loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkakati wa STHEP ulivyolenga kuikomboa elimu ya juu

Huo ni ushauri uliotolewa hivi karibuni na Makamu wa Rais Dk Mohammed Bilal, wakati akizindua Mradi wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu (STHEP) unaolenga kuongeza idadi ya wahitimu nchini na kuwapa uwezo walimu katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Teknolojia.

Mradi huo ambao umeanzishwa kwa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia umejikita katika nyanja kuu nne ambazo ni kuboresha rasilimali watu kwa kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi, kujenga, kupanua na kukarabati vyumba vya mihadhara, maktaba, maabara na karakana.

Aidha mradi huo pia umejikita katika kununua vifaa vya kufundishia vikiwemo vifaa vya maabara na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), vitabu na magari, kuboresha mitaala, sera na usimamizi kwa kutumia wataalamu washauri. Anafafanua kuwa maeneo yatakayoguswa na mradi huo ni pamoja na madini, uchukuzi, sayansi na teknolojia, elimu, uhandisi kilimo, uchumi na sayansi ya chakula.

Katika uzinduzi huo, Dk Bilal anafafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo, ni moja ya vipaumbele ambavyo Serikali imejiwekea katika kuhakikisha inatekeleza dira ya maendeleo ya mwaka 2025 kwa kujenga mazingira bora ya ufundishaji masomo ya sayansi. Anasema Serikali imejipanga kutekeleza sera mbalimbali ikiwemo ya kuhakikisha ina maliza tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabu.

“Mradi huu utakuwa chachu ya ongezeko la ukuaji wa masomo ya sayansi nchini yatakayosaidia kupatikana kwa walimu wengi wenye uwezo katika masomo hayo na wahitimu,” anasema. Akielezea mradi huo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi anasema umeshaanza kutekelezwa na taasisi 15 za umma ambazo ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).

Taasisi zingine ni Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE), Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Serikali cha Zanzibar (SUZA).

Aidha Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia (MCST) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nazo zinatekeleza mradi huo.

Dk Kawambwa anasema mradi huo wa STHEP uliofadhiliwa na Benki ya Dunia umeegemea katika mambo mbalimbali, ikiwemo kuwasomesha walimu katika viwango vya shahada ya uzamili na uzamivu katika masomo ya sayansi na kujenga maabara, kununua vitendea kazi na ofisi.

Pamoja na hayo anafafanua kuwa kupitia STHEP sasa changamoto za elimu kama vile uhaba wa vyumba vya mihadhara na maabara za sayansi na teknolojia na mapungufu katika idadi ya wahadhiri wa sayansi teknolojia na ualimu wenye sifa zinatafutiwa ufumbuzi. Changamoto nyingine zitakazoshughulikiwa na mradi huo ni pamoja na uhaba wa vifaa vya maabara na vitabu na tatizo la idadi ndogo ya wanaopata mikopo ya Elimu ya Juu.

Naye Mratibu wa Mradi huo wa STHEP Dk Kenneth Hosea anafafanua kuwa kupitia mradi huu ambao ni moja ya miradi mikubwa ya elimu ya juu kuwahi kutekelezwa nchini, hadi sasa umewasomesha jumla ya watumishi 191 wa taasisi za umma masomo ya Shahada ya Uzamivu na watumishi 208 wanasoma masomo ya Uzamili katika fani za sayansi teknolojia na ualimu.

“Watumishi hawa wanasomeshwa katika vyuo vikuu bora katika Dunia ya Kwanza, mfano Uingereza asilimia 30, na wengine katika Dunia ya Pili, mfano Afrika Kusini na kwingineko asilimia 30 na waliobaki asilimia 40 wanasomeshwa hapa nchini.

Anaongeza kuwa “Katika eneo la mafunzo ya muda mfupi tayari watendaji wa Serikali na watumishi wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu watatu wamepelekwa India kujifunza masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano na sasa Bodi ya Mikopo inapokea maombi ya wanafunzi kupitia mtandao tofauti na zamani.”

Anafafanua kuwa asilimia 15 ya watumishi wanaosomeshwa na mradi huo wamekamilisha masomo yao na wengine watamaliza mwishoni mwa mwaka huu.

Aidha anasema watumishi 467 wamesomeshwa mafunzo maalumu ya muda mfupi, huku wanafunzi 1,831 wakitarajiwa kufaidika na mradi huo vifaa vya maabara takribani 5,400 vimenunuliwa pamoja na vifaa vya TEHAMA 1,831, vitabu 4,598, mitambo ya kufundishia na vitatumika katika majengo 25 yanayojengwa katika taasisi 15 zinazoutekeleza mradi huo.

“Lakini pia majengo haya yatatumiwa na jumla ya wanafunzi 36,344 wa elimu ya juu na wakufunzi na wahadhiri 1,640 katika taasisi za ARU, DUCE, DIT, OUT, MUCE, SUA na UDSM,” anasema.

Anasema tayari mafanikio ya mradi huo yameanza kuonekana ambapo kwa upande wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) umeweza kujenga uwezo wa TEHAMA na kuwezesha kudahili wanafunzi wote wanaojiunga na elimu ya juu kwa pamoja na kuiwezesha tume hiyo kutoa mwongozo wa ubora wa vyuo vikuu.

“Lakini pia mradi umewezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuandaa miundombinu ya TEHAMA ili waombaji wa mikopo ya Elimu ya juu waombe kwa kutumia mtandao (OLAS),” anafafanua. Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na vyuo vyake vikuu vishiriki vya elimu DUCE na MUCE ni wanufaika wakubwa wa mradi ukiwa umelenga katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo maabara, kumbi za mihadhara na ofisi za waalimu.

Akifafanua kuhusu utekezaji wa mradi huo UDSM, Makamu Mkuu wa Pili wa chuo hicho Profesa Makenya Maboko, anaeleza kuwa takribani majengo sita ya kisasa yamejengwa eneo la kampasi kuu na kufanya ukarabati mkubwa wa jengo lingine moja.

Aidha katika chuo cha DUCE mradi huo pamoja na kusomesha baadhi ya wahadhiri pia umejenga majengo mawili, kwa upande wa Chuo Kikuu Huria OUT mradi huo umegharimia ujenzi wa jengo kubwa la ghorofa kumi litakalokuwa na nafasi kubwa zaidi ya kujifunzia, maktaba, maabara pamoja na ofisi za walimu.

Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kupitia mradi wa huo wa STHEP kilipatiwa fedha ili kuendeleza miradi mbalimbali ya kilimo chuoni hapo na hivyo kuanzishwa kiwanda cha kuongeza thamani ya mazao ya wakulima. Kwa mujibu wa Dk Hosea mradi huo tangu uanzishwe mwaka 2008 hadi kufikia Septemba mwaka huu, utekelezaji wake umefikia asilimia 92 na unatarajiwa kukamilika rasmi Desemba mwakani.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi