loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mazingira magumu shuleni yafelisha wengi

Kiashiria hicho kimeelezwa sio kizuri na kuifanya Mamkala ya Elimu ya Mkoa kushauri sheria, kanuni na taratibu zizingatiwe ili kuondoa changamoto hiyo kubwa. Kwa mujibu wa takwimu hizo, wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2011 katika halmashauri zote sita, walikuwa 57,215 na waliohitimu darasa la saba walikuwa 51,775 na wasiohitimu wakiwa 5,440 sawa na asilimia 10.

Mwaka 2012, wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza walikuwa 53,884 na waliohitimu darasa la saba walikuwa ni 47,302 na wasiohitimu walikuwa ni 6,582 sawa na asilimia 12 , wakati mwaka 2013, walioandikishwa walikuwa 52,634 na waliohitimu ni 44,068 , ambapo wasiohitimu ni 8,566 sawa na asilimia 16.

Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Morogoro- Elimu, Wariambora Nkya, kwenye taarifa yake wakati wa uchaguzi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2014 Mkoa wa Morogoro na kwa mujibu wa takwimu ya wanafunzi walioanza darasa la kwanza na kufika darasa la saba na kuandikishwa kufanya mtihani kwa mkoa ni asilimia 85.

Anabainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro wanafunzi walioandikishwa kufanya mtihani lakini hawakufanya kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro kwa mwaka 2013 ni 204, kati ya hao utoro ni 158, wavulana ni 119 na wasichana 39.

Halmashauri nyingine ni Kilosa ikiwa na wanafunzi 175 kati ya hao watoro ni 141 , wavulana 82 na wasichana 59, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero wanafunzi 165 , kati ya hao watoro ni 153 , wakiwemo wavulana 95 na wasichana 58.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala Msaidizi Mkoa – Elimu, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ilikuwa na wanafunzi 100 kati ya hao watoro ni 79, wakiwemo wavulana 42 na wasichana 37, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga wanafunzi 67 kati ya hao watoro 58 , wavulana 28 na wasichana 30.

Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, pamoja na shule nyingi kuwa na miundombinu duni, ilikuwa na wanafunzi wasiofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2013 ni 57 kati ya hao 53 wakiwa ni watoro ambao wavulana 33 na wasichana 20 , na ugonjwa wakiwa wawili.

Hata hivyo anasema, takwimu zinaonesha kuwa pamoja na utoro kuwa ni changamoto kubwa mwaka 2012, mwaka 2013 wanafunzi watoro wamepungua kutoka 1,327 hadi 642 mwaka 2013 sawa na asilimia 14. Pia anasema, wanafunzi wenye mimba wamepungua kutoka wanafunzi 22 mwaka 2012 hadi 20 kwa mwaka 2013, vifo kutoka wanafunzi 43 mwaka 2012 hadi 30 mwaka 2013.

“Tunawapongeza wadau wote wa elimu kwa kusimamia na kudhibiti utoro na mimba katika shule zote, juhudi hizi ziwe endelevu,” anasema Nkya. “Utoro na mimba ni masuala ambayo yanatakiwa mikakati ya pekee ili kuondokana na changamoto hizo mbili, elimu na ushauri itolewe kwa wazazi, walezi, wanafunzi na jamii kwa ujumla katika kupiga vita hali hii,” amesisitiza.

Pia amewasisitizia wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya kuweka utaratibu wa wanafunzi kupata chakula cha mchana shuleni ili kusaidia kupunguza utoro, kuvuta usikivu darasani na kujenga afya za wanafunzi.

Moja ya mambo ambayo ni vyema Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo ni kuzifanyia kazi kwa haraka changamoto hizo ambazo ni pamoja na walimu waliopo kwenye mazingira magumu kupewa motisha kama vivutio vya kubaki na kufanya kazi katika mazingira hayo.

Katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2013, kati ya wanafunzi 44,068 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huo , ni wanafunzi 21,976 walifaulu , wakiwemo wavulana 10,669 na wasichana 11,307 , ufaulu huo ni sawa na asilimia 50.

Halmashauri tatu za Wilaya ziliongoza kwa kufanya vuziri ambazo ni Manispaa ya Morogoro iliyoshika nafasi ya kwanza kwa kufaulisha wanafunzi kwa asilimia 74, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ikishika nafasi ya pili kwa kufaulisha asilimia 60.2 ya wanafunzi na Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga ikishika nafasi ya tatu kwa kufaulisha asilimia 60.

Katika matokeo hayo shule 52 zilifaulisha wanafunzi kwa asilimia 100 , ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kushika nafasi ya pili, kwa shule zake 14 zilifaulisha wanafunzi wote ikitanguliwa na Manispaa ya Morogoro ikiwa na shule 17.

Kutokana na matokeo hayo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Uongozi wa Halmashauri, Serikali ya Wilaya zimechukua hatua mbalimbali za kuweza kukabiliana na changamoto zinazoweza kurudisha nyuma maendeleo ya elimu ya msingi na sekondari. Pamoja na Uongozi wa Halmashauri na Serikali ya wilaya kujipanga kukabiliana na changamoto za sekta ya elimu, pia baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yamejitokeza kuipiga jeki Halmashauri ili kuboresha viwango vya elimu.

Miongoni mwake ni Shirika lisilo la kiserikali la ROOM TO READ la nchini Marekani ambalo limetumia zaidi ya Shilingi bilioni moja kukamilisha ujenzi wa vyumba 60 vya madarasa ya kisasa Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kinda, Tarafa ya Mvomero wakisiliza jambo huku baadhi ya katika shule za msingi 15 wilayani Mvomero.

Licha ya Shirika hilo kutoa fedha, wananchi wa maeneo yaliyojengwa vyumba vya madarasa hayo walijitokeza kuchangia kiasi cha Shilingi milioni 91.5. Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo ambalo linashughulika na ujenzi wa madarasa hayo, Theodory Mwalongo, amekabidhi hivi karibuni vyumba vya madarasa yaliyojengwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo kwa kutambua umuhimu wa elimu, lilifikia uamuzi wa kujenga vyumba vya madarasa kuanzia Desemba, 2012, na tayari umekamilisha vyumba vya madarasa 45 na vyumba vya maktaba 15.

“Lengo la shirika ni kuboresha miundombinu ya shule ya kujifunzia na kufundishia na kwamba shule 15 zilizopo katika wilaya hiyo zimenufaika na mradi wa kuboresha miundombinu na upatikanaji wa elimu bora,” anasema na kuongeza. “Shule hizi 15 zimejengewa vyumba vya madarasa na maktaba chini ya mradi unaoendeshwa na shirika hili,” anabainisha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo.

Mbali na kujenga vyumba vya madarasa, shirika pia limechapisha vitabu 25,000 vya hadithi na kuwekwa kwenye maktaba za shule ili vianze kutumiwa na wanafunzi. Shirika hilo pia limeanzisha mradi wa kuwasaidia wasichana kumaliza elimu ya sekondari unaotekelezwa katika shule tatu za Diongoya, Nasoro Seif na Mziha zilizopo wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero alipokea vyumba vya madarasa hivyo na kulipongeza shirika hilo kwa kutoa msaada huo unaolenga kuboresha elimu kwa wanafunzi wa wilaya na kuzitaka shule zilizobahatika kupata mradi wa ujenzi wa madarasa na maktaba hazina budi kuyatunza.

Walimu Wakuu wa Shule za Msingi zilizonufaika na mradi huo kupitia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja ,Tiba Yahaya, amelishukuru shirika hilo kwa kuona matatizo yanayozikabili shule za msingi katika wilaya hiyo.

“Shule nyingi za wilaya hii zinachangamoto mbalimbali na zinazotofautiana na pia mahitaji yasiyolingana lakini tunashukuru kwa jambo hili jema,” anasema Mwalimu Mkuu huyo.

Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makalla, ameahidi kufanya kila liwezekanalo katika shule za msingi zilizopo kwenye hali duni na mazingira magumu ya kufundishia zitapewa kipaumbele cha kwanza ili kuinua ubora wa elimu kwa wanafunzi pamoja na mazingira mazuri ya kuishi walimu.

Makalla ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Maji, amezitaja baadhi ya shule zilizopo katika hali duni na mazingira magumu ni za vijiji vya Kinda, Kisimaguru, Mndela na Masalawe. Mbunge huyo amesema hayo hivi karibuni, wakati akizungumzia mkakati wa kuboresha elimu ya msingi hasa kwenye shule duni zilizopo kwenye maeneo yenye mazingira magumu ya kutofikika kwa urahisi.

Hata hivyo anazielezea kuwa shule hizo baadhi wanafunzi wake wamekuwa wakiketi chini kwa ukosefu wa madawati, uhaba wa vyumba vya madarasa, walimu wachache licha ya shule hizo kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi.

“Nimezitembelea shule za msingi zilizo kwenye hali duni na mazingira magumu na baadhi nimezisaidia vifaa kama madawati, pia hazina vyumba vya kutosha vya madarasa,” anasema. “Baadhi ya shule hizi ikiwemo ya Kinda, kuliona dawati ni msamiati, wanafunzi wanakaa chini, hazifikiki kwa urahisi, lakini ninashukuru zote nimezitembelea na kujionea mwenyewe nini mahitaji yao,” anasema mbunge huyo.

Hata hivyo anasema, ili kuweza kuleta mafanikio ya maendeleo katika shule hizo, juhudi za pamoja zinahitajika kati ya wananchi wa vijiji hivyo kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji, kata, tarafa, madiwani pamoja na mbunge na serikali ya wilaya katika kusukuma maendeleo ikiwemo ya sekta ya elimu na afya.

Hata hivyo juhudi za kuboresha elimu ya msingi na sekondari zimeshirikisha upatikanaji wa maji safi na salama ambapo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji kwenye vijiji 10 wilayani humo shule zake zitapatiwa maji ya visima ama ya bomba. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Wallace Karia, amesema hayo , alipoelezea mkakati wa utekelezaji wa miradi ya maji na programu mbalimbali za miradi ya maji wilayani humo.

Hivyo anasema, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaochangia katika mfuko wa mpango wa maendeleo ya sekta ya maji inajenga na itajenga mradi wa maji katika vijiji 10. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo anavitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Hoza/Salawe, Doma, Bumu, Bunduki, Kigugu, Mlumbilo, Mlali, Kipera, Melela na Kwa Doli.

“Faida ya mradi huu ni nyingi kwa wananchi wa vijiji husika ni kuboresha kipato cha wananchi kwa kutumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi badala ya kutumia muda huo kutafuta maji safi na salama,” anasema . Hata hivyo anasema, ni kujenga mazingira mazuri ya mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari ya kuwa na muda mwingi wa kujisomea badala ya kuutumia kutafuta maji atokapo shuleni.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwa Doli , Tarafa ya Turiani wilayani Mvomero, Mganga Msemwa , anasema mradi wa maji vijijini umeinufaisha shule yake kwa kuwekewa bomba la maji na kujengewa vyoo bora.

“Katika uboreshaji wa sekta ya elimu, mradi wa maji uliokamilishwa hapa kijijiji umesaidia mambo mengi kama kujengewa vyoo na bomba la maji na kupunguza utoro wa wanafunzi kukacha masomo,” anasema.

Naye Msimamizi wa mradi wa ujenzi wa maji katika kijiji cha Kwa Doli, Stephen Kisse, anasema mradi wa maji umeenda sambamba na Shule ya Kwa Doli kujengewa vyoo vya kisasa matundu sita kati ya hayo matatu ni kwa wavulana na mengine wasichana pamoja na sehemu ya kujisaidia haja ndogo kwa wavulana.

“Mradi wa ujenzi wa maji umehusisha kwa kiasi kikubwa ujenzi wa vyoo na unatekelezwa kwenye vijiji 10 kiwilaya,“ anasema msimamizi huyo. Tayari bomba za maji zimetandazwa shuleni hapo tayari kwa matumizi ya wanafunzi, na pia mradi unaendelea kujenga choo cha walimu wa shule hiyo.

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Godwin ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi