loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbio za Urais kwa sasa ni upofu wa kisiasa

Pamoja na kuandika maelezo yake kwa undani kuhusu makundi yanayotaka kuwania Urais 2015 ndani ya CCM yanavyosumbua, lakini pia kuna eneo maelezo ya Naibu Waziri huyo yanaonesha shaka ya utendaji katika mazingira ya kutokuaminiana.

Hali hiyo inaonekana wazi katika mazungumzo yake yanayofanya watu wa kawaida kuanza kujiuliza kulikoni, kwani badala ya kutekeleza sera zilizoifanya ipewe haki ya kutawala, viongozi hao wa CCM wanabaki kuendesha vita binafsi ambayo inaondoa ushirikiano kiutendaji katika mizania halisi.

Hali hii si nzuri na inapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwa kuwa mazingira hayo yanachelea kuleta umimi na huenda hata hujuma ili mradi mtu mwingine aonekane hafanyi kazi zake sawasawa.

Kumekuwapo na mazungumzo na maneno ya kila mara kuhusu uwapo wa makundi hayo na kauli ya Nyalandu ya kuwapo kwa makundi yanayohusishwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta yanaondoa shaka ya maneno ya kichinichini, kwamba kumbe kweli yapo.

Pamoja na maelezo ya Nyalandu ambayo tunaamini ni ya ndani kabisa, tunadhani wakati umefika kwa wahusika kuangalia zaidi mustakabali wa taifa hili kuliko kuendeleza siasa za ndani ambazo zinasababisha kutokuelewana hali ambayo inajenga hali ya kuchanua kwa chuki.

Kuonana wasaliti kunakoelezwa na Nyalandu ni dalili ya kujikita zaidi katika maslahi binafsi ambayo ama hakika hayatajenga taifa hili bali kulibomoa kama hali hiyo haitodhibitiwa.

Sote tunafahamu nguvu walizonazo waliotajwa, katika siasa za nchi hii ; na kutokana na kuelewa huko sisi tunadhani kwamba hawastahili kuendelea na mfumo huo kwani wanahitaji kushirikiana ili kusukuma mbele maendeleo.

Tunaamini kwamba misuguano iliyopo inanyima fursa pana ya wateuliwa wa Rais kuwatumikia wananchi kwa jinsi walivyoapa kwa hofu tu ya kudhani fulani anaweza kunifikiria vibaya.

Tunapenda kuamini kwamba hali ya kisiasa nchini haijawa tete sana pamoja na ukweli kuwa kuna makundi hayo yanayopingana vikali, lakini vitendo vyao vyenye lengo la kuzoroteshana ama kujiimarisha yenyewe kwa yenyewe, ili ifikapo 2015 yawe na nafasi ya kutwaa urais nchini yanatengeneza mauti kwa Watanzania.

Ni kweli kama alivyosema Nyalandu wakati wa sasa si kuwa kubabatizana kwani inaonekana taifa limejaa malalamiko, hisia za kupigana vijembe, kutafutana ubaya na kuoneana kisiasa, shauri baya kabisa katika ukuzaji wa uchumi.

Sisi tunasema ipo haja ya mamlaka zinaohusika kuwajibika kwa kuhakikisha kwamba viongozi wote nchini na hasa vinara wa makundi husika, kuona ni jinsi gani watakaa pamoja na kuijenga nchi na kuwapatia matumaini ya maisha wananchi badala ya kutengeneza hila za mkizi.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi