loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mgogoro machimboni Ulata wamalizwa

Mgogoro huo unaelezwa kumalizwa baada ya mwekezaji, Ibrahim Msigwa anayemiliki leseni sita za uchimbaji katika machimbo hayo, kuelekezwa atoe hisa mbili katika kila leseni na kukipatia kijiji, jambo ambalo aliliafiki.

Akitoa taarifa ya mgogoro huo kwa waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa huu, Amina Masenza alisema, “Mgogoro ulimhusisha Msigwa, wachimbaji wadogo wa dhahabu pamoja na kijiji cha Ulata na umemalizwa kwa kuzihusisha pande zote kwenye mazungumzo”.

Kwa mujibu wake, Masenza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, pamoja na kamati yake walikwenda machimboni huko kujionea hali halisi, baada ya kutokea vifo vya watu watano waliofukiwa kwenye moja ya machimbo katika kijiji hicho.

Kutokana na maelezo ya Masenza, kamati iliamua kumaliza mgogoro huo kwa kufanya mazungumzo na wahusika wote ambapo mambo kadhaa yaliamuliwa kwa makubaliano ya wahusika, na mgogoro kwisha.

Aliyataja makubaliano yaliyofikiwa baina ya mwekezaji, uongozi wa kijiji, wachimbaji wadogo na kamati hiyo ya ulinzi kuwa ni mwekezaji kutoa hisa mbili katika kila leseni anayomiliki. “Tulikubaliana kuwa hisa hizo azitoe kwa kijiji cha Ulata zitumike kwa shughuli za maendeleo ya kijiji hicho”, Masenza alisema.

Makubaliano mengine aliyoyataja ni Mwenyekiti wa kijiji hicho kuvaa vazi la uongozi na kuwaongoza wanakijiji kwa mujibu wa taratibu na miiko ya uongozi, lengo likiwa kuhakikisha usalama kijijini hapo.

Pia, ilikubaliwa kuwa, Ofisi ya Madini Kanda ya Kusini Magharibi, ikakague usalama wa eneo lote la machimbo huku Mwenyekiti akitakiwa kuitisha kikao cha kijiji na kufafanua makubaliano hayo kukiwezesha kijiji kuingia katika umiliki wa machimbo hayo kihalali.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huu aliitaka ofisi hiyo ya madini kanda iwajengee uwezo wachimbaji vijana waweze kukopesheka na kuchimba madini hayo kwa mujibu wa taratibu na ufanisi.

Katika hatua nyingine, Masenza aliwataka wachimbaji vijana kuacha tabia ya anasa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vileo yaliyokithiri ili, pamoja na mambo mengine, watunze na kulinda afya zao dhidi ya ulevi uliopindukia na maambukizi ya VVU.

Alisema, “Pombe maarufu kama viroba inawamaliza wanangu jitahidini kuachana nayo mjitafutie maendeleo. Acheni ulevi kwa sababu mkishalewa mnashindwa kufanya maamuzi sahihi kuhusu maendeleo yenu na taifa”.

Mbali na hayo, aliwakumbusha wachimbaji kuheshimu na kutii sheria akisema kuwa hakuna aliye juu ya sheria za nchi. Aliwaonya pia kuacha kushambulia maofisa wa serikali kwa kuwapiga na kuzuia wasitekeleze wajibu wao, pindi wanapokwenda kwenye machimbo hayo kikazi.

Naye Mhandisi Migodi katika kanda hiyo, Zephania Msungi alisema, awali hali ilikuwa tete katika machimbo hayo ,kwa sababu maofisa kutoka ofisi ya madini ya kanda hawakuruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

“Kwa muafaka huu, itakuwa rahisi kutekeleza majukumu yetu ya kusimamia sheria ya madini ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake, na kuhakikisha serikali inapata mapato yake kutokana na shughuli za machimbo,” Msungi alisema.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Dennis Gondwe, Iringa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi