loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Moto: Janga ambalo jamii haijikingi ipasavyo

Moto unatajwa kama janga kutokana na ukweli kuwa aghalabu madhara yake huwa makubwa kama vile, kupoteza mali na kusababisha majeraha na hata vifo. Sikia tu kwa mwingine lakini ikitokea nyumba yako na mali vikateketea kwa moto unaweza hata kukufuru Mungu. Zipo simulizi zinazoonesha kwamba baadhi ya watu walioshuhudia nyumba zao na mali zote zikiteketea kwa moto walitamani nao kujitosa ili wateketee.

Kuna matukio kadhaa ya moto yaliyowahi kutokea hapa nchini ambayo bado yako kwenye kumbukumbu za wengi. Mfano wa majanga hayo ni tukio la lori la mafuta kupinduka katika kijiji cha Isongole mkoani, Mbeya Mwaka 1999 na kuangamiza mamia ya wanakijiji waliokuwa wakizoa mafuta baada ya moto kulipuka eneo hilo.

Inasemekana kuna mtu alijaribu kutaka kuiba ama kuchomoa betri ya gari hilo la mafuta lililopata ajali na kulipusha moto!

Tukio lingine linalokumbukwa ni kuungua kwa bweni la Shule ya Sekondari ya Shauritanga mwaka 1994 na kuua wanafunzi 41, kisha tukio lingine ni la mwaka 1999 ambapo wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari Idodi, Iringa, walikufa baada ya bweni lao kushika moto huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Yapo pia matukio ya gari za abiria kuungua moto na mfano ni ajali ya kampuni ya mabasi la Deluxe iliyoanguka Oktoba 25 Mwaka 2011, Kibaha mkoani Pwani na kisha kuteketea kwa moto sambamba na kusababisha vifo vya watu 25 waliokuwa wakisafiri na basi hilo.

Mbali na matukio ya moto yanayoteketeza idadi kubwa ya watu kwa mpigo, yapo matukio ya kuungua kwa nyumba, viwanda na masoko na mfano ni ajali za mara kwa mara katika masoko ya mkoani Mbeya na hata Moshi.

Yote haya na mengineyo yanadhihirisha ukubwa wa tatizo hilo ambalo kukabiliana nalo kunahitaji uwepo wa ushirikiano na mikakati mbalimbali kutoka kwa wadau wote.

Kuna matukio ya ajali ya moto yanayotokana na uzembe wa watu na yapo baadhi ya matukio ambayo chanzo chake ni vigumu kukielezea lakini kwa pamoja, tiba yake ni kwa kila mwananchi kuchukua tahadhari mapema ili kufanya yasitokee ili kuepusha madhara ya mali na maisha na hasa kuzingatia msemo wa Wahenga kwamba ‘kuzuia ni bora kuliko kuponya’.

Yapo matukio mengi ya majanga ya moto yaliyotokana na hitilafu za umeme katika majumba, masoko na maeneo mengine ambayo kimsingi kuyauzuia yasitokee kunahitaji utaalamu na umakini ukiwemo wa matumizi sahihi ya vifaa mbalimbali vinavyotumia nishati hiyo.

Matumizi ya vibatari, na hususan mishumaa, inatajwa pia kuwa chanzo cha majanga mengi ya moto majumbani. Kimsingi jamii kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya namna ya kujikinga na matukio ya moto, ni kitu kingine kinachosababisha kuendelea kutokea kwa ajali za moto za mara kwa mara na kuleta madhara ambayo mwisho wake ni majonzi na masikitiko kwa jamii nzima.

Uwepo wa elimu juu ya jambo lolote ndiyo msingi wa mabadiliko ya jambo husika hivyo madhara yanayosababishwa na moto pindi unapotokea katika shule, taasisi, makazi ya watu na maeneo mengine ni wakati pia wa wahusika kutoa elimu kuhusu vitu vinavyosababisha moto na namna ya kujikinga.

Kikosi cha zimamoto na uokoaji kilichoko katika Wizara ya Mambo ya Ndani kina dhima kubwa ya kusimamia shughuli zinazohusu masuala ya majanga ya moto. Ingawa majukumu yake makubwa ni kuzuia na kuokoa mali na watu pale linapotokea janga la moto, Zimamoto wanaa dhima ya kutoa elimu kwa wananchi kadri wanavyoweza bila hata kusubiri kutokea kwa majanga ya moto.

Ingefaa wahusika wawape hata bajeti ya kutoa vipindi kwenye redio, televisheni na makala kwenye magazeti.

Katika utekelezaji wa majukumu yake Kikosi cha Zimamoto kimejikuta kikikabiliana na changamoto nyingi ikiwemo ya uokoaji pale tatizo linapotokea huku hali hiyo ikichangiwa na sababu mbalimbali.

Baadhi ya sababu zinazotajwa ni miundombinu ya barabara kutokidhi haja na msongamano wa makazi unaotokana na ujenzi holela na usiofuata utaratibu wa kitaalam wa ujenzi.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara, ni ukweli usiofichika kuwa maeneo mengi hasa katika miji yamekuwa na msongamano mkubwa majumba na magari, hali inayowawia ugumu magari ya uokoaji kuwahi katika eneo la tukio na kutoa msaada pale tatizo la moto linapojitokeza na hivyo kusababisha mali au nyumba kuteketea.

Hali hiyo pia inachangiwa na ujenzi holela wa makazi usiofuata sheria, kanuni na taratibu. Hiki ni kikwazo kingine kinachosababisha matukio mengi ya moto kuathiri kwa kiasi kikubwa wananchi na hii inatokana na ugumu wa kimazingira unaosababisha vikosi vya uokoaji kushindwa ama kuchelewa kufika kwa wakati katika eneo la ajali.

Ingawa hakuna takwimu sahihi zinazoonesha ukubwa wa tatizo hilo, lakini ukweli ni kwamba makazi mengi hasa katika miji kama ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya yapo katika hali ya msongamano huku baadhi ya maeneo katika miji hiyo yakiwa hayaingiliki kirahisi kwa magari.

Kamishana Mkuu wa kikosi cha zimamoto nchini, Pius Nyambacha anathibitisha suala hilo na kusisitiza kuwa hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na Wizara ya Ardhi na halmashauri za miji kupitia idara za mipango miji kuchelewa katika kupanga mitaa na hivyo watu kujijengea kiholela.

Lakini hata kule ambako mitaa imepangwa, Nyambacha anasema kikosi chake kimekuwa hakishirikishwi katika upangaji wa mitaa kwa kuzingatia namna nzuri ya kuokoa wananchi kunapotokea majanga ya moto.

Anasema kama wangeshirikishwa wangekuwa wakitoa ushauri wao wa kitaalamu wa ujenzi wa makazi wenye kuzingatia tahadhari za pale tatizo la moto linapojitokeza. Pamoja na hilo pia anasema msongamano wa magari unaochangiwa na miundombinu ya barabara pia n

kikwazo kingine kinachokwamisha utekelezaji wa kazi zao kikamilifu hasa pale linapotokea tatizo la moto eneo fulani na kuhitaji msaada wa haraka wa kukabiliana na tatizo hilo.

“Mara nyingi suala hilo limekuwa likichangia utekelezaji wa majukumu yetu kuwa mgumu, mara nyingi miundombinu hii husababisha tusimame muda mrefu katika foleni wakati tukielekea katika uokoaji, hatua inayoifanya kazi yetu inayohitaji uharaka mwingi kutokuwa ya uhakika kwa asilimia kubwa,” anasema Kamishna Nyambacha.

Anasema hata baadhi ya madereva mitaani, licha ya magari ya uokoaji kupigia king’ora cha tahadhari, wamekuwa wagumu kuchukua uamuzi wa kuyapisha magari hayo kwa haraka, hali inayochangia ugumu wa kuwahi kwenye maeneo ya matukio.

Nyambacha anaona pia haja ya kuwaelimisha madereva juu ya masuala yanayohusu dharura mbalimbali zinazojitokeza barabarani.

Anasema katika nchi za wenzetu suala la dharura limepewa kipaumbele cha juu kiasi cha kuwepo kwa barabara maalumu zilizotengwa kwa ajili ya kupitisha kila gari lenye dharura kama hiyo ya moto, jambo analosema kwa kiasi kikubwa limekuwa likifanikisha uhakika wa kuyakabili kwa haraka matukio mbalimbali yakiwemo ya moto.

Anasema suala hili linabaki kuwa mikononi kwa Serikali kupitia wizara yake ya Ujenzi kuweka kipaumbele cha kujenga barabara zake kwa kuangalia umuhimu wa dharura ili kupunguza usumbufu wa mara kwa mara unaotokana na na msongamano wa magari barabarani na hivyo kuchelewesha uokoaji wa maisha ya watu na mali zao. Lakini anasema tatizo la moto linapotokea na kusababisha madhara mara nyingi lawama zote huelekezwa kwa jeshi hilo kwa madai ya kuchelewa kufika kwa wakati bila kutambua kuwa chanzo cha hayo yote kwamba ni msongamano wa magari na hata jiografia ya eneo husika.

“Kuna eneo jingine unaweza ukakuta pengine nyumba inayoungua ipo katikati ya nyumba mia moja na ili kuifikia ni lazima ufanya kazi ya kuunganisha mipira ya maji zaidi ya minne hadi mitano, jambo ambalo kimsingi husababisha kupunguza kasi ya msukumo wa maji na uharaka wa kuzima moto... Kuna changamoto nyingi kwetu ambazo kiukweli zinapunguza ufanisi mzuri wa kazi zetu,” anasema Kamishna Nyambacha.

Pia anasema kutokuwepo kwa vituo vya kutosha vya uokoaji hasa katika Jiji la Dar es Salaam ni sababu nyingine inayochangia ugumu wa kazi hiyo, kwani kati ya vituo zaidi ya kumi vinavyohitajika walau ili kutosheleza mahitaji ya Jiji zima ni vituo vitatu pekee ndivyo vilivyopo.

Anasema vituo hivyo ni pamoja na kituo kikuu kilichopo eneo lililopewa jina la ‘Fire’ pamoja na vituo viwili vilivyopo eneo la Mchicha na Mwenge vilivyoanzishwa hivi karibuni kwa ajili ya kusaidia suala zima la uokoaji pale linapojitokeza huku akisisitiza kuwa bado kuna umuhimu mkubwa wa kujenga vituo ikibidi kila baada ya umbali wa kilomita tano kama utaratibu unavyoelekeza.

TANZANIA na dunia nzima kwa sasa ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi