ardhi hivyo hufuga kwa kutegemea malisho ya asili na kufuga kwa kuhamahama, jambo ambalo husababisha kutokuwepo na haja ya kupanda malisho bora.

Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza na umasikini (MKUKUTA ) kwa kufikia dira ya maendeleo Tanzania ya mwaka 2025 huenda usifanikiwe kwani umasikini utaendelea kuwepo kwa wafugaji kutotengenezewa maeneo yao ya malisho kwa muelekeo wa kibiashara kwani maeneo ya malisho kila mkoa yapo ila hakuna utekelezaji.

Mfugaji atashindwa kumudu mifugo yake kutokana na kukosekana kwa malisho bora hivyo aliyezoea kufuga ataendelea kuwa masikini na kufuga pasipo kuwa kibiashara, serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi waliangalie hili ili kuweza kumkomboa mfugaji kwa kuwa maeneo yapo kinachotakiwa ni kuelimishwa ili waboreshe malisho.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi