loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maswali yanayoulizwa sana kuhusu Mfungo wa Ramadhani

Nia ni ya moyoni mwa mtu na si kutamkishwa na mtu mwingine kama wengi wanavyodhani au kama inavyofanyika katika baadhi ya misikiti wakati wa sala ya Isha. Wanazuoni wengi wanasema nia ya kufunga ipatikane kila siku kabla ya kuingia alfajiri na kwamba hata kujiandaa kwa ajili ya daku kwa lengo la kufunga kesho yake ni nia tosha.

Lakini wapo pia wanaoamini kwamba ukichukulia Ramadhani nzima kama ibada moja basi ukinuia kufunga mwezi mzima tayari ni nia inayotosha pia. Wanazuoni pia wanasema kufunga si kujuzuia na kula na kunywa pekee bali pia kujizuia na machafu kama vile kusengenya, kusema uongo, kutazama maovu na hata kuyaendea.

Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua zaidi. Dua wakati wa kufuturu Swali: Ni dua gani mtu anatakiwa kuleta wakati wa kuanza kula futari.

Kuna wanaosema hadithi inayotaja dua hii ya “Allaahumma laka sumtu wa ‘ala rizqika aftartu” (Ewe Mwenyezi Mungu Mlezi, kwa ajili yako nimefunga na kwa riziki ulionipa ninafungua swaumu ya leo).” JIBU: Kufuturu kwa kuanza na dua hiyo kunatokana na hadithi dhaifu iliyoelezewa na Abu Dawood (2358) kutoka kwa Mu’aadh ibn Zuhrah, ambaye anasema alimsikia Mtume Muhammad (Amani na Rehema za Mwenyezi Mungu Mlezi ziwe juu yake) akisema dua hiyo wakati wa kufuturu.

Hakuna haja ya kutumia dua hii dhaifu kwa sababu kuna ripoti sahihi kutoka kwa Abu Dawood huyo huyo (2357) kutokana na hadith ya Ibn ‘Umar (Mwenyezi Mungu awe na radhi naye) ambaye anasema: Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu Mlezi (Amani na Rehema za Mwenyezi Mungu Mlezi ziwe juu yake) akianza kufuturu alikuwa akisema: “Dhahaba al-zamau’a, wa abtallat al-‘urooq wa thabata al-ajr insha Allah (Kiu imeondoka, mishipa ya damu imejaa, na malipo yatapatikana, kama Mwenyezi Mungu Mlezi atataka).”

(al-Albaani katika Saheeh Abi Dawood). Pili, ni muhimu kwa mtu aliyefunga kuomba dua wakati wote ikiwa ni pamoja na wakati wa kufuturu.

Hii ni kutokana na mapokezi ya Ahmad (8030) kutokana na hadithi ya Abu Hurayrah (Mwenyezi Mungu Mlezi awe radhi naye) ambayo ina meneno mengi lakini inaisha kwa kumkariri Mtume wa Allaah akisema: “Kuna watu watatu ambao dua zao hazirejeshwi (bila kupokelewa na Mwenyezi Mungu Mlezi): kiongozi mwadilifu, mtu aliyefunga swaumu hadi anapofuturu, na maombi ya mtu aliyepotezwa...” Hadithi imepewa daraja la usahihi na Shu’ayb al-Arna’oot katika kitabu cha Tahqeeq al-Musnad.

Hadithi hii pia imepokelewa na al- Tirmidhi (2525) kwa lafdhi tofauti, “… na mtu aliyefunga wakati wa kufuturu…” nayo imepewa daraja la usahihi na al-Albaani katika Saheeh al-Tirmidhi. Kwa mantiki hiyo mfungaji anatakiwa kumuomba sana Mwenyezi Mungu Mlezi amfanye kuwa mtu wa peponi na amuepushe na moto.

Anaweza kumuomba Allaah amsamehe makosa yake pamoja kuomba dua kadhaa zinazokubalika kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Uislamu. Na Mwenyezi Mungu Mlezi ndiye mwenye kujua zaidi.

Vitu vinavyotengua swaumu

SWALI: Ninaomba kujua vitu ambavyo vinaharibu swaumu.

JIBU: Mwenyezi Mungu Mlezi ametupa ibada ya kufunga katika misingi ya busara ya hali ya juu. Anamtaka mja wake afunge lakini katika mazingara ambayo hayatakuwa sababu ya yeye kudhurika lakini mfungaji hatakiwi kufanya kile ambacho kitaharibu funga yake.

Kwa msingi huo, vitu vinavyoharibu/ kubatilisha swaumu vinaweza kugawanyika katika makundi mawili; mosi ni vinavyotoka mwilini kama vile kujitapisha kwa makusudi, kufanya tendo la ndoa mchana wa Ramadhani, kupata damu ya hedhi na kupiga chuku (tiba inayohusisha kutoa damu ama pia inajulikana kama kuumika -blood cupping).

Vitu hivi vinapotoka ndani ya mwili huufanya kuwa dhaifu. Kwa mantiki huyo Mwenyezi Mungu Mlezi amevieleza kama vitu vinavyotengua swaumu (funga) na Mwenyezi Mungu Mlezi hataki mja wake ambaye funga imeshamfanya dhaifu halafu vitu hivi vinavyotoka mwili vizidi kumdhoofisha zaidi.

Aina ya pili ya vitu vinavyoharibu saumu ni vile vinavyoingia kwenye mwili wa binadamu kama vile kula na kunywa. Kama mtu atakula na kunywa hatofikia lengo la kufunga. Rejea Majmoo’ al-Fataawa, 25/248. Mwenyezi Mungu amezungumzia kwa kifupi vitu vinavyofungua saumu pale anaposema (tafsiri yetu): “Hivyo mnaweza kujamiiana nao katika kutafuta kile ambacho Mwenyezi Mungu Mlezi atawajaalia (watoto), pamoja na kunywa hadi uzi mweupe (mwanga wa alfajiri) utakapojitokeza na giza la usiku kutoweka, hapo kamilisheni funga yenu (saumu) hadi giza litakapoingia.”

[al-Baqarah 2:187]

Katika aya hii Mwenyezi Mungu Mlezi ametaja vitu vitatu vinavyotegua saumu; kula, kunywa na kufanya tendo la ndoa. Vitu vingine vinavyotengua saumu vimetajwa na Mtume (Amani na Rehema za Allah ziwe juu yake) kupitia hadithi zake (matamshi, matendo ama yale yaliyofanywa mbele yake akayaridhia ama kuyakataza).

Kwa ushahidi wa Quran na hadithi za Mtume (Amani na Rehema za Allah ziwe juu yake) baadhi ya wanazuoni wametaja mambo saba yanayotengua saumu ambayo ni: kufanya tendo la ndoa mchana wa Ramadhani, kujichua hadi kutoa manii, kupatwa hedhi (kwa akinamama) au damu ya uzazi (nifaas), kula na kunywa, chochote kinachoweza kuchukuliwa kama “kula na kunywa”, kutoa damu kwa njia ya kuumika ama yanayofanana na hayo na kutapika kwa makusudi.

Kufanya tendo la ndoa mchana wa Ramadhani ni kosa kubwa kwa mfungaji. Ufafanuzi wa hili ni mpaka tupu mbili zinapokutana na hata kama mshindo haukutokea, watu hao wanakuwa wametengua funga yao. Licha ya kwamba hawatotakiwa kula isipokuwa kumalizia siku, wanakabiliwa na kufanya kafara kubwa.

Wakati anayefungua kwa sababu sita zilizobaki analipa siku alizokosa peke yake, mwenye kufanya tendo la ndoa na mkewe anatakiwa kulipa kwa kufunga siku 60 au kulisha masikini 60 ama kumwachia mtumwa huru kama anaye.

Ushahidi wa hili unatokana na hadithi ya Abu Hurayrah (Mwenyezi Mungu Mlezi awe na radhi naye) ambaye alisema: Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Amani na Rehema za Allah ziwe juu yake) huku akitweta na kusema, “Nimeangamia, nimeangamia miye, Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mlezi!” Akamuuliza, “Kwa nini umeangamia?” Akasema, “Nimefanya tendo la ndoa na mke wangu (mchana wa )Ramadhani.” Mtume (Amani na Rehema za Allah ziwe juu yake) akamuliza, “Unaweza kucha huru mtumwa?” Akasema, “Hapana.”

Akamuuliza, “Unaweza kufunga kwa miezi miwili inayofuatana?” Akajibu, “Hapana.” Akamuuliza “Unaweza kulisha masikini sitini?” Akasema “Hapana.”… Unaweza kuiona hadithi hii katika al-Bukhaari, 1936 na Muslim, 1111. Ufafanuzi kuhusu kujichua kwa kutumia mkono hadi kufikia mshindo (masturbation) kunaelezwa kuwa, mbali ya kuwa kitendo hicho ni haramu kwa Muislamu, pia kinatengua saumu ya mfungaji.

Ushahidi wa mtu kufungua kwa kufanya kitendo hicho haramu ni kutokana na maeneno ya Mwenyezi Mungu Mlezi katika hadithi qudsi anapomzungumzia mfungaji kwa kusema: “Anaacha chakula chake, kinywaji na matamanio kwa ajili yangu...” (al- Bukhaari hadithi namba 1894 na Muslim, 1151).

Kitendo cha mtu kufikia mshindo (kutoa manii kwa kujichua) kunaingia kwenye eneo la ‘matamanio’ ambayo mwenye kufunga anatakiwa kujizuia nayo. Kwa hiyo anayejichua, tena mwezi wa Ramadhani anapaswa kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu Mlezi na kuacha kula na kunywa lakini siku hiyo anatakiwa kuilipa.

Wanazuoni wanakubaliana kwamba kama ataanza kujichua kisha akaacha bila kufikia mshindo, anapaswa kuleta toba kwa kosa hilo lakini funga yake itakuwa haijatenguka. Mtu aliyefunga anapaswa kujiweka mbali na mambo yanayotamanisha kama vile kutoangalia watu waliovaa nusu uchi, picha za utupu na asikaribishe mawazo yanayoweza kumfanya atamani kufanya tendo la ndoa ama kujichua.

Kuhusu mtu kutokwa na madhii (majimaji ambayo si manii), wanazuoni walio wengi wanakubaliana kwamba hayatengui saumu ya mtu. Kuhusu kifunguzi cha tatu, kula na kunywa, wanazuoni wanafafanua kwamba chochote kitakachofika tumboni kupitia mdomoni kitakuwa kimetengua saumu ya mtu.

Hata Mtume (Amani na rehema za Mwenyezi Mungu Mlezi ziwe juu yake) anasema: “Ingiza maji zaidi ndani ya pua (wakati unashika wudhu), isipokuwa unapokuwa umefunga.” imesimuliwa na al-Tirmidhi, 788. Kama maji yanayofika tumboni kupitia pua yangekuwa hayatngui saumu, Mtume (Amani na rehema za Mwenyezi Mungu Mlezi ziwe juu yake) asingewaambia waliofunga wasizidishe maji ndani ya pua.

Kuhusu yale yanayoingia kwenye kichwa cha habari kula na kunywa yanahusisha mambo yafuatayo: Mosi ni kuongezewa damu kwa mtu ambaye anafunga kama ametokwa na damu kwa wingi kiasi cha kutakiwa kuongezwa damu. Hili linabatilishwa swaumu kwani damu inatokana na chakula na vinywaji. Pili ni kulishwa chakula ama kitu mbadala wa chakula kwa njia ya mpira ama dripu.

(Fatwa ya Shekhe Ibn Uthaymeen katika Majaalis Shahr Ramadhaan uk 70). Sindano haiharibu swaumu Kuhusu sindano ambayo mtu hachomwi kwa ajili ya kuwa mbadala wa chakula ama kinywaji isipokuwa kwa ajili ya tiba ama chanjo, yaani kama vile sinadano ya kutibu malaria ama kuchomwa insulin kwa ajili ya kisukari havitengui saumu hata kama zinachomwa kwenye mishipa ya damu.

Hata hivyo, katika kuwa katika hali ya usalama zaidi inashauri kwamba ni vyema sindano mtu akachoma usiku (Aangalia katika Fataawa Muhammad ibn Ibraaheem, 4/189). Kusafishwa figo (Kidney dialysis) ambapo mgonjwa huongezewa kemikali fulani na sukari wanazuoni wengi wanakubaliana kwamba inatengua swaumu (Angalia katika Fataawa al-Lajnah al-Daa’imah, 10/19).

Kitu cha tano kilichoorodheshwa kutengua swaumu ni kupiga chuku ama kuumika (cupping). Hii inatokana na hadithi ya Mtume (Amani na rehema za Mwenyezi Mungu Mlezi ziwe juu yake) aliyekaririwa akisema: “Mpiga chuku na yule anayefanyiwa tiba hiyo wote funga zao zinabatilika.” (Abu Dawood, 2367; imepewa daraja la usahihi na al-Albaani katika Saheeh Abi Dawood, 2047).

Kutoa damu kunaingia kwenye kichwa cha habari cha kupiga chuku kwa sababu kunahusisha kitu ambacho kinamfanya mfungaji kuwa dhaifu. Kwa mantiki hiyo, haishauriwi kwa mtu ambaye anafunga kutoa damu isipokuwa kama ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya mtu mwingine.

Hilo linapotokea mtoa damu anakuwa ametengua swaumu na atalazimika kulipa siku hiyo (Ibn ‘Uthaymeen, Majaalis Shahr Ramadhaan, uk 71). Lakini kama mtu anapata ugonjwa wa kutokwa na damu puani funga yake haitenguka kwani ni jambo linalomtokea bila yeye kutaka (labda kama itamdhoofisha kwa hali ambayo hawezi kufunga na anahitaji tiba).

Angalia katika Fataawa al-Lajnah al-Daa’imah, 10/264 Kuhusu kutoka damu kwa ajili ya kung’oa jino, kufanyiwa upasuaji, kupima damu ama kupata jeraha na mengine kama hayo hayatengui swaumu kwa sababu hayafanani na kupiga chuku, isipokuwa, kama ilivyosemwa hapo juu, yatakuwa na athari kwa maana ya kumdhoofisha mfungaji. Itaendelea Jumatatu.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments