loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mpango wa kukuza uchumi kupitia kodi migodini utafanikiwa?

Mpango wa kukuza uchumi kupitia kodi migodini utafanikiwa?

Kiasi hicho ni kwa mujibu wa ripoti za kihesabu za Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) zinazoonesha uwezekano wa Serikali kulipwa mamilioni ya Dola za Marekani mwishoni mwa mwaka huo kutokana na utekelezwaji wa mikakati ya kuhakikisha inapata inachokistahili kutoka katika migodi hiyo.

Kutokana na maelezo yaliyoko kwenye ripoti hiyo, baadhi ya kodi hizo ni pamoja na inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi (PAYE), mrahaba, kodi ya mapato, ushuru wa huduma kwenye Serikali za Mitaa (Service Levy), kodi ya zuio na nyinginezo.

HabariLeo imebaini kuwepo kwa mikakati tofauti na ile ya mwaka 1998 inayotekelezwa na Serikali, ambapo, kupitia sera mpya ya madini ya mwaka 2010, imelenga kukuza mchango wa sekta ya madini katika uchumi kwa kutegemea zaidi utoaji wa huduma mbalimbali kwenye sekta hiyo, badala ya kusubiri mauzo ya jumla ya bidhaa za madini pamoja na kodi zinazopatikana baada ya migodi kupata faida (Corporate Tax).

Kwa mujibu wa sera hiyo mpya ya madini ambayo kwa kiasi kikubwa inatokana na marekebisho na maboresho ya ile ya mwaka 1998, iliyolenga zaidi ubinafsishaji, ya sasa imetamka wazi lengo la Serikali kukuza uchumi kupitia sekta ya madini kuwa ni kuhakikisha utoaji wa huduma mbalimbali katika sekta ya madini unaingiza mapato yatakayoonesha manufaa ya moja wa moja kwa watu na uchumi wa taifa.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa pamoja na mikakati hiyo, ajira ikiongezwa zaidi ya ilivyo sasa katika maeneo mbalimbali ya sekta ya madini kama vile migodini na kwenye kampuni zinazotoa huduma katika migodi mikubwa na midogo, uchumi utakua maradufu.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Bruno Mteta anasema, “Pale ambapo Tanzania itakuwa imeongeza kampuni kubwa kama vile KASCO, Caspian, Fusch, Mantrac, UKWAZ, Ausdrill, Major Drilling,Capital Drilling, Sandivik na nyingine halafu zikaajiri wataalamu zaidi watanzania, pato kubwa litabaki nchini na kusaidia kukuza uchumi.

Alifafanua na kusema ikumbukwe kuwa makusanyo ya mapato ya kodi yanategemea kwa kiasi kikubwa kodi ya mishahara yaani (PAYE) ya wafanyakazi, hivyo ajira ikiongezeka na mapato kupitia kodi hiyo yataongezeka zaidi.

Kutokana na kinachoelezwa katika sera mpya ya madini, kwa kuhakikisha inawatengenezea wazawa fursa ya kutoa huduma kwenye sekta ya madini hususan migodini kupitia kampuni zinazoanzishwa kwa lengo hilo pamoja na kuweka sheria inayowataka wawekezaji wawaajiri wazawa katika kampuni zao, Serikali imelenga kukuza ajira nchini.

Taarifa ya TMAA inaonesha kuwa migodi saba mikubwa ya uchimbaji madini nchini imeajiri moja kwa moja jumla ya watu 8,134 kuanzia mwaka 2005 hadi 2012. Katibu Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Wachimbaji na Watafutaji Wakubwa wa Madini na Nishati (TCME), Emmanuel Jengo kwa upande wake alisema kampuni zote za utoaji huduma ya uchimbaji migodini zimeajiri jumla ya watu 15,000 wanaolipa kodi kwa mujibu wa sheria za kodi za Tanzania.

Mikakati mingine iliyo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ni pamoja na mpango wa Serikali wa kuiongezea uwezo TMAA hasa katika eneo la rasilimali watu na vitendea kazi, ili iwajibike kwa ufanisi kama sera mpya ya madini inavyoeleza. Mikakati iliyotekelezwa kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alivyolieleza gazeti hili ni pamoja na kuachana na kipengele cha sheria ya madini ya mwaka 1998.

Kipengele hicho, kilikuwa kikimpa mwekezaji ruhusa ya kukopa benki kiasi chochote cha fedha kama mtaji, hivyo kukaa kwa miaka mingi bila kulipa kodi kwa kigezo cha kutumia muda huo kurejesha mkopo na riba kwenye benki husika.

“Najua Serikali haijashindwa katika sekta hii ya madini na wala haitapata hasara kwa sababu tumepitisha sheria kuwa mwekezaji yeyote kuanzia sasa atapaswa kuwa na mtaji wa asilimia 30 na asilimia 70 (uwiano wa 70:30) ndiyo atatakiwa kukopa benki. Hii ni sheria na hata hazina wanajua,” Maswi alisema na kuongeza kuwa tofauti ya muda wa kuanza kulipa kodi baada ya faida na kiasi cha kodi hiyo itaonekana zaidi kwa wawekezaji wapya kwa sababu mikopo yao na riba sasa itakuwa na kipimo,” Maswi anaeleza.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo anabainisha kuanzia sasa Serikali haitakuwa msimamizi pekee wa sekta ya madini bali itashiriki uchimbaji na uzalishaji madini kwa kulitumia shirika lake, STAMICO litakalomiliki kuanzia asilimia 20, za hisa katika kila mgodi utakaoanzishwa kwa niaba ya watanzania.

HabariLeo imebaini kuwa sheria ya madini ya mwaka 1998 ndiyo iliyoua STAMICO kutokana na masharti yake kuwa uwekezaji katika sekta ya madini uongozwe na sekta binafsi na kwamba Serikali iwe msimamizi, mtoa huduma na mhamasishaji na sio kujihusisha kuwekeza. Serikali kumiliki hisa hizo inamaanisha nini?

Philbert Rweyemamu aliyekuwa Meneja Mkuu wa mgodi wa Tulawaka kabla ya kuuzwa kwa STAMICO ambaye pia ni mtaalamu wa madini wa siku nyingi alisema, kumiliki hisa kwenye kampuni za madini za wawekezaji wa nje, serikali itakuwa na wawakilishi katika Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni husika.

Hivyo kuweza kuhoji juu ya mambo mbalimbali yatakayoonekana kuwa na walakini kwa mfano maamuzi kuhusu ajira na mambo mengine ya kisera.

“Sasa hivi hakuna mtanzania anayeingia kwenye bodi ya wakurugenzi kwa sababu inawahusu wenye hisa kwenye kampuni, hiyo ilitufunga kuhoji jambo lolote linalopangwa au kupitishwa na bodi ya wakurugenzi hata kama lilikuwa likituumiza sisi.Kwanza kwenye bodi hatuingii, tungewezaje kuhoji nje ya bodi?”Rweyemamu anasema na kuhoji.

Ukiachilia mbali ufafanuzi huo, aliyekuwa Kamishna wa madini, Dalaly Kafumu naye alitaja mikakati mingine iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na kurekebisha vipengele vingine zaidi ya vitano vya sheria ya madini ya mwaka 1998, vilivyowafanya watanzania wafikirie kuwa madini yao yanaibwa, kutokana na wawekezaji wa nje kuchukua muda mrefu kabla ya kuanza kulipa kodi.

Akiwa miongoni mwa waliopendekeza marekebisho ya baadhi ya vipengele vya sheria hiyo (MDAs), vilivyokuwa vikichelewesha kulipwa kwa kodi baada ya faida, hivyo kuufanya uwekezaji wa wageni katika sekta ya madini ufananishwe na wizi, Kafumu alisema, “Zaidi ya vipengele vitatu tulivifuta katika marekebisho ya sheria yaliyofanywa mwaka 2010…”. “Mfano kipengele kilichompa mwekezaji haki na uhuru wa kuhamisha faida ya mgodi mmoja kati ya kadhaa anayoimiliki, kwenda kwenye mgodi uliopata hasara, kuanzisha mgodi mwingine, hivyo kutolipa kodi hadi migodi yote itakapopata faida.

Jambo hilo liliwahi kufanywa na African Barrick Gold (ABG) ilipohamisha faida ya mgodi wake wa Tulawaka na kwenda kuanzisha mgodi wa Buzwagi,”Kafumu alisema. Aliongeza kuwa sheria iliruhusu uhamishaji huo ilimradi mgodi au mradi ulikuwa ni wa mmiliki mmoja, jambo lililowafanya wananchi wawalamike adini yao kuibwa kwa kuwa hawakuwa wakifahamu kinachoendelea kuhusu sheria na vipengele hivi.

Kafumu anakiri kuwa jitihada za kuwaelewesha wananchi kila jambo kuhusu mikataba na sheria hiyo hazikuwepo, ndio maana waliweza kuwaita wawekezaji kuwa ni wezi bila kufahamu kwamba vivutio vya uwekezaji walivyotengenezewa kwenye sheria za kodi za mwaka 1998, vililenga kuwahamasisha wawekeze nchini kwa kuwaonesha kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji, ingawa kwa kiasi fulani vivutio hivyo vimewaumiza watanzania wenyewe.

Alitaja vipengele vingine vya sheria hiyo ya madini vilivyofutwa mwaka 2010 kuwa ni kilichomtaka mwekezaji alipe Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka kwa Serikali ya Mtaa kama ushuru wa huduma, badala yake, kuanzia sasa watakuwa wakilipa ushuru wa awali wa asilimia 0.3 ya mapato kabla ya kuondoa gharama za uendeshaji au kodi nyingine kama sheria ya Serikali za mitaa ya mwaka 1982 inavyoelekeza.

“Serikali iliamua kufumba macho na kufuta kipengele hicho baada ya kuona kinazipunja halmashauri na kuzinyima uhuru wa kudai chochote pindi mapato mengi zaidi yanapopatikana,”Kafumu aliyeanzisha mazungumzo ya kufuta vipengele hivyo alipokuwa Kamishna wa Madini alisema hayo na kueleza kuwa mazungumzo yalifanyika kuwashawishi wawekezaji wenye mikataba wakubali kulipa kwa asilimia huku wapya wanaokuja wakilazimishwa kuitekeleza kwa kuwa ni sheria.

Kipengele kingine kilichotajwa na Kafumu kuwa kilifutwa mwaka 2010 kwa lengo la kupunguza muda mrefu wa mwekezaji kutoanza kulipa kodi ni kile kilichoitaka Serikali impe mwekezaji husika msamaha wa kodi ya mtaji kwa asilimia 15, ili aendeshe mradi wake kwa miaka saba kabla ya kuanza kulipa kodi.

“Kilichokuwa kikifanyika ni kumwongezea mwekezaji asilimia 15 ya mtaji wake pindi anapoanza kulipa mkopo wa asilimia 100 kutoka benki ambapo, kama alipaswa kurejesha riba ya asilimia 20 baada ya mradi kuanza na kubakiwa na asilimia 80 ya mtaji, Serikali ilimwongezea asilimia hiyo ili kimahesabu aonekane analipa mrejesho benki kwa miaka miwili zaidi ya inayotakiwa,hivyo kuwa na miaka saba ya kukaa bila kulipa kodi badala ya mitano inayostahili”, anasema Kafumu na kuongeza…“ …Lakini asilimia hiyo 15, haikuwa kumwongezea fedha bali ni mahesabu tu ndio yaliyokuwa yakirekebishwa ili kumpa haki ya kuwa na miaka miwili zaiidi ya kutolipa kodi.

Serikali ilifanya haya yote kwa nia njema ya kutaka kutengeneza mabepari wake yenyewe na kuachana na mfumo wa uchumi wa kijamaa.”

Ushawishi wa kuweka vivutio hivyo ulitoka wapi?Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zilifika Tanzania mwaka 1994 wakati nchi ilipoanza kufanya mabadiliko ya kiuchumi kutoka ujamaa kwenda ubepari na kusema kuwa ziko tayari kusaidia kufanya mageuzi ya sera na sheria za uchumi zikiwemo za madini ambapo zilitoa Dola za Marekani kati ya milioni 11 hadi milioni 20 kwa ajili ya mradi wa mageuzi wa miaka mitano.

Mradi huo ni kuanzia mwaka 1994 hadi 1998, ambapo sera na sheria mpya zilipotoka zilikuwa zimesheheni matakwa yao. SuluhishoPamoja na kutungwa sheria inayolenga kuwatafutia soko watoa huduma katika migodi na kwenye sekta ya madini kwa ujumla, kuna haja ya Serikali kutafuta namna ya kutengeneza miundombinu tayari kwa wawekezaji kuitumia na kulipia matumizi yake.

Kwa kufanya hivyo, gharama zitakazotumika katika uzalishaji zitakuwa si kubwa kiasi cha kuwashinda wazawa kuzimudu. Kodi baada ya faida nayo itaweza kulipwa kwa harana kama hakuna mlolongo wa gharama zenye kuhitaji kufidiwa kwanza.

Serikali itumie busara kufuta vipengele vyote vya sheria vinavyoinyima fursa ya kufanya maamuzi ya maendeleo juu ya wawekezaji wake katika sekta ya madini ili kuepuka kushitakiwa kwa kukiuka mikataba ya uwekezaji. Itaendelea Jumatano ijayo

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Namsembaeli Mduma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi