loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Minyororo jela imesababisha nizae mlemavu’

Kwa namna mwanamke huyo alivyoteseka sijashangaa kauli ya mumewe, Daniel Wani (27) kwamba, ingawa mkewe yupo huru nchini Marekani, itachukua muda mrefu kusahau mateso aliyopitia.

Alinyimwa uhuru, akateswa, akanusurika kuchapwa viboko 100 na kunyongwa kwa sababu ya dini ikiwa ni pamoja na kukataa kuuasi Ukristu, na imekuwa ni baraka kwake na familia kwa kuwa, kiongozi wa kwanza kukutana nao, ni Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.

Meriam amekutana na Baba Mtakatifu jijini Vatican nchini Italia mara tu baada ya yeye na familia yake, mumewe, Daniel Wani, na watoto wao, Martin na Maya kuondoka Sudan. Papa Francis amekutana faragha na Meriam akiwa na Maya, amewabariki. Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi amesema, Papa ameguswa sana kukutana na Meriam na familia yake.

“Papa amemshukuru Meriam na familia yake kwa ujasiri waliouonesha na msimamo wao katika imani,” anasema Lombardi.

Meriam amemshukuru Baba Mtakatifu kwa msaada mkubwa na faraja aliyompa kupitia sala zake na za watu wengine wenye mapenzi mema. Meriam na familia yake walikuwa Vatican kwa wiki moja.

Kwa mujibu wa Lombardi, mkutano kati ya Papa na familia ya Wani katika makazi ya kiongozi huyo wa kanisa, St. Martha, ulikuwa na mguso mkubwa.

Amesema, kwa mtazamo wake, mkutano huo umeonesha ukaribu na mshikamano kwa watu walioteseka kwa sababu ya imani yao.

Meriam alikamatwa Agosti 2013, Septemba mwaka huohuo akawekwa gerezani, Mei mwaka huu, mahakama jijini Khartoum ikamtia hatiani kwa makosa ya uzinzi na kuiasi dini ya Kiislamu, akiwa na ujauzito wa miezi minane akahukumiwa kuchapwa viboko 100 kwa kosa la kwanza, na kunyongwa kwa kosa lingine.

Sudan inafuata sheria za Kiislamu (Sharia), na kwa mujibu wa sheria hizo, ni kosa kwa mwanamke Muislamu kuolewa na mwanaume Mkristu.

Serikali ya Sudan inamtambua Meriam kwa jina la Kiislamu la Abrar. Meriam ni mke wa Daniel Wani, raia wa Marekani mwenye asili ya Sudan, wamefunga ndoa katika Kanisa Katoliki.

Sheria za Sudan zinamtambua Meriam kuwa ni Muislamu kwa kuwa baba mzazi wa mwanamke huyo alikuwa Muislamu. Mama mzazi wa Meriam ni Mkristu muumini wa madhehebu ya Orthodox, na ndiye aliyemlea mwanamke katika misingi ya ukristu tangu akiwa na umri wa miaka sita kwa kuwa mume wa mama huyo aliwatelekeza.

Meriam angechapwa viboko 100 siku chache baada ya kujifungua na angenyongwa miaka miwili baadaye.

Alipata mtoto Mei 27 mwaka huu wakati akiwa kwenye shinikizo kubwa la kumtaka auasi ukristu, akakataa na kutamka kwamba, alikuwa tayari kufa kwa ajili ya imani yake, kwa sababu hajawahi kuwa Muislamu.

Kwa sababu ya shinikizo kutoka sehemu mbalimbali duniani, Juni 23 mahakama ya Sudan ilibatilisha hukumu ya kifo, Meriam akaachiwa, siku iliyofuata, yeye na familia yake wakakamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Khartoum kwa tuhuma za kughushi hati za kusafiria.

“Ni haki yangu kutumia hizi nyaraka na kuwa na hati ya kusafiria ya Sudan Kusini kwa sababu mume wangu ni raia wa Sudan Kusini, ana hati ya kusafiri ya Marekani na hati ya kusafiria ya Sudan Kusini…sijawahi kughushi nyaraka zozote,” anasema Meriam.

Sudan ilisema Meriam asingeweza kutoka nje ya nchi hiyo kwa kutumia nyaraka za kusafiri za Sudan Kusini lakini Marekani ikasema, mwanamke huyo alikuwa na nyaraka zote zilizohitajika kwa ajili ya kuondoka huko (Sudan).

“Tulikuwa na nyaraka, tuliruhusiwa kusafiri kupitia eneo la VIP (watu mashuhuri), sifahamu kwa nini walifanya vile, ni ujinga. Walifanya kosa na wakataka kuficha na hawakuwa na agizo kutuzuia,” anasema Wani.

Anasema, ‘mawakala wa hofu’ walijaribu kuwapiga, na kwamba, wanasheria wao walibughudhiwa wakakimbia.

“Walivyokuja kwetu niliwauliza, mna amri ya kutuzuia? Walisema hapana, na wakaanza kutumia nguvu, waliwatupa mawakili nje ya uwanja wa ndege, wakawapiga,” anasema.

“Ilikuwa inatisha, watu wa ulinzi wa siri, usalama wa taifa, ilizidi, walituchukua, walipoanza kutumia nguvu kwa mke wangu nilimwambia ‘usikatae, nenda tu’…walificha walichokifanya kutoa huu uamuzi,” anasema Wani.

Msemaji wa Serikali ya Marekani, Marie Harf anasema ilikuwa ni juu ya serikali ya Sudan kumruhusu Meriam aondoke nchini humo.

Mawakili wa Meriam walithibitisha kwamba, mwanamke huyo alituhumiwa kughushi nyaraka za kusafiria, na ikadaiwa kwamba, kama angepatikana na hatia, kwa mujibu wa sheria za Sudan, angeweza kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela. Ofisi ya Rais wa Sudan Kusini imesema, Meriam alipewa hati za kusafiria za nchi hiyo kwa sababu mumewe, Wani, pia ana uraia wa huko.

Meriam, mumewe na watoto wao waliwekwa kizuizini, siku mbili baadaye tuhuma dhidi yao zilifutwa, wakapelekwa kukaa katika ubalozi wa Italia nchini Sudan hadi walipochukuliwa kupelekwa Vatican wakifuatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Lapo Pistelli ambaye alikuwa anafuatilia kwa karibu kesi ya mwanamke huyo.

Wakati wakiwa kizuizini Sudan, Meriam alikaririwa akisema, yeye, mumewe na watoto wao walikuwa eneo salama, lakini hayakuwa mazingira mazuri.

Ingawa Meriam yupo huru, kuna jambo linalomuumiza, na kwa mujibu wa kauli yake, binti yake, Maya mwenye umri wa miezi miwili, ana ulemavu wa viungo uliosababishwa na namna alivyojifungua akiwa amefungwa minyororo Mei 27 mwaka huu akiwa katika gereza la wanawake liitwalo Omdurman kaskazini ya Khartoum.

Kwa mujibu wa Meriam, alilazimishwa kujifungua wakati miguu yake ikiwa imefungwa minyororo, na kwamba, Maya hakuzaliwa katika mazingira anayostahili kujifungulia mwanamke hivyo mtoto huyo ni mlemavu wa viungo.

“Nilijifungua nikiwa nimefungwa,” anasema Meriam na kuongeza kuwa,“ si nguo, lakini minyororo miguuni. Sikuweza kupanua miguu kwa hiyo wanawake walinibeba kunitoa mezani, sikulala juu ya meza.”

“Kuna kitu kimetokea kwa mtoto, sifahamu baadaye kama atahitaji msaada kutembea au la,” anasema.

Wakati anayasema hayo, Meriam anabainisha kwamba, kwa kuzingatia mambo yaliyokuwa yametokea, hafahamu ni uamuzi upi ulikuwa sahihi ambao ungepunguza hatari kwa familia yake.

“Siwezi hata kuamua cha kufanya sasa. Nataka kusafiri lakini wakati huo huo sitaki kusafiri, lakini kwa hali niliyopo sasa ina maana nalazimika, kuna tatizo jipya kila siku kwa ajili ya mimi kuishi,” anasema Meriam.

Wakati wakiwa kizuizini nchini Sudan, Mchungaji William Devlin anayeongoza Kanisa la Biblia la Manhattan jijini New York alikwenda kuwatembelea, akawaombea na kujitolea kuwalipia nauli ya kwenda Marekani, kuwapa makazi kwenye nyumba ya kanisa hilo, na kuwapatia fedha za matumizi watakapokuwa huko.

“Mimi na kaka mwingine mtumishi wa Mungu tumeweza kwenda kwenye ‘nyumba salama’ inapoishi familia hii hivi sasa Khartoum na kuwahubiria kwa zaidi ya saa,” anasema Devlin.

“Nilikuwa na furaha kumuuliza Meriam kama ningeweza kumbeba Maya ambaye wakati huo alikuwa analia, na macho yangu yalitokwa machozi wakati huyu mtoto aliyezaliwa gerezani alipolala usingizi mikononi mwangu na nikamkumbatia. Na wakati tunaondoka niliweza kuweka mikono kwenye hii familia na kuwaombea kwa jina la Yesu,” anasema.

Makala haya yataendelea wiki ijayo ambapo yataangalia safari ya familia ya Wani alipokaribishwa mjini Vatican na Papa Francis. Walipitia Vatican kwa mwaliko wa Papa ikiwa ni sehemu ya safari yao ya kuelekea New Hampshire, Marekani.

TAMKO la Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu (UDHR 1948), Mkataba ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi