loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mfumo wa Malipo Afrika Mashariki ulivyorahisishwa

Hii inatokana na ukweli kwamba, wakati nchi hizi zikifanya maandalizi ya kwenda kwenye sarafu moja, ufanywaji wa malipo kwa EAPS umerahisishwa ambapo mlipaji analipa kwa fedha ya nchi yake na mpokeaji aliye katika nchi nyingine halikadhalika anapata pesa zake kwa thamani ya pesa ya nchi yake.

Mchumi mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Alli Liyau, anasema mfumo huu mpya wa malipo unamwezesha mtu kutuma pesa Kenya au Uganda ama kutumiwa pesa kutoka katika nchi hizo na kuzipata ndani ya saa mbili tu zikiwa na thamani ileile baada ya kufika kwenye benki inayotakiwa kulipa.

“Kama Mtanzania anatuma pesa Kenya, kwa mfano, mtumiwaji atazipata kwa pesa ya Kenya kwa kiwango cha thamani ya pesa ya nchi hiyo kwa siku hiyo na kama ni Mtanzania ndiye anatumiwa na Mkenya, basi naye atazipata kwa pesa za Tanzania kwa kuzingatia kiwango cha kubadilisha pesa cha siku hiyo kinachotolewa na Benki Kuu ya nchi inayotuma pesa,” anasema.

Liyau ambaye ni mmoja wa watendaji wa BoT katika Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo anasema mfumo wa pamoja umewezekana baada ya nchi hizo kuwa na mifumo ya haraka ya kuhaulisha fedha kibenki kwa njia ya kielektroniki ambayo inajulikana kama Real Time Gross Settlement (RTGS).

“Sisi Tanzania, kwa mfano, mfumo wetu wa RTGS unajulikana kitalaamu kwa jina la Tanzania Interbank Settlement System (TISS), Kenya wao unaitwa Kenya Electronic Payment System (KEPS) na Uganda wao wameuita Uganda National Interbank System (UNIS). Sasa kwa kuunganisha mifumo hii ndipo tunapata huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa EAPS,” anasema.

Mchumi huyo anasema mfumo wa EAPS unaruhusu nchi zingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki za Rwanda na Burundi nao pale zitakapokuwa zimekamalisha mifumo yao ya RTGS.

“Si nchi hizo pekee, bali nchi yoyote itakayojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kuunganishwa katika mfumo wa EAPS na kuwezesha wananchi wake kuhaulisha fedha kirahisi katika eneo hili la Afrika Mashariki,” anasema na kuongeza kwamba mfumo huo unaruhusu kutumia Sh za Tanzania, Kenya na Uganda na si aina nyingine za pesa wala Dola ya Marekani katika kufanya miamala.

Akifafanua zaidi kuhusu mfumo huo, Liyau anasema mwananchi anachopaswa kufanya ni kwenda kwenye benki yake ya biashara na kujaza fomu maalumu na kwamba gharama za kutumia EAPS kutuma pesa hazizidi Sh 10,000 za Tanzania.

“Faida za huu mfumo ni nyingi lakini kubwa ni kuondoa mfumo wa zamani ambao benki moja, tuseme ya Tanzania, ililazimika kuwa na ushirikiano wa kimalipo na benki nyingine ya Kenya ama Uganda na gharama za kutuma pesa zilikuwa juu. Huu pia ni mfumo wa haraka, wenye usalama na uhakika na pia ni mfumo unaotumia fedha za nchi zetu,” anasema.

Akizungumzia historia ya malipo nchini, Liyau anasema nchi imetoka kule ambako malipo makubwa yalikuwa yanachukua siku kadhaa hata ndani ya nchi lakini sasa muda wa malipo umepunguzwa na unazidi kupunguzwa.

“Sisi katika BoT, tumegawa malipo katika mafungu mawili; malipo makubwa na madogo ambayo pia tunayaita ya rejareja. Malipo ya hundi (ambayo kiwango chake cha juu kwa sasa ni Sh 10,000,000), malipo ya mashine za ATM, malipo kupitia simu za mkononi, Western Union na mengine ya aina hiyo ni mifumo ya malipo ya reja reja,” anasema.

Anasema malipo ya hundi zamani yalikuwa yanachukua hadi siku 90 kulingana na hali ya miundombinu ilivyokuwa wakati huo, lakini yakapunguzwa kwa usimamizi wa BoT hadi siku tatu ndani ya mji mmoja ama siku tano za kazi kati ya mji mmoja na mwingine.

“Lakini tunakoelekea, na si siku nyingi sana, tutataka malipo ya hundi yawe ndani ya siku moja tu kwa kuwa yatalipwa kwa mfumo wa kielektroniki,” anasema.

Anafafanua kwamba mfumo huo wa malipo wa TISS ambao uko kwenye malipo makubwa unazidi kupanuliwa na sasa unatumika kwa benki zenyewe kwa zenyewe, watu binafsi hadi kwenye taasisi za Serikali kama vile kwenye Hazina ndogo, Mamlaka ya Mapato (TRS), Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na kwamba malengo ni kufikia idara zote za Serikali.

Akizungumzia kuhusu mfumo wa malipo ya fedha kwa njia ya simu (Tigo-Pesa, M-Pesa ama Airtel Money), Liyau anawatoa wasiwasi Watanzania wanaodhani kwamba sasa kampuni za simu zinafanya kazi za benki.

“Watanzania wajue kwamba, haya makampuni ya simu, yanalazimika kwanza kuwa na kampuni ndogo inayosimamia malipo kwa njia ya simu na kampuni hiyo lazima iwe na akaunti kwenye benki. Kwa hiyo kimsingi biashara kuu ya malipo ya simu mwisho wa siku inadhibitiwa na benki,” anasema.

Anasema Serikali kupitia BoT imeruhusu hatua hiyo kwani inasaidia wananchi, hususan walio vijijini kusiko na benki kutuma na kutunza pesa zao kwa njia bora zaidi.

“Zamani hapa BoT tulikuwa tunaletewa pesa zimeungua ama zimeliwa na wadudu kutokana na kukosekana sehemu sahihi za kuzihifadhia pesa huko vijijini lakini siku hizi, kutokana na mfumo wa malipo ya simu, hayo yamepungua,” anasema. Wakati huo huo, Watanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa za kukopa vitu halisi kama matrekta ama mashine badala ya pesa.

Ofisa wa BoT katika Kurugenzi ya Usimamizi wa Benki, Ng’waka Mong’ateko, anasema zipo kampuni kadhaa nchini zilizosajiliwa na benki hizo zinayotoa mikopo ya karadha, kwa maana ya vifaa vya uzalishaji. “Mtu anaweza kuwa na ujuzi fulani, lakini anachokosa ni vifaa na si pesa. Huyu mkopo wa karadha unamfaa zaidi,” anasema.

Anafafanua kwamba mkopaji wa vifaa katika kampuni hizi za karadha, kimsingi kifaa hubaki kuwa mali ya kampuni husika ambapo mkopaji anaingia mkataba wa kuilipa kampuni hiyo kadri anavyotumia kifaa hicho. “Hata wenye kuendesha mikopo ya karadha vichochoroni, tunawashauri wajitokeze, wasajiliwe Benki Kuu ili wafanye shughuli zao kwa misingi ya taratibu na sheria,” anasema.

Bibi Ng’waka Mong’ateko anasema kurugenzi yao imekuwa imara katika kusimamia utendaji wa benki wa kila siku kwa hiyo wananchi wasihofu kutumia benki zetu kwa shughuli zao kifedha za kila siku, kwani fedha ambazo ni ziada, zinapowekwa benki, zinafanya kazi ya kukuza uchumi kwa kukopwa na mtu mwingine kuliko zinapochimbiwa mchagoni ama kwenye kibubu.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimembariki Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi