loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mbeya City yahofu joto Sudan

Mbeya City yahofu joto Sudan

Ufinyu wa muda kwa ajili ya maandalizi ndiyo unaosababisha timu hiyo kutokwenda katika maeneo ya joto kufanya maandalizi ya michuano hayo yatakayofanyika kuanzia Mei 25, mwaka huu nchini Sudan kuliko na kiwango cha juu zaidi cha joto ikilinganishwa na kiwango cha mkoani Mbeya ilikopiga kambi.

Akizungumza na gazeti hili, msemaji wa timu hiyo, Fredy Jackson alisema wachezaji waliingia kambini Jumatatu wiki hii kuanza mazoezi.

Jackson alisema Mbeya City ilipaswa kufanya maandalizi kwa kuweka kambi kwenye maeneo ya joto ili kujiandaa walau kwa kiasi kukabiliana na hali joto iliyopo Sudan, lakini haiwezi kufanya hivyo kutokana na ufinyu wa muda.

“Ikumbukwe kuwa tumepewa taarifa kwa kuchelewa kwa kuwa nafasi hiyo tumeipata kwa upendeleo.

Tunaamini hali joto iliyopo nchini Sudan itakuwa changamoto kwetu, lakini hatuna namna tutakwenda kupambana na tunaamini tutafanya vizuri kwani si timu zote zitakazoshiriki zinatoka katika maeneo yenye joto kali kama ilivyo pale Sudan,” alisema msemaji huyo.

Alisema ufinyu wa muda wa kufanya maandalizi hauwezi kukwamisha kushiriki michuano mikubwa, bali itaheshimu heshima waliyopewa na Cecafa kwa kuwa pia itakuwa nafasi ya kujifunza na kuongeza uzoefu.

Alisema mchezaji Sad Kipanga kuwa pekee ambaye hatoambatana na timu hiyo kwenda Sudan kutokana na uwepo wake katika kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes).

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, vituo vinne vitatumika kwa Kombe la Bonde la Mto Nile ambavyo ni viwili vitakuwa Khartoum, kimoja Port Sudan na kingine mji wa Alshant.

Mbali ya Mbeya City, timu nyingine zitakazoshiriki ni AFC Leopards (Kenya), Victoria University (Uganda), Polisi (Rwanda), Melakia (Sudan Kusini) na El Merreikh, Shandy na El Arab, zote za Sudan.

Timu nyingine ni Elmei (Somalia), Ulinzi (Ethiopia), Arab Contractors na Ismailia kutoka Misri, Polisi (Zanzibar), Ports (Djibouti) na Flambeau kutoka Burundi.

Mshindi wa kwanza atajinyakulia fedha taslimu Dola za Marekani 30,000, mshindi wa pili dola 20,000 na mshindi wa tatu atajishindia dola 10,000.

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Mbeya

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi