loader
Picha

Mercy Kitomari: Mbunifu wa ice cream ya Nelwa Gelato

Ni jina la Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nelwa inayojishughulisha kutengeneza Ice Cream. Ili kulinda mila na desturi la kabla lake hilo, Mercy Nenelwa Kitomari, ameamua kuondoa neno ‘ne’ katika neno Nenelwa na kupata neno Nelwa. Mercy anatengeneza bidhaa hizo kwa kutumia utaalamu wa Kitaliano wa Gelato, Kitanzania na kuziita kwa jina la Nelwa Gelato.

Kijana huyo Mercy anasema lengo la kuita jina hilo ni kutaka bidhaa hiyo iwe na asili ya kitanzania na kila anayekula asiseme ice cream bali asema anakula Nelwa, ikiwa ni pamoja na kuweka tofauti na ice cream zinazopatikana kwa wingi nchini. Msichana huyo ambaye hivi karibuni ameingia miaka 30 aliamua kuacha kazi katika Benki ya Exim Septemba mwaka 2012 na kuamua kujiajiri kutengeneza bidhaa hizo.

Mercy alizaliwa nchini Lesotho na kusoma Shule ya Msingi ya Kimataifa ya Arusha na baadaye Sekondari ya Kiraeni iliyopo Rombo mkoani Kilimanjaro na kumaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Morogoro. Anasema baada ya kumaliza kidato cha sita alifanya kazi katika Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo na baadaye alienda nchini Uingereza na kumaliza shahada ya Masoko na Ujasiriamali katika Chuo Kikuu cha UKin 2006.

Akiwa nchini humo kimasomo, Mercy alikuwa akifanya kazi ya ziada ya kutembeza watoto kuwapeleka sehemu mbalimbali kula ice cream kwa lengo la kujiongezea kipato. Anasema akiendelea na kazi hiyo aliona kuna fursa itakayomwezesha kujiajiri akirejea nchini ya kutengeneza ice cream kwani alipoondoka nchini aliacha kuna aina chache za bidhaa hiyo.

Hivyo aliamua kuanza mikakati ya kuhakikisha anapata nafasi ya kusoma utengenezaji wa bidhaa hiyo lakini kwa Kitaliano ambazo nyingi zilikuwa za asili kutokana na bidhaa zilizopo katika nchi husika. Anasema kwa kuwa alikuwa amemaliza masomo yake ya masoko aliamua kusoma utengenezaji wa ice cream kwa kumuomba Mtaliano mmoja aliyekuwa akiuza bidhaa hizo aweze kumfundisha.

“Alikubali kunifundisha kwa kusoma siku mbili kwa wiki kwa pauni za Uingereza 2,000 au 3,000, nikapata masomo hayo pamoja na mengine ya ziada ambayo yanawezesha kutengeneza ladha mbalimbali,” anasema. Mercy anasema baada ya kumaliza masomo na kujiona amekidhi aliamua kununua mashine ndogo kwa ajili ya kutengeneza aina hiyo ya ice cream.

Anasema aliporejea nchini, kazi yake ya kwanza ilikuwa katika benki ya Exim kwa lengo la kutafuta mtaji ambapo alifanikiwa kununua mashine nyingine za kutengeneza bidhaa hiyo. Anasema akiwa kazini katika benki hiyo, alianza kutengeneza ice cream hizo kidogo na kupeleka ofisini katika benki hiyo ambapo wafanyakazi walipokea vizuri na kumuomba kuwatengenezea lita moja kwa Sh 10,000 jambo lililomfanya kuingiza kipato cha ziada.

Anasema ice cream hizo anazitengeneza kwa kutumia bidhaa za kitanzania za asili kama matunda na vyakula mbalimbali bila kuwekwa ladha yoyote isiyo ya asili. Anasema mara baada ya kuuza ofisini zilianza kujitokeza fursa mbalimbali ambazo alikuwa akitengeneza na kupeleka kuuza kama mashindano ya mbuzi, riadha na mengineyo na kupata mwitikio mzuri sana.

Mercy anasema alijipa miaka miwili kufanya kazi kwa lengo la kutafuta mtaji jambo ambalo alifanikiwa kwa msaada wa wafanyakazi wenzake na wananchi wengine waliompa moyo kila kukicha. Anasema wakati akitafuta wawekezaji ili kuboresha huduma hiyo kwani alikuwa hana mtaji wa kutosha alikutana na mzungu (jina limehifadhiwa) ambaye walikubaliana kutengeneza bidhaa hiyo.

Anasema mara baada ya kuanza biashara na kuona imekubalika kwa jamii alivunja mkataba na alitumia wazo lake la biashara kufungua ya kwake. “Ingawa alinidhulumu wazo langu nilimuachia sehemu hiyo ya biashara lakini mpaka sasa hajafanikiwa lolote kwani ana sehemu moja tu ile ile anayofanya biashara wakati mimi nikiwa na sehemu zaidi ya tano nikisambaza bidhaa hiyo,” anasema.

Ilipofika mwaka 2012 Mercy alipeleka bidhaa yake hiyo kwenye Hoteli ya Southern Sun na kuwaomba kuijaribu bidhaa hiyo kwa wateja wao na baada ya kujaribu ilikubalika sana na wakamtaka apeleke lita 20 kwa wiki. Anasema Septemba mwaka huo alijikita katika ujasiriamali pekee ambapo alianza kupeleka katika matamasha mbalimbali ikiwemo mbio za Mbuzi,Tamasha la Nyama Choma na mengineyo ambapo alipata soko kubwa.

Mwaka 2013 alipata nafasi ya kupeleka bidhaa yake katika maonesho ya kimataifa ya Sabasaba kupitia banda la Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) lililo chini ya Mama Anna Mkapa na kupata mafanikio makubwa. Anasema baadaye alipata mkataba wa kusambaza katika migahawa mitano jijini Dar es Salaam ambapo alisambaza lita 80 kwa wiki.

“Sasa niko ‘busy’ kutengeneza bidhaa hiyo wakati wote, kwa kuchukua oda mbalimbali za ladha na kupeleka katika sherehe na matamasha kama hivi sasa nasambaza katika matamasha ya Fiesta yanayoendelea,” anasema. Anasema kwa sasa ana kampuni ndogo aliyoajiri watu sita na sasa amepata mwekezaji wa kitanzania mwenye malengo yatakayomwezesha kufikia malengo ambaye ni Mkurugenzi wake Ben Mashiba Jr.

Anasema kwa sasa anataka kuwa na sehemu zake za kuuzia bidhaa ambazo zitakuwa zake binafsi huku akisambaza maeneo mengi zaidi kwani kwa sasa ameingia ubia na watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha uzalishaji kwa kuajiri watu wengi zaidi. Anasema malengo yake ni kuwa na kiwanda cha kimataifa ili kuwa na uwezo wa kupeleka bidhaa yake hiyo nje ya nchi kwa kujiwekea malengo ya kufanya hivyo baada ya miaka miwili ijayo.

Mercy anasema kwa mwaka huu anataka kuongeza usambazaji kupeleka sehemu nyingi zaidi katika maduka makubwa ambapo alisema wanauza kuanzia Sh 4,000 hadi Sh 6,000 na kubwa ya lita tano Sh 45,000. Anasema pia watu wanaweza kumualika kupeleka huduma hiyo katika matukio mbalimbali ambapo anaweza kupeleka na kutoa huduma kwa gharama nafuu au kuwaletea tu.

Akizungumzia gharama za bidhaa yake hiyo anasema inakuwa kubwa kutokana na utengenezaji wake hautumii vitu visivyo asili ambavyo havina gharama. “Nikikwambia ni ya ladha ya tunda lolote kama chungwa au embe ninatumia tunda halisi la kitanzania kwa lengo la kulinda afya za walaji na kuwa za asili kweli,” anasema.

Mercy anasema ili kuwezesha Watanzania wengi kumudu gharama na kufurahia bidhaa hiyo kwa sasa ameanza kutengeneza lamba lamba za bei nafuu anazoweka ladha mbalimbali kwa Sh 2,000. Mercy anashukuru Watanzania kwa jinsi walivyopokea bidhaa yake hiyo yenye ubora kwa kumpa moyo na kuona bidhaa hiyo ni ya Watanzania wote.

Mercy ambaye ni binti wa pekee kwa mama yake ambaye ni Mwalimu wa Sekondari mstaafu, anasema “wakati akiacha kazi ya kuajiriwa na kuanza ujasiriamali mama yake alikuwa na wasiwasi iwapo atamudu. “Nyumbani mama yangu alikuwa na wasiwasi na mipango yangu ya kutaka kuacha kazi na kujiingiza katika masuala ya ujasiriamali lakini nilikuwa jasiri na kumpa moyo kuwa lazima nitafanikiwa,” anasema.

Anasema baba yake ambaye kwa asili ni Mgogo kutoka Mkoa wa Dodoma kwa sasa ni marehemu huku mama yake akitokea Mkoa wa Arusha katika kabila la Wameru. Mercy anawaasa wasichana na Watanzania kwa ujumla kutambua kitu cha thamani wanavyokuwa navyo na kuangaliwa watu wa kushirikiana nao kwani kuna watu wanatumia mawazo ya watu kufanikiwa.

Anasema “ni kweli Watanzania wengi tumekuwa na changamoto ya mitaji kwa kutaka wawekezaji kushirikiana nao lakini ni vyema kuwa makini kwa kuwasoma vizuri kabla ya kukubali kuwapa wazo lako”.

Akizungumzia changamoto, anasema alizokabiliana nazo wakati wa safari yake ya mafanikio kuwa ni kutokana na kuwa msichana mdogo anakabiliwa na ulimwengu wa wanaume lakini anapambana nao kwa kuwa makini na biashara. Anawataka wasichana kuwa na maisha ya uthubutu na kujiamini huku akiamini kuwa anaweza kuleta tofauti katika dunia na siyo nchini pekee.

“Lazima msichana uwe na mawazo ya kuwa na mchango katika dunia kwa kufanya kitu tofauti na kutokubali kuvunjika moyo kwa hali yoyote kwani kufikia malengo haiwezekani kwenda kwa mteremko bali lazima kupitia masuala tofauti ,“ anasema. Anasema ndoto zake ni kuwezesha mabinti kujitegemea na kamwe wasikubali kutegemea wanaume kwa kuwajengea misingi itakayowawezesha kujiamini na kuona wanaweza.

Anasema mikakati hiyo inaenda sambamba na kuanzisha shule ya kutengeneza bidhaa hiyo kwa njia mbalimbali zitakazowezesha kuwapatia ajira wasichana wengi. Anasema wazo hilo anatarajia kulianza kidogokidogo mwakani ikiwa ni pamoja na kuajiri wengine kwa ajili ya kuuza bidhaa zake.

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi