loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mamba: Mnyama hodari wa kuwinda majini kuliko wote

Mamba: Mnyama hodari wa kuwinda majini kuliko wote

Hata hivyo wanasayansi wa viumbe wanawaweka wanyama hao katika familia tofauti ikiwamo familia ya Alligatoridae na Gavialidae. Mamba wanaishi majini na hupatikana maeneo mengi ya kitropiki katika bara la Africa, Asia Australia na Amerika. Mamba hupenda kuishi katika maji baridi kama vile maziwa, mito, kwenye mabwawa pia katika ardhi tepetepe.

Mamba hula hasa wanyama wenye uti wa mgongo kama vile samaki, aina nyingine za mijusi, wanyama wadogo pamoja na wakubwa wanaofika maeneo yao kwa ajili ya kutafuta maji. Pia kuna rekodi sehemu mbalimbali za dunia kuhusu binadamu walioliwa na mamba. Mamba ni miongoni mwa wanyama wa kale na wataalamu wanatofautiana kuhusu umri wao.

Baadhi ya wataalamu hao wanadai mamba wamekuwepo kwa zaidi ya miaka milioni 200 lakini hawakuwa kama mijusi mikubwa zaidi maarufu kwa jina la dinosania ambayo waliishi miaka milioni 230 kisha kutoweka miaka milioni 65 iliyopita. Inadaiwa kuwa mamba wamepona na kunusurika katika matukio mengi ambayo yangeweza kusababisha kutoweka.

Wataalamu wa masuala ya viumbe wanasema mamba ni miongoni mwa wanyama wenye mfumo wa kipekee wa maumbile tofauti na aina nyingine ya wanyama jamii ya mijusi. Mamba wana ubongo wa mbele; moyo wenye vyumba vinne, sehemu ya fumbatio inayofanya kazi kama diaframu kwa msaada wa misuli inayotumiwa kumuwezesha kuogelea na kupumua akiwa kwenye maji.

Muonekano wao wa nje unaendana na maisha yao ya kila siku kwa kuwa hata mtu asiyekuwa na elimu ya viumbe akimuona mamba kwa mara ya kwanza atatambua kuwa ni kundi la wanyama wawindaji hodari. Wana umbo lililochongoka linalowawezesha kuogelea vizuri mamba hubana miguu yao kwenye pande zao wakati wakiogelea, na huongeza mwendokasi wao kwa kupunguza ukinzani wa maji.

Miguu yao mifupi, japokuwa haitumiki kupiga kasia wawepo kwenye maji, lakini huwasaidia sana katika kukata kona za haraka na miondoko ya ghafla kwenye maji au kuanzisha mwendo. Mamba wana tishu ngumu, ndani na mwishoni mwa vinywa vyao. Tishu hiyo huzuia maji yasipite.

Wana pua zenye matundu yenye uwezo wa kujifunga wakati wa kuzama majini na kujifungua wanapotoa kichwa nje au anapokuwa nchi kavu. Ingawa katika uumbaji wamependelewa baadhi ya mambo, ulimi wa mamba umeshikwa na tishu hivyo hawawezi kutoa ulimi nje. Pia mfumo wa memo yao unawazuia kutafuna hivyo hulazimika kumeza chakula chote bila kutafuna.

Meno ya mamba yamechongoka vizuri na taya zenye misuli yenye nguvu hivyo kumuwezesha kukamata kitoweo chake kwa nguvu kisha kufunga mdomo kwa haraka na kwa kutumia nguvu kisha kukaa muda mrefu bila kufungua kinywa ili kuzuia adui huyo kupata hewa au kujinasua kutoka midomo ya mamba.

Mamba ni wanyama wawindaji na wanatabia ya kushambulia kwa kushitukiza. Husubiri mawindo, samaki au wanyama wengine wa nchi kavu wasogee karibu na kisha kufanya shambulizi la ghafla. Kwa kuwa wako kwenye kundi la wanyama wenye damu baridi wanaoishi kwa kula nyama, mfumo wao wa kumeng’enya chakula hufanya kazi kwa taratibu sana jambo linalomuwezesha kukaa muda mrefu bila kusikia njaa.

Mamba wengi wakubwa humeza mawe ambayo husaidia kusawazisha chakula. Ingawa mamba wanaonekana kuwa ni wataratibu sana mamba ndiyo wanyama wawindaji wa hatari kuliko wote wanaoshi majini. Taarifa za uchunguzi zinasema kuwa kuna aina ya mamba wenye uwezo wa kushambulia hata papa ambaye anasemekana ndio hatari zaidi kuliko wanyama wengine wa baharini.

Mamba ameshikilia rekodi ya mnyama wa kwanza mwenye uwezo wa kufunga taya kwa nguvu kubwa ili kubana mnyama aliyemkamata. Mnyama wa pili mwenye uwezo huo ni papa akifuatiwa na fisi. Hata hivyo taarifa za kisayansi zinasema taya za midomo ya mamba hufunguliwa kwa seti ya misuli laini na dhaifu.

Jambo hilo huwawezesha watu wenye uzoefu na mamba kuwafungua midomo yao kwa kutumia uzi au hata kamba iliyotengenezwa kwa mpira laini hivyo kujipatia umaarufu kuwa wanamiujiza ya kiuchawi kumbe jambo hilo linatokana na udhaifu asili katika maumbile ya mamba.

Ingawa mamba ni hatari inaelezwa kuwa akiwa ameshiba anaweza kuchezewa hata na watoto kwa kumfungua mdomo kwa kutumia uzi na kisha kumpanda mithili ya punda. Hivyo basi mamba wanaweza kutumika kwa masomo au safari kwa kufunga tu taya zao kwa hata mipira laini. Mamba pia wana uwezo mdogo wa kugeuza shingo yao upande mpaka upande.

Magamba ya mamba yanaaminika kuwa na matundu yenye uwezo wa kuhisi. Matundu hayo yapo kwenye taya zao za juu na za chini. Inaelezwa kuwa matundu hayo ni ya kutolea taka mwili kwa sababu hutoa jasho mithili ya mafuta ambayo hutumika kuondosha matope katika mwili. Mamba wana kasi sana katika mwendo mfupi akiwa majini na hata nchi kavu.

Mamba ana sifa ya kipekee ya kuwa na upekee maarufu kwa mamba ni ule wa mahusiano yake na ndege aina ya kitwitwi wa Misri. Ndege huyo huonekana kuwa ana mahusiano tegemezi ya kibaiolojia na mamba. Kulingana na taarifa zisizoaminika, ndege hao hula wadudu kutoka kwenye kinywa cha mamba, na mamba huachama mdomo wake ili kuwaacha ndege hao wasafishe mdomo wake.

Ingawa mamba wanasura zilizojawa na husuni kutokana na macho yao kujaa machozi mara kwa mara, inadaiwa kuwa ni miongoni mwa wanyama wenye mahaba na wanaofurahia tendo la kujamiiana. Suala la kujamiiana linatofautiana kulingana na aina ya mamba. Kitendo cha kujamiiana hufanyika majini. Jike anapokuwa katika kipindi cha joto huwa na rangi ya kuvutia dume.

Dume naye hupita kwa mbwembwe na kutoa sauti yenye mvuto ili jike aweze kumfuata. Pia dume hunyoosha mwili wake na wakati anajinyoosha mwili huo hutoa mtisisimko ambao hufanya mwili wa jike kusisimka. Dume na jike wanapokaribiana hupapasana kwenye shingo na mgongoni kisha kuingia kwenye mashindano ya kuogelea kwa mbwembwe zilizochanganyika na mahaba jambo ambalo wataalamu wanaliita onesho la mahaba ya mamba.

Wakimaliza onesho hupumzika huku wakipapasana na hapo jike hulegea na hunyoosha mwili wake kuashiria kuwa yupo tayari kupandwa. Kitendo cha kujamiiana kuchukua dakika 10 hadi 15. Kuna mamba ambao madume kupanda majike mengi kadiri wawezavyo na hii hutegemea uhodari wa wake wa kushawishi jike, pia nguvu za kiume.

Aina hii ya mamba wanapatikana sehemu nyingi ikiwa ni pamoja na Afrika. Katika mfumo huo madume huweka mipaka ya himaya yake yenye idadi ya majike mengi. Baadhi ya utafiti zinaonesha kuwa huko Marekani kuna aina ya mamba ambao kila dume huwa na uhusiano na jike moja tu. Pia kuna aina ya mamba ambao jike hupandwa na madume mengi.

Jike anayepandwa na madume mengi ana uwezo wa kupokea mbegu za kiume kutoka kwa madume watatu katika uzao mmoja. Hii inamaanisha kuwa anaweza kutaga mayai yanayotokana na madume matatu tofauti na baada ya mayai hayo kuanguliwa kila mamba dume huweza hutambua mtoto wake bila kukosea.

Mamba dume ambao hugombea jike huwa na onesho maalum la kuogelea ambapo jike hutazama kisha huchagua dume lililoonesha umahiri zaidi katika kuogelea kwa mbwembwe na mahaba. Jike hupokea dume huyo kwa mahaba makubwa ambapo dume hutoa sauti ya furaha kuashiria ushindi.

Pia wapo mamba ambao madume hupigana na mshindi huchukua mamlaka ya kuweka mpaka wa himaya yenye majike ambayo ni mali yake. Kama ilivyo kwa mamba wengine, dume anayepata ushindi humpapasa jike na kumtekenya hadi atakapokuwa tayari kupandwa.

Inadaiwa kuwa katika mfumo huo wa kugombea jike, dume anayekuwa wa kwanza moja hujiamini kupanda jike hujawa na furaha kwa kujipatia fursa ya uhakika ya kupata kizazi ikilinganishwa na madume mengine. Taarifa za utafiti wa kibailojia juu ya mamba zinasema ukubwa wa mwili wa mamba sio wingi wa mbegu za kiume kwa kuwa hata mamba wa mwisho kupanda jike huweza kuwa na watoto wengi kuliko dume wa kwanza.

Mamba jike hutengeneza kiota chake ndani ya mwenzi mmoja baada ya kupandwa. Kiota hutengenezwa kwenye mapango au kwa kuchimba shimo kando ya maji sehemu yenye kichaka ambao adui hawawezi kuona kwa urahisi. Kiota kimoja kinaweza kuwa na mayai kati ya manne hadi 15 kulingana na aina ya mamba.

Baadhi ya mamba huchangia kiota kimoja na wengine huweka viota vyao karibu karibu. Joto lililopo kwenye kiota ndio husaidia kutabiri jinsia ya watoto wa mamba watakavyoanguliwa. Dume huanguliwa kwa joto la juu zaidi ikilinganishwa na joto linalohitajika kuangua mama jike.

Kwa kawaida dume huanguliwa kwa juzi joto zaidi ya 32 wakati jike kuanguliwa kwenye kiota chenye nyuzi joto chini ya 31. Kiota chenye joto linalobadilika badilika huangua mamba jike na dume ila wakati mwingine watoto wa jinsi moja huweza kuanguliwa. Mayai ya mamba huanguliwa baada ya miezi miwili hadi mitatu kulinganisha na aina ya mamba, watoto wote kuanguliwa katika usiku mmoja.

Mamba hukaa karibu na kiota ili kuchunga mayai yasichukuliwe na husaidia watoto wakati wa kuanguliwa kisha kuwapeba na mdogo na kuwahamishia majini. Watoto wa mamba hukaa chini ya uangalizi wa wazazi kwa miezi mitano hadi miaka miwili kulingana na aina ya mamba.

Mamba huanza maisha ya ushirikiano kwa kufanya mawasiliano hata kabla ya kuiona dunia. Watafiti wa maisha na mwenendo wa mamba wanasema wanyama hao huanza kufanya mawasiliano hata kabla ya kuanguliwa ambapo yai la kwanza kutoa mwanga na sauti huku likitingishika. Baada ya muda yai la pili hufanya hivyo hivyo na kitendo hicho huendelea kwa kupokezana hadi yai la mwisho.

Utafiti huo unaonesha kuwa yai la kwanza hufanya mawasiliano na huwa la kwanza kuanguliwa kisha yai la pili hadi la mwisho kitendo kinachosadikiwa kuwa huenda mawasiliano hayo yanaambatana na kushika namba za kuiona dunia katika uzao wao. Mara baada ya kuanguliwa kutoa sauti ya mshtuko kisha kulia kitendo kinachosababisha mamba wengine kujibu kwa nia ya kuwatuliza.

Sauti ya mshtuko hutafsiriwa kuwa ni ya utambulisho wa uwepo wao duniani na kupokelewa na mamba wote hata wale wasiokuwa wa nasaba ya mamba hao wachanga. Watoto wa mamba hukua na kupevuka kwa kuzingatia kipindi ambacho hufikiwa katika umri wa miaka mitano hadi 10 kulingana na urahisi wa kupata chakula cha kutosha.

Hivyo kitendo cha kubalehe kinategemea zaidi kimo kuliko miaka. Mamba jike kupevuka akishafikia urefu wa mita 2.2 hadi 2.5 takribani futi saba hadi nane wakati dume hufikia umri wa kubalehe akiwa urefu mita tatu takribani futi 9.8.

Dume huendelea kukua kwa kipindi cha maisha yake yote. Mamba huishi kwa wastani wa miaka 35 hadi 75 kulingana na aina ya mamba na umri wake hujulikana kutokana na pingili za mifupa yake. Makaya haya yametayarishwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali ya habari vinavyopatikana katika mtandao.

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi