loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbowe abanwa Polisi kwa saa 4

Katika muda huo, Barabara ya Ghana yalipo makao makuu ya jeshi hilo, hakuna gari lolote lililoruhusiwa kupita, kwani ilifungwa na kuwa chini ya ulinzi mkali.

Wakati Jeshi la Polisi likimhoji kiongozi huyo mkuu wa Chadema nchini, jeshi hilo limefanikiwa kuzima maandamano ya chama hicho, yaliyotarajiwa kuanza nchini kote jana kwa lengo la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba, linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara) ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema Mbowe alifika katika makao makuu hayo ya Polisi kuanzia saa 5:09 asubuhi.

Mnyika alisema katika mahojiano, Mbowe alioneshwa video yenye kauli yake ya kuitisha maandamano na migomo nchi nzima bila kikomo, aliyoitoa hivi karibuni, lakini alikana kuandika maelezo kuhusu kauli ya kuitisha maandamano nchi nzima.

Kuitwa kwa Mbowe makao makuu ya jeshi hilo jana, kulisababisha vurugu mbalimbali kuzunguka makao makuu hayo.

Wafuasi wake na wanahabari walipigwa na wengine kufukuzwa na askari wa Kikosi cha Mbwa, ikielezwa hawakutakiwa kuwepo katika eneo hilo.

Mbowe alifika makao makuu ya Polisi akiwa na msafara wa magari matano, likiwemo la Mnyika na mawakili wake. Gari la Mbowe lilipofika eneo hilo, polisi walimtaka ashukie nje ya geti la kuingia katika ofisi hizo. Wanachama waliojitokeza eneo hilo, walipiga kelele za kutokukubaliana na hatua hiyo.

Polisi waliruhusu gari hilo kuingia huku wengine wote hawakuruhusiwa kuingia. Awali, kabla ya Mbowe hajawasili, walitangulia mawakili Profesa Abdallah Safari ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) na Mabere Marando, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu.

Baada ya Mbowe kuingia ndani, waliwasili Tundu Lissu, John Mallya, Nickson Tufala na Peter Kibatala, ambao walizua tafrani katika lango la Polisi, wakitaka kuingia ndani huku wakikataa kusikia maelekezo. Mvutano huo ulidumu kwa dakika kadhaa.

Kisha filimbi za polisi zilipigwa huku kikosi cha mbwa, kikiwasili na polisi walihamia upande wa wanachama na kutoa taarifa ya ilani, kuwa watoke eneo hilo na kusogea umbali wa mita 200.

Kabla wanachama hao hawajatii amri hiyo, walianza kushambuliwa na polisi, wakitakiwa kuondoka eneo hilo. Mwanachama mmoja wa chama hicho alikamatwa na kuingizwa katika moja ya magari ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), yaliyotanda eneo hilo.

Majira ya saa 7:00, Mnyika alitoka nje na kuzungumza na wanachama na wafuasi wa chama hicho, akieleza kwa kifupi yaliyokuwa yanaendelea katika mahojiano baina ya Mbowe na maofisa wa Polisi.

Alisema Mbowe alihojiwa na kuoneshwa video ya kauli yake aliyoitoa katika Mkutano Mkuu wa Chadema mwishoni mwa wiki, ambapo alisikika akiwataka wana-Chadema kuanza maandamano nchi nzima bila kikomo, kauli zilizotajwa na polisi kuwa ni za kichochezi na hivyo kutakiwa kuandika maelezo.

Hata hivyo, Mnyika alisema muda wote huo, Mbowe akiwa na mawakili sita alikataa kukubaliana na kauli hiyo na pia alikataa kuandika maelezo hayo, badala yake alikubali kuandika maelezo ya kukataa kuandika maelezo ya awali.

Saa 8:45 Lissu alitoka akiwa ameongozana na mawakili wote na kuwafuata wanachama, ambapo aliwaeleza kuwa mahojiano ya Mbowe na Polisi, yamekamilika na kwamba ataachiwa kwa dhamana, hivyo wanachama watawanyike kwa amani.

“Polisi wametuomba tuzungumze na ninyi wanachama na tuwaambie kuwa mtawanyike, kwani Mwenyekiti amemaliza na hawapendi kuona kundi kubwa la watu lenye kuonesha kama kuna maandamano, kwani wanaweza kutumia nguvu,” alisema Lissu.

Aliwataka watawanyike kwa amani, kwa kuwa polisi hawatapenda kuona mtu yeyote anajeruhiwa katika eneo hilo. Baadaye Mbowe aliachiwa kwa dhamana na kutolewa mahali hapo kwa kupitia lango la nyuma la makao makuu ya Polisi, huku akisindikizwa na magari mawili ya Polisi, moja mbele na lingine nyuma.

Maandamano yadhibitiwa Wakati hayo yakitokea Dar es Salaam, Jeshi la Polisi kote nchini limeripotiwa kudhibiti maandamano ya Chadema yaliyokuwa yanatarajiwa kuanza sehemu mbalimbali, kwa lengo la kuitikia wito wa kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba. Hali imetajwa kuwa shwari katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa na Kilimanjaro.

Mkoani Dodoma, udhibiti wa jeshi hilo uliwafanya Chadema kushindwa kuandamana. Hata hivyo, polisi walifanikiwa kukamata gari la chama hicho likiwa na bango lenye maneno ya uchochezi.

Hayo yalithibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula, aliyelitaja gari linaloshikiliwa kuwa ni aina ya Ford Ranger Pick Up, lenye namba za usajili T 792 CAQ.

Pia watu wanne waliokuwa katika gari hilo, wanashikiliwa. Alitaja watu hao kuwa ni Christopher Nyamwanji (52), ambaye ni Mratibu wa Chadema Kanda ya Magharibi, mkazi wa Tabora, Laurent Mangweshi (36), mkazi wa Mpanda, Agnes Stephano (26) mkazi wa Ubungo Maziwa, Dar es Salaam na Elisha Daudi (49), mkazi wa Tabora.

Kamanda alisema gari hilo, lilikuwa na bango lenye maandishi yanayosomeka “Tunapinga ufisadi unaofanywa na Bunge Maalum la Katiba”.

Alisema ili kukamata gari hilo lenye wafuasi wa Chadema, lenye maandishi mbele na nyuma ya M 4 Change, iliwalazimu polisi wakiwa na gari lao, kukimbizana nalo mitaani. Wakati polisi wakiendelea kufukuzana nalo, watu wawili waliruka kutoka kwenye gari hilo na kukimbia na bango hilo.

Waliobaki kwenye gari, walikuwa wanne ambao walikamatwa. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Idd Kizota alisema licha ya polisi kuzima maandamano hayo kufanyika, wako tayari kufanya maandamano hayo hata usiku ili lengo la kupinga kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba, litimie.

Nape na Mbowe Katika hatua nyingine, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye ameibuka na kusema kama Mbowe anataka maandamano, anatakiwa pia ashiriki, huku akiitanguliza familia yake mbele wakati wa maandamano. Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Maneromango, Kisarawe jana, alisema kama Mbowe anaona maandamano na umwagaji damu ni jambo jema na kama atafanya hivyo, atangulize familia yake badala ya kutanguliza mbele vijana wa Tanzania ambao ni nguvu kazi ya taifa.

“Natuma salamu kwa Mbowe, kama anataka sana kuandamana basi aache kuwatanguliza vijana wetu na kumwaga damu zao,” alisema. Nape alisema wakati viongozi wa CCM wanazunguka maeneo mbalimbali nchini, kuhimiza maendeleo na kutatua kero za wananchi, wapinzani wamekuwa wakihimiza maandamano, ambayo mara nyingi husababisha madhara makubwa kwa wananchi.

“Sisi tunajenga nchi, wenzetu wanahimiza chuki... wanasema kuwa Nape anatutukana kila siku, lakini wana hoja nyepesi ndio maana nitaendelea kuwasema bila hofu,” alisema.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema kazi ya CCM, si kutukana au kuandamana, bali kuwapelekea maendeleo wananchi.

“Nasikia leo (jana) wanakwenda Polisi kwa maandamano, hivi kule Polisi kuna kura? Au kule Polisi ndiko yanakopatikana maendeleo?” Alihoji Kinana wakati akizungumzia suala hilo kwenye kikao cha Halmashauri ya CCM Wilaya ya Kisarawe. Kinana aliwataka viongozi wa upinzani nchini, kuachana na maandamano ya mara kwa mara kwa sababu hayasaidii chochote katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Imeandikwa na Lucy Lyatuu, Dar, Sifa Lubasi, Dodoma na Anastazia Anyimike, Kisarawe.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi