loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mji Mkongwe: Hazina ya historia ya Zanzibar inayostahili kuenziwa

Kisiwa hiki kipo Bahari ya Hindi karibu na Dar es Salaam. Unguja ni kisiwa kikuu cha Zanzibar ambacho ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Kisiwa hicho kina mikoa mitatu ambayo ni Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na Unguja Mjini Magharibi na eneo lake ni takribani kilomita za mraba 1,658.

Mji Mkongwe uko katika fukwe za Magharibi ya kisiwa cha Unguja, ndio mji mkuu wa eneo hili na ni miongoni mwa maeneo yanayoiwakilisha Tanzania kuingia katika orodha ya nchi zenye vivutio vya kipekee vilivyoorodheshwa katika urithi wa Dunia uliohifadhiwa na Shirika la Kimataifa ya Maendeleo ya Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO).

Mji Mkongwe umebeba hazina ya historia ya Zanzibar kwa sababu ndani yake kuna vivutio vingine na kumbukumbu za kipekee kuhusu maendeleo ya binadamu, mila na desturi za watu wa Zanzibar. Kwa mujibu wa historia mji huo ulianza mwaka 1830 wakati SultaniSayyid Said alipohamisha mji wake mkuu kutoka Omani na kuweka makazi yake mapya katika kisiwa cha Unguja, Zanzibar.

Mji huo uliitwa Mkongwe kwa sababu ulikuwa mji wa kwanza kujengeka na kuipatia Zanzibar umaarufu katika biashara kati ya Waarabu na Waafrika hasa biashara ya utumwa. Hivi sasa Mji Mkongwe ni mji mkubwa wa kisiwa cha Unguja, pia jina hilo linatumika kuwasilisha Wilaya ya Mji Mkongwe iliyopo katika Mkoa wa Unguja Mjini Magharibi.

Mji mkongwe ulikuwa kitovu cha biashara ya viungo mbalimbali vya kupikia na uliendelea kuwa mji mkuu wa Zanzibar hata wakati wa utawala wa mkoloni mwa Kiingereza. Baada ya Uhuru na muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mji huo uliendelea kuwa makao makuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mji huo unaendelea kuboreshwa na Serikali la Mapinduzi ya Zanzibar inajitahidi kutunza vitutio vyote vya utalii vinavyopatikana katika mji huo ili kutunza kumbukumbu ya Zanzibar kwa ajili ya urithi wa kizazi cha sasa na kijacho. Miongoni mwa vivutio vinavyopatikana katika mji huo ni nyumba ya maajabu, boma la kale, Kanisa Kuu la Kianglikana ambalo limejengwa sehemu iliyokuwa inatumia kama soko la watumwa.

Pia mji huo una nyumba nyingi za kihistoria za ghorofa zilizojengwa na famila za tabaka ya matajiri wa Kiarabu ambazo milango yake imechongwa kitaalamu na kuwekwa nakshi kwa kutumia michoro mbalimbali yenye mvuto wa kipekee. Mji Mkongwe ni maarufu kwa kuwa na sanaa ya kipekee hasa katika ujenzi wa majengo katika Kanda ya Afrika Mashariki.

Ujenzi wa majengo unawakilisha tamaduni za Waswahili ambao umejengeka kutokana na mwingiliano wa tamaduni za mataifa mbalimbali yaliyofika Zanzibar ikiwa ni pamoja na Waarabu, ghuba ya Uajemi, Waasia na Waingereza. Mji Mkongwe unajumuisha pia mji mpya wa Ng’ambo.

Jengo la kwanza la Mji Mkongwe lilijengwa mwaka 1830 na mji huo uliendelea kujengeka eneo ambalo awali lilikuwa kijiji cha uvuvi. Mji huo uliendelea kujengwa chini ya utawala wa Sultani kutoka Oman.

Mabadiliko muhimu katika Mji Mkongwe yalianza kuonekana Mwaka 1840, Sultan Said bin Sultan alipohama kutoka Maskati, Omani na kuishi katika Mji Mkongwe, kipindi ambacho Zanzibar ilikuwa katika hatua ya maendeleo kwa kujenga makazi ya Sultani na maendeleo ya Zanzibar kwa ujumla.

Mnano mwaka 1861 ilitokea vita miongoni mwa familia ya Kifalme ya Sultani wa Omani na Zanzibar jambo lililosababisha kuvunjika kwa uhusiano wa Zanzibar na Oman. Zanzibar ilijitegemea chini ya utawala wa Majid bin Said. Mji Mkongwe uliendelea kujengeka na mwanzoni mwa karne ya 19 ulipata umaarufu na kuwa kituo cha biashara ya kimataifa hasa ya karafuu pia biashara ya utumwa.

Hata hivyo biashara ya utumwa ilikomeshwa mwaka 1897 na kuufanya mji huo kuendelea kuwa kituo cha kihistoria kuhusu biashara ya utumwa. Katikati ya karne ya 19 wafanyabiashara wengi kutoka Oman, Uajemi na India walihamia Zanzibar na kuufanya Mji Mkongwe kuwa kitovu cha biashara ya kimataifa.

Wakati wa utawala wa mkoloni wa Uingereza Mji Mkongwe uliendelea kuwa kituo muhimu cha biashara ingawa utawala huo ulitoa upendeleo wa mji wa Mombasa na Dar es Salaam kama vituo vya biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mji Mkongwe umehifadhi kumbukumbu ya kipekee ya ukombozi halisi wa Wazanzibari kwa kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalifanyika katika mji huo na kuondoa utawala wa Kisultani na kuweka Utawala kijamaa chini ya chama cha Afro – Shirazi (ASP).

Mji Mkongwe una mandhari nzuri iliyozungukwa na bahari ya Hindi, una majengo marefu yaliyojengwa kwa mpangilio kwenye mstari na kufanya mitaa mirefu iliyonyooka. Pia kuna maduka na misikiti iliyojengwa vizuri na kuufanya mji huo kuwa kivutio kikubwa kwa wageni.

Majengo ya mji huo yamejengwa kwa muundo wa kipekee na kuufanya ufukwe wa Zanzibar kuwa kivutio kikubwa kwa wageni ambao wanafika au kupita Zanzibar kwa usafiri wa majini au angani kwa kuwa majengo hayo huonekana kwa urahisi wakati meli au ndege inapokaribia kuwasili katika visiwa vya Zanzibar.Majengo hayo yanajumuisha jumba la kifahari na la kihistoria la utawala wa Kisultani, makanisa, misikiti na taasisi mbalimbali.

Mwaka 2000 mji huo uliingizwa kwenye orodha ya urithi wa dunia ili kuhakikisha kuwa unaendelea kutunzwa na kuhifadhiwa vyema kwa kuwa una mambo mengi muhimu yanayopaswa kuhifadhiwa vyema ili yatumike kama kumbukumbu ya sanaa za kale pia kama kituo cha mafunzo juu ya historia, utamaduni, maendeleo ya jamii na ukuaji wa miji ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Mji mkongwe umekuwa hazina ya historia Zanzibar kwa kuwa umehifadhi kumbukumbu nyingi za utamaduni, siasa na uchumi pia unajumuisha maeneo mengi yanayotumika kama makumbusho ya Taifa. Jumba la Maajabu maarufu kama Beit-al-Ajaib kwa lugha ya kiarabu ni miongoni mwa vitu vya kipekee vinavyopatikana katika Mji Mkongwe.

Jumba hilo lipo barabara ya Mizingani katika ufukwe wa bahari na linaonekana kwa urahisi unapoingia Zanzibar kwa njia ya bahari. Pia katika mji huo inapatikana Ngome Kongwe ambayo ipo mkabala na Jumba la Maajabu. Ngome iliyojengwa na mawe mazito ilijengwa na watu wa Omani karne ya 17 kwa ajili ya kujihami dhidi ya maadui.

Hivi sasa ngome hiyo inatumika kama kituo cha utamaduni. Ina maduka na eneo la maonesho ya ngoma za asili kwa ajili ya kudumisha mila la utamaduni wa watu wa Zanzibar. Pia mji huo una zahanati kongwe maarufu kama Ithnashiri ambayo ilijengwa kati ya mwaka 1887 na 1894 kama hospitali ya kusaidia watu masikini ila baadaye ilibadilishwa na kuwa zahanati.

Zahanati hiyo ni miongoni mwa majengo yaliyojengwa kwa muundo wa kipekee ambapo sehemu ya jengo imejengwa kwa mbao nzito zilizochongwa maua na maumbo mbalimbali ya kupendeza yanayovutia. Maumbo hayo yanadhihirisha ujuzi wa binadamu wa kubuni vitu mbalimbali na kuviweka katika maumbo kwa njia ya sanaa.

Kitu kingine muhimu katika mji mkongwe ni Jumba la Makumbusho ambalo pia linajulikana kama jumba la Sultani au Beit el-Sahel kwa lugha ya kiarabu.

Jumba hilo liko kaskazini mwa Jumba la Maajabu na lilijengwa mwishoni mwa karne ya 19 na sasa linatumika kama jumba la Makumbusho Zanzibar na limesheheni kumbukumbu juu ya maisha ya familia ya Kifalme Zanzibar ikiwa ni pamoja na mali za Princess Sayyida Salme ambaye alitoroka na kwenda kuishi ulaya na mume wake.

Makao makuu ya Kanisa Anglikana Zanzibar yaliyopo katika barabara ya Mkunazini ni miongoni mwa urithi na kumbukumbu muhimu iliyopo katika Mji Mkongwe. Kanisa hili lilijengwa mwishoni mwa karne ya 19 wakati wa uongozi wa Askofu Edward Streere ambaye alikuwa askofu wa tatu wa Anglikana Zanzibar.

Kanisa hilo linachukua eneo kubwa la Mji Mkongwe kwa kujumuisha eneo lililokuwa linatumika kama soko kubwa la la biashara ya watumwa.

Eneo hilo limekuwa maarufu zaidi kwa kuwa limetumika kutokomeza kwa hiari biashara ya utumwa. Kitendo hicho kinalifanya eneo hilo kuwa kitovu cha kukataa ukatili dhidi ya binadamu, kulinda heshima na utu wa binadamu pasipo kuangalia tabaka linalosababishwa na kipato, utamaduni, rangi, itikadi za kidini wala kisiasa.

Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph lililojengwa na wamisionari wa Kifaransa kati ya mwaka 1893 na 1897 ni miongoni mwa vivutio na kumbukumbu muhimu iliyopo katika Mji Mkongwe. Bafu maarufu kwa jina la Hamamni na msikiti wa Malindi pia ni miongoni mwa majengo ya kale yaliyoachwa kama urithi kwa ajili ya kuendeleza Uislamu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Msikiti huo ulijengwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni na umekuwa miongoni mwa majengo yenye muundo wa kipekee katika misikiti iliyopo ukanda wa Afrika Mashariki. Jumba la Livingstone lilikuwa miongoni mwa kasri ndogo iliyojengwa kwa ajili ya Sultani Majid bin Said, lakini baadaye matumizi ya jengo hilo yalibadilishwa na kwa nyuma ya Wamisionari wa Kiingereza ambapo David Livingstone aliishi.

Jengo la Tippu Tip limehifadhiwa kama sehemu ya historia muhimu kwa kuwa ndio alipokuwa akiishi mfanyabiashara aliyejihusisha na biashara ya watumwa. Jengo la Mahakama Kuu lililopo katika Barabara la Kaunda karibu na bustani ya Victoria pia liko kwenye kumbukumbu muhimu kwa kuwa lina mchanganyiko wa kumbukumbu za utamaduni wa Kiislamu na utamaduni wa Kireno.

Uzuri wa mji huo umekuwa kivutio cha watalii ambao hufika Zanzibar kila mwaka kwa ajili ya kujifunza juu ya mambo ya kale na kujionea wenyewe juu ya uzuri wa visiwa wa Zanzibar. Hata hivyo, ni Watanzania wachache wanaofika eneo hilo kwa ajili ya kujifunza mambo ya kale jambo ambalo linasababisha Watanzania kuendelea kuwa mbumbumbu wa historia na mazingira na yao wenyewe.

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa ...

foto
Mwandishi: Kaanaeli Kaale

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi