loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mizani ya dijiti yadaiwa kuwapunja wakulima

Kabla ya ujio wa mzani wa dijiti, mzani wa rula ndio uliokuwa ukitumika, ukapigwa marufuku kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya kupunja wakulima. Taarifa kwa vyombo vya habari zilizotolewa na wakala wa vipimo mkoani Shinyanga zinaonesha kwamba katika kilo 90 mkulima anazouza kwa wanunuzi wa pamba, kwa mfano, anaweza kuibiwa kuanzia kilo nane hadi 40.

Katika msimu wa pamba wa mwaka 2011/12 imebainika kwamba kiwango cha chini ambacho mkulima aliibiwa ni kilo nane na kiwango cha juu ni kilo 32.

Kaimu wakala wa vipimo, Juma Chacha, anasema katika tukio lililotokea Agosti 16 mwaka jana, mnunuzi wa pamba aliyefahamika kwa jina la Mabula alikutwa na kosa la kutumia mizani ya dijiti inayopunja hadi kilogramu 40 katika furushi moja la pamba la kilo 90 na alipohojiwa alikiri kuwa alikwishanunua tani 100 huku akitumia mzani huo unaopunja.

Kilo moja ya pamba mwaka huo iliuzwa Sh 660 na hesabu za wakala wa vipimo (WMA) zinaonesha kuwa wakulima wameibiwa jumla ya Sh 26,330,400. Takwimu za Bodi ya Pamba zinaonesha kwamba wakulima kwa kutumia mizani ya rula kwa msimu uliopita na kiasi kidogo kwa kutumia mizani ya digiti wameibiwa kati ya Sh bilioni 8.4 hadi 6.

Taarifa kwamba hata mzani wa dijiti nao unachakachuliwa na wanunuzi na hivyo kuwa chanzo cha kuwaibia wakulima wa pamba zimewashitua wadau wengi wa pamba wakiwemo wakulima na sasa wanataka serikali ihakikishe inakomesha wizi huu. Mkulima mmoja wa Shinyanga aliyejitambulisha kwa jina moja la Lukanya amesema wanunuzi wanafanya dhuluma hiyo utadhani hawajui adha aipatayo mkulima kutokana na kufanya uchakachuaji wa waziwazi.

Lukanya anawaona watu wanaomdhulumu mkulima kupitia mzani kama majambazi mwingine ambaye anapaswa hata kuchomwa moto kwa kupigwa na wananchi.

Matatizo mizani ya dijiti

Uchunguzi unaonesha kwamba mzani wa digiti unatumia umeme wa jua (solar) na kwamba kama umeme ukipungua unapoteza ufanisi wake na kuweza kumpunja mkulima. Imeelezwa kwamba umeme ukipungua ama kuisha, mzani unaweza kusema kinyume (anticlockwise) na kwa vile wakulima wengi hawana utaalamu basi ni rahisi sana kuibiwa.

Kadhalika, inadaiwa kwamba utunzaji wake ni mgumu kwa kuwa hauvumilii mitikisiko kwenye gari, na hasa ikizingatiwa kwamba barabara nyingi za kuelekea maeneo ya vijijini mbovu, lakini kubwa ni kwamba mzani wa dijiti ukipata baridi kali ama unyevu unaufanya pia kupoteza vipimo na mara nyingi humpunja mkulima.

Mzani huo pia unaelezwa kwamba una kitu kama mnyororo ambacho mtu akikivuta, basi unasoma kadri anavyotaka na hivyo kuwa rahisi kumwibia mkulima. Lakini kubwa na lililowatatiza wakulima wengi katika kupindi cha miaka mitatu tangu mizani hiyo kuingia nchini ni kuwekewa programu maalumu inayomkata mkulima kilo 10 (tare weight).

Hii ni tofauti na mizani ya rula iliyokuwa inakata kilo moja kufidia shuka ama kitenge alichofungia pamba mkulima. Hata hivyo, tayari mamlaka husika zimeagiza mizani hizo za dijiti ziondoe ukataji huo wa kilo 10 na badala yake iwe moja, lakini kwa miaka mitatu ambayo wakulima wamekatwa ni maelfu kwa maelfu ya kilo.

Bodi ya Pamba inasema malalamiko yaliwafikia yakionesha kuwa mizani inapunja kwa kupitia tare-weight iliyowekwa. Kwa mantiki hiyo bodi inasema malalamiko hayo yameshapelekwa nchini India kulikotengenezwa mizani hizo kwa kutaka tareweight ziondoke. Mizani ya dijiti ziliingizwa nchini kwa maombi maalumu kutoka India ambapo mmoja unagharimu dola 200.

Vipimo wathibitisha

Wakala wa vipimo nchini (WMA) ndio wenye jukumu la kumlinda mlaji akiwemo mkulima kwa kuhakikisha kwamba vipimo vinavyotumika katika biashara viko sahihi. Akitoa taarifa kwenye kikao cha ushauri wa mkoa (RCC) mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Kaimu Wakala wa Vipimo mkoani hapa, Juma Chacha alisema mizani zimekuwa zikiharibika ama kuharibiwa na hivyo kuwapunja walaji.

Alisema kati ya Julai 2012 hadi Septemba 2012 jumla ya vituo 1593 vilikaguliwa na wakala huo na kubaini kwamba miongoni mwa mizani 1287 iliyokaguliwa, 936, sawa na asilimia 73 iligundulika kwamba inapunja wakulima. Asilimia 90 ya mizani iliyokaguliwa ilikuwa ni mizani ya rula na asilimia 10 ya digiti.

Katika kipindi hicho cha ukaguzi, mizani za digiti hazikuwa zinatumiwa sana kwa kuwa ndio zilikuwa ziko kwenye uhamasishaji mkubwa wa utumiaji wake na makampuni mengi hayakupata fursa ya kununua mizani hizo na hivyo kuruhusiwa kuendelea na utumiaji wa mizani za rula.

Pia anasema katika ukaguzi ulioendelea baadaye ulibaini kuwa wakulima hupunjwa kati ya kilo saba au zaidi katika furushi la kilo 90. Anasema upigaji marufuku mizani za rula ulilenga katika kukabiliana na wahalifu wanaochezea mizani ili kuwapunja wakulima wakati wa ununuzi wa pamba na kwamba ni agizo lilitolewa katika msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2009/10 kupitia tangazo la Serikali namba 233 la tarehe 03/07/2009 Mizani ya rula irejeshwe?

Baadhi ya wadau wa pamba wanasema kwamba kwa vile mzani wa dijiti inapunja endapo utachezewa na ni rahisi kuichezea, ni vyema ile ya rula ikaendelea na hizi kupigwa marufuku mara moja.

Mkulima mmoja wa pamba anadai kuwa mzani wa rula ulipigwa marufuku na serikali mwaka 2009 kwa shinikizo la Chama cha Wafanyabiashara (TCA), lakini inaonekana lengo lilikuwa ni kuwafanya watu wafanye biashara ya kuuza mizani ya dijiti kuliko ukweli wa mambo.

Kumbukumbu zinaonesha kwamba mizani ya rula ilianza kutumika hata kabla ya uhuru na mara baada ya kuingia soko huria kwenye miaka ya 1990 katika sekta ya pamba mizani hiyo iliendelea. Inaelezwa kwamba huko nyuma hakukuwa na malalamiko yoyote lakini hujuma ilianza kuenea kidogokidogo, mawakala wakaongezeka, uharibifu wa mizani ukatokea baada ya kuwepo mafundi wa kuzikarabati mizani za rula.

Mdau mmoja wa pamba anasema kilichogundulika sasa ni kwamba, mbali na kutofaa katika mazingira yetu ya vijijini, ni rahisi kuchezea mzani wa dijiti kuliko ule wa rula, jambo ambalo linaendelea kuwa kama silaha ya maangamizi kwa mkulima masikini.

Jambo lingine linaloonesha umuhimu wa serikali kufikiria upya kuhusu kurejesha matumizi ya mzani wa rula, ni ukweli kwamba mzani huo ambao umekuwa ukitumika tangu enzi za mkoloni unakabiliana na mazingira ya aina zote iwe jua, mvua, vumbi na vinginevyo kuliko ilivyo kwa mizani inayotumia umeme ya dijiti.

Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (Shirecu), Joseph Mihangwa, bado anaamini kwamba mzani wa rula ndio unaofaa bado kwa mazingira ya sasa na kwamba bado unatumika nchi nyingi.

“Wanaozichezea hizi mizani za rula wanajulikana lakini kuna kigugumizi tu cha kuwakomesha... Ni mizani zinazotufaa bado kuliko hizi za dijiti. Ni lazima turudi kwenye mizani za rula kwa sababu zinafaa,” anasisitiza Mihangwa. Mihangwa anasema faida nyingine ya kutumia mzani wa rula ni kwamba mkulima anaona kwa macho yake vipimo, tofauti na mzani wa dijiti ambapo wakulima wengi hawajui vizuri kusoma namba zinazojitokeza.

Wadau wa pamba wanaamini pia kwamba kutokana na ulegevu wa kuwachukulia hatua kali wachakachuaji ndio maana mizani ya rula ikaonekana kama haifai. Wanasema ilifikia hatua hata fundi wa baiskeli ‘akaonekana mitaani akikarabati’ mzani wa rula ili kumpunja mlaji bila wasiwasi, hali ambayo ilisababisha serikali kuzuia matumizi yake badala ya kupambana vikali na wahusika wanaozichakachua.

Mkurugenzi wa Kanda wa Bodi ya Pamba, Buluma Kalidushi naye anasema hakuna haja ya kupambana na vipimo vilivyopo bali kupambana na wanadamu, kwani ndio wanaovichakachua kwa lengo la kuwaibia mkulima na kujipatia utajiri wa haraka.

Kuhusu kukomesha tatizo la uchakachuaji wa mizani, Ofisi ya Wakala wa Vipimo Shinyanga, inasema wakala huo pekee hauwezi kumaliza tatizo hilo hasa ukizingatia idadi ndogo ya watumishi waliopo ambao pia wanawajibika kufanya kazi katika mikoa ya Simiyu, Geita na Shinyanga yenyewe. Ofisi hiyo ina wafanyakazi sita.

Aidha ofisi hiyo imekuwa inawataka madiwani na watendaji wa vijiji kusimamia zoezi hili kwa kushirikiana na wakala ili kuhakikisha uchakachuaji wa mizani unakomeshwa. Wakala huo unaamini kwamba viongozi hao wa wananchi, wakishirikiana vyema na wakala badala ya kushirikiana na wanaochakachua, basi itakuwa njia mwafaka ya kumaliza tatizo hilo.

Kuhusu matumizi ya sheria, wakala huo umesema sheria iliyopo ya kuwaadhibu wanaokutwa na makosa ya kuchezea mzani haina nguvu kwani inaeleza kuwa mtu anayepatikana na kosa la kuchezea mzani anatozwa faini au kifungo na kuendelea na kazi yake. “Hapo utaona sheria bado inampa mwanya mhalifu aendelee kuiba.

Ingekuwa mtu akikutwa na kosa haruhusiwi tena kununua pamba na kunyang’anywa leseni mpaka mwisho wa maisha yake, tatizo hili lingeweza kutibika,” anasema ofisa wa WMA akitaka jina lake lisitajwe gazetini.

Wakulima na wasiwasi

Wakulima bado wana wasiwasi kwamba huenda kupunjwa kukaongezeka kutokana na kukosa elimu ya kuzitambua mizani za dijiti licha ya agizo la kutaka kilo 10 wanazokatwa ziondolewe na kukatwa kiko moja pekee kama enzi za kutumia mzani wa rula.

Wakulima wengi wameshangaa kuambiwa kwamba kilo 10 walizokuwa wanakatwa kwa miaka mitatu eti ni kufidia shuka, khanga ama kitenge wanavyofungia pamba, vitu ambavyo ni nadra kuzidi kilo moja.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga, Ngassa Mboje anasema, halmashauri imekuwa ikikusanya mapato kidogo kutoka kwa wanunuzi ya pamba kwa vile mahesabu yanafanywa kwa pamba iliyonunuliwa. Kwa mantiki hiyo anasema halmashauri yake itahahakikisha inafuatilia kwa karibu wizi huo ili kuudhibiti.

Nani anachakachua?

Chanzo cha uchakachuaji kimekuwa kikieleza kuwa ni vijana kutaka utajiri wa haraka kwa madai kwamba wenye makampuni hawawezi kufanya hivyo kutokana na mizani zao kukaguliwa na wakala wa vpimo na kisha kupatiwa kibali.

Inaelezwa kwamba wakishapata vibali, wanachokifanya ni kuwapatia wasimamizi wanaonunua pamba kwenye vituo ambao ndio kucheza mchezo wa kuchakachua.

Aliyekuwa mhasibu wa Mamlaka ya Pamba Tanzania katika miaka ya 1980 kabla ya kuwa chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (Shirecu), Leornad Derefa anasema kuwa kilimo cha pamba kinafanyiwa hujuma kubwa, jambo ambalo linawarudisha nyuma wakulima na kwamba halipaswi kuacha likaendelea.

Derefa naye anaona kwamba mzani wa dijiti haumfai mkulima ambaye hana mazoea ya kusoma namba na kwamba ni rahisi kudanganywa akaridhika hata kama mzani haujachakachuliwa. Anasema enzi zao, wizi kwa mkulima haukuwepo na hata kama ulikuwepo ni wa siri kubwa sio huu wa sasa unaofanywa waziwazi.

Naye anawatupia lawama wasimamizi wa sheria kwamba ndio chanzo cha mizani kuchezewa.

Waungaji mkono dijiti

Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa pamba (TCA), Boaz Ogola anasema kuwa mizani za digiti zimefanyiwa utafiti na kubainika kwamba zinafaa na zinapunguza udanganyifu na hasa kwa vile zinakwenda na wakati kwa kutumia teknolojia ya ksasa.

Yeye anadhani kwamba baadhi ya matatizo yanatokana na wakulima kukosa elimu juu ya mizani za aina hiyo. Kuhusu umeme anasema mzani huo ukikolea jua unakaa hata siku saba na kwamba hilo halijawahi kuwa tatizo. Lakini katika hili malumbano hayana maana.

Kinachoaminika sasa ni kwamba mkulima anaibiwa na kwamba kumbe mzani wa dijiti ni rahisi kuuchezea kuliko wa rula. Pengine ni wakati mwafaka sasa wa kurekebishe sheria huku vyombo vinavyosimamia vipimo vikiongeza umamini na ukali. Vinginevyo vyombo hivyo, hususan wakala wa vipimo, unaweza kufikiriwa kwamba unashirikiana na wahalifu.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi