loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbinu za wauza nguo za ndani zina ‘viwango’ kuliko za TBS?

Maofisa wa TBS ndio walioendesha operesheni hiyo katika masoko mbalimbali ya mitumba yaliyopo jijini Mbeya huku jeshi la polisi na wawakilishi wa vyombo vya habari pia wakishuhudia operesheni hiyo. Lakini inaonekana mbinu zilizotumiwa na Shirika la Viwango zilizidiwa ‘viwango’ na zinaendelea kuzidiwa hadi sasa na mbinu za wauza mitumba katika masoko karibu yote ya Mbeya.

Wafanyabiashara walificha nguo hizo wakati wa operesheni yao iliyoendana na kuwakamata wauzaji. Inaonekana hakukuwa na usiri kwa wadau walioshiriki operesheni hiyo kwa maana ya kwamba zoezi lilivuja, wafanyabiashara wakawa na taarifa ya nini kitafanyika na hivyo wakaficha nguo hizo zinazodaiwa kuwa hatari kwa afya za wavaaji.

Wakati wa ukaguzi, taswira ilioonekana ni kwamba wauza mitumba wameshaachana na kuuza nguo hizo. Lakini ukweli ni kwamba baada ya kumalizika kwa operesheni hiyo, wauza mtumba walizirejesha sokoni, tena kwa kasi nguo za ndani ambazo wanaendelea kuziuza kama kawaida hadi nilipokuwa ninaandika makala haya huku wakijigamba kuwa serikali haiwawezi.

Katika operesheni ya TBS ya ‘ghafla’ iliyolenga katika kukamata nguo na wahusika wanaouza chupi za mitumba, sidiria na soksi katika masoko ya Sido na Mwanjelwa, maofisa wa TBS hawakufanikiwa kukamata hata nguo moja katika masoko hayo yaliyo maarufu kwa uuzaji wa nguo za mitumba.

Mahali pekee ambako maofisa hao waliambulia kukamata nguo za ndani za mitumba ni katika soko la Mbalizi. Katika soko hilo maofisa hao walimkamata mfanyabiashara mmoja, Lusekelo Adam akiuza soksi za mtumba na kumfikisha katika ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya na kisha kuteketeza soksi hizo ambazo muuzaji alisema zilikuwa na thamani ya shilingi laki mbili.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa operesheni hiyo, Ofisa wa TBS, Paul Manyirifa alikiri zoezi hilo kufanyika kwa wafanyabiashara wadogo na kusema shirika lao linaamini wapo wafanyabiashara wakubwa ambao ndio huziingiza kwa njia za panya nguo hizo zilizopigwa marufuku na kuwataka waache mara moja na kuzisalimisha kwao.

Kwa upande wake, mwanasheria wa shirika hilo, Baptista Bitao alisema adhabu kwa mtu anayeuza nguo hizo ni kati ya shilingi milioni 50 hadi 100 na kwamba mkurugenzi mkuu wa shirika ana mamlaka ya kutoa adhabu isiyopungua Sh milioni 20 kwa anayekutwa na nguo hizo.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi, aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kina katika kukamata nguo hizo akisema lengo ni kuona watanzania hawawi watu wa kupokea vitu vitakavyolisababishia hasara taifa lao kwa kuingia gharama ya kutibu maradhi yatokanayo na nguo hizo, hususan maradhi ya ngozi.

Kinachoweza kusemwa ni kwamba rasilimali zilizotumika katika zoezi zima hazikuzaa matunda kwani ninaandika makala haya nikiwa na uhakika kuwa nguo hizo hatari bado zinauzwa jijini Mbeya na huenda ni kwa kasi kubwa tofauti na awali.

Ni vyema kukiri kuwa mipango ya kuendesha operesheni hii katika miji mbalimbali nchini haikuwekwa katika kiwango chenye kuleta tija kwa walipa kodi ambao ndiyo hasa operesheni ililenga kuokoa afya zao dhidi ya magonjwa yanayoweza kuwaambukiza kupitia nguo za ndani.

Nijuavyo mimi, operesheni yoyote inapoendeshwa ni vyema ikawekewa mikakati madhubuti inayoanza kwa uchunguzi wa kina juu ya ukubwa wa tatizo na maeneo hatarishi zaidi. Hii husaidia wakati wa operesheni wahusika kwenda moja kwa moja wakiwa wanajua ni lazima bidhaa husika itakutwa sehemu fulani na kama haitokuwa mahala hapo inatakiwa pia kujua ni wapi wahusika wanaweza wakawa wameficha mali zinazotafutwa.

Kadhalika ufuatiliaji na zoezi la kushitukiza linapaswa kufanywa baada ya muda mfupi, zoezi ambalo halionekani kufanywa. Baada ya maofisa wa TBS kukosa nguo hizo katika meza na vibanda vya wauza mitumba hawakuwa na njia mbadala, walikamilisha zoezi wakiamini kwamba pengine wakazi wa Mbeya ni waelewa wasiouza wala kuvaa nguo za ndani za mtumba. Ukweli ni kinyume chake.

Ninachotaka kusema pia ni kwamba oparesheni nzuri, licha ya kuwa na muda maalumu wa utekelezwaji wake ni vyema pia ikawa endelevu ili kukomesha jambo husika lisijirudie tena. Pamoja na kamanda wa polisi, Ahmed Msangi kuahidi kutoa ushirikiano kwa TBS kwa kuhakikisha wale watakaokutwa wakiuza ama kununua nguo zilizopigwa marufuku wanakamatwa, hali ni tofauti na ahadi hiyo.

Hii ni kutokana na ukweli kamba nguo hizo zilirejeshwa sokoni mara tu baada ya maofisa kuondoka katika masoko yaliyofikiwa na uchunguzi wangu unaonesha kwamba hadi ninaandika makala haya uuzaji wa chupi za mitumba, sidiria na soksi unaendelea kama kawaida.

Ukipita katika masoko na magulio mengi yanayofanyika mkoani Mbeya nguo hizi zilizopigwa marufuku zinauzwa, tena sehemu za wazi na wateja wanapita na kuchagua watakavyo. Magulio ambayo hufanyika kila siku za Jumapili katika eneo la Uyole nia kati ya yanaoongoza kwa kuwa na nguo hizi.

Si kwamba wauzaji hawajui kama zimepigwa marufuku, wanachoangalia wao ni uelewa mdogo wa wavaaji ambao bado wanaonesha kuzihitaji kwa kutojua athari zake na hasa kwa vile zinauzwa bei ya chini kulinganisha na bidhaa mpya za aina hiyo.

Wapo wananchi wachache wanaojua serikali imepiga marufuku nguo hizo lakini hawajui kwa kina ni kwa sababu gani hasa na hivyo wanadhani hawatendewi haki kwa vile zinawafaa walalahoi kwa upande wa bei na wakati mwingine wanaona kama hilo ni agizo la mpito tu.

Juzi nilikutana na mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mwama Simwela akitokea katika moja ya hospitali binafsi zilizopo jijini hapa alikokwenda kuonana na daktari kutokana na maradhi ya kutokwa vipele vingi katika matiti yake yote mawili. Simwela aliniambia kwamba anatokwa na vipele hivyo vilivyokuwa vikimwasha sana na kwamba alivipata mara baada tu ya kuvaa sidiria ya mtumba aliyoinunua hivi karibuni katika soko la Sido.

Inaonekana alinunua sidiria hiyo baada ya zoezi la TBS kumalizika! Anasema anaamini kuwa aliambukizwa ugonjwa huo kutoka katika nguo hiyo kwa kuwa hakuwahi kuwa na tatizo hilo maishani mwake kabla ya kuvaa sidiria hiyo.

Simwela anakiri kuwa hakuwa na taarifa sahihi kuhusu upigwaji marufuku wa nguo hizo za mitumba wala madhara yake lakini sasa anaamini kwamba wapo watu wengi ambao hujikuta wakiwa na maambukizi mbalimbali hususani sehemu za siri kutokana na kuvaa nguo za ndani za mtumba.

“Wengine hupata maambukizi lakini wasijue kama yametokana na wao kuvaa nguo hizi. Ni wachache sana wanaoweza kuamini kama mimi kuwa nguo niliyovaa ndiyo iliyoniletea ugonjwa huu. Inawezekana kabisa kuwa mtu aliyekuwa akiivaa sidiria niliyonuanua alikuwa na ugonjwa wa ngozi,” anasema Simwela ambaye kimsingi ndiye chanzo cha kunifanya nikaamua kuandika makala haya.

Mmoja wa wauzaji wa nguo hizo ambaye huuza kwa kupita maofisini aliyeomba kutoandikwa jina lake gazetini anasema wanunuzi wake wengi anaowauzia nguo hizo za ndani za mtumba wana uelewa wa kutosha. Yeye anaamini kuwa kama watu walio na uelewa kama hao wanaendelea kununua chupi na sidiria za mitumba, watu wa kawaida wataendelea kununua sana alimradi kama bidhaa hizo zitaendelea kupatikana sokoni.

“Mimi nawapekelea maofisini na wananunua. Imefika mahali mpaka natambua na saizi za nguo wanazovaa kwani ni wateja wangu wa muda mrefu. Sasa ukinambia zina madhara kwa wavaaji ni lazima hawa waelewa wangeacha kununua. Na wanazipenda kwa kuwa ni imara zaidi ya zile zinazouzwa madukani zikitokea viwandani sisi tunaita special,” anasema muuzaji huyo ambaye ni mwanamke pia na anaamini kwamba hazina madhara kama serikali inavyodai.

Hii inaonesha kwamba elimu kuhusu madhara ya nguo hizi za mitumba za ndani haijatolewa ipasavyo na hivyo TBS wanapaswa kutambua kuwa bado wana kazi kubwa ya kutoa elimu juu ya athari za uvaaji nguo hizi. Hatua hii inapaswa kwenda sambamba na kuwakamata wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza nguo hizo, iwe kwa njia ya panya au bandarini kwa kutoa rushwa.

Ni wakati wa TBS kuonesha kuwa imejipanga vyema kuhakikisha biashara ya nguo za ndani za mtumba inakomeshwa nchini na si kupapasa kwa kufanya operesheni zisizo na tija ambazo bila shaka zinaandamana pia na kula posho.

Biashara ya uuzaji mtumba si tembo aishie msituni ambaye operesheni ya kuzuia kuuawa kwake ni lazima zifanyike msituni ambako kumwona jangili inaweza kuwa kazi. Nguo za ndani za mitumba zinauzwa mchana kweupe na kwenye maeneo ya wazi tena yanayofikika kirahisi na watu wengi.

Niseme tu kwamba TBS na Polisi hawajajipanga vyema katika kukomesha hili na kama wanataka kuonesha dhamira yao basi wajipange upya.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi