loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ni jibu la matatizo ya wengi

Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ni jibu la matatizo ya wengi

Mfano, mzazi kumpeleka mtoto shule ni uwekezaji kwenye elimu na hata serikali kujenga barabara ni uwekezaji katika kurahakisha maendeleo ya jamii. Ili kufanya uwekezaji uwezekane, lazima kuwe na fedha ambazo hutumika kama kichocheo cha kuweza kutimiza uwekezaji unaouhitaji.

Sasa kama suala ni kufanya kazi au biashara ili tupate fedha za kuchochea uwekezaji, ni kwa nini usifikirie njia muafaka zaidi za kutunza fedha zako kabla au tukisubiri kufanya shughuli husika katika mfumo wa kuziwekeza zikakua na kuongeza mtaji kwani si rahisi mtu kupata fedha za mkupuo.

Watu wengi wamekuwa wakiweka akiba za fedha zao sehemu tofauti kwa nyakati tofauti bila ya kukua au kupata ongezeko lolote. Lakini Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ni njia mbadala ya uwekaji akiba kwa mfumo wa Uwekezaji.

Uwekezaji wa pamoja una maana nyingi inaweza kuwa mtu mmoja anataka kuchimba madini, lakini hamudu gharama za uchimbaji ule hivyo ni vyema akawahusisha wenzake, mtu mmoja mmoja, vikundi au kampuni wakachangisha mtaji wa pamoja wakachimba madini wakauza wakapata faida na wakagawana faida kutokana na uwiano wa mtaji wa kila mmoja, ambapo huu ndio Uwekezaji wa Pamoja kwa njia ya kampuni.

Mfano mwingine wa uwekezaji wa pamoja ni watu kuweka fedha zao kwenye kapu moja au mfuko mmoja na fedha zile zikasimamiwa na Meneja waliyemchagua huku akiangaliwa na vyombo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa masharti na sheria zote zimezingatiwa.

Na meneja huyo akawekeza fedha zile kwenye masoko ya mitaji, masoko ya fedha na dhamana mbalimbali za serikali na binafsi zinazokubalika kisheria. Uwekezaji huu utakuwa ni wa fedha ili kupata fedha zaidi kutokana na hali ya soko ambapo ni aina ya uwekezaji wa pamoja kwa njia ya amana.

UTT- Asset Management and Investor Services Plc (UTT-AMIS) ni kampuni inayomilikiwa na serikali chini ya Wizara ya Fedha. Pamoja na majukumu mengi, jukumu kubwa la UTT-AMIS ni kuanzisha na kuendesha Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja hapa nchini kwa mfumo wa amana.

Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa UTT-AMIS, Daudi Mbaga anaitaja mifuko iliyoanzishwa na inayoendeshwa na UTT-AMIS ni Mfuko wa Umoja, Mfuko wa Wekeza Maisha, Mfuko wa Watoto, Mfuko wa Kujikimu na Mfuko wa Ukwasi. Kutokana na hilo, mwekezaji huchagua mfuko anaotaka kutokana na malengo yake kisha huweka fedha zake humo na kuiachia UTT-AMIS kuziwekeza fedha hizo kutokana na waraka wa makubaliano.

Sehemu ya uwekezaji aliyonayo mwekezaji katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja huitwa Kipande. Hivyo basi, UTT-AMIS kama meneja wa mfuko huwekeza fedha hizo. Fedha za Wawekezaji huwekezwa katika uwiano mbalimbali kama inavyoelekezwa katika waraka wa makubaliano na zinawekezwa katika masoko ya mitaji na katika masokao ya fedha.

Mbaga anasema kwa upande wa masoko ya mitaji yaweza kuwa hisa za kampuni yaliyoorodheshwa katika Soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) ambayo kwa tathimini ya meneja msimamizi anaona zina nafasi kubwa ya kurejesha gawio zuri. Kwa upande wa masoko fedha hizo huwekezwa katika akaunti za muda maalumu, hati fungani za muda mfupi na dhamana zingine za serikali.

Uwekezaji huu ni mzuri sababu ni mseto hivyo hupunguza nafasi ya uwekezaji kutoleta faida. Tukichukulia kipengele kimoja mathalani, akaunti ya muda maalumu hutoa faida kutokana na kiasi cha fedha kilichowekwa na muda, jinsi fedha inavyokuwa nyingi ndio na faida nayo huongezeka.

“Jambo kubwa la kujiuliza hapa ni watanzania wangapi wanaweza kuwa na fedha nyingi kwa mkupuo ili wawekeze wapate faida kubwa katika akaunti za muda maalumu, basi jibu lake ni wachache.

Kumbe wanaweza kuweka fedha zao kila mtu kidogo kwa pamoja zikawekwa katika akaunti hiyo hiyo ya muda maalumu wakapata faida kubwa zaidi,” “Mfano mwingine ni ule wa hisa, hisa peke yake pamoja na mambo mengi hutegemea ufanisi wa kampuni husika kama kampuni husika haifanyi kazi kwa ufanisi kampuni hiyo huanguka na kupelekea gawio kutopatikana na hata mwenye hisa kama mmiliki wa kampuni kupata hasara,” anasema.

Ilhali vipande vya uwekezaji wake ni anuai, athari za uwekezaji zimetawanywa katika masoko ya fedha na masoko ya mitaji. Labda katika soko la fedha na dhamana kuwe na hali hatarishi katika kila kipengele cha zilipowekezwa fedha. Uzuri mwingine ni urahisi wa kujiunga kwenye mifuko hii ya Uwekezaji.

Mwekezaji anaweza kuwasiliana na UTT-AMIS au kutembelea tawi lolote la Benki ya CRDB nchi nzima, pia anaweza kujiunga kupitia kwa dalali wa soko la hisa. Hata hivyo, UTT-AMIS inaweka bayana kuwa kujitoa kwenye mfumo wa uwekezaji ni rahisi, mwekezaji anaweza punguza kiasi fulani cha fedha au kuongeza sawa na waraka wa makubaliano wa mfuko husika.

Uhuru wa mwekezaji umezingatiwa kwa kiasi kikubwa. Uwazi katika mifuko ni jambo lingine kubwa. Kila siku ya kazi bei ya kipande hutangazawa katika magazeti na tovuti ya UTT-AMIS hivyo basi mwekezaji hufahamu hali halisi ya mwenendo wa uwekezaji wake. “Mpaka sasa kupitia mifuko yake mitano, UTT -AMIS inasimamia zaidi ya Sh bilioni 182 za kitanzania ambapo idadi ya wawekezaji ni zaidi ya 90,000.

Ukubwa huu wa mifuko umechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa ufanyaji vizuri wa masoko ya fedha na masoko ya mitaji hapa nchini ambapo ndiyo sehemu fedha za wawekezaji zinawekezwa,” anafafanua.

Kama ilivyoelezwa awali, faida inaweza kuongezeka au kupungua kutokana na mwenendo wa masoko ya fedha na mitaji ambapo historia inaonesha mifuko imekuwa ikitoa faida ya asilimia 10 na kuendelea kwa mwaka baada ya makato ya kodi kwa kiasi chochote ambacho mwekezaji amewekeza.

Pamoja na hayo, mifuko imekuwa ikifanya vizuri siku hadi siku, hii inamaanisha kuwa, UTT-AMIS imeweza kutoa faida zaidi ya matarajio ya wawekezaji wake. Mathalani tukiangalia mwekezaji aliyewekeza Sh milioni moja katika mfuko wa Umoja tangu Juni 20,2013 hadi Juni 20,2014 pesa yake itakuwa imeongezeka kwa kiasi cha Sh 515,412.9826.

Hii ni sawa na asilimia 51.1 baada ya makato ya kodi. Faida hii ni shindani na ni vigumu kwa wawekezaji kuipata kwenye masoko ya fedha. Kwa kuwekeza kwenye mfuko wa Umoja mwekezaji anapata mseto mzuri wa uwekezaji ambapo zaidi ya asilimia 70 ya pesa huwekezwa kwenye masoko ya fedha ambayo hatari ya kupata hasara ni ndogo na kiwango kisichozidi asilimia 30 huwekezwa kwenye masoko ya mitaji.

Mfuko wa kujikimu ndiyo mfuko pekee kati ya mifuko mitano ambayo UTT –AMIS unatoa gawio moja kwa moja kwa wawekezaji, lakini licha ya kutoa gawio pia hukuza mtaji wa mwekezaji. Gawio hufanyika kila baada ya miezi mitatu au mara moja kwa mwaka. Mfuko huu umekuwa faraja kwa wastaafu au mtanzania yeyote anayepata kipato kikubwa mara moja na hatarajii kupata kipato kingine mapema.

“Mfano mwekezaji aliyewekeza milioni 50 anatarajia kupata takribani Sh milioni 1.5 kila miezi mitatu sawa na Sh 500,000 kila mwezi au takribani Sh milioni sita kwa mwaka huku milioni 50 yake ikikuwa inaendelea kuwekezwa,” anasema Mbaga. Hivyo wawekezaji wanaopata kipato cha mkupuo na kupenda kupata uhakika wa mwendeleo wa mapato kama wakandarasi,wastaafuu, wataalamu washauri, kampuni na taasisi mbalimbali zinaweza kunufaika na mfuko wa kujikimu.

Mfuko mwingine ni Wekeza Maisha, ambapo mfuko huu umeambatanisha uwekezaji na faida za bima. Hivyo, Mtanzania yeyote aliye na umri kati ya miaka 18 hadi 55 anayo fursa ya kuwekeza kwenye mfuko huu ambapo muda wa uwekezaji ni miaka 10. Kiwango cha chini cha kuwekeza kwa muda wa miaka 10 ni Sh milioni moja tu.

Mwekezaji ana uwezo wa kuwekeza kiasi kisichopungua Sh 8,340 kila mwezi ili kutimiza mpango wake, hata hivyo hakuna ukomo wa kiwango cha juu cha kuwekeza. Faida za bima ziambatanazo na mfuko huu ni bima ya maisha, bima ya ulemavu wa kudumu, na bima ya ajali.

Bima hizi hulipwa pale mwekezaji atakapopata janga husika na hulipwa kulingana na kiwango na muda mwekezaji aliowekeza katika mfuko.Hata hivyo, faida za ziada za mfuko huu ni pamoja na gharama za za mazishi iwapo mwekezaji atafariki wafiwa watapewa Sh 500,000 na kuna mkono wa pongezi wa kati ya asilimia tano na saba kiwango cha uwekezaji uliowekezwa kwa wawekezaji watakaoweza kutimiza miaka 10.

Mfuko wa watoto hakika huu ni faraja kwa watoto ambapo dhumuni lake ni kuwanufaisha watoto wetu kwa ajili ya maisha ya baadaye. Hapa uwekezaji hufanyika kwa jina la mtoto mnufaika mwenye chini ya umri wa miaka 18.

Mbaga anasema mfuko una uwekezaji wa aina mbili, ambao ni kwa ajili ya malipo ya ada (hufanyika mara moja au mbili kwa mwaka baada ya mtoto kutimiza umri wa miaka 12) umri tunaotarajia awe anaanza elimu ya sekondari na mpango wa kukuza mtaji, hapa hakuna malipo yanayofanyika moja kwa moja badala yake mzazi au mlezi atauza vipande sawa na mahitaji yake baada ya mtoto kutimiza umri wa miaka 12.

Mbaga anasema uwekezaji unaweza kuanza kufanyika kwa kiasi cha Sh 10,000 na kiwango cha chini cha uwekezaji wa nyongeza ni Sh 5,000. “Vile vile tuone mzazi au mlezi aliyemwekezea mtoto wake Sh 500,000 tangu Juni 20,2013 hadi Juni 20,2013, atapata faida ya Sh 162, 275.7,” anafafanua.

Aprili mwaka jana, UTT-AMIS ilianzisha mfuko wa Ukwasi, ambapo mfuko huu ni mahsusi kwa wawekezaji wenye kiwango kikubwa cha pesa na wangependa kuwekeza kwa muda mfupi na muda wa kati huku wakikuza mtaji wao. Mfuko huu unawekeza kwenye masoko ya fedha ambapo hatari za uwekezaji ni ndogo zaidi hivyo kumhakikishia mwekezaji kiwango kikubwa cha usalama wa fedha zake na faida shindani.

Mkurugenzi huyo wa Masoko anasema tangu kuanzishwa mpaka Juni mwaka huu mfuko huo umetoa faida ya asilimia 12 kwa wawekezaji wake. Mwekezaji anaweza kuanza kuwekeza kiwango cha chini cha Sh milioni tano na kiwango cha chini cha uwekezaji wa nyongeza ni Sh milioni moja na hakuna ukomo wa uwekezaji kwenye mfuko huu.

“Faida inaweza kuongezeka au kupungua kutokana na mwenendo wa masoko ya fedha na mitaji,” anabainisha. Licha ya ya mafanikio makubwa ambayo mifuko ya uwekezaji wa pamoja hapa nchini kwa mfumo wa amana imeendelea kupata hadi hivi sasa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, inaonekana bado kuna changamoto kubwa hasa kwa watanzania wengi kutokuwa na tabia na utamaduni wa kuweka akiba.

Changamoto nyingine anazotaja Mbaga ni uelewa mdogo juu ya uwekezaji kwenye masoko ya fedha na mitaji imeonekana kuwa changamoto kubwa kwa watanzania wengi ambao iwapo watapata elimu hii, basi uchumi na maisha yao kwa ujumla wake yataboreka zaidi.

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi