loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Masasi wanavyonufaika na mradi wa upimaji wa viwanja

Kwa kuwekeza katika rasilimali hiyo, wengi wameshanufaika nayo, ikiwa ni pamoja na kupata fursa za mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha nchini. Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilianzisha mradi wa viwanja 20,000 katika miji inayokua kwa kasi ambayo ni pamoja na Dar es Saalam, Mbeya, Mwanza na Arusha.

Hata hivyo, kwa sasa serikali inashirikiana na kampuni binafsi zenye uwezo wa uendeshaji michoro, ulipaji fidia, upimaji na ugawaji kama sehemu ya huduma ya kupima viwanja zaidi kwa ajili ya wananchi. Dhana ni kwamba, viwanja vikishapimwa, mbali na watu kupata nafasi ya kuvimiliki kihalali, kunakuwa na mgawanyo mzuri wa matumizi ya ardhi katika eneo husika.

Katika kuitikia mwito wa huo wa serikali, Makazi Solutions (T) Ltd ni kampuni ambayo imepiga kambi katika Halmashauri ya mji Masasi tayari kuanza kazi ya kupima viwanja kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo. Zoezi hilo la uendelezaji na upangaji wa mji huo, linalenga pia kuuweka katika sura ya kuvutia kwa wageni wanaoingia na kutoka.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Said Suleiman anasema kuwa taratibu za ugawaji wa viwanja katika mji huo zinatakiwa kuzingatia sheria namba 4 ya mwaka 1999 na kanuni zake za mwaka 2001. Anasema bei ya mauzo kwa kiwanja kimoja ni Sh 3,000 kwa kila mita moja ya mraba kwa viwanja vya makazi.

Makazi na biashara anasema ni Sh 3,500, shule za awali Sh 4,000 lakini maeneo ya ibada kwa kila mita moja ya mraba itakuwa ni Sh 3,000. Aidha anasema baada ya fomu za maombi kupitiwa, wananchi watakaokuwa wamepata viwanja watatakiwa kulipia gharama hizo kulingana na mapendekezo na ushauri utakaotolewa na kamati ya kugawa ardhi.

“Kimsingi, taarifa tulizo nazo zinaonesha kwamba wananchi wamefurahia sana kuwepo kwa mradi huu ambao unatoa mwanga wa maisha bora kwa wakazi wa wilaya ya Masasi,” anasema.

Suleiman anasema mpaka sasa kampuni yao imekuwa ikitoa ushirikiano mzuri kwa wananchi wa maeneo husika kwa kuuza maeneo kwa bei ya soko bila ya kuwepo kwa malalamiko yanayotokana na migogoro ya ardhi kama ilivyo kwa makampuni mengine ambayo hushughulika na masuala ya upimaji na uuzaji wa viwanja hapa nchini.

“Nachukua fursa hii kutoa mwito kwa wananchi kutumia fursa hii kujipatia viwanja kwa kupitia mradi huu. Tunategemea mradi huu utatoa mwanga wa mafanikio kwa wananchi na pia kwa Halmashauri ya Mji Masasi na utasaidia kubuni mbinu zaidi za kushirikiana na wadau wenye nia njema kwa maendeleo na upanuzi wa mji,” anasema Suleiman.

Anasema mfumo unaotumiwa na kampuni ya Makazi Solutions katika kufanikisha zoezi la ugawaji na upimaji wa viwanja katika maeneo ya Mailisita-Mtandi na maeneo mengine hapa nchini ambayo tayari kampuni hii imepima viwanja umeungwa mkono na wadau mbalimbali wilayani humo na kwamba hadi sasa zoezi zima linakwenda vizuri.

Akisimulia, Mkurugenzi huyo anasema kuwa zoezi la upimaji na ugawaji wa viwanja wilayani Masasi katika eneo la Mailisita-Mtandi lilianza mapema mwaka huu baada ya kampuni hiyo kuingia mkataba wa upimaji na ugawaji viwanja na Halmashauri ya mji Masasi. Anasema tayari jumla ya wananchi wapatao 100 wameshalipwa fidia ya zaidi ya Sh milioni 190 kwa ajili ya uendelezaji wa viwanja hivyo na lengo ni kupima viwanja zaidi ya 600.

Anasema kuna jumla ya fomu za maombi ya viwanja 500 zinazotolewa kwa kiasi cha Sh 10,000 kila moja na kwamba Halmashauri inatarajia kupata Sh 5,000,000 kutokana na fomu hizo. Kadhalika, anasema halmashauri inatarajia kupata fedha kutokana na malipo ya viwanja hivyo, hatua ambayo itaiwezesha halmashauri hiyo kutekeleza shughuli zake mbalimbali za kuwahudumia wananchi.

Anafafanua kwamba kupitia mradi huo, halmashauri imegharamia huduma ya wataalamu na ushauri na kwamba mradi huu umetoa jumla ya viwanja 600 kwa ajili ya matumizi mbalimbali, ikiwemo viwanja vya makazi.

Mbali na Masasi, Makazi Solution (T) Ltd inaendesha miradi mingi katika mikoa mbalimbali hapa nchini, ikiwa ni pamoja na pamoja na wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani katika eneo la Tengerea ambako jumla ya viwanja 1,000 vinatarajiwa kupatikana.

Eneo lingine linalopimwa viwanja wilayani Mkuranga ni Sotele ambako viwanja 900 vinatarajiwa kupimwa huku eneo la Mkokozi wilayani likitajkiwa kutoa viwanja 2000. Anasema wilaya nyingine ambako Makazi Solutions wanaendesha shughuli zao ni Bagamoyo katika eneo la mboga ambako jumla ya viwanja 2400 vimeshapimwa ili kuyafanya maeneo hayo yawe bora na ya kisasa zaidi.

Mradi mwingine wa kampuni hiyo ni ule wa Mangamba katika manispaa ya Mtwara, umbali wa kilometa nne kutoka mjini ambao una jumla ya viwanja 46 vya makazi, makazi na biashara, viwanda vidogovidogo na viwanda vikubwa.

“Ipo pia miradi tarajali ambayo inatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia sasa ambayo ni mradi wa Masasi awamu ya pili, Muheza na Pangani mkoani Tanga, Arumeru katika mkoa wa Arusha, Mafia mkoani Pwani, pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara,” anasema.

Akizungumzia kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo katika zoezi la upimaji wa viwanja Mkurugenzi huyo anazitaja kuwa ni pamoja na uhaba wa wataalamu wa upimaji viwanja (surveyors), gharama kubwa ya vifaa vya upimaji. Changamoto zingine anasema ni gharama kubwa katika utengenezaji wa miundombinu kama vile barabara kwenye maeneo yaliyopimwa pamoja na ugumu wa upatikanaji wa mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha.

Kuhusu mafanikio, Suleiman anasema kampuni ya Makazi Solution (T) Ltd inaendelea kukua siku hadi siku sambamba na ongezeko la wateja kwani huduma zake zimeonekana kukubalika kwa maana ya kusaidiana na serikali katika kupanga miji iwe ya kisasa zaidi na salama. Pia kampuni inatarajia kufungua matawi mbalimbali hapa nchini ili kufikisha huduma muhimu na kwa haraka kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Bravo Lyapembile, anasema kumekuwa na changamoto nyingi juu ya upimaji na uendelezaji na upangaji miji katika Halmashauri nyingi hapa nchini ambapo maeneo mengi ya miji yamekuwa yakiendelezwa kiholela bila ya kufuata taratibu na kanuni za uendelezaji miji.

Anasema kuwa Halmashauri ya Mji Masasi imepata mbia aliyeonesha nia njema na kukubaliwa kufanya mradi huu, kwa kuwa kampuni hiyo imeonesha kwamba imekuwa ikifanya vizuri katika shughuli za upimaji na ugawaji viwanja katika maeneo ilikopitia. Kizito anasema kupitia mradi huo, halmashauri nyingi zimeshindwa kutoa huduma bora ya upimaji viwanja katika maeneo ya miji sababu kubwa, ikiwa ni ukosefu wa fedha za ulipaji wa fidia kwa wananchi.

Kwa mantiki hiyo, anasema kuingia kwa mradi huu katika Halmashauri ya Mji wa Masasi kutasaidia kuondoa kero hizo sambamba na kuboresha mwonekano wa mji sambamba na matumizi bora ya ardhi. Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kama mchangiaji katika gazeti hili.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimembariki Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea ...

foto
Mwandishi: Clarence Chilumba

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi