loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbio za mwenge ni chachu ya maendeleo

Huu ni mwaka wa 22 tangu mbio za mwenge zirejeshwe serikalini na hivyo kuwashirikisha Watanzania wote bila kujali itikadi zao katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa sekta ambazo maendeleo yake yameendelea kuchochewa na mbio za mwenge ni pamoja na afya, elimu, maji, kilimo, mifugo, ujenzi wa miundombinu ya barabara, ushirika, maliasili na mazingira.

Mbio hizo pia zimekuwa zikijielekeza kwenye uimarishwaji wa utawala bora, ulinzi na usalama, mawasiliano, viwanda na biashara sambamba na matumizi endelevu ya ardhi. Mkoa wa Morogoro ulipokea Mwenge huo wa Uhuru Juni 17 mwaka ukitokea mkoani Dodoma na kisha ukakimbizwa ndani ya halmashauri saba zilizipo katika wilaya sita za mkoa wa Iringa kabla ya kukabidhiwa mkoani Iringa Juni 24, mwaka huu.

Ukiwa mkoani Morogoro ulikokimbizwa kwa muda wa siku saba, wananchi, viongozi wa serikali na wa vyama vya siasa wakiwemo wa upinzani walijitokeza kushiriki kila ulikokuwa unapitia na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo. Kutokana na hilo, lugha sahihi ya kusema ni kwamba katika halmashauri saba ulikopita, Mwenge umefufua matumaini mpaya ya upatikanaji wa huduma bora za kijamii.

Huduma za afya Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ambako ulizindua miradi 10, baadhi ya wafadhili mbalimbali walijitokeza katika kuchangia fedha za miradi hiyo na bila shaka mwenge utaendelea kuhamasisha wengine.

Miongoni mwao ni Lions Club kutoka nchini Sweden ambao wamejenga jengo la kisasa la upasuaji katika kituo cha Afya cha Tawa, hatua ambayo itawaondolea adha wananchi hasa wanawake wajawazito wakati wa kujifungua.

Jengo hilo la upasuaji ambalo lilizinduliwa na Mbio za Mwenge limegharimu Sh milioni 182.1. Kati ya fedha hizo, Sh milioni 110.8 zimechangwa na Lions Club, Sh milioni 28 Serikali kuu, Sh milioni 43 halmashauri ya wilaya huku wananchi wakichangia Sh 300,000.

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Tawa, Nuhu Muwinge anasema kwenye taarifa yake mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Rachel Kassanda, ambaye pia alifungua jengo hilo, kwamba huduma ya upasuaji zinazotolewa baada ya kukamilika kwa jengo hilo zitapunguza sana vifo vya akinamama na watoto.

Kata ya Tawa ina jumla ya watu 11,912 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, kati ya hao wanaume ni 5,358 na wanawake 5,661. “Tumeanza kutoa huduma upasuaji kwa akina mama wajawazito. Huduma nyingine zinazotolewa ni upimaji macho, na magonjwa mengine yakiwemo mabusha na hernia,” anasema Mganga wa Kituo hicho cha Afya.

Nao baadhi ya wakazi wa Kata ya Tawa, kwa nyakati tofauti wameipongeza serikali, halmashauri na hasa wafadhili wa Lions Club kwa kuwezesha ujenzi wa jengo hilo la upasuaji katika Kituo hicho cha Afya. Christina Makonde, anasema uhakika wa kufanyika kwa upasuaji kwa wanaopatwa na matatizo, hasa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua, ni jambo la kupongezwa sana kwani litaokoa wengi.

“Kabla ya ujenzi wa wodi hii ya upasuaji, watu waliokuwa na matatizo na kuhitaji upasaji walikuwa wakisafirishwa umbali mrefu kwenda Hospitali ya Rufaa iliyopo Mjini Morogoro, kwa gharama kubwa na wanaoshindwa gharama ilikuwa ni hatari sana kwao hata kupoteza maisha,” anasema Makonde.

Hata hivyo, anasema ili kuboresha zaidi huduma kwa wananchi wa kata hiyo ni wajibu kwa serikali kuongeza wauguzi, kuboresha maabara na kuajiri mfanyakazi wa kufua nguo hasa shuka na kufanya usafi wa mazingira. Mjamzito Joanite Jorvin, baada ya kushindwa kujifugua kwa njia ya kawaida, alifanyiwa upasuaji na kutolewa mtoto akiwa salama ambaye alipewa jina la mzazi wa kiongozi wa mbio hio za mwenge, Stephen.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, moja ya mradi mkubwa uliopitiwa na kuthaminiwa na mbio za mwenge ni ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, anasema watakapopatiwa fedha kwa awamu nyingine na serikali kuu, ujenzi wake umepangwa kukamilishwa ifikapo Januari 2015.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha kiongozi wa mbio za mwenge, Mkuu wa wilaya anasema ujenzi wa hospitali hiyo ni matunda ya serikali ya awamu ya nne iliyojielekeza katika kuboresha huduma za afya ili kupunguza vifo vya watoto na wajawazito. Kaimu Mganga wa Wilaya ya Mvomero, Dk Omary Mbena, katika risala aliyoisoma mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge anasema, wilaya ilikuwa haina hospitali yake.

“Huu ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Nne kuhakikisha kila wilaya inakuwa na hospitali. Lengo ni kuipatia jamii huduma ya afya kwa ukaribu zaidi ili kupunguza vifo ambavyo vingeweza kuepukwa,” anasema Dk Mbena. Kaimu Mganga wa Wilaya hiyo anasema ujenzi umegharimu Sh milioni 353.3, na kwamba kati ya fedha hizo Sh milioni 347.1 ni kutoka Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), na Sh milioni 6.1 ni Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo (LGCDG).

“Hospitali hii kijiografia ipo sehemu ya kati kati ya wilaya na itawapunguzia wagonjwa gharama za kusafiri na ipo maeneo ya barabara kuu iendayo Dar es Salaam na Mwanza ili kuwahudumia kwa haraka watakaopata ajali,” anasema Kaimu Mganga huyo wa wilaya. Wilaya mpya ya Gairo haikuwa nyuma katika kuhakikisha miradi yake saba mingine ikilenga uboreshaji wa huduma za afya kwa ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Kwipipa na kijiji cha Madege inazinduliwa na mbio za mwenge.

Wananchi walianza kupata huduma za matibabu, upimaji wanawake na watoto katika kliniki pamoja na uwepo wa sehemu salama ya kujifungulia wajawatizo baada ya zahanati ya Madege iliyojengwa kwa gharama ya sh milioni 29.3 kuzinduliwa na mbio hizo.

Ujenzi ulianza kutekelezwa mwaka 2008 na ulikamilika Januari mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 inayoelekeza kuwa na zahanati kwa kila kijiji, lengo likiwa ni kusongeza huduma ya afya karibu na wananchi.

Dk Mussa Mayala, anasema kijiji hicho kilikuwa hakina zahanati na kwamba kukamilika kwake na kuanza kutoa huduma kumeharakisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati wote kwa wananchi kwani awali ilikuwa ikipatikana katika makao makuu ya Kata na maeneo mengine.

Huduma za elimu Katika uboreshaji wa sekta ya elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na makazi ya walimu, serikali kwa kushirikisha wananchi wa mkoa pamoja na wafadhili wa ndani na nje ya nchi wamekuwa mstari wa mbele kuongeza chachu ya maendeleo.

Baadhi ya Wafadhili wanaochangia sekta ya elimu wilayani Kilosa ni kutoka Jimbo la Kanisa Katoliki Gaborone nchini Botswana, wakipitia Shirika la Stigma Fathers na Parokia ya Kisanga ambapo wamejenga jengo la hosteli ya wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Kisanga.

Ujenzi wa hosteli unaenda sambamba na nyumba ya mlezi wa wananafunzi na katika hatua ya kwanza ujenzi umegharimu Sh milioni 73. Lengo la kuwajengea hosteli wanafunzi wa kike wanaosoma shule hiyo ni kuwaondolea adha ya kupanga mitaani na kuwaepushia na kupata mimba wakiwa kwenye masomo yao na hata kubakwa.

Paroko wa Parokia ya Kisanga, Padre Harrison Mlenga katika taarifa fupi ya ujenzi wa hosteli hiyo kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru wakati ulipotinga wilayani Kilosa anasema kati ya fedha hizo, wananchi wa kata hiyo wamechangia Sh milioni tatu, wakati wafadhili hao wakichangia Sh milioni 70. “Jengo la hosteli hii itakuwa na vitanda 40 kwa ajili ya wasichana,” anasema.

Kwa mujibu wa Paroko huyo, wafadhili wamesukumwa kutoa msaada wa kujenga hosteli na nyumba ya mlezi baada ya kuona wanafunzi wa wa kike wanaopanga nje ya shule hiyo wakikabiliana na changamoto mbalimbali. Anasema matarajio ni kuongeza hosteli nyingine zaidi za wavulana ili nao wapate nafasi karibu na shule.

Mkakati mwingine unaotekelezwa katika sekta ya elimu ni ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari za kata za masomo ya kemia, fizikia na baolojia ambao unatekelezwa na halmashauri zote za mkoa. Kupitia mbio za mwenge ilidhihirika kwamba halmashauri ya wilaya ya Mvomero, inakamilisha ujenzi wa maabara tatu katika shule za sekondari za Wami na kwa Manispaa ya Morogoro ni katika Sekondari ya Mafiga.

Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero pia inatekeleza mpango huo ikiwemo maabara iliyokamilika katika shule ya Sekondari Mlabani. Lengo la ujenzi wa maabara hizo ni mkakati wa serikali ya awamu ya nne wa kuboresha elimu ili kuinua ufaulu wa wanafunzi kwenye masomo mbalimbali yakiwemo ya sayansi.

Kiongozi wa mbio za mwenge, Kassanda, amekuwa akiwahimiza wanafunzi wa shule za sekondari kujituma na pia kuzitumia vyema maabara hizo ambazo zinajengwa kwa gharama kubwa. “Mpango huu wa ujenzi wa shule za kata ulipoanza wapo waliozibeza na kuzipachika majina tofauti, lakini kila mwaka zimekuwa zikiboreshwa na kasi yake ni nzuri,” anasema kiongozi huyo wa mbio za Mwenge.

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi