loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mengi yanarudisha nyuma kasi ya utalii Tanzania

Licha ya kuiingizia nchi fedha za kigeni, utalii unatoa ajira kwa watu wengi wanaohusika kwenye sekta hiyo. Kwa msingi huo, kwa nchi maskini kama Tanzania ambayo pia ina tatizo kubwa la ajira linalokua siku hata siku, utalii ni kitu kinachopaswa kuzingatiwa, kusimamiwa vyema na kushikiliwa kwa mikono miwili.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, utalii ni huchangia zaidi ya asilimia 17 kwenye pato la taifa na wengi wanaamini kwamba kwa vivutio tulivyonavyo mchango wa utalii ulipaswa kuwa zaidi.

Utalii ukiongeza mchango kwenye pato la taifa, bila shaka ujenzi wa miundombinu nchini utaboreka zaidi, upatikanaji wa maji safi na salama ya kutumia utaongezeka, umeme wa uhakika utapatikana, utoaji wa elimu bora utaongezeka na huduma nyingine kadha wa kadha za jamii zitaimarika na kuboreka.

Vitu vinavyovutia watalii kuja nchini mwetu ni vingi lakini baadhi ya hivyo ni mito, maziwa, milima, wanyamapori, ndege, malikale, makumbusho, fukwe, hoteli bora na zenye sifa, misitu na nyuki na mila na desturi. Tanzania ina jumla ya hifadhi 11 mpaka sasa.

Hifadhi hizo pamoja na ukubwa wa eneo lake kwenye mabano Ruaha (20,300), Mikumi (3,230), Gombe (52), Tarangire (2,850), Serengeti (14,763), Manyara (648.7), Arusha (552), Kilimanjaro (1,668), Katavi (2,253) na Rubondo (457).

Hifadhi zingine za taifa ni Sadan (1,100), Kitulo (442), Mkomazi (3,234.5), Mahale (1,577), Udzungwa (1,990) na Saanane (0.5). Eneo jingine muhimu katika kuboresha utalii ni ushirikishwaji wa jamii katika kulinda na kuendeleza uhifadhi wa utalii wa ndani na nje, rasilimali za wanyamapori na misitu ili na yenyewe (jamii) ijione ni sehemu ya utalii huo nchini.

Jamii kwa kushirikiana na askari wanyamapori wanapaswa kushiriki katika kufanya doria kwenye maeneo ya hifadhi dhidi ya watu wanaoharibu raslimali na vivutio vya utalii nchini.

Faida mojawapo inayopatikana ni jamii kuwa na dhana ya umiliki wa rasilimali na vivutio hivyo vya utalii na kuwa walinzi wa rasilimali hizo za taifa Kwa mujibu wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2013/14, jumla ya siku za doria 54,574 zilifanyika ndani na nje ya mapori ya akiba, ambapo watuhumiwa 391 walikamatwa kwa makosa mbalimbali.

Makosa hayo ni pamoja na kuingia ndani ya hifadhi kuwinda bila ya kibali na wengine kukutwa na nyara za taifa zinazotokana na mazao ya uvuvi. Dhana ambayo kila Mtanzania anapaswa kuwa nayo kichwani ni kwamba utalii ukifa kwa maana ya vivutio vyetu kuharibiwa, manufaa ambayo nimeyataja hapo juu yanayotokana na utalii yatakuwa pia yamekoma.

Nani atakuja kutalii Tanzania kama vivutio kama tembo na wanyama wengine wa kuvutia watakuwa wamemalizika kwa kuuliwa na majangili? Nani atakuja kuona nini kama hatutunzi misitu yetu, mito, maziwa, fukwe, milima, uoto wa asili na vivutio vingine lukuki ambavyo Tanzania imejaaliwa kuwa navyo?

Ni muhimu wakati unaendelea kusoma makala haya kujua kwamba katika mwaka wa fedha wa 2013/14, jumla ya watalii 1,135,884 waliingia nchini na kuliingizia taifa kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.8 ikilinganishwa na watalii 1,077,058 walioliingizia taifa kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.7 kwa mwaka 2012.

Lengo limekuwa ni kuongeza idadi hii maradufu hasa ikizingatiwa kwamba majirani zetu hapo Kenya, ambao hawana vivutio vingi kama sisi ukiwemo Mlima Kilimanjaro, inasemekana kwamba wamekuwa wakipata watalii wengi kulinganisha na sisi. Hii si kwa ajili ya kuongeza idadi ya watalii wa nje pekee, bali hata wa ndani hasa ikizingatiwa kwamba utalii ni kitu cha kujivunia kwani pia ni tiba kwa afya ya binadamu.Unashangaa kusikia hivyo?

Wanasaikolojia wanasema kuwa kutazama wanyama na mandhari za kuvutia za asili huifanya akili ya mtu kuwa na ufahamu mkubwa wa fikra mbali na kuburudika kiakili. Hii ndio maana watu wenye kutembelea mbuga na hifadhi za wanyama mara kwa mara huwa ni wagunduzi wakubwa wa mambo.

Katika bonde la ufa ya Santa Barbara, Honduras kwa mfano, wanasayansi waligundua kuwa idadi kubwa ya upatikanaji wa mimea jamii ya ‘amazilia luciae’ ilifikiriwa kwamba huenda ilikuwa ikiharibiwa na watu kutokana na uasilia wake. Watalii waligundua zaidi jinsi ya kuitunza vizuri mimea hiyo ambapo baadaye ilistawi vyema na kuleta manufaa makubwa ya kujivunia katika jiji la Honduras.

Katika kuongeza idadi ya watalii maradufu, lazima tuimarishe mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ubora wa miundombinu, rasilimali watu na ukarimu kwa watalii, wawe ni wa ndani ama wale wanaotoka nje ya nchi. Nikizungumza kwa mfano, hivi karibuni niliingia katika mgahawa mmoja maarufu jijini Mwanza lakini nilikaa takribani nusu saa bila ya kuhudumiwa.

Baada ya kuona hakuna wa kunihudumia, ilinibidi ninyanyuke niende kutafuta huduma hiyo peke yangu. Licha ya kuifuata, ilichelewa na nililetewa chakula kilichopoa. Nilipomuuliza mhudumu kuhusu kupoa kwa chakula kile alinijibu kwamba anachojua yeye ni kugawa chakula, hajui kama ni kimepoa au la! Wiki iliyopita nilisafiri kwenda mbuga ya wanyama ya Serengeti.

Njiani nikiwa na wenzangu fulani, tulikwama mara tatu kutokana na miundombinu mibovu ya barabara baada ya mvua kunyesha kwa wingi. Tukiwa njiani pia tulipotea mara tatu. Kulikuwa hakuna vibao vinavyoonesha njia za kutupeleka kule mbugani tulikokuwa tunakwenda. Kwa bahati tuliokolewa na msamaria mmoja ambaye ilimbidi tumkodishe atupeleke huko.

Kuna pia hii siku ambayo nilienda hoteli moja maarufu jijini Dar es Salaam, nikiwa na marafiki zangu watatu. Alikuja mhudumu mmoja kutusikiliza ambapo mimi niliagiza maji madogo ya chupa, mwenzangu akaagiza bia aina ya Kilimanjaro na dada mmoja tuliyekuwa naye aliagiza juisi ya matunda. Lakini cha ajabu alipoleta vitu tulivyoagiza, alileta tofauti.

Mimi aliniletea bia huku akinihoji; “umesema ya baridi au moto?” Yule aliyeagiza bia akawa kamletea maji ya baridi na mwenzetu aliyeagiza juisi ya matunda akaletwa soda ya Coca-Cola. Nimetoa mifano hiyo kuonesha namna tusivyo makini katika mambo muhimu. Ninataka kuamini kwamba hata kwenye baadhi ya hoteli za kitalii bila shaka wageni wanakutana na adha kama hizo.

Kadhalika ninataka kuweka msisitizo kwamba suala la miundombinu ni muhimu sana katika kuendeleza utalii wetu. Lazima tuimarishe barabara zetu za mbugani, pamoja na kwamba ni za changarawe lakini ziwe zinapitika muda wote. Kama leo hii unaenda mbuga ya Serengeti kupitia wilayani Bunda unakwama njiani mara tatu huku kukiwa hakuna vibao vya kukuelekeza unapokwenda, je hii inaonesha kweli tuko makini na jambo hili?

Ama tunadhani kwamba kukwama na kupata adha ya kukwamua gari porini ambapo unaweza kuvamiwa na simba ama kugongwa na nyoka pia ni utalii! Nchini Kenya ukiingia tu katika mbuga ya Masai Mara unakutana na vibao vya maelekezo pamoja na waongoza watalii wa ndani. Hutachelewa kuona ukarimu na ucheshi wa hali ya juu hadi kuona safari ikiwa si yenye kuchosha.

Kwa vile utalii unawahusu hata wazawa na si wazungu pekee, unafikiria nini pale unapoingia kwenye mgahawa huulizwi unachohitaji, hata baada ya kuamua kujihudumia mwenyewe unaishia kula chakula kilichopoa? Je, hii haioneshi tusivyo makini ama kuajiri watu ambao hawamudu kazi zao? Je, vyuo vyetu vya utalii vinatoa vijana walioiva sawasawa?

Je, tunaajiri watu wenye taaluma sahihi au tunabeba watoto wa shangazi na mjomba? Je, kwa nini ajira za wafanyakazi mahotelini zinaendelea kutawaliwa na Wakenya? Endapo haya machache hayataboreshwa sambamba na kuyapatia majibu sahihi maswali hayo, utalii Tanzania utadumaa na utashindwa kufikia malengo tuliyojiwekea kama taifa kwenye mkakati wa miaka mitano wa utangazaji utalii Tanzania ndani na nje ya nchi.

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi